Thu
12
Dec
24
Dec 12, 2024 at 10:55AM
MBIVU na mbichi itajitokeza kwenye kinyang’anyiro cha uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) Ijumaa, Desemba 13, 2024 Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga atakapogaragazana na wapizani wake wawili kwenye mdahalo utakaopeperushwa kwenye runinga kote Afrika. Bw Odinga atashiriki jukwaa moja na wapinzani hao, Mohmoud Ali Youssouf wa Djibouti na Richard Randriamandrato wa Madagascar, kila mmoja akifafanua maono yake mbele ya hadhira itakayojumuisha wanachama wa Baraza Kuu la Umoja wa Afrika na Kamati ya Wawakilishi wa Kudumu (PRC), jijini Addis Ababa, Ethiopia. Kwenye ukumbi ambako mdahalo huo, almaarufu “Mjadala Afrika” utaendeshwa pia watakiwemo Makamishna wa AU, wanahabari na wageni wengine maalum. Kwenye taarifa, Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) inasema mdahalo huo unatoa jukwaa kwa wawaniaji kuelezea ndoto zao katika kutimiza lengo la AU la kusuka bara la Afrika lenye umoja, amani na ufanisi. “Mjadala huo utapeperushwa mubashara kuanzia saa moja jioni, saa za Afrika Mashariki kote Afrika na nje. Aidha, utapeperushwa kupitia tovuti ya AU na mashirika ya habari ya mataifa wanachama,” taarifa hiyo ikaeleza. Aidha, ikasema, mjadala huo utapitishwa kwa lugha sita rasmi za AU ambazo ni; Kiingereza, Kifaransa, Kiarabu, Kireno, Kihispania na Kiswahili. Mjadala huo utakita katika masuala ya kisera huku kila mgombeaji akielezea jinsi analenga kufanikisha kufikiwa kwa Ndoto na Malengo ya Agenda ya AU ya 2063 na utekelezaji wa miradi na mipango yenye umuhimu kwa Afrika na Watu wake. Wakati wa mjadala huo, unaoashiria kilele cha kampeni za uenyekiti wa AU, wagombeaji pia wataonya uelewa wao wa changamoto zinazoisibu Afrika huku akipendekeza namna ya kuzitatua. Miongoni mwa changomoto hizo ni; mapigano, misukosuko ya kisiasa, mapinduzi ya uongozi haswa magharibi mwa Afrika, ukame, baa la njaa, makali ya babadiliko ya tabianchi, miongoni mwa zingine. Tume ya AUC imetoa wito kwa umma kutuma masuala yao kwa wagombeaji hao kupitia sehemu ya kutolea maoni katika mtandao wa kijamii wa X, wakitaja majina yao na nchi waliko wanapofuatilia mjadala huo. Mdahalo huo unajiri baada ya Bw Odinga kukamilisha ziara yake katika mataifa ya Kaskazini mwa Afrika kusaka kura kutoka marais na viongozi wa nchi hizo. Majuma mawili yaliyopita Waziri huyo Mkuu wa zamani alibisha hodi katika mataifa mbalimbali ya Afrika Magharibi. Mnamo Agosti mwaka huu, Bw Odinga alipata uungwaji mkono kutoka kwa marais sita ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Wadadisi wanasema Bw Youssouf, ambaye ni Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Djibouti ndiye mpinzani mkuu wa Bw Odinga, kwa misingi kuwa anaungwa mkono na mataifa mengi yanayozungumza Kiarabu na Kifaransa.
Dec 12, 2024 at 10:14AM
MSANII wa Bongo, Diamond Platnumz, amevunja kimya chake kufuatia hatua yake ya kutotumbuiza katika tamasha la Furaha City Festival jijini Nairobi. Msanii huyo inasemekana alipokea kitita cha dola 150,000 (takriban Sh19.3 milioni) ili kupamba hafla hiyo lakini akaondoka ukumbini bila kutumbuiza, na ameweka wazi kuwa hatarejesha donge hilo. Katika video iliyoelekezwa kwa mashabiki wake, Diamond anaeleza kuwa yeye hufuata kikamilifu sera zake za utendakazi, ikiwa ni pamoja na kuheshimu muda uliopangwa. “Siwezi kulipwa dola 150,000 kisha nije kupigana kutumbuiza jukwaani,” alisema. “Nitafika ukumbini kwa wakati kusubiri mwandalizi wa hafla aniite jukwaani, nitaendelea kuangalia saa yangu, na muda wangu wa kutumbuiza ukiisha nitatoka nje ya ukumbi huo na sirudishi pesa zozote." Diamond alisisitiza kuwa hajihusishi na mabishano na wasanii wengine au waandalizi ili kupata nafasi yake jukwaani. "Sihitaji kujadiliana na waandalizi au kupigana na wasanii wengine ili niruhusiwe kutumbuiza. Hiyo sio nidhamu yangu," alisema kwenye video hiyo. Mwimbaji huyo pia alizungumzia madai yaliyotolewa na msanii wa Kenya Willy Paul, ambaye anadai kuwa uongozi wa Diamond ulimzuia kutumbuiza ili kuruhusu nyota huyo wa Tanzania kupanda jukwaani kwanza. "Itakuwa upumbavu kwangu kufanya hivyo; ina maana gani?" Diamond alihoji. "Mimi ndiye mhusika mkuu, ambayo ina maana wasanii wengine wote wanaigiza kabla yangu. Willy Paul anajaribu tu kutengeneza drama kwa sababu bado anatafuta umaarufu. Huu ni upuuzi—muziki unahitaji bidii na usimamizi mzuri, si ushupavu na huruma." Alisema kuwa alifika mapema na kusubiri kwenye gari lake, kwani anapendelea kutokaa nyuma ya jukwaa. “Tangu nilipofika kulitokea fujo ambazo hazikuisha, meneja wangu alimpigia simu mratibu kumuuliza kwa nini kuna fujo nyingi na kwanini mambo hayakusimamiwa ipasavyo, alijibu na kusema alihitaji dakika 10 zaidi. Kwa bahati mbaya, ghasia zilfika mahali nilipoketi," Diamond anaelezea. Hali ilipozidi kudorora, meneja wa Diamond aliamua ni bora amrudishe hotelini kwake. "Kulikuwa na fujo  pande zote za hafla, na sielewi kwa nini ilifanyika," anasema. "Msanii hawezi kutumbuiza chini ya hali kama hizi, na wengine wanaweza kuiona kama kukosa heshima." Diamond anasema alisubiri kwa takribani saa tatu bila kupanda jukwaani, akieleza kusikitishwa kwake lakini akathibitisha kuwa hakuwa na la kufanya. Wakati huo huo waandalizi wa tamasha wamejitetea. “Tunasikitika sana kutangaza kuwa Diamond Platnumz hakutumbuiza katika tamasha la Furaha City kama ilivyopangwa, sisi tukiwa waandalizi tulijitahidi yeye na timu yake walikuwa sawa, kuhakikisha mipango na dharura zote zilishughulikiwa ili kusiwe na matatizo.. Hata hivyo tabia na matakwa ya timu yake yalionekana kuwa ya kusikitisha na ya kupindukia kupita kiasi," ilisema taarifa hiyo. Huku wakikiri kulitokea suala dogo la kiusalama linalomhusisha msanii mwingine, walifafanua, "Tulitatua kwa haraka na kuhakikisha kwamba tamasha iliendelea kwa njia salama na ya kitaaluma. Tunaamini katika kuwatendea wasanii wote usawa na kudumisha viwango vya ubora wa juu kwa kila mtu anayehusika." IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA
Dec 12, 2024 at 10:12AM
HUJAMBO Shangazi? Kwa miezi mwili nimekuwa nikijaribu kumrushia mistari binti huyu mtaani. Yeye ni mrembo sana na amekuwa kivutio kwa akina kaka wengi. Licha ya jitihada zangu za kutaka kumnasa amekuwa akinipuuza na hata wakati mwingine kunionyesha dharau kupitia jumbe zake. Nifanyeje? JIBU: Sijambo! Anayokuonyesha binti huyu ni ishara tosha kwamba hana haja nawe. Usijikosee heshima kwa kuendelea kumfuata mtu ambaye hana haja nawe.
Dec 12, 2024 at 09:55AM
HUKU taifa likiadhimisha Sikukuu ya Jamhuri, wakazi wa Shimba Hills, Kaunti ya Kwale, wanahisi kusahauliwa kimaendeleo kwa kukosa barabara ya lami. Barabara ya Mrima–Mwabungo yenye urefu wa kilomita 56 ni ya mchanga na inaunganisha Shimba Hills na Barabara Kuu ya Likoni-Lungalunga. Hata hivyo, hali mbaya ya barabara hiyo hasa msimu wa mvua imekuwa changamoto kwa wakazi ambao usafiri wao unaathirika pakubwa kwani haiwezi kupitika. “Barabara hii imekuwa ahadi ya kisiasa kwa miaka mingi. Wanasiasa huahidi kuitengeneza kila uchaguzi, lakini baada ya kupigiwa kura, sisi husahaulika,” alisema Boaz Mwakasimu, Katibu wa Wakazi wa Shimba Hills. Akizungumza na Taifa Leo, alielezea kuwa mara nyingi magari ya kubeba bidhaa kama vile matunda, ambulensi, na hata bodaboda, hushindwa kupita kutokana na matope na mashimo makubwa. Shimba Hills, ambayo sasa ni kaunti ndogo, ni eneo la ukulima Kwale, huku matunda na mimea mingine ikipandwa na kuuzwa kwa wakazi katika miji kama vile Ukunda. Rhoda Matheka, mfanyabiashara wa eneo hilo, alisema hakuna magari ya usafiri wa umma yanayopita barabara hiyo. “Lazima utumie bodaboda ambayo inatoza hadi Sh500 kufika Ukunda. Mvua ikinyesha, hatuwezi hata kupata bidhaa tunazouza,” alisema. Kwa upande wake, Richard Sitoti alilalamika kuwa hali ya barabara imekuwa kikwazo kikuu kwa maendeleo. “Tumepata kiwanda cha kutengeza sharubati kutokana na matunda mbalimbali, lakini hali ya barabara itafanya iwe vigumu kusafirisha matunda hayo kufika kiwandani,” alisema Bw Sitoti, ambaye pia ni mkulima. Mbali na kilimo, huduma muhimu kama vile afya na elimu zimeathiriwa vibaya na hali mbovu ya barabara. Wakazi wanasema kuwa kufikia huduma za afya katika Hospitali ya Rufaa ya Msambweni pia ni changamoto kubwa, hasa wakati kuna dharura.
Dec 12, 2024 at 09:52AM
RAIS William Ruto anaongoza taifa katika maadhimisho ya Jamhuri Dei 2024, yanayofanyika leo, Alhamisi, Desemba 12 Uhuru Gardens, Nairobi. Kenya inaadhimisha miaka 61 baada ya kupata uhuru wa kujitawala kama Jamhuri Desemba 12, 1963, miezi sita na siku 11 baada ya kupata uhuru wa ndani kwa ndani kutoka kwa Mbeberu. Maadhimisho ya Jamhuri hufanyika kila mwaka. Rais Ruto, tayari ametua katika Bustani ya Uhuru, ambapo alitanguliwa na naibu wake, Prof Kithure Kindiki na Mkuu wa Mawaziri, Musalia Mudavadi. Dakika chache kabla ya saa nne asubuhi, kiongozi wa nchi alikagua gwaride la heshima lililoandaliwa na kikosi cha majeshi ya ulinzi ya Kenya (KDF). Kwenye hotuba yake, anatarajiwa kuainisha sera zake na ajenda za maendeleo kwa taifa. Rais wa Gambia, Adam Barrow ni kati ya viongozi mashuhuri Barani Afrika ambao wamealikwa kushiriki maadhimisho ya Jamhuri 2024.  
Dec 12, 2024 at 09:46AM
HUSEIN Mohamed ndiye kinara wa shirikisho la soka nchini FKE na anaingia afisini kukiwa na changamoto chungu nzima za kulemaza soka nchini. Hussein anatakiwa kubadilisha sera na sura ya FKF kutoka kwa ile ya msururu wa kashfa hadi shirikisho kubalifu ndani na nje ya Kenya. Anatakiwa afikirie namna ya kuhakikisha timu ya taifa Harambee Stars inanawiri na kuzima hii mizozo inayotokana na kukosa kuwalipa ujira wao makocha wa timu ya taifa na kuichia Kenya sifa mbaya Sijawa mzee wa kusahau mambo kwa hiari ama shuruti. Lakini tangu nilipoelewa soka vizuri, viongozi wa FKF walikuwa wa hadhi kubwa hata wakati shirikisho hilo halikuwa na fedha za kujipiga kifua kama wakati huu. Job Omino angekohoa mapema ya miaka ya tisini, ungefahamu yupo kiongozi. Peter Kenneth aliposhika ngazi 1996 mashabiki wa soka walikubali kazi lifanyika. Sasa tunamtaka Hussein ataayeoneana kwa hoja na vitendo. Inajulikana kuwa Hussein anapoingia uongozini tayari bundi amelilia kwa ngome yake. Kwanza, Kenya imepoteza fursa ya kuandaa mashindano ya kombe la mataifa barani Afrika mwaka ujao kwa kukosa kutimiza matakwa ya shirikisho la soka Afrika CAF. Rwanda wametunikiwa fursa hiyo kutokana na ubora wa viwanja vyake. Kasarani na Nyayo zetu zinadhaniwa na wakuu wa viwango kuwa nyuga za vijijini. Watangulizi wa Hussein walikuwa wameahidi kutimiza masharti hayo ila hilo halikutimia. Awe mtu wa kusema na kutenda. Asiwe mraibu wa msamiati wa “tumepanga, tutatenga na tumeweka mikakati.” Mojawapo ya masuala muhimu aliyoweka katika manifesto yake ni kushirikiana na wachezaji wa zamani wa soka na kuhakikisha kuna mfuko wa kulinda masilahi yao. Hii ni hoja komavu inayostahili uzingativu wa kina. Kenya kuna majina makubwa ya wanasoka kama vile Mahamoud Abbas ama 'Kenya One' ambaye alikuwa mlinda lango wa haiba kubwa. Baadhi hawajui jinsi bwana huyo alivyokuwa akinyaka mpira kama komba na kuifaa Kenya na AFC Laeopards kwa dhati katika miaka hiyo ya zamani. Wapo wachezaji wengine ambao wanapitia hali ngumu na wanafia kwa mazingira ovyo sana licha ya kuisaidia Kenya katika michuano ya zamani. Wachezaji hao inawezekana misuli yao ni hafifu; baadhi hawawezi kukimbia hata mita hamsini ila siku zao walichuana na nyasi. Kuna kitu wanachoweza kushauri. Tuwafanye mabalozi wa FKF na soka nchini jinsi yanavyofanya mataifa ya nje. Ndio sababu bado unasikia majina kama Maradona, Pele, Romario na Bebeto wa Brazil. Hussein ana bahati naibu wake alisukuma ngozi ya kulipwa Parma na Inter Millan. Anaelewa haya mambo ya kuyanadi majina ya wanasoka hata wanapostaafu. Kazi kwake, tunataka FKF yenye maono
Dec 12, 2024 at 09:31AM
ORTUM, POKOT MAGHARIBI MGANGA mmoja alishtua watu alipofungua kanisa na kugeuka mchungaji baada ya nyumba aliyokuwa akifanyia kazi kuchomeka mara kadhaa na vyombo vyake vya uganga kuharibiwa. Nyumba ya kazi ya babu huyo ilichomeka mapema mwaka huu kwa mara ya kwanza, lakini moto huo ulizimwa upesi. Miezi miwili baadaye, nyumba hiyo hiyo ilishika moto tena ambao wakazi walimsaidia kuuzima. Wiki hii, nyumba hiyo inayohifadhi nyenzo za kazi yake ilishika moto na kuchomeka yote na hakuna chochote kilichookolewa na jamaa akaamua kuokoka.Aliita mafundi na papo hapo shughuli za kujenga kanisa zikaanza. Kwa sasa,kanisa hilo limekamilika huku likitarajiwa kufunguliwa hivi karibuni. "Ni kama Mungu anataka niachane na uganga nimgeukie," jamaa alisema.
Dec 12, 2024 at 08:55AM
LEO ni Sikukuu ya Jamhuri. Siku ya Jamhuri ni mojawapo ya siku za kitaifa katika Jamhuri ya Kenya. Jamhuri ni nchi huru inayojitawala. Kenya inatambuliwa kama Jamhuri na mataifa mengine ulimwenguni. Katiba ya Kenya ya 2010, inataja wazi kuwa Kenya ni Jamhuri inayojitawala. Lugha ni mojawapo ya vipengele vinavyoitambulisha Jamhuri. Katiba ya Kenya ya 2010, inaeleza kwamba lugha ya kitaifa ya Jamhuri ya Kenya ni Kiswahili. Kwa hivyo, Kiswahili ni nyenzo inayoitambulisha Kenya kama Jamhuri. Kiswahili kama lugha ya taifa hutumiwa katika mikutano nchini kuwaunganisha wananchi kutoka maeneno mbalimbali nchini. Tunaposherehekea Sikukuu ya Jamhuri, ni muhimu kutambua Kiswahili kama lugha ya kukuza utangamano nchini. Tukumbuke kuwa hotuba nyingi katika mikutano ya sherehe za Jamhuri Dei zitatolewa kwa Kiswahili. Hii ni kwa sababu Kiswahili ndiyo lugha ya kukuza utaifa, uzalendo na utangamano nchini. Kiswahili ni lugha ya walio wengi. Kiswahili ni lugha ya wananchi katika Jamhuri ya Kenya. Kwa sababu ya umuhimu wa Kiswahili katika sherehe za Jamhuri Dei, mara nyingi hotuba ya Rais wa Jamhuri hutafsiriwa kwa Kiswahili. Watumishi wa serikali wanaomwakilisha Rais katika daraja mbalimbali za kiutawala wanatarajiwa kuwasomea wananchi hotuba ya Rais kwa lugha inayoeleweka na wengi. Lugha hiyo ni Kiswahili. Mojawapo ya utambulisho wa Jamhuri ni lugha rasmi zinazotumiwa katika shughuli za kiserikali katika Jamhuri husika. Katiba ya Kenya ya 2010 inataja wazi kwamba lugha rasmi za Jamhuri ya Kenya ni Kiswahili na Kiingereza. Ni jambo la kujivunia kwamba Katiba ya Kenya inatambua Kiswahili kuwa lugha rasmi ya Jamhuri. Tunaposherehekea Sikukuu ya Jamhuri, juhudi za kimaksudi zinahitajika ili kukifanya Kiswahili kiwe lugha rasmi ya kweli kiutekelezaji katika Jamhuri ya Kenya.
Dec 12, 2024 at 07:55AM
ALIYEKUWA Balozi wa Kenya katika Shirika la Umoja wa Mataifa (UN), Dkt Koki Muli anaonekana kutothaminiwa nyumbani licha ya kusaidia nchi nyingi za Afrika kuweka msingi bora katika mifumo yao ya uchaguzi. Dkt Muli alijaribu kuwa mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini (IEBC) mara tatu lakini hajafanikiwa licha ya uzoefu wake mkubwa. Kwa sasa, Dkt Muli anakabiliwa na kikwazo kingine kutokana na mzozo ambao unaendelea kutokota katika kambi ya Azimio kuhusu mwakilishi wa muungano huo kwenye jopo la kuwapiga msasa makamishna wapya. Nafasi hiyo imekuwa ikizozaniwa na Wiper ambayo imethamini Dkt Muli na chama cha NLP ambacho kimewasilisha jina la Augustus Muli ili ateuliwe katika jopo hilo. Mtaala wa uchaguzi ambao aliuandika Dkt Muli ndiye mwanamke pekee Afrika ambaye amehitimu kuwafundisha wanafunzi na kuwaidhinisha baada ya kumaliza masomo yao akitumia mtaala wa uchaguzi ambao aliuandika. Iliyokuwa Tume ya Kriegler ambayo ilibuniwa kuchunguza ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007, ilitambua juhudi na mafanikio yake. Kati ya nchi ambazo zimefanikiwa kutumia mtaala wa demokrasia, uongozi na uchaguzi ulioandikwa na Dkt Muli ni Afrika Kusini, Botswana, Lesotho, Msumbiji, Zimbabwe, Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Uganda, Tanzania, Liberia, Ghana miongoni mwa mingine. Nchini, Dkt Muli anaonekana kutokuwa na bahati kwenye jaribio lake mara tatu akitaka kuwa mkuu wa IEBC. Mnamo 2009 alihojiwa ili ateuliwe mwenyekiti wa tume ambayo ingesimamia kura ya maamuzi ya 2010. Cecil Miller aliteuliwa lakini jina lake likakataliwa na bunge. Miaka miwili baadaye Dkt Muli aliomba kazi hiyo lakini akapoteza kwa Isaack Hassan. Kabla ya kuteuliwa kwa Bw Hassan majina ya Dkt Muli na Murshid Abdalla yalikuwa yamewasilishwa kwa aliyekuwa Rais Mwai Kibaki na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga. Jopo la IEBC chini ya Aukot Jopo la uteuzi wa mkuu mpya wa IEBC wakati huo liliongozwa na Dkt Ekuru Aukot. Kama njia ya kumliwaza alipewa kazi ya kuwa naibu balozi wa Kenya kwenye Shirika la Umoja wa Kimataifa. Hata hivyo, ilikisiwa kuwa alikosa kazi hiyo kwa kuwa alitoka kwenye kijiji cha karibu Kaunti ya Kitui na alikokuwa akitoka Jaji Mkuu wa wakati huo Willy Mutunga. Kuelekea uchaguzi wa 2017, Dkt Koki alijaribu bahati yake tena lakini nafasi hiyo ikaendea Wafula Chebukati ambaye alimaliza muhula wake wa miaka sita. Dkt Muli ni mkuu wa kitivo cha sheria katika Chuo Kikuu cha Southeastern Kenya na mzozo wa sasa unaonekana kushusha azma yake kwa kuwa hatawania kuwa mkuu wa IEBC bali kuwepo kwenye jopo la kuwapiga msasa makamishna na mwenyekiti mpya. Katika mahojiano ya hapo awali, Dkt Muli alikataa mjadala kuhusu kuporomoka kwa azma yake mara tatu licha ya kuwa alionekana kuhitimu zaidi kuliko walioishia kukabidhiwa kazi hiyo. Japo bahati haijasimama Alisema kuwa japo bahati yake haijawahi kusimama, ataendelea kutumikia taifa lake. “Hii ni nchi yangu na nina ari ya kuona kuwa uchaguzi mkuu unakuwa huru na haki. Kwa hivyo niko tayari iwapo nitaitwa kusaidia tume kuhakikisha hilo,” akasema. “Si lazima nifanikiwe kuwa mkuu wa IEBC ila jambo muhimu ni kuwa anayeteuliwa anafahamu kazi anayoifanya, jinsi ya kuifanya na kupokea ushauri unaohitajika,” akaongeza.
Dec 12, 2024 at 06:55AM
UHUSIANO baina ya Shirikisho la Soka Nchini (FKF) na kocha wa Harambee Stars, Engin Firat umeporomoka baada ya maafisa wapya kuchaguliwa kuongoza soka nchini. Jana, Desemba 11, 2024, Firat alitangaza kujiuzulu akilalamikia kutolipwa malimbikizi ya mshahara wake ambao duru zinasema unaweza kuwa wa miezi 11. Rais mpya wa FKF Hussein Mohammed alithibitisha kung'atuka kwa kocha huyo ambaye aliajiriwa Septemba 2021. Serikali kupitia kwa Wizara ya Michezo ilikuwa imegusia nia yake ya kusitisha majukumu ya kocha huyo baada ya kushindwa kusaidia Harambee Stars kufuzu kwa fainali za Mataifa Bingwa barani Afrika (AFCON) zitakazofanyika Morocco, mwaka ujao. Mahojiano ya Waziri Kipchumba Murkomen Katika mahojiano na waandishi wa habari, Jumanne jioni, Waziri wa Michezo, Kipchumba Murkomen alidokeza mwisho wa enzi ya raia huyo wa Uturuki mwenye umri wa miaka 54. Murkomen aliyezungumza huku akiwa na matuamini makubwa kwa viongozi wapya waliochaguliwa, alimlaumu aliyekuwa rais wa FKF, Nick Mwendwa kwa kumteua Firat, bila kuchunguza vizuri rekodi yake. “Hata sielewi Firat aliteuliwa vipi kunoa timu ya taifa, kwa sababu hakuna rekodi kamili inayoonyesha ufanisi wake. Kuna wakati nilimuambia Nick machoni mwake kwamba huyo kocha wake wakati mmoja alipigwa 7-0 akiwa na timu ya taifa ya Moldova. Nilijaribu kusoma historia yake na sikuona ufanisi wowote. “Lakini tulipoingia ofisini tulitulia na kumuunga mkono kikamilifu. Hata kuna wakati alitaka ndege maalum ya kupeleka timu Cameroon na tukampa. Walitaka kuchezea Afrika Kusini, tukagharamia hiyo safari. Lakini baadaye akaanza kusema Stars haikufuzu kwa sababu ilichezea mechi zake katika mataifa ya kigeni! Nilijiuliza kwa nini watu wanashinda mechi za ugenini, ikiwa hiyo ndio sababu?” Murkomen alisema Serikali itafanya hesabu za Firat na kumlipa kufikia Juni mwaka huu, pamoja na marupurupu mengine kulingana na mkataba wake. Hussein akisaidiana na Mariga Alisema ana hakika afisi mpya ya FKF chini ya Hussein Mohamed akisaidiana na McDonald Mariga itatafuta kocha mzuri atakayeongoza timu ya taifa kitaaluma. “Nimesoma mkataba wake vizuri na nikapata mahali unasema tusipofuzu kwa AFCON 2025 anatakiwa aondoke. Kwa vile hatukufuzu, lazima aheshimu mkataba.” Baada ya kubanduliwa nje ya Afcon 2025, Firat alieleza nia yake ya kutaka kuendelea kunoa Harambee Stars, lakini baada ya mabadiliko ya uongozi, hali imekuwa ngumu kwake. Kulingana na mkataba huo, Firat alikuwa akipokea kati ya Sh1.5 na Sh2 milioni kila mwezi, huku kukiwa na madai kwamba hajapokea malipo yoyote kwa kipindi cha mwaka mmoja. Firat alipewa jukumu la kunoa Harambee Stars mnamo Oktoba 2020, mechi yake ya kwanza ikiwa dhidi ya Mali ugenini ambapo Stars ilizabwa 5-0 katika pambano hilo la mchujo wa Kombe la Dunia la 2022. Kusuasua kwa timu hiyo katika mchujo wa kufuzu kwa Kombe la Dunia la 2026 pamoja na kushindwa kufuzu kwa Afcon 2025 kulimweka katika hali ngumu.

Support Our Website

Ads help us keep our content on kenyalivetv.co.ke free for you. Please consider supporting us by disabling your ad blocker or whitelisting our site in your ad blocker settings.

You are currently offline.
You are back online.