Mwongozo Wa Mapambazuko Ya Machweo Na Hadithi Nyingine
Utangulizi
Mwongozo huu una nia ya kuwa mwanga gizani kwa wasomi wa diwani ya ‘Mapambazuko ya Machweo na Hadithi nyingine, kwa kutoa maelezo maridhawa kuhusiana na hadithi tofauti zilizomo humu. Ili kufanikisha hili, mwongozo huu umeangazia masuala kadhaa katika hadithi. Kabla ya kwenda katika hadithi binafsi, ni vyema kuangazia vipengele Fulani vya diwani.
Mada: Mapambazuko ya Machweo.
Mada ya diwani za hadithi fupi huwa ni mada ya mojawapo wa hadithi zilizomo. Hata hivyo, sharti iwe mada ya kuvutia wasomaji na pia yenye kubeba uzito katika diwani husika. Lnafaa kuwa mada ambayo ina uzito wa kutosha kubeba ujumbe wa diwani.
Mada ‘Mapambazuko ya Machweo’, ina athari ya kipekee kwa msomaji. Mapambazuko ni majira ya alfajiri, kabla ya jua kuchomoza hali Machweo ni wakati wa jioni, jua linapotua. Ukinzani katika mada unazua taharuki kwa msomaji, ambayo inamtuma kupitia hadithi za diwani hiyo ili kufahamu vipi Mambazuko yanatukia wakati wa Machweo.
Mada hii inaleta fikra tofauti. Kwanza, ujumbe wake unaweza kurejelea hali ya mafanikio baada ya tabu tele. Isitoshe, majira haya yananweza kurejelea umri, mapambazuko yakirejelea ujana nayo machweo uzee. Inaweza pia kumaanisha mafanikio katika machweo ya maisha(uzee).
Mada hii, hivyo basi, inabeba taarifa muhimu kwa ajili ya diwani nzima. Suala la matumaini au mafanikio katika/baada ya taabu limesawiriwa katika hadithi nyingi kwenye diwani hii. Hivyo, tunaweza kusema mada hii imefumbata ujumbe wa diwani nzima. Mifani ya hadithi zinazodhihirisha hali ya ‘Mapambazuko ya Machweo’ ni kama’Mapambazuko ya Machweo’, ‘Fadhila za Punda’, ‘Toba ya Kalia’, ‘Nipe Nafasi’,
‘Ahadi ni Deni’, ‘Sabina’ na nyinginezo.
Hivyo basi, ni wazi kwamba mada ‘Mapambazuko ya Machweo’ inafaa kabisa kwa diwani hii.
Jalada:
Jalada katika diwani ya hadithi fupi aghalabu hubeba ujumbe wa hadithi iliyobeba anwani. Hali si tofauti katika diwani hii. Jalada linaakisi hali katika hadithi ya ‘Mapambazuko ya Machweo.
Kuna bwana aliyevaa suti ambaye anaingia kwenye gari. Haikosi huyo ni Makutwa, anayemiliki gari la kibinafsi pekee mjini Kazakamba.
Kando yake, kuna mwanamume na mwanamke wanaoonekana kuwa katika hali ya majibizano kwa jinsi walivyoinua mikono, mwanamume mkono wa kulia na mwnamke mkono wa kushoto nyuso zikielekeana. Hawa bila shaka ni Makucha na mkewe Macheo ambao wana mjadala mara kwa mara kuhusiana na suala la Makutwa kumkebehi Makucha.
Kando ya wawili hao pembeni kulia, kuna kimeza kidogo chenye vifaa fulani na kiti chake. Haikosi hapo ni sehemu anapouzia vitafunio Makucha. Pembeni kulia kulia nako kuna sehemu ya nyumba, ambayo itakuwa ya Makucha na mkewe Macheo.
Mbele yao mbali kidogo, kuna watoto wadogo wanaoonekana kuwa katika shughuli za kuzoa mchanga. Hawa ni watoto ambao Makutwa anawatumikisha katika mgodi wake kinyume cha sheria.
Hali ya anga inadhihirisha kwamba ni wakati wa machweo. Kuna jua ambalo linaelekea kutua na anga imetamalaki rangi ya samawati. Mchanga walikokanyaga wahusika wote unatuhakikishia ni mandhari ya mji wa Kazakamba.
Kuutumia Mwongozo.
Mwongozo huu umechambua kila hadithi kwa mapana na marefu. Umeangazia masuala tofauti tofauti katika hadithi zote, ili kuhakikisha kwamba maomaji anaelewa yanayoshughulikiwa kwa ubainifu wa kipekee. Masuala haya yanaanzia kwa mtiririko wa hadithi na ufaafu wa anwani hadi mitindo ya uandishi. Masuala yaliyoshughulikiwa ni pamoja na;
Dhamira ya Mwandishi.
Ni lengo la mwandishi, yaani sababu ya kuandika hadithi husika. Inaeleza ujumbe ambao mwandishi alinuia kupitisha kwa msomaji. Inaweza pia kuelezwa kama mafunzo ambayo msomaji anapata kutokana na kusoma hadithi husika. Dhamira inaweza kuwa kupitisha ujumbe kwa njia tofauti ikiwemo kuonya, kusawiri hali Fulani katika jamii au kuelimisha kuhusu suala fulani.
Maudhui
Ni masuala nyeti yanayoshughulikiwa katika hadithi. Ni mambo makuu hasa kuhusu jamii yanayoibuka kutokana na kusoma hadithi Fulani. Baadhi ya maudhui yanayojitokeza katika hadithi nyingi ni pamoja na elimu, utamaduni, mapenzi na ndoa, migogoro na migongano, uzinzi, ulaghai na unafiki, usaliti, nafasi ya mwanamke, ubabaedume na mengi mengine.
Wahusika
Ni watu au viumbe ambao wanatumiwa na mwandishi kuwasilisha ujumbe wake kwa hadhira. Katika hadithi zote, wahusika waliotumika ni binadamu, wanaoakisi jamii halisi. Wahusika hawa hutofautiana kwa hulka(sifa) kulingana na ujumbe toofauti ambao mwandishi anawatumia kupitisha. Hivyo basi, kila mhusika, wahusika wakuu na wasaidizi huwa na sifa zake na umuhimu katika hadithi.
Mbinu za Uandishi.
Ili kuleta mvuto, mwandishi hawezi kutumia lugha iliyo kavu. Lazima aifinyange lugha na kuisuka kipekee ili kuleta mnato kwa msomaji anapoanza kupitia kazi yake. Kuna aina tofauti za mitindo ya uandishi ambayo hutumika kutimiza hili.
1. Istilahi za Lugha/ Tamathali za Usemi
Tashbihi/Tashbiha/Mshabaha. Hii ni mbinu ya kufananisha vitu viwili vyenye sifa sawa kwa kutumia vihusishi vya ulinganisho kama vile mithili ya, kama, sawasawa na, mfano wa na nyinginezo. Kwa mfano; Kamau ni mrefu mithili ya twiga.
Istiara/Sitiari. Hii ni mbinu ya kulinganisha vitu viwili vyenye sifa sawa moja kwa moja bila kutumia vihusishi vyovyote. Kwa mfano; Siku hizi amekuwa wali wa daku(yaani ameadimika, haonekani)
Tashihisi/Uhuishi/Uhaishaji. Ni mbinu ya kuvipa sifa za uhai vitu visivyo na uhai kama vile kuongea, kutangamana na kutekeleza mambo ya kibinadamu. Kwa mfano; hofu ilimkumbatia.
Methali. Ni tungo fupi zilizogawika katika sehemu mbili ambazo hubeba ujumbe wenye hekima. Huwa na maana ya juu, inayotokana na maneno yaliyotumiwa na maana ya ndani isiyohusiana na maneno hayo, ambayo huongoza matumizi yake. Kwa mfano; mla na miwili hana mwisho mwema.
Semi(Misemo na Nahau). Ni tungo fupi zinaoundwa kwa kuunganisha maneno, na ambazo maana yake na matumizi huwa tofauti na maneno yaliyotumika. Kwa mfano; enda segemnege- haribika, enda kombo.
Takriri/ Uradidi. Ni mbinu ya kurudiarudia neno au fungu la maneno kwa nia ya kutilia mkazo hoja fulani au kusisitiza. Uradidi huu unawea kutumiwa na mwandishi moja kwa moja katika usimulizi au ukatumiwa na mhusika katika mazungumzo. Kwa mfano;misitu kwa misitu ya mahindi na maharagwe.
Tabaini. Ni mbinu ya kutumia ukinzani kwa nia ya kudhihirisha wingi. Aghalabu hudhihirika kwa
matumizi ya ‘si’ ya ukanushi. Kwa mfano; kila kitu kwake kilipendeza, si macho, si uso, si mavazi, si viatu, si sauti.
Chuku. Ni matumizi ya maelezo yaliyotiliwa chumvi kwa ajili ya kuonyesha uzito wa jambo au hoja fulani, na pia kumtumbuiza msomaji. Maelezo huelezwa kwa kiasi cha kuchekesha, kwani huzua hali ambazo ni wazi haziwezekani, lakini zinazokubalika kifasihi. Kwa mfano; hasira zake zingeweza kuivunja bilauri kwa kuiangalia tu.
Balagha/Maswali Balagha. Ni mbinu ya kutumia maswali yasiyohitaji majibu, kwa kuwa aidha majibu yako wazi, hayapo au hayahitajiki. Maswali haya husaidia kuelewa fikra za mhusika, kutoa taarifa zaidi au kumchochea msomaji kuwaza zaidi. Kwa mfano; kwa nini haya yanipate mimi?
Uzungumzi Nafsia/Monolojia. Ni mbinu ambapo mhusika hujizungumzia mwenyewe aidha kwa sauti au akilini. Huwezesha msomaji kujua mawazo, maoni au mipango ya mhusika. Kwa mfano; “Muradi haya yashatokea, sina budi kukubali,” Mercy alijisemea moyoni.
Tanakali/ Tanakali za Sauti. Ni mbinu ya kuiga milio au sauti zinazotokea katika hali tofauti za kimazingira au sauti za wanyama na vitu tofauti. Kwa mfano; kriii! Kriii! Kriii! Simu yangu ilikiriza.
Dayolojia. Ni mbinu ya kutumia mawasiliano ya moja kwa moja kati ya wahusika wawili katika usemi halisi. Mawasiliano haya huhusu mada fulani wanayochangia wote. Mbinu hii busaidia kuonyesha mkinzano wa kimawazo, migogoro, maoni gofauti ya wahusika, n.k.
Kuchanganya Ndimi/ Lugha Mseto. Hii ni mbinu ya kutumia lugha mbili tofauti katika usemi, Kiswahili na lugha nyingine. Mara nyingi, maneno kutoka lugha ya pili huandikwa kwa mtindo wa italiki. Aghalabu huwa Kiingereza lakini yaweza kuwa lugha nyingine kama lugha ya mama, Kiarabu, n.k. kwa mfano; “Mwanao ni mzima. He’s out of danger.”
Utohozi. Ni matumizi ya maneno kutoka lugha nyingine, aghalabu Kiingereza yaliyobadilishwa muundo na matamshi kuwa ya Kiswahili. Kwa mfano. Daktari(doctor), begi(bag), ticket(tiketi),n.k
Kejeli/ Stihizai/ Dhihaka. Ni mbinu ya kutumia maneno ya kumsimanga mtu, tukio au suala fulani. Hali hii huweza kupunguza uzito wa hali au jambo au kumtilia mtu hamu ya kubadilika. Inaweza kutumiwa na mwandishi mwenyewe katika maelezo ya suala au mhusika kwa mwingine. Kwa mfano; alipata alama 10 katika hisabati. Kweli alijaribu, kama binadamu.
Nidaa. Ni mbinu ya kudhihirisha hisia za ndani kwa kutumia vihusishi na alama ya hisi(!). Kwa mfano, alifurahi sana kufika nyumbani. Popote ambapo alama hiyo imetumika, hiyo ni mbinu ya nidaa. Mtihani mkuu kwa mwanafunzi ni kufahamu hisia ambazo zinaakisiwa na alama hiyo. Zinaweza kuwa furaha, huzuni, mshangao, mtamauko, hasira, amri, n.k. Laiti angalijua!
Koja. Ni mbinu ya kudhihirisha wingi wa vitu kwa matumizi ya koma kwa ajili ya kuorodhesha. Mbinu hii inaweza kuwasilisha kuwepo kwa lukuki ya vitu au mfuatano wa matukio mengi. Kwa mfano; Maria alifika nyumbani, akavua sare za shule, akaoga, akaenda mtoni kuchota maji, akapika, akala na kulala.
Mdokezo. Ni mbinu ya kuachia mambo yakining’inia, yaani kuacha bila kukamilisha ujumbe fulani kwa kutumia alama za dukuduku(…). Inaweza kuwa sehemu inayoweza kujazwa, itakayoelezwa mbeleni au kumwachia msomaji kujijazia. Pia inaweza kuwa zao la kukatizwa kalima wakati wa mazungumzo. Kwa mfano; aliingia ndani na kusubiri akijua wazi kuwa mgaagaa na upwa…
Tasfida. Ni mbinu ya kutumia msamiati wenye adabu ili kuepuka lugha chafu. Hutumika kuepuka lugha inayoweza kuzua hisia hasi au kutia kinyaa. Kwa mfano, mja mzito badala ya kuwa na mimba, kubaua/kutabawali au kwenda haja ndogo badala ya kukojoa.
Tadmini. Ni mbinu ya kutoa marejeleo katika misahafu(vitabu vya kidini) kama vile Biblia na Korani, na kuyahusisha na hali fulani katika kazi ya kifasihi. Kwa mfano; ukaidi haujaanza leo, ulianza na Adamu na Hawa kwenye bustani la Edeni.
Tanakuzi. Ni mbinu ya kutumia maneno yenye kinyume katika sentensi moja na kuzua kauli zenye ukinzani. Aghalabu hutumika kuonyesha hali ya utata. Kwa mfano; asali iligeuka shubiri. Alikufa na kufufuka ilipobidi.
Lahaja. Ni matumizi ya maneno ya lahaja tofauti za Kiswahili ambayo hayapo katika Kiswahili sanifu. Upekee wake ni matumizi ya maneno yasiyo ya Kiswahili sanifu bali vilugha vyake. Kwa mfano; kahawa tungu(kahawa chungu), mwananti kuivunda nti(mwananchi kuivunja nchi).
2. Mbinu za Kimtindo
Sadfa. Ni mtindo ambapo matukio mawili yanayohusiana hutukia kibahati kwa wakati mmoja, au kwa mfululizo kama kwamba yamepangwa. Matukio haya aghalabu huwa na matokeo fulani. Kwa mfano; kukutana na msaada wakati wa tatizo bila kutarajia.
Kinaya. Ni mtindo ambapo matukio huenda kinyume na matarajio yetu, aidha kulingana na mfululizo wa awali wa matukio, au kwa kuyalinganisha na maisha halisi. Pia mbinu hii inaweza kudhihirishwa kupitia kwa usemi wa mhusika. Kwa mfano; kumpa hongera mtu aliyefeli au kusherehekea baada ya kufeli.
Majazi. Ni mtindo wa kuwapa wahusika majina kulingana na tabia au maumbile yao. Majina haya huitwa majina ya majazi/kimajazi. Kwa mfano; mtu katili anaweza kupatiwa jina ‘Kedi’.
Taswira. Mtindo wa kutoa maelezo ya ndani kuhusu suala fulani kiasi cha kujenga picha ya kile kinachorejelewa kwenye akili ya msomaji. Kuna taswira toofauti kama vile mwonekano, mnuso au harufu, hisi na mguso, kulingana na picha inayozalishwa. Kwa mfano; kaptura yake nyeusi iliyochakaa ilirembwa kwa viraka vya kila rangi, hungetambua rangi yake asilia.
Taharuki. Ni mtindo wa kutoa maelezo taratibu kwa kusaza habari fulani ili kumtia msomaji hamu ya kujua zaidi. Pia huweza kumwacha msomaji akining’inia mwishoni mwa kisa na kumwacha kujijazia kuhusu masuala fulani.
Kisengerenyuma/Mbinu Rejeshi. Ni mtindo wa kurejelea matukio yaliyotukia muda uliopita, lakini yenye uhusiano na yale yanayosimuliwa. Yanaweza kurejeshwa na msimulizi au mhusika fulani kupitia kumbukumbu zake.
Kiangaza Mbele/Kisengerembele/Kionambele. Ni mtindo wa kudokeza mambo yatayotukia mbele kabla hayajatukia, na kuyahusisha na yale yanayotukia wakati huo.
Utabiri. Ni mbinu ambapo mhusika hudokeza jambo kisha likatukia baadaye bila yeye kutarajia. Tofauti yake na Kiangazambele ni kwamba utabiri huwa jambo la kukisia au kudokeza tu, bila uhakika wake wa kutokea.
Jazanda. Ni ufananisho wa mzito wa vitu viwili visivyo na uhusiano wa moja kwa moja, ambavyo hulinganishwa na kulinganuliwa kwa njia ya mafumbo. Kwa mfano, Bi. Sarafu alilalamika kuwa jembe la mumewe lilishindwa na kazi.
Ishara. Ni mambo, vitu au matukio ambayo huonekana au kutukia kabla ya jambo fulani yanayoashiria. Mambo haya huwa na uhusiano fulani na matukio yanayoashiria. Kwa mfano; milio ya bundi inayomtia mhusika wasiwasi kabla ya janga fulani kutokea.
Ritifaa. Ni mtindo ambapo mhusika aliye hai humzungumzia mhusika aliyefariki kama kwamba yuko hai na anamsikia. Huweza kuonyesha uhusiano kati yao, kueleza hisia za ukiwa au kumtakia neema.
Lakabu. Ni matumizi ya majina ya kupanga kuwarejelea wahusika. Majina haya huambatana na sifa fulani za mhusika. Tofauti na majazi ni kuwa lakabu huwa majina ya kupanga, bali si majina halisi ya wahusika.
Ushairi Nyimbo. Barua
Mwingiliano wa Vipengele.
Ni muhimu kuelewa kwamba kuna mwingiliano wa kipekee katika vipengele hivi tofauti vya hadithi, kwani haviwezi kushughulikiwa kwa ukamilifu. Baadhi ya mwingiliano ni kama ufuatao;
Dhamira ya Mwandishi na Maudhui. Dhamira ndiyo huongoza maudhui ambayo yanashughulikiwa katika hadithi. Hivyo basi, mambo haya mawili huingiliana pakubwa. Dhamira ndiyo hufungua nafasi kwa maudhui ya hadithi. Kwa mfano, iwapo mwandishi anadhamiria kudhihirisha maovu yanayotendewa wananchi na wanasiasa au viongozi, lazima kuwepo maudhui ya siasa au uongozi au yote.
Dhamira na Wahusika. Kila dhamira huwasilishwa kwa kutumia mhusika au wahusika fulani. Bila wahusika, dhamira haiwezi kutimizwa wala wahusika hawawezi kuwa na maana bila dhamira. Sifa za wahusika zinalingana na dhamira na kubwa zaidi, umuhimu wao huhusiana moja kwa moja na dhamira ambayo wanatekeleza. Kwa mfano, iwapo mwandishi anadhamiria kudhihirisha madhila ya wanawake katika jamii, lazima awepo mwanamke anayetekeleza dhima hiyo.
3. Maudhui na Wahusika.
Maudhui huwasilishwa kupitia kwa wahusika pia. Vitendo vya wahusika ndivyo huzalishwa maudhui yanayoangaziwa katika hadithi. Hivyo basi, kuna uhusiano mkubwa kati ya sifa za wahusika na maudhui. Kwa mfano, kukiwepo na maudhui ya usaliti, lazima kuwepo mhusika msaliti, iwapo kuna maudhui ya tamaa na ubinafsi, lazima kuwepo mhusika mbinafsi na mwenye tamaa. Hivyo basi, ni vyema msomaji kuoanisha masuala haya pale ambapo hayashughulikiwa yote mawili.
Maudhui na Mtindo/Mbinu za Uandishi. Kuna pia mwingiliano wa kadri kati ya vipengele hivi. Japo si kila mara haya hutokea, baadhi ya mbinu huingiliana na Maudhui. Baadhi ya mbinu husawiri maudhui fulani. Kwa mfano, mtindo wa kinaya aghalabu huhusiana pakubwa na maudhui ya usaliti. Mbinu tofauti pia hubeba maudhui mengine kama vile dayolojia, ushairi, nyimbo, n.k.
Mtindo na Wahusika. Mitindo pia huweza kusaidia kuelewa wahusika na hulka zao zaidi. Kwa mfano, mbinu za majazi na lakabu husaidia katika kuelewa sifa za wahusika fulani. Mbinu nyingine zinazoleta haya ni kama dayolojia, kinaya, uzungumzi nafsia na nyinginezo.
Kutokana na maelezo haya, ni muhimu kutilia maanani kila ujumbe unaopatikana kwenye hadithi zote ili kuimarisha uelewa wake na pia kuwa na uwezo wa kukabiliana nazo katika mtihani.
1.Fadhila za Punda- Rachel Wangari. Mtiririko
Lilia anagutuka kutoka usingizini kwa hofu. Anamsubiri mumewe Luka. Amelala kochini ili amfungulie haraka. Anagundua kwamba bado hajafika kama alivyodhania, lakini hili halimpunguzii hofu, kwani ana hakika kuwa atakuja tu, tena kwa hasira tele kwa kukosa kupokea simu yake, ambayo ilipigwa akiwa bafuni. Ni saa nane za usiku na watu wamelala.
Anafahamu kuwa mumewe haji na kuamua kuelekea kitandani kulala. Anapita kwenye kioo kilichopasuka, tokeo la pigo moja la awali la mumewe. Anajiona alivyobadilika, kovu shavuni na donda linaloelekea kupona kipajini. Anakumbuka uso wake awali ulivyokuwa laini na wa kupendeza, na kushangaa hasa sababu ya Luka, mumewe, kubadilika na kuwa mkali hivi. Hatimaye analala.
Tunarejeshwa awali, Lilia alipomwona Luka mara ya kwanza, katika kanisa la babake, alipoingia ghafla tu. Alilazimika kukaa karibu na Lilia kwa kuwa ndipo palikuwa na nafasi. Alivaa mavazi ya kimaskini, lakini alipoomba kuimba, aliisikia sauti yake iliyokuwa tamu ajabu, iliyompendeza hata babake Lilia.
Babake Lilia ni mjane kwa miaka mitatu, lakini kila mara Lilia anamwondolea mawazo ya marehemu mkewe, kwanza kwa jinsi wanavyofanana na pia kwa ule ulimi wake usiotulia. Anamweleza kuhusu Luka na sauti yake yake ya kipekee. Anapomsumbua kuhusu kijana huyo, anaamua kumwalika ofisini Jumapili inayofuata. Mhubiri anajuta kuchelewa kupata mtoto mwingine kabla ya mkewe kufariki kwa ajali.
Shinikizo la kuoa tena haliridhii, kwani haoni yeyote anayeweza kujaza pengo la mkewe.
Anampa mamake Luka kazi ya kusafisha kanisa, naye Luka anajiunga na shule ya msingi kwa hisani ya mhubiri. Anaondokea kuwa mwerevu. Urafiki wake na Lilia unamtia mchungaji kiwewe, na hivyo anamtuma Luka kwa mhubiri rafikiye upande mwingine wa nchi. Urafiki wao haukatishwi na hili.
Wanazidi kuwasiliana kwa simu na barua. Wanakutana tena katika chuo kikuu kimoja. Baba anamwonya bintiye lakini hamsikizi kutokana na mapenzi.
Lilia anamkumbusha babake kuhusu amri ya Mungu ya mapenzi. Luka anamsisitizia kuwa ana nia safi kwa mwanawe na ataka kumuoa. Japo hisia fulani zinamfanya kutomwamini Luka, hana ushahidi na pia hataki kumvunja moyo bintiye. Anawapa Baraka zake. Wakati huu Lilia ni meneja wa benki moja. Luka anaongoza mahubiri kanisani kutokana na uzee wa baba Lilia, mhubiri mkuu. Kanisa linakua na kufurika hadi mahema kuongezwa.
Baba Lilia anafariki na Luka kuchukua uongozi kamili wa kanisa. Anamshinikiza mkewe kuacha kazi ili atunze fedha za kanisa, japo kuna mhasibu anayefanya kazi nzuri. Anamtaka kukaa nyumbani na kuandamana naye anapohitajika. Umaarufu wa Luka unazidi hadi anafika ikulu.
Luka anaamua kuingilia siasa japo mkewe hapendezwi. Anauza kanisa, lakini Lilia ananyamaza kulinda ndoa. Kampeni zanamchosha Lilia hadi siku moja anapokataa kabisa kushiriki, akiwa na uja uzito wa miezi mine. Luka anaudhika na kuondoka nyumbani. Jioni ya siku inayofuata, anapelekwa hosppitalini na majirani na kupoteza uja uzito. Luka hahuzuniki sana, kwa kuwa hataki kuwa mzazi wakati wa uchaguzi.
Luka anafaulu kuwa gavana lakini anawasahau wananchi. Anakuwa mzinzi. Anapohamia kasri la gavana, anamsahau mkewe na kumtaka kubaki vijijini ili awe karibu na raia. Anamtembelea mkewe wikendi.
Anapata taarifa kuwa mumewe ana vimada, lakini haamini hadi anapomtembelea ofisini bila habari na kumpata na mwanamke mwingine. Wanazozana na kuamrishwa arudi nyumbani, jambo analotii. Jioni hiyo, Lilia anapigwa na kuonywa vikali dhidi ya kwenda ofisi bila idhini ya mumewe. Hatimaye anaishia kutawishwa, haongei na watu kwa hofu ya kupigwa. Anamwona mumewe akiandamana na yule mwanamke aliyepata ofisini, anayetaniwa kuwa mshauri wake.
Wakati mmoja anaamua kuripoti polisi. Anapofika, anapelekwa kwa mkuu wa kituo. Mkuu huyu anaposifia ukarimu wa mumewe waliyekuwa pamoja wiki jana, anajua kuwa hatasaidika. Anadanganya kuwa anamtafuta askari polisi aliyemfaa siku moja na kujiendea. Anatoka kwa hofu akijua Luka ataambiwa. Siku mbili zikapita, kisha siku ya tatu ndipo akakosa kupokea simu yake, naye Luka akakosa kufika.
Luka anafika siku tano baada yake kutembelea kituo cha polisi na kumpiga vibaya hadi anapopoteza fahamu na kutoweka. Anaiona simu yak chini na kuichukua, na kumpigia mama mkwe na kuzirai tena. Anapopata fahamu, yuko mikononi mwa mama mkwe anayemhudumia. Anamlaani Luka kwa anayomtendea mkewe licha ya fadhila za baba Lilia kwake. Anampigia Luka kumwamrisha atume ambulensi, akimtishia kupiga simu polisi na kituo cha habari. Anakata na kuendelea kumshughulikia mkaza mwanawe. Kabla ya fahamu kumtoka, Lilia anasikia mlio wa ambulensi.
Anapogutuka, anajipata peke yake kitandani kwenye chumba cha hospitali. Mama mkwe anamtembelea kila siku kumuunguza, wala hajamwona mumewe. Siku ya nne, anamwona mtu kando yake, hamtambui kwani amefungwa bendeji usoni, nao mguu umeinuliwa. Mama mkwe anapokuja, anaelekea kwa kile kitanda. Akija, anawahudumia wote wawili. Anamrejelea kuwa gavana, lakini Lilia haelewi ni gavana yupi na kwa nini wamo chumba kimoja, naye mama mkwe hana nia ya kumweleza.
Mgonjwa mwenzake anaanza kutembelewa na marafiki na wafanyakazi waliokunja nyuso. Anawasikia wauguzi wakisema huenda asitembee tena kutokana na ajali aliyopata, ambayo nusura imwangamize. Lilia anaelewa mambo siku ya nne, mama mkwe anapofika na kumwita mgonjwa kwa jina, Luka!
Anamweleza kuwa kiruukanjia wake aliondoka baada ya kusikia hawezi kutembea tena. Lilia naye ameruhusiwa kwenda nyumbani. Anapomwangalia mumewe, anadhani anaona chozi likitoka kwenye jicho la kushoto ambalo halijafungwa bandeji.
Ufaafu wa anwani ‘Fadhila za Punda’.
Anwani hii inatokana na methali isemayo, ‘Fadhila za punda ni mashuzi’, kama ilivyotumiwa katika hadithi yenyewe. Pia huweza kuwa ‘Fadhila za punda ni mateke’. Matumizi ni kwa ambaye hulipa hisani kwa nuksani, yaani wema kwa uovu. Fadhila za punda, hivyo basi, ina maana ya matendo mabaya kutoka kwa mtu aliyetendewa mema. Mada hii inaafiki hadithi.
Luka ana fadhila za punda. Kwanza, kanisa ambalo linamlea na kumjenga akiwa maskini anaponeemeka analiuza bila kujali. Umaarufu na utajiri anaopata hapa unamtia kiburi sana.
Luka analipa fadhila za Lilia kwa mashuzi. Lilia ndiye anampigania kwa mhubiri hadi anaposaidiwa kimaisha na kimasomo, akasoma hadi chuo kikuu.
Lilia vile vile anapigania penzi lake kwa Luka kwa kila hali. Anatia bidii kuhakikisha mapenzi yao yanadumu kila babake anapojaribu kuwatenganisha. Hata maonyo ya baba mtu hayamfanyi kubadili msimamo. Hatimaye wanaruhusiwa kuoana.
Licha ya haya yote, anamtesa Lilia katika ndoa yao kwa kipigo cha kila mara kutokana na visingizio vya hapa na pale, kama vile chakula kukosa chumvi ya kutosha na kuchelewa kumfungulia. Anamtia makovu katika uso uliokuwa mzuri na mwororo awali.
Licha ya kutopenda siasa, Lilia anamsaidia Luka katika azma yake ya kuwa gavana hadi anapofaulu. Hata hivyo, anamdhalilisha na kumtelekeza anapotwaa wadhifa huo na kutomjali kabisa.
Lilia anampenda mumewe kwa dhati ya moyo na yuko tayari kufanya kila awezalo kulinda ndoa yake. Anaridhia matakwa ya Luka na kuwa mwaminifu kwake. Luka kwa upande wake, badala ya kulipa fadhila hizi kwa kuwa mume mwema, ana vimada wa pembeni wal hafanyi lolote kumficha mkewe ukweli huu.
Baba Lilia anamtendea Luka mengi. Anafadhili elimu yake na kumlea kama mwanawe na hatimaye kumkubalia kumwoa bintiye. Anapofanikiwa baadaye, anaanza kumtesa bintiye aliyeahidi kumtunza.
Luka anpiga kampeni kabambe katika azma ya kuwa gavana, nao wananchi wanamuunga mkono. Anapofanikiwa, halipii fadhila zao kwani anawasahau kabisa, wala dhiki yao haimshtui.
Kimada wake Luka pia anakejeli fadhila za Luka. Anamzuzua na kumfanya kumsahau kabisa mkewe wa ndoa. Anaandamana naye kila mahali akiwa gavana. Anapopata ajali na kulazwa hospitali, kimada huyu anamtoroka baada ya kusikia hawezi kutembea tena.
Dhamira ya Mwandishi
Kuonya dhidi ya kuwaamini waja wanaojitia ucha Mungu, kwani unaweza kuwa bandia. Ucha Mungu si kilemba cheupe tu. Ni vyema kufanya uchunguzi wa ndani kabla ya kumwamini yeyote.
Anadhamiria kutoa ushauri kuhusiana na nafasi ya mzazi katika makuzi ya mwanawe au wanawe na jinsi ya kutekeleza malezi kwa tija.
Ananuia pia kutoa maonyo kwa viongozi wasiowajibikia wajibu wao wanapotwikwa mamlaka kuwa siku yao itafika.
Kuonya watenda maovu kuwa siku ya kuyalipia itakuja, kwani malipo ni hapa hapa duniani.
Kuonya dhidi ya uvumilivu usio na tija katika ndoa za dhuluma ambao unaweza kuleta madhara yasiyomithilika kwa wahusika.
Kudhihirisha jinsi mwanamke anavyodhulumiwa katika jamii na jinsi anavyoweza kukabili na kupinga dhuluma hizi.
Kuonyesha sura za migogoro katika jamii na jinsi zinavyoathiri maisha.
Maudhui Mapenzi na Ndoa
Mapenzi ndiyo chemchemi inayochangia ndoa. Kuna ndoa ya babake Lilia ambayo ilitawaliwa na mapenzi, kwani wakati huu mkewe ashaaga. Kila mara mhubiri huyu anamkumbuka. Hata anashindwa kuoa mke mwingine kutokana na mapenzi yao ya dhati. Anapatwa na huzuni tele baada ya kuaga kutokana na ajali ya barabarani. Mwandishi anasema kuwa lau si ulimi wa bintiye usiotulia, dhiki ya kuachwa na mkewe ingemsukuma kaburini. Fahari kuu ya ndoa inadhihirika kupitia kujaliwa kwao binti huyu, Lilia, ambaye anfanana na mamake.
Ndoa kuu, hata hivyo, ni kati ya Luka na Lilia. Mapenzi yao yanaanza Lilia anapomwona Luka kwenye kanisa la babake, huku amevalia kimaskini. Sauti yake tamu inamvutia mara moja na hapo haachi kumwaza. Mapenzi yake kwa Luka yanamsukuma kumwomba babake amsaidie. Babake anampeleka katika shule ya msingi na kumpa mamake kazi ya kusafisha kanisa. Anamwelimisha hadi chuo kikuu, yote kwa ajili ya bintiye anayempenda Luka kwa dhati.
Usuhuba kati ya wawili hawa unaanza mapema, tangu wakiwa wachanga. Unamtia kiwewe babake Lilia, ambaye anajaribu kila mbinu kuwatenganisha bila mafanikio. Anapompeleka Luka upande mwingine wa nchi kwa mhubiri mwenzake, bado wanawasiliana kwa barua na simu. Bintiye anamsisitizia amri ya Mungu ya mapenzi na kumtaka awape baraka zake. Licha ya hisia za hofu kwa Luka, anawaruhusu kuoana.
Ndoa yao inaenda vizuri hadi babake Lilia anapofariki. Hapo Luka anabadilika na kuwa mwovu. Anamshinikiza mkewe kuacha kazi na kumtawisha. Hatimaye anaamua kujitosa katika siasa na mkewe anatakiwa kuwajibika, licha ya kuwa hapendi siasa. Anapokataa kushirikiana naye baada ya muda, anamkumbusha kuwa wanawake ni wengi na kumwacha pekee nyumbani. Analazimika kukimbizwa hospitalini na majirani na anapoteza uja uzito wake wa miezi minne, lakini Luka hahuzuniki sana.
Anaamini bado upo muda wa kupata watoto.
Mambo yao yanaharibika kabisa Luka anapokuwa gavana. Anaanza kuwa na vimada, huku akimlazimisha mkewe kuishi vijijini ili awe karibu na raia. Anamtembelea wikendi lakini hana muda naye, shughuli muhimu kwake ni kujiandaa kwa ajili ya wiki inayofuata. Mkewe anapomtembelea bila habari na kumpata na mwanamke mwingine, hajali chochote bali anamfokea mkewe na kumtaka arejee nyumbani na kuacha ujumbe Jioni hiyo anaporudi nyumbani, Luka anampiga mkewe vibaya, huku akimkanya dhidi ya kufika ofisini kwake bila taarifa na kutoheshimu wageni wake. Huu unaondokea kuwa mwanzo wa vipigo vya mara kwa mara. Ata kuhusiana na marafiki na majirani ananyimwa. Mumewe anaandamana na yule kimada wake katika hafla zote bila haya.
Lilia anaamua kuripoti polisi lakini anaghairi anapogundua mkuu wa polisi anajuana na mumewe. Anahofia usalama wake kutokana na kisa hicho, akijua mumewe atajua, pamoja na kukosa simu yake akiwa bafuni. Hofu yake inaondokea kuwa ukweli, kwani Luka anaporejea, anampiga vibaya hadi anapozirai na kumwacha. Anapopata fahamu, anamwita mama mkwe anayemwauni kwa kumpeleka hospitali. Hata haamini Luka anaweza kumfanyia Lilia hivi!
Haibainiki ndoa ya Luka inachukua mkondo gani mwishowe. Mkewe anatibiwa na kuruhusiwa kuondoka hospitalini, hali Luka mwenyewe amelazwa baada ya kupata ajali. Kimada wake naye amemtoroka baada ya kusikia huenda asiweze kutembea tena maishani.
Nafasi ya Mwanamke Katika Jamii.
Mwanamke katika jamii hii amepatiwa nafasi finyu sana, licha ya kuwa na mchango wa kipekee. Kwanza, mwanamke anadhihirika kuwa mpenzi wa dhati ya moyo. Mhubiri anamkumbuka mkewe waliyependana kwa dhati na ambaye anapofariki, anashindwa kabisa kuoa mke mwingine wa kujaza
pengo lake. Anashinikizwa na wahubiri wenzake, wazee wa kanisa na hata washirika wake lakini anashindwa kabisa kumwoa mwingine.
Lilia anapomwona Luka mara ya kwanza tu, anampenda kwa dhati hasa kutokana na sauti yake ya kupendeza. Anamshinikiza babake hadi anapompa mamake kazi ya kusafisha kanisa na hata kumpeleka Luka shule. Majaribio ya babake kuwatenganisha hayazai matunda kwani Lilia yuko mstari wa mbele kumpigania Luka wake hadi wanaporuhusiwa kuoana na baba kuwapa baraka zake.
Hata Luka anapoingilia siasa, Lilia anamsaidia licha ya kutopenda siasa. Anamvumilia na ukware wake na kubaki kuwa mwaminifu siku zote. Anampiga mara kwa mara, lakini anazidi kumshughulikia kama mumewe hadi anampiga na kumsababisha kulazwa hospitalini. Wanakutana huko baada ya Luka kupata ajali ya barabarani na kupoteza uwezo wa kutembea. Hatujui ndoa yao inachukua mkondo gani.
Mamake Luka pia ana mapenzi ya kipekee. Anampenda mwanawe Luka na anajitolea kumlea vyema licha ya umaskini wake. Lilia anapopoteza fahamu baada ya kipigo, anachukua simu na kumpigia. Anafika mara moja na kumhudumia. Anampigia mwanawe na kumlazimisha kutuma ambulensi, kisha kumpeleka Lilia hospitalini na kumuuguza.
Mwanamke pia anachukuliwa kama kiumbe dhaifu cha kuendeshwa na kuelekezwa na mwanamume. Luka anampa mkewe maagizo anayotaka kila mara. Anamkataza kujumuika na marafiki na anapofanya hivyo anampiga vibaya. Anamlazimisha kukaa nyumbani kama mtawa na kumtaka kumpigia simu akitaka kufika ofisini. Anapokosa simu yake akioga, anaingiwa na hofu kuu, kwani anajua yatakayofuatia. Luka anampiga mara kwa mara hadi mwisho anapolazwa hospitalini.
Mwanamke pia anasawiriwa kama chombo cha kumstarehesha mwanamume. Luka anamwambia mkewe kuwa wanawake ni wengi anapokataa kuandamana naye katika kampeni. Kulingana naye, ni rahisi kwake kupata wanawake wengine. Anapokuwa gavana, ana vimada wengi wala hajali hili linavyomwathiri mkewe. Anapomtembelea anampata na mwanamke mwingine. Badala ya kuwa na haya anamfokea na kumlaumu. Mwanamke yule naye pia anaendelea kuhusiana na Luka kimapenzi licha ya kujua ana mke.
Mwanamke pia anachorwa kama msaliti. Kimada wa Luka anajua kuwa ana mke lakini bado anasuhubiana naye na hata kuandamana naye katika shughuli rasmi. Hajali machungu anayomletea mkewe Luka. Isitoshe, anamtoroka Luka anapomhitaji zaidi, pale anapopata ajali na kupoteza uwezo wa kutembea.
Usaliti
Luka anamsaliti babake Lilia. Mzee huyu anajitolea kumfaa kwa kila hali tangu akiwa mchanga. Anamsomesha na kumpa uongozi wa mahubiri katika kanisa lake. Anapofariki, anauza kanisa lake kwa nia ya kujifaidi binafsi. Pia anamsaliti kwa kuvunja ahadi aliyotoa ya kumlinda bintiye, kwani baada ya kumwoa anaanza kumtesa.
Luka pia anamsaliti mkewe Lilia. Kwanza, anamsaliti kwa kumwendea kinyume licha ya uvumilivu wa madhila ya mumewe na pia uaminifu wake. Pia, mkewe anapigania penzi tangu wakiwa wachanga. Anamshinda hata babake anayemshuku Luka. Licha ya haya yote, Luka anamtesa kwa mapigo ya kila siku hadi mwishowe anapolazwa hospitalini kwa mapigo haya.
Luka pia anasaliti dini na imani kwa kutumia kanisa kwa ajili ya manufaa ya kibinafsi. Kanisa linakua na kuimarika chini ya mahubiri yake, lakini linapokua, analigeuza biashara. Hatimaye analiuza na kuingilia siasa. Anasaliti dini na Imani pia kwa kubadilika na kuwa laghai, mkware, dhalimu miongoni mwa maovu mengine.
Kimada wa Luka anamsaliti kwa kumwacha anapomhitaji zaidi. Licha ya kumtelekeza mkewe kwa sababu ya kimada huyu, anamwacha kwenye kitanda cha hospitali anapopoteza uwezo wake wa kutembea.
Isitoshe, anamsaliti Lilia kwa kuhusiana na mumewe akijua vyema amemwoa.
Dini
Jamii hii imejikita katika dini ya kikristo. Dini inachukua mkondo wake wa kuwapa waja tumaini na kuwatia shime. Dini pia inasaidie walio katika taabu kuwa na tumaini la maisha.
Lilia anakutana na Luka mara ya kwanza katika kanisa. Wako katika darasa la mabaleghe anapofika. Sadfa kuwa ni pale alipokaa tu Lilia penye nafasi anaiona kama ni Mungu anamjaribu. Anaketi na masomo kuendelea. Mwishoni mwa somo anapatiwa nafasi ya kujitambulisha. Anamtukuza Mungu kwa wimbo unaowapendeza waliomo humu, hata mhubiri anayekuja kuwajulisha muda umekwisha.
Lilia pia amelelewa katika misingi ya kikristo, kwani babake, Lee Imani ni mhubiri. Anamlea pekee baada ya mkewe kuaga kutokana na ajali ya barabarani.
Dini ndiyo inayopalilia penzi kati ya Luka na Lilia. Lilia anamwomba babake wamsaidie Luka kama dini inavyoelekeza. Babake anakubali kumpeleka shule na pia kumpa mamake kazi ya kusafisha kanisa.
Wanapojuana wakiwa watoto, Luka na Lilia ni marafiki wa kufa kuzikana. Wanapoingia ujanani, babake Lilia anahofia usalama wa bintiye na kujaribu kuwatenganisha kwa kumpeleka Luka upande mwingine wa nchi kwa mhubiri rafikiye. Bado wanawasiliana kwa simu na barua.
Mhubiri huyu anapotilia shaka mwelekeo wa uhusiano wa bintiye na Luka, bintiye anamkumbusha mahubiri yake mwenyewe kila mara kuwa Mungu ni upendo. Anamwambia kuwa hafai kumbagua Luka au kuona kama hamfai. Lee Imani analazimika kumuuliza Luka kuhusu nia yake kwa Lilia, naye anasisitiza kuwa ana nia safi kabisa. Licha ya mashaka aliyo nayo, hana lingine ila kuwapa Baraka zake.
Lilia anamshawishi babake kumpa Luka jukumu la kuhubiri kanisani, jukumu ambalo anatekeleza vilivyo. Anahubiri na baada ya muda, kanisa linafurika hadi mahema kuongezewa. Washirika wanampenda sana. Watu wanatoka nchi za mbali kufuatilia miujiza huku.
Lee anapofariki, Luka anageuza kanisa kuwa kitega uchumi. Anamwachisha mkewe kazi yake ya umeneja wa benki ili aje kutunza pesa za kanisa, japo kuna mhasibu anayefanya kazi vizuri. Baada ya muda, anauza kanisa lile na kuingilia siasa. Anasahau kabisa mambo ya dini na kubadilika kabisa. Anawatenga watu waliomchagua, anamtesa mkewe na kuwa mkware kupindukia. Mkewe naye anaishi kumwombea kwa imani kuwa atabadilika siku moja.
Migogoro
Mwanzo wa hadithi unadhihirisha mgogoro mkuu katika kisa hiki. Lilia yuko katika hali ya wasiwasi mkuu huku akimsubiri mumewe. Amezoea vitimbi vya mumewe anayemjia kwa makeke kila siku. Anapopita karibu na kioo akielekea kwenye chumba cha kulala, mabadiliko katika uso wake yanadhihirisha
migogoro ya awali kati yake na mumewe. Kwanza, kioo chenyewe kimepasuka. Ana kovu shavuni na donda linaloelekea kupona shavuni, zote kumbukumbu za mapigo ya awali.
Lilia anapokumbuka walivyokutana na Luka, tunapata taswira ya migogoro ya awali. Anapompenda Luka, anazua mgogoro kati yake na babake, ambaye hapendelei sana ukaribu kati yao. Anahofia usalama wa bintiye. Hata hivyo, Lilia anamsisitizia kwamba mapenzi ni moja kati ya amri za Mungu wala hafai kumbagua Luka au kumwona hafai.
Hisia za Lee Imani, babake Lilia, kumhusu Luka zinazua mgogoro kati yake na nafsi yake. Japo Luka anamhakikishia kuwa nia yake kwa bintiye ni safi, hisia fulani zinamfanya kumshuku. Hatimaye, kwa ajili ya furaha ya bintiye, analazimika kuwapa baraka zake.
Baada ya babake Lilia kufariki, ndipo migogoro inaanza kati yao. Luka anauza kanisa lao. Japo hakubaliani na hatua hii, Lilia ananyamaza ili kutunza ndoa yake. Mumewe anamwachisha kazi na kumtaka kubakia nyumbani, na hatimaye kumtawisha. Anapoingilia kampeni, anambembeleza aghairi nia lakini anakataa kabisa. Anamlazimisha Lilia kuandamana naye japo yeye hapendi masuala ya siasa. Wakati mmoja anaambulia vitisho anapokataa katakata kuandamana naye, huku akimkumbusha kuwa wanawake ni wengi.
Migogoro kati ya wawili hawa inazidi Luka anapotwaa ugavana. Anamtaka mkewe kukaa vijijini eti ili awe karibu na raia. Mumewe anafika huko wikendi wala hana wakati wake, anajiandalia masuala ya wiki inayofuata. Wakati mmoja anapomtembelea bila habari, anampata na mwanamke mwingine. Luka hajali chochote bali anamlaumu mkewe kwa kumtembelea bila taarifa. Anaporejea nyumbani jioni hiyo, anampiga vibaya mkewe na kumwonya dhidi ya kutoka nje ya nyumba.
Mafarakano yanazidi baada ya tukio hili. Luka anampiga mara kwa mara anapotangamana na majirani na marafiki. Lilia ashakuwa mtawa. Anapoamua kuripoti, anaambulia patupu baada ya kugundua mkuu wa polisi anayeenda kupigia ripoti anajuana na mumewe. Isitoshe, siku ya tatu baada ya kufika kituoni, anakosa simu ya mumewe akiwa bafuni, na hapo anajua kuwa yuko hatarini. Anangoja mumewe, ambaye anafika siku mbili baadaye.
Luka anamvamia mkewe tena na kumvuta nywele kumwelekeza kwenye chumba cha kulala, ambapo anampiga kwa ngumi, mateke na makofi. Anamvunja mkono na hatimaye anapoteza fahamu. Luka mwenyewe hajali bali anaondoka na kumwacha pale. Anahofia hata kuwaita majirani kumwauni kwa kumwogopa mumewe. Hatimaye, anaiona simu yake na kuamua kumpigia mama mkwe.
Simu ya Lilia kwa mkwewe inaibua mgogoro kati ya Luka na mamake hasa anapomjulisha ni Luka aliyetekeleza hayo. Mama mtu anashangazwa na ukatili wa Luka kwa mkewe licha ya fadhila alizotendewa na babake Lilia. Anampigia simu na kumwamrisha atume ambulansi, huku akimkumbusha kuwa akichelea, simu itakayofuata itaelekea polisi kisha kituo cha habari. Hana lingine ila kumtii mamake.
Mabadiliko
Lilia anapoelekea kwenye chumba cha kulala, anapita karibu na kioo na hapo kushuhudia mabadiliko yaliyokumba uso wake. Awali, ngozi yake ilikuwa laini bila alama yoyote na kila mara ilifanya vidu vya kupendeza alipotabasamu, tena tabasamu lenyewe halikukosa usoni mwake. Sasa hivi, uso huo umebadilika pakubwa. Ana kovu shavuni na donda linaloelekea kupona kipajini. Isitoshe, siku hizi anatabasamu kwa nadra sana.
Luka pia anakumbwa na mabadiliko. Anapokutana na Lilia mara ya kwanza, ni maskini, mchafu asiyeonekana kuwa na lolote la maana. Hata hivyo, Lee Imani anambadilisha anapomkaribisha kwake na kumpeleka shule. Anasahau umaskini na kuzidi kufana. Anaanza kufanya hata uhubiri, na hatimaye anaimarika hadi kiwango cha kuwa gavana.
Mabadiliko pia yanamkumba Luka katika sekta ya maadili. Anapomwoa Lilia, ni mhubiri na mcha Mungu mkubwa. Watu wanatoka pembe zote kufuatilia miujiza katika kanisa lake. Anawajaza wengi imani kutokana na mahubiri yake. Hata hivyo, babake Lilia anapoaga, anabadilika ghafla. Kwanza, anageuza kanisa lile kitega uchumi na kuliuza. Anawania ugavana na kuwa laghai, mzinzi na katili mkubwa asiyejali maslahi ya watu waliomchagua.
Lilia anaathiriwa zaidi na mabadiliko ya Luka. Wanapofunga pingu za maisha, maisha ni raha mstarehe kabla ya Luka kubadilika. Anamwachisha kazi na kubadili taaluma kutoka kuwa mhubiri na kujitoma katika siasa. Pia anabadilika na kuanza kumtesa mkewe. Anampiga mara kwa mara na kumwendea kinyume na vimada wengine. Anamtelekezea kijijini wala hamjali tena. Anamchukulia kama kiumbe asiye na sauti anayefaa kuendeshwa huku na huku.
Maudhui mengine katika hadithi hii ni pamoja na Elimu, Umaskini, Kazi, Utabaka, Familia na Malezi, Ulaghai, Ubabedume, Uwajibikaji, Uongozi, Kutowajibika, Uzinzi na Kifo/Mauti.
WAHUSIKA: Sifa na Umuhimu Lilia
Ni mwenye mapenzi ya dhati. Anapompenda Luka, anafanya kila jambo kuhakikisha amempata. Anamsisitizia babake kuwa Luka pia anastahili mapenzi. Hata anapomtesa, ananyenyekea kwake kwa imani kuwa atabadilika.
Ni mvumilivu. Mumewe anampiga kila mara na hata kumwumiza, lakini anajitia moyo huku akiomba kuwa atabadilika.
Ni mcha Mungu. Ana imani thabiti ya kidini. Anamweleza babake kuhusu amri ya Mungu ya mapenzi. Anakutana na Luka kanisani na anapokuwa mwovu, anamwombea kwa imani kuwa atabadilika.
Ni mpelelezi. Anapomweleza babake kuhusu Luka anapomwona kanisani, tunaambiwa kuwa macho yake mapelelezi hayakosi kuchunguza na ulimi wake kutangaza matokeo ya uchunguzi huo. Anafahamu kuwa mumewe ana vimada wa nje licha ya kuwa anatawishwa.
Ni mwoga. Anapomgoja mumewe, amejawa na hofu. Anaamka roho mkononi na pumzi zikimwenda mbio. Mumewe anapofika baada ya kukosa simu yake, anamfungulis huku akitetemeka kwa hofu kubwa.
Ni mpenda amani. Anafanya kila awezalo kuepuka ugomvi na mumewe. Ananyamaza anapouza kanisa. Anakatiza ukuruba na majirani kuepuka migogoro na kumwombea mumewe abadilike.
Ni msomi. Anatia bidii katika masomo yake na kufaulu katika viwango vyote hadi kufikia chuo kikuu.
Umuhimu wa Lilia
Ni kiwakilishi cha wanawake wanaokandamizwa katika jamii kwa misingi ya kijinsia. Anadhihirisha sura tofauti za migogoro katika jamii na jinsi inavyoathiri maisha.
Kupitia kwake, madhila yanayowapata wanawake katika ndoa yanadhihirika. Ni kiwakilishi cha imani na dini na nafasi yake katika jamii
Luka
Ni mwenye bidii. Anatia bidii katika kila afanyalo. Anapoanza kuhubiri, anachukua muda mfupi kupata umaarufu hata kumliko mhubiri mkuu. Licha ya kuzaliwa maskini, anatia bidii hadi kuwa gavana.
Ni laghai. Anajitia ucha Mungu bandia, kumbe ni mwovu kupuindukia. Anajiaminisha kwa babake Lilia. Anapokufa, anauza kanisa na kuanza kumtesa bintiye. Anajiaminisha kwa wapiga kura lakini anawapuuza wanapomchagua.
Ni mzinzi. Licha ya kuwa na mke, ana vimada wengine nje. Mkewe anapomtembelea ofisini, anampata na mwanamke mwingine ambaye ni kimada wake. Anaandamana na kimada wake katika shughuli zake huku watu wakitania kuwa ni msaidizi wake.
Ni msaliti. Anamsaliti mkewe Lilia kwa kumtesa licha ya poenzi lake la dhati. Anamsaliti babake Lilia kwa kuuza kanisa lake anapofariki na kumtesa bintiye. Anasaliti dini na nafsi kwa kubadilika kuwa mwovu.
Ni katili. Hana hata chembe cha utu. Anampiga mkewe mara kwa mara bila huruma. Anamwacha anapozirai wala hajali. Mamake anapomwamrisha kutuma ambulansi, anasita hadi anapomtishia kuripoti polisi na kumwanika kwenye kituo cha habari.
Ni mnafiki. Anajipendekeza kwa babake Lilia na kujitia wema. Anajinufaisha kwa kumwoa bintiye na kutajirika kupitia kanisa lake. Anawashawishi watu kumchagua kuwa gavana, lakini nia yake ni kujinufaisha.
Ni mwenye dharau. Anamdharau mkewe na kumdhalilisha. Anapomtembelea, anamfokea na kumwambia amwachie sekretari ujumbe. Anampiga jioni hiyo, huku akidai kuwa haheshimu wageni wake.
Ni msomi. Anakutana tena na Lilia katika chuo kikuu baada ya bidii zake katika masomo.
Umuhimu wa Luka
Ni kiwakilishi cha viongozi wanaowatelekeza wapiga kura baada ya kuwakweza mamlakani Kupitia kwake, ubabedume unadhihirika na madhara yake katika jamii.
Ni kiwakilishi cha wanafiki wa kidini wanaowafumba macho wengine na kuitumia kujinufaisha Kupitia kwake, mshahara wa watenda maovu unawasilishwa kwa msomaji
Lee Imani(Babake Lilia)
Ni mcha Mungu. Ni mhubiri mkuu katika kanisa. Anawalisha kondoo wa Mungu kwa neno vilivyo.
Ni mwenye mapenzi ya dhati. Anampenda mkewe kwa dhati. Tunaambiwa kuwa lau si uchangamfu wa bintiye, kumbukumbu za mkewe waliyependana kwa dhati zingemsukuma kaburini. Anashindwa kabisa kuoa tena. Pia anampenda bintiye kwa dhati.
Mwenye tahadhari. Anapogundua ukaribu kati ya Luka, anahofia madhara yake kwa bintiye na kumtuma Luka upande mwingine wa nchi kuwatenganisha. Anachelea kuwapa baraka zake kwa hisia za shauku dhidi ya Luka.
Ni mwenye utu. Anajitolea kumsaidia Luka kwa kila hali. Anamkaribisha nyumbani, kumlipia karo na hata kumpa mamake kazi.
Ni mkakamavu. Anaposhikilia lake, habadili msimamo. Anabaki pekee baada ya kifo cha mkewe. Rai za wahubiri wengine, waumini na marafiki zake hazibadili msimamo wake.
Ni mwajibikaji. Anatekeleza wajibu wake kila mara, kama mzazi na pia mhubiri. Anawalisha chakula cha roho waumini. Anamshauri bintiye na kumpa baraka zake anapoona mapenzi yake kwa Luka.
Ni mlezi mwema. Anamlea bintiye kwa staha chini ya misingi ya kidini. Anaondokea kuwa mwenye heshima na bidii na mke mwema kwa Luka.
Umuhimu wa Lee Imani
Anawasilisha nafasi ya mzazi katika malezi na maisha ya mwanawe kwa jumla Ni kiwakilishi cha imani na dini na nafasi yake katika kujenga jamii.
Anadhihirisha matatizo yanayowakumba wazazi wanaojukumika kulea wanao peke yao. Kupitia kwake, wema miongoni mwa wanajamii unadhihirika.
Mama Luka.
Ni mwenye bidii. Anajitolea kwa kila hali kumkimu mwanawe licha ya matatizo mengi. Hatimaye anapatiwa kazi na babake Lilia kunadhifisha mazingira ya kanisa, anayoitekeleza vilivyo.
Ni mwajibikaji. Anapopokea simu ya Lilia baada ya kupigwa na Luka, anawajibika kumshughulikia kwa kumpeleka hospitalini na kumtunza. Anamshughulikia Luka pia anapolazwa humo baada ya ajali.
Ni mwerevu. Anapompigia mwanawe simu, anasita kutuma ambulensi. Anamtishia kumripoti kwa polisi na kituo cha habari, jambo linalomlazimu kumtii mara moja.
Ni mwenye utu. Anaacha shughuli zake na kumwendea mkaza mwanawe. Anampeleka hospitalini kisha kumtunza kila mara hadi anapopata afueni.
Umuhimu wake
Anawakilisha majukumu na nafasi ya mzazi katika malezi na makuzi ya mwanawe. Ni kielelezo cha wakwe wanaojali maslahi ya wakaza wanao
Anadhihirisha nafasi na umuhimu wa fadhila katika jamii.
Mbinu za Uandishi Tashbihi
Atakuja tu, labda ghamidha itakuwa imezidi, imefura kama hamuri lililotiwa hamira. Sasa kucheka kwake kulikuwa nadra kama kupatwa kwa mwezi.
Swali likajitunga akilini mwake, na kama mwangwi, likawa linajirudia tena na tena. Shati lenyewe limekuwa mararu, limemganda kama kigaga.
Watoto waliokuwa na hamu kutoka nje wakawa watulivu kana kwamba viti vimekuwa sumaku. Wamefika nusu safari, bintiye katulia kama maji mtungini.
Sasa kazi kukilea kitoto chao, kibinti hiki kilichomlanda mamake kama shilingi kwa ya pili. Badala yake liliuchochea, kama moto kuvuvia.
Nia yangu nyeupe kama pamba.
Sasa mumewe anataka kujisiriba uchafu ule na kama mchezea tope, atarukiwa tu. Ona umbo lako sasa, kama nguruwe.
Kisha kofi likaandamwa na teke lililomlaza kochini kama zigo lililosukumwa likajiangukia ovyo. Ilikuwa kama kuchokoza nyuki.
Lilia alimfungulia mlango akitetemeka kama unyasi upepo uvumapo.
Tashihisi
Saa ukutani ilimwambia saa nane za usiku,
Fikra zimechoka, mwenyewe hajiwezi; nusura yake usingizi uliomsomba, ukampa utulivu, japo wa muda tu.
Kama si ulimi wa bintiye ambaye hatulii, kihoro kingemvamia labda hata kumvuta kuelekea kaburini. Lakini hawakujua ajali ya barabara ingeyafuta maisha ya mama mtu.
Nguo zilezile, usafi bado unampiga chenga. Lakini dhiki ziliwaandama.
Istiara
Isije ikawa mwenye nyumba kaja na yeye mpangaji akachelewa kumfungulia mlango. Mbona Luka akageuka kuwa mzigo wa moto, habebeki, habebeki kamwe?
Yamekolezwa ladha na sauti, asali kando.
Akatamani kufika nyumbani apumzike, kazi ya kuwalisha kondoo wa Mungu si kazi rahisi.
Lilia, malaika wake, hampi utulivu wa kuwazia sana kuhusu upweke wake. Naye wembe masomoni, akili zake sumaku, hunasa yote wafunzayo walimu. Kaloa, katota hili penzi la jogoo la mji.
Na ule ulimi wake uliodondoka asali, waumini wakampenda. Kwake siasa ni mchezo mchafu.
Lilia akatambua rangi halisi ya mumewe. Tamaa ndiyo ibada yake, Ulaghai sasa ndiyo ibada yake kubwa, mhubiri keshakuwa mhadaifu.
Ulimfanya mkeo ngoma kwa sababu ya hawara ambaye hakuthamini hata chembe.
Semi na Nahau
roho mkononi, pumzi zikimwenda mbio- yaani kwa wasiwasi tele. nyanyaso moto mmoja- yaani tele, zisizokoma.
hakuwa na budi- alilazimika, hakuwa na lingine yalikuwa yale yanayodaiwa kumtoa nyoka pangoni- yalivutia sana akawa hoi- akachoka sana.
kufunga pingu za maisha- kuoana. unampiga chenga- unamhepa
rafiki yake wa kufa kuzikana- rafiki mkubwa/wa dhati.
binti hasikii la mwadhini wala la mteka maji msikitini- hasikii lolote wala yeyote. kumvunja moyo- kumuumiza hisia.
wakafunga pingu za maisha- wakaoana. Lilia alipigwa na butwaa- alishangaa alipokataa katakata- alipokataa kabisa.
kumuunga mkono- kumsaidia kutimiza azma yake, kukubaliana naye. hajali habali- hajali hata kidogo, hajali chochote.
utajua kilichomtoa kanga manyoya shingoni- utaingia mashakani/utaumia. Akamkaribisha kwa mikono miwili- akamkaribisha vizuri, kwa ukuruba mzuri. amepata nafuu- hali yake imeimarika/ afya yake imeimarika
aage dunia- afariki, akufe.
Kisengerenyuma/Mbinu Rejeshi
Lilia anapopita karibu na kioo, anaona mabadiliko usoni mwake; kovu na donda linaloelekea kupona. Yanamkumbusha vita vya awali vya mumewe, na sura yake ya zamani.
Anakumbuka alipokutana na Luka kanisani, akampenda na kumsihi babake wamsaidie. Wakaenda shule pamoja hadi wakaoana na babake kuaga, huku akimwachia Luka usukani wa kanisa.
Anakumbuka mabadiliko ya Luka baada ya babake kuaga; kuuza kanisa na kuanza kumdhulumu. Akaingilia siasa licha ya kujaribu kumshawishi, na kutwaa ugavana, kisha akageuka katili.
Anakumbuka zaidi hatua yake ya kumripoti ilivyotibuka baada ya kugundua mkuu wa kituo ni rafiki ya mumewe, na wasiwasi uliompata akijua mumewe ataambiwa.
Lilia anapofika katika kituo cha polisi, mkuu wa kituo anamweleza kuwa alikuwa na mumewe Lilia siku iliyotangulia katika hoteli moja.
Mama Luka anapompeleka Lilia hospitali, anashangaa vipi Luka amesahau fadhila alizofanyiwa na babake Lilia.
Mamake Luka anamkumbusha alivyomgeuza mkewe ngoma kwa ajili ya kimada asiyemjali. Alimweleza kuwa alikuja siku ya kwanza kumwona, kisha siku ya pili akageuka na kuondoka aliposikia hawezi kutembea tena.
Maswali Balagha
Mbona ikawa hivi? Mbona Luka akageuka kuwa mzigo wa moto, habebeki, habebeki kamwe? Nitapata wapi mwandani kama mke wangu marehemu?
Afanye nini baba mtu?
Chuo kimoja, bahati gani hii?
Mume wako? Tena lipi haliwezi kusubiri hadi mwisho wa juma? Je, huyu mwenzangu kapiga simu naye?
Bwana gavana, uko hapa?
Gavana yupi huyu na mbona wako chumba kimoja?
Siku nne wamekuwa chumba kimoja na mumewe na hana habari?
Yu wapi yule kirukanjia wako? Wajua yuko wapi? … waona sasa? Atakutunza nani? Atakuuguza nani, maana kwako fadhila za punda ni mashuzi!
Taharuki.
Kisa kinapoanza, tunaachwa na maswali mengi. Tunashangaa ni nani haswa Lilia anayengoja na kwa nini anamwogopa kiasi hicho. Kumbukumbu zake zinatujibu baadaye.
Baada ya masimulizi kuhusu matukio ya awali katika maisha ya Lilia, ni wazi kwamba mumewe atamtesa akirejea. Tunabaki na hamu kubwa ya kujua tendo atakalofanya akirejea baada ya mkewe kukosa simu yake na kujaribu kumripoti polisi.
Lilia anapoamka na kupata mtu mwinine kalazwa kando yake, hajui ni nani. Tunabaki na hamu ya kujua ni nani hadi mama mkwe anapoeleza baadaye, ndipo tunafahamu ni Luka.
Mwisho wa hadithi pia unatuacha na maswali mengi. Hatujui maisha ya Luka yanachukua mkondo gani baada ya kupoteza uwezo wa kutembea, hatujui iwapo mkewe atamtunza, hatujui iwapo atabakia kuwa gavana. Hatujui kama mienendo yake itabadilika au atabakia katili alivyo.
Kinaya
Tunaambiwa kuwa Lilia ana tabia za kiutu uzima wala hana marafiki wa umri wake. Ni ajabu kwa kuwa aghalabu watu huwa na marafiki wa umri wao.
Babake Lilia anawatenganisha Luka na bintiye ili kukatiza urafiki wao. Badala yake, tendo hili linachochea zaidi urafiki huo.
Luka anamwachisha mkewe kazi kwa madai ya kumtaka kudhibiti pesa za kanisa. Kinaya ni kuwa bado yupo mhasibu wa kanisa anayefanya kazi nzuri.
Luka anamtaka mkewe kuandamana naye katika kampeni ili watu waone kiongozi anayethamini ndoa na familia. Ukweli ni kuwa hamthamini mkewe wala familia. Hata mkewe kupoteza mimba si hoja kwake.
Luka anampiga mkewe kwa kumtembelea bila habari akidai anamwaibisha na kuwafanya wapinzani wake kusema ameshindwa kudhibiti mkewe, sembuse kaunti nzima. Ukweli ni kuwa Luka anajiaibisha mwenyewe kwa vitendo vyake, na kaunti imemshinda kudhibiti.
Lilia anapomwuliza mumewe kuhusu mwanamke wanayeandamana, anapokea kichapo, huku Luka akimwonya kuwa akichezea ukarimu wake atajipata nje akiombaomba. Ukarimu wake si ukarimu.
Methali
Mvumilivu hula mbivu.
Usione wembamba wa reli ukashangaa garimoshi kupita pale. Mstakabali wa binadamu ni usiku wa giza
Yaliyopita si ndwele Umdhaniaye ndiye kumbe siye Kuro haisemi uongo
Lisemwalo lipo, kama halipo li njiani laja. Mwanzo wa ngoma ni lele
Fadhila za punda ni mashuzi Uliacha mbachao kwa msala upitao Taswira
Sura ya Lilia anapojitazama kiooni na ile ya awali; “kovu shavuni, donda linaloelekea kupona kipajini. Alikumbuka sura aliyozoea kuiona. Lile kovu shavuni halikuwepo, badala yake ngozi nyororo,
iliyojishobwekea na vidu kudhihiri kila alipocheka.”
Luka anapoingia kanisani mara ya kwanza. “Nywele zilikuwa matimutimu, uso umechora mistari
mieupe… Shati refu limemfika magotini, upande mmoja halikuchomekwa kiunoni. Shati lenyewe lilikuwa mararu, limemganda mwilini kama kigaga. Suruali fupi ambayo uzi umetokeza kiunoni, bila huo uzi
ingejidondokea.”
Kipigo cha kwanza cha Lilia; “Jioni ile alipofungua mlango…,alipokezwa kofi ambalo lilimfanya kuona vimulimuli. Kisha kofi likaandamwa na teke lililomlaza kochini…”
Taswira ya kipigo kinachomlaza hospitali; “Lilia alimfungulia mlango akitetemeka kama unyasi upepo uvumapo. Mara akashikwa nywele, karibu zing’oke. Kisha akabururwa hadi kwenye chumba cha malazi. Si kipigo hicho. Si makofi, si ngumi, si mateke, tena ya mtu aliyevaa buti.”
Tabaini
Si bughudha hizo, nyanyaso moto mmoja.
Si utamu wa maneno huo! Ni yale yanayodaiwa kumtoa nyoka pangoni.
Si wahubiri wenza, si wazee wa kanisa, si washiriki, waote walimtaka kuoa tena… Na si kichapo hicho alichochapwa.
Si makofi, si ngumi, si mateke, tena ya mtu aliyevaa buti.
Tanakali za Sauti Alitega sikio ndi! Chumba cheupe pe!
Lilia alikuwa amelala fofofo,
Sadfa
Anapoelekea kwenye chumba cha kulala, Lilia anasadifu kupita mkabala na kioo, na hapo anayaona mabadiliko ya sura yake.
Luka anapoingia kanisani, inasadifu kuwa nafasi iliyo wazi ni pale tu alipoketi Lilia, hivyo analazimika kuketi naye. Pia, mjo wake unasadifiana na funzo linaloendelea kuhusu kumpenda jirani, Lilia anauona mjo huo kama mtihani kutoka kwa Mungu kuhusu funzo hilo.
Luka anapowasilisha wimbo wake, inatokea sadfa kuwa mhubiri ndio anakuja kuwataarifu muda umekwisha, na hapo anaisikia sauti yake tamu.
Babake Lilia anafanya kila juhudi kuwatenganisha Lilia na Luka. Sadfa inawakutanisha tena wanapohudhuria chuo kikuu kimoja.
Inasadifu kuwa Lilia anapomtembelea Luka ofisini mwake bila taarifa, kimada wake pia amefika, hali inayozua mtafaruku kati yao.
Lilia anapofika kuripoti mumewe, anaitiwa mkuu wa polisi. Inasadifu kuwa mkuu huyo anajuana na mumewe, na hata walikuwa pamoja siku iliyotangulia.
Lilia anapogutuka baada ya kuzirai kutokana na kipigo cha mumewe, hajui amwite nani kwani mumewe anamkataza kuwa na urafiki na majirani. Kisadfa, anaiona simu yake chini ya kitanda na anapoibonyeza, nambari anayokutana nayo kwanza ni ya mama mkwe.
Lilia na mumewe wanakutana hospitalini kisadfa. Lilia akiuguza majeraha ya kupigwa naye, Luka anahusika kwenye ajali na kuletwa pale pale alipolazwa Lilia.
Majazi
Lilia. Anamlilia babake hadi anapokubali kumsaidia Luka. Analilia ndoa yake Luka anapobadilika na kuanza kumpiga. Anamlilia Mungu kwa maombi ambadilishe mumewe. Anapopigwa na kuzirai, anachukua simu na kumlilia mkwewe.
Imani. Jina la babake Lilia. Anawajaza watu imani katika dini kwa kuwa yeye ni mhubiri. Licha ya shauku yake kwa Luka, anamruhusu kumwoa Lilia akiwa na imani wataishi vyema. Anamsaidia Luka kupata elimu na hata kumpa mamake kazi.
Luka. Ni jina la mmojawapo wa waandishi wa Biblia na wahubiri wa injili ya Yesu. Kabla ya kuingiwa na uovu, Luka ni mhubiri mzuri mwenye waumini wengi na anayefahamika sana. Watu wanatoka pembe zote kuja kupokea miujiza kwake.
Mbinu nyingine ni kama vile Utohozi, Lakabu, Kejeli, Nidaa, Takriri, Dayolojia, Kuchanganya Ndimi, Chuku na Uzungumzi Nafsia.
2. Msiba wa Kujitakia- D. W. Lutomia Mtiririko wa hadithi
Wakazi wa Matopeni wako katika kipindi kigumu sana cha maisha, taabu zinawaandama kila uchao wala hawana wa kumlilia. Machoka ni mmoja kati ya Wasakatonge wanaoishi mtaa wa matopeni. Amefika nyumbani jioni akitoka katika shughuli za kutafuta kibarua ili kupata cha kutia tumboni lakini hajaambulia chochote. Anaona tofauti kubwa iliyopo kati ya wapiga kura na wale wanaopigiwa kura.
Hali yake inamkumbusha shairi alilowahi kusoma, la ‘Msiba wa Kujitakia’, ambao kamwe hauna kilio. Ndio hali waliyo nayo baada ya kuwachagua viongozi wasiojali maslahi yao. Anakumbuka wakati wa siasa kabla ya uchaguzi. Serikali inajinaki jinsi ilivyoleta maendeleo huku upinzani nao ukipuuzilia mbali hoja hizo. Wanatoa ahadi tele za kuboresha maisha ya wakazi wa mtaa huu.
Machoka anakumbuka kauli ya jirani yake, Zuhura kuwa wanafaa kumchagua mtu wa ukoo wao, awe anafaa au la, tendo ambalo hata Zuhura mwenyewe anajutia. Tofauti kati ya uteuzi wao wa viongozi
uliwafanya kuzua uadui, lakini sasa dhiki inawaleta pamoja. ‘Mtu wake’ aliyechagua Zuhura hawafai kitu. Bidhaa zinapanda bei na maisha kuwa magumu. Anagundua kosa lake.
Wakati wa uchaguzi, jimbo la Matopeni linageuzwa ngome ya watu fulani. Wananchi wanarauka mapema kwenda kupiga kura kwa matumaini kuwa viongozi hao wataboresha maisha yao. Hata hivyo, wanawatelekeza. Zuhura anakumbuka akimweleza Machoka walivyokosea kwa kumchagua kiongozi kwa
kuwa ni wa ukoo wao, au kutokana na vizawadi vidogo vidogo walivyopatiwa na visenti vya kununulia pombe. Hali inazidi kuwa ngumu kwa wakazi wa Matopeni. Udhalimu unazidi, huku mapato yao madogo yakimegwa na ushuru.
Fumo Matata ni mpinzani mkuu wa Sugu Junior. Anawakumbusha wapiga kura kukoma kupigia viongozi kura kwa kuwa ni wa ukoo wao kwani hali hiyo inawaathiri. Kauli yake haitiliwi maanani. Fumo mwenyewe anawania kiti hiki kwa mara ya tatu mfululizo.
Ni miaka arobaini na mitatu tangu jimbo la Matopeni likombolewe kutoka kwa walowezi kwa uongozi wa Sugu Senior, babake Sugu Junior. Zuzu Matata, babake Fumo Matata alipendelewa na wakoloni kuongoza lakini akakataa akiwataka kumwachilia kwanza Mzee Sugu Senior kutoka gerezani.
Alipoachiliwa, akawa na umaarufu kumshinda na kutwaa uongozi kwa shuruti za wazee wa jamii yake. Hali hii ikazua uhasama kati yao hadi Zuzu Matata alipofariki bila kuongoza jimbo hili. Mwanawe pia anazidi kupambana kutimiza ndoto hiyo. Ni familia hizi mbili tu zinazozozania uongozi wa Matopeni.
Fumo Matata anapigiwa upatu kushinda ila mambo yanabadilika. Matokeo yanapokuja, Sugu Junior ameshinda licha ya Fumo kuwa na wafuasi wengi na kupiga kampeni ya kupigiwa mfano. Yasemekana kuwa upigaji kura si hoja, kwani katika kuzihesabu, mambo huenda kombo na wananchi kulimbikiziwa viongozi wasiowataka.
Fumo Matata anapata ujumbe kutoka kwa mwandani wake, Kahindi Mlalama, akimpongeza kwa ‘ushindi’. Hata hivyo, anamwonya kuwa ushindi huo huenda usione jua, lakini siku zijazo uchaguzi
utakuwa huru na wa haki, bali si wa kulimbikiziwa viongozi madikteta na wakoloni mamboleo. Vipimo vya uongozi vitategemea sera na tajriba bali si ukoo, umaarufu au utajiri.
Kiwanjani Mamboleo, shughuli ya kumwapisha Sugu Junior inaandaliwa. Saa tatu asubuhi, watu washafika huku wanahabari wakinasa matukio yanayopeperushwa moja kwa moja. Wapo viongozi wa majimbo mengine, mawaziri, wabunge na viongozi tofauti serikalini. Sherehe bila shaka imegharimu mamilioni ya pesa za watoaushuru kama kina Machoka na Zuhura.
Yasemekana serikali ndiyo imegharamia nauli ya ndege ya viongozi wa majimbo mengine kutokana nao kutilia shaka ushindi wake. Sherehe kama hii iliandaliwa tena miaka arobaini na mitatu iliyopita baada ya Sugu Senior kuachiliwa huru.
Watu washaanza kufika. Sugu Junior ndiye anatarajiwa kufika wa mwisho baada ya wageni wengine. Zuhura ni mmoja wa wananchi waliofika kushuhudia. Uwanja umegawa pande mbili, kwa viongozi na kwa wananchi. Upande wa viongozi una hema, viti vizuri na soda na maji huku wananchi wakipigwa na miale mikali ya jua.
Muda unasonga, na kufikia saa sita, viongozi waalikwa hawajafika ila wachache tu. Hata viongozi wa majimbo jirani waliolipiwa nauli hawajafika. Watu wameanza kuchoka lakini mfawidhi anawatuliza. Hatimaye Sugu anafika chini ya ulinzi mkali. Anapigwa na butwaa kuona hali ilivyo. Jioni hiyo, mada kuu katika vyombo vya habari ni taarifa ya viongozi kususia sherehe za kuapishwa kwa Sugu Junior.
Ufaafu wa anwani ‘Msiba wa Kujitakia’
Msiba ni tukio linalosababisha huzuni tele na kilio kingi kwa wahusika. Msiba wa kujitakia ni sehemu ya methali inayosema kuwa ‘Msiba wa kujitakia hauna kilio’. Mada hii basi inarejelea matatizo yanayomkumba mtu kutokana na matendo yake mwenyewe.
Machoka anapitia hali ngumu kimaisha. Ametoka kutafuta kibarua lakini hajaambulia chochote, hata cha kutia tumboni. Wakazi wengine wa jimbo hili pia wanapitia hali ngumu kama hiyo. Hali yao ni Msiba wa Kujitakia, kwa kuwa wanfanya uchaguzi bila kuzingatia vigezo vinavyofaa kupata kiongozi anayefaa.
Machoka anakumbuka shairi la Malenga Mteule alilowahi kusoma mahali fulani. Shairi hili linahusu msiba wa kujitakia. Kibwagizo chake ni ‘Msiba wa kujitakiya, kweli hauna kiliyo’. Linaoana na hali ilivyo katika jimbo la Matopeni. Linaongelea visanga vilivyojaa nchini watu wakifilisika. Mtunzi anamwomba Rabana awafungue macho ili waweze kuona.
Kauli ya Zuhura ni ithibati kuwa hali yao ni msiba wa kujitakia. Anamwambia Machoka kuwa wanafaa kumchagua kiongozi wa ukoo wao hata kama hafai kwa kuwa ni mtu wao. Sasa hivi, Zuhura anajutia uamuzi wake huo kutokana na dhiki inayomkumba.
Ugomvi kati ya Zuhura na Machoka ni msiba wa kujitakia. Wanatofautiana kwa kuwa wana misimamo tofauti katika uchaguzi wa viongoiz. Ajabu ni kuwa baada ya uchaguzi, dhiki inawaleta pamoja kwani viongozi wenyewe hawawajibiki kwa vyovyote vile.
Wakazi wa Matopeni wanaruhusu jimbo lao kugeuzwa ngome ya watu fulani wanaowania uongozi. Wanarauka asubuhi na mapema na kustahimili jua la mchana ili kuwapigia kura viongozi, ambao baadaye wanawapuuza na kutojali matatatizo yao. Zuhura anakiri kuwa walikosea kwa kumchagua kiongozi kwa kuwa aliwanunulia vijizawadi vidogo vidogo. Anasema kuwa yanayowakumba ni zao la kumchagua kiongozi kutumia matumbo badala ya akili. Wao ni msiba wa kujitakia.
Fumo Matata anawakumbusha wakazi wa Matopeni kuwa si busara kuwachagua viongozi kwa kuzingatia koo, kwani hali hiyo inaendeleza uongozi mbaya. Hata hivyo, wanampuuza na kumteua Sugu Junior kuwa kiongozi. Wanazidi kutaabika kutokana na mapuuza yao hata baada ya kuonywa.
Zuzu Matata kukosa uongozi wa Matopeni ni msiba wa kujitakia. Anapendekezwa na walowezi kutwaa uongozi lakini anasisitiza kuwa lazima Sugu Senior kwanza aachiliwe kutoka gerezani. Anapoachiliwa, anakuwa maarufu kumliko na kutwaa uongozi. Anakosa fursa nyingine ya kutwaa uongozi huo na kubakia kuwa mpinzani wake hadi kifo chake.
Wananchi wanakubali kukandamizwa. Wanatengewa upande wa kiwanja wanapoadhibiwa na jua huku viongozi wakitengewa upande wenye hema na kuongezewa vinywaji na ulinzi. Wanakubali kukaa siku nzima wakimsubiri kiongozi wao huku wakiumizwa na jua hilo.
Sugu anakosa washirika katika hafla ya kuapishwa, licha ya kuwalipia nauli ya ndege viongozi wa majimbo jirani. Huu ni msiba wa kujitakia, kwani hatilii maanani maslahi ya wananchi. Anataka kuwatumbuiza viongozi kutoka nje kwa fedha za walipa ushuru. Hali hii pia inatokana na ushindi wake anaopata kupitia mlango wa nyuma.
Dhamira ya Mwandishi
Kuwaonya wapiga kura dhidi ya kuwachagua viongozi kwa kutegemea misingi ya kikabila na zawadi wanazowapa na badala yake kutumia vigezo muhimu kama uwajibikaji na kujali maslahi yao.
Anadhamiria kuwatoa matongo wananchi wanaozozana kwa sababu ya misimamo yao tofauti kuhusu viongozi kwani mwisho wa siku ndio wanaobaki katika taabu, na hatimaye dhiki yao itawaleta pamoja tena.
Kuwakanya viongozi wanaotwaa uongozi kupitia mlango wa nyuma na kuendeleza ukoloni mamboleo na udikteta kwamba siku yao ya kulipia maovu hayo itafika.
Kudhihirisha hali halisi inayowakumba Waafrika na binadamu kwa jumla kutokana na maamuzi yao wenyewe.
Anasawiri utofauti uliopo katika jamii nyingi kutokana na toafuti za kiuchumi kati ya watu.
Maudhui Utabaka
Jamii ya jimbo la Matopeni imegawanywa katika makundi mawili makuu kwa kutegemea hali ya kiuchumi. Kuna wenye hadhi na kina yakhe kwa kutegemea hadhi yao katika jamii. Wananchi ambao ndio wapiga kura na watozwa ushuru wako katika kundi la chini linalohangaikia maisha kila uchao.
Maisha kati ya makundi haya mawili tunaambiwa kuwa yametengana kama mbingu na ardhi. Baada ya ahadi za uongo, viongozi wanatwaa nyadhifa zao na kujiendea kuishi kwa fahari.
Zuhura na Machoka wanalazimika kurejelea uhusiano wao mzuri baada ya uchaguzi. Tunaambiwa kuwa dhiki ndiyo inayorejesha uhusiano wao ambao unavurugwa awali na misimamo yao inayokinzana kuhusiana na viongozi wanaopendelea. Wanagundua kuwa wako katika kundi moja kijamii, kundi la wasakatonge wala viongozi wanaopigania hata hawayajali maslahi yao.
Utabaka pia unadhihirika katika safu ya uongozi. Inavyooonekana, ni kana kwamba kuna wale waliozaliwa kuongoza huku wengine wakiwa wafuasi. Katika jimbo la Matopeni, Sugu Junior na Fumo Matata ndio wanaozozania nafasi ya kuongoza. Nafasi hizi wanaridhi kutoka kwa wazazi wao. Sugu Senior, babake Sugu Junior ndiye alikuwa kiongozi wa matopeni baada ya walowezi kuondoka, hali Zuzu Matata, babake Fumo Matata akiwa mpinzani wake. Yashangaza kuwa ni familia hizo mbili tu zinazozozania uongozi hadi sasa.
Hali ya utabaka pia inaonekana katika mkutano wa kumwapisha Sugu Junior. Kiwanja kimegawanywa mara mbili. Kuna upande uliotengewa wenye ulwa katika jamii kama mawaziri, viongozi wa serikali na viongozi wa majimbo jirani. Upande huu umewekwa hema la kuwazuia jua, kuna vinywaji na walinzi pia. Upande wa pili ni ule wa raia wa kawaida. Huko, jua linawateketeza inavyofaa. Isitoshe, wanalazimika kufika mapema kusubiri kiongozi wao, ambaye anafaa kuwasili mwisho wa wote. Anapofika, yuko na walinzi wanaoimarisha usalama wake, tena anafika saa sita.
Usaliti
Jimbo la Matopeni linadhihirisha usaliti wa viongozi waliochaguliwa kwa matumaini ya kuboresha maisha ya wananchi. Wakati wa kupiga kampeni, wanatoa ahadi si haba ambazo wanaahidi kutimiza pindi tu wakiingia mamlakani. Wanaaahidi kuimarisha sekta ya afya, kutengeneza barabara, kuimarisha ukulima, elimu na kuwapa kina mama mikopo ya kuanzisha biashara pamoja na ajira kwa vijana. Hata hivyo, wanasahau ahadi hizi zote wanapoingia mamlakani na kuwatelekeza wananchi waliowachagua.
Zuhura na Machoka wanasaliti demokrasia, jimbo lao na kujisaliti wenyewe wanapochagua viongozi wasiofaa. Zuhura anamwambia Machoka kuwa wanafaa kumchagua mtu wao, awe anafaa au la.
Wanazozana kutokana na misimamo yao inayotofautiana kuhusiana na viongozi wanaotaka. Ajabu ni kuwa viongozi hao hawawafaidi kwa lolote. Zuhura anakiri kwamba walikosea kwa kuwachagua viongozi kwa misingi ya kikabila na pia kwa kuwaziba macho kwa vijizawadi vidogovidogo. Hatimaye wanabaki katika dhiki na kurejesha ujirani wao.
Wahesabu kura pia wanasaliti demokrasia na wapiga kura kwa kuwalimbikiza viongozi wasiotaka. Tunaambiwa kuwa pale Matopeni kupiga kura na kutopiga ni mamoja kwani uamuzi wa mwananchi hauheshimiwi. Tunaambiwa kuwa zoezi la kuhesabu kura ndilo muhimu, na kuwa hata wafu hutoka maziarani wakapiga kura na kurejea huko huko. Ina maana kuwa uamuzi wa wananchi unapuuziliwa mbali na kupatiwa viongozi wasiowafaa.
Viongozi wa majimbo jirani wanamsaliti Sugu Junior kwa kususia sherehe yake ya kuapishwa, licha yake kugharamia nauli zao za ndege. Sugu anawasili saa sita, kwani ndiye anatarajiwa kufika wa mwisho kulingana na itifaki. Anashangaa kuwa ukumbi wa viongozi ukona watu wachache tu, licha ya kuwa amewalipia nauli ya ndege. Nauli ambayo anawalipia kufuta shauku yao kuwa alipata uongozi kupitia mlango wa nyuma. Nauli ya pesa za wananchi, wapiga kura, watozwa ushuru.
Ukabila na Unasaba
Wakati wa kampeni, Zuhura anamwambia Machoka kuwa wanastahili kumchagua mtu wao, awe mzuri au mbaya, awe amesoma au la. Hoja yake ni kuwa wanastahili kuchagua mtu kwa kuwa anatoka kabila lao tu. Mfumo uu unawaletea matatizo mengi kwani huyo mtu wao hajali maslahi yao hata kidogo.
Anatarajia kuwa serikali ya mtu wao itawafaa lakini wapi, wanabakia katika lindi la umaskini bado. Zuhura anakiri makosa yake ya kumchagua kiongozi kwa kuwa ni wa kabila lao. Bado matatizo yanawazidi. Mahitaji yanazidi kuwakaba huku mapato yao yakimegwa na ushuru unaopanda kila uchao.
Katika mahojiano na Radio Salama iliyopo Matopeni, kiongozi wa upinzani Fumo Matata anawakanya wanannchi dhidi ya mfumo wa kupiga kura kwa kuegemea kwenye misingi ya kijinsia. Anawaeleza kuwa mfumo huo umepitwa na wakati na bado wataendelea kutaabika chini ya uongozi wa mtu huyo licha ya kuwa wa jamii yao. Fumo anawaona kama miti ambayo inakubali kuangamizwa na shoka huku ikidhani na mwenzao kwa kuwa mpini wake umetokana nao. Wananchi wanapuuzilia mbali usemi wake na kuendeleza mtindo huo wa uchaguzi, hali ambayo inawaletea matatizo mengi. Wanazidi kutaabika.
Ni wazi kwamba suala la ukabila lilianza pindi tu baada ya kuondoka kwa walowezi wala si jambo geni. Tunaambiwa kuwa baada ya walowezi kuondoka, Zuzu Matata anaazimia kuchukua uongozi na kupendekezwa na walowezi. Hata hivyo, anasisitiza kwamba Mzee Sugu Junior aachiliwa kutoka jela alikofungwa. Anapoachiliwa, anapata umaarufu kumliko. Tunaambiwa kuwa Sugu alitwaa uongozi kwa shuruti za wazee wa kabila lake.
Hali ya unasaba pia inadhihirika katika uongozi wa jimbo la Matopeni. Mzee Sugu Senior anatwaa uongozi huku Zuzu Matata akiwa mpinzani wake. Baada yao kufariki, wanao wanachukua nafasi zao katika taifa. Sugu Junior, mwanawe Sugu Senior, anatwaa uongozi huku Fumo Matata, mwanawe Zuzu Matata akiwa mpinzani wake wa karibu. Inastaajabisha kuwa ni familia mbili tu ambazo zinazozania uongozi wa Matopeni, ni kana kwamba ndizo zilizaliwa kuongoza na hakuna familia nyingine inayoweza kuchukua uongozi huo.
Ukoloni
Kuna sura mbili za ukoloni katika hadithi; Ukoloni Mkongwe na Ukoloni Mamboleo. Tunasimuliwa kuwa wakati fulani huko nyuma, jimbo la Matopeni lilikuwa limetawaliwa na walowezi, lakini hatimaye wakatimuliwa. Walikuwa wamemweka kizuizini kiongozi Mzee Sugu Senior lakini Zuzu Matata akampigania hadi kuachiliwa, kisha akachukua uongozi baada ya kuachiliwa kutoka seli. Hatimaye jimbo la Matopeni likawa huru.
Hata hivyo, bado ukoloni unaendelezwa na waliotwaa uongozi kutoka kwa walowezi. Viongozi wa Matopeni hawajali maslahi ya wanyonge wanaowachagua. Wanapania kujinufaisha tu. Wanajitenga nao na kujiboreshea maisha huku wapiga kura wakizidi kutaabika. Wanawatoza ushuru ambao wanatumia vibaya kama vile kulipia nauli ya viongozi majirani kuja katika sherehe za kuapishwa kwa Sugu Junior.
Ukoloni Mamboleo pia unaonekana kupitia shughuli ya uchaguzi wa viongozi. Wananchi wanaruhusiwa kupiga kura lakini kura zao hizo hazitiliwi maanani, licha yao kuvumilia jua kali kuteua chaguo lao.
Inasikitisha kuwa baada ya hayo yote, bado kura zao hazitiliwi maanani bali wanalimbikiziwa viongozi wasiowataka. Shughuli ya kupiga kura haitiliwi maanani bali mchakato unaofuata wa kuhesabu kura hukumbwa na tafrani na hatimaye viongozi wasioshinda kuteuliwa, badala ya uteuzi wa wapiga kura kuheshimiwa.
Hali sawa pia inadhihirika katika sherehe za kumwapisha kiongozi Sugu Junior kiwanjani Mamboleo. Viongozi wanastahiwa na kupatiwa hadhi ya juu, kinyume na usawa uliopiganiwa wakati wa kuwafukuza wakoloni. Viongozi wamewekewa hema la kuwasitiri jua na pia kupatiwa vinywaji pamoja na ulinzi wa kipekee, kinyume na wananchi wanaotelekezwa juani. Isitoshe, Sugu Junior anawasili baadaye baada ya wananchi kumngoja kwa kitambo huku wakiunguzwa na jua.
Migogoro
Kuna hali ya mgogoro kati ya viongozi na raia kutokana na hali mbaya ya maisha inayowakumba wananchi. Tunaambiwa kuwa mzigo wa maisha ambao Wanamatopeni walikuwa wamebebeshwa walikuwa tayari kuutua. Wanawachagua viongozi ambao wanawatelekeza na kutojali maslahi yao. Wako tayari kupigania haki zao.
Zuhura na Machoka pia wanajipata katika mgogoro. Zuhura anapendekeza kuwa wanafaa kumchagua kiongozi kwa kuwa anatoka katika kabila lao, lakini Machoka ana msimamo wake. Mgogoro huu unaisha baada ya uchaguzi pale viongozi wao wanapowatelekeza na dhiki yao kuwaleta pamoja.
Kuna mgogoro kati ya Sugu Junior na Fumo Matata, wawaniaji wakuu wa uongozi katika jimbo la Matopeni. Fumo amekuwa mpinzani wa Sugu, na sasa anawania uongozi kwa mara ya tatu mfulululizo. Serikali inasifia maendeleo iliyoleta lakini upinzani unaona hizo kuwa porojo tupu.
Mgogoro kati ya vinara hawa wawili tunagundua kuwa ulianza kwa wazazi wao, waanzilishi wa jimbo hili. Zuzu Matata, babake Fumo Matata alikuwa mpinzani sugu wa Mzee Sugu Senior, babake Sugu Junior, alipotwaa uongozi baada ya kuondoka kwa walowezi.
Umaskini
Hali ya umaskini inadhihirika katika makazi ya Machoka, akiwa tu kama mfano wa umma mkubwa wa wakazi wa Matopeni. Ametoka katika shughuli za kutafuta kibarua lakini hajafanikiwa. Tumbo
28
linamwuma kwa njaa kwani hajala tangu asubuhi. Inasemekana kuwa taswira ya chumba chake ingeweza kumliza kipofu.
Zuhura ni mfano mwingine wa hali hii. Yeye pia anahisi ugumu wa maisha baada ya viongozi kutotimiza ahadi walizotoa wakati wakampeni. Ushuru nao uko juu na unawakandamiza. Dhiki inarejesha uhusiani mzuri kati yake na Machoka uliovurugwa na misimamo yao tofauti wakati wa uchaguzi.
Maudhui mengine ni kama vile Ufisadi, Kutowajibika, Udhalimu na Uongozi Mbaya.
Wahusika: Sifa na Umuhimu Machoka
Ni mwenye bidii. Anarauka asubuhi na mapema kwenda kusaka kibarua ili kukidhi mahitaji yake. Hakati tamaa hadi jioni anapokosa kabisa.
Ni mkakamavu. Anaposhikilia lake, habanduki. Ana msimamo wake katika uchaguzi wala kauli ya Zuhura haibadilishi msimamo wake. Anahiari kukosana naye badala ya kufuata ushawishi wake.
Ni mzalendo. Siku ya kupiga kura, anaungana na Wanamatopeni wengine kwenda kupiga kura kwa nia ya kumteua kiongozi wao.
Ni mwenye kumbumkumbu. Anapokinai hali yake, anakumbuka shairi alilowahi kusoma kuhusiana na msiba wa kujitakia lililoandikwa na mshairi mwenye lakabu ya Malenga Mteule.
Umuhimu wa Machoka
Ni kiwakilishi cha mateso wanayopitia raia chini ya utawala mbaya
Ni kielelezo cha bidii na kujituma katika shughuli licha ya matatizo ya maisha. Anadhihirisha mgawanyiko uliopokatika jamii kwa misingi ya kiuchumi na mamlaka. Zuhura
Ni mzalendo. Siku ya kupiga kura, anrauka bukrata na wenzake kwenda kupanga foleni na kusubiri hadi zamu yao kupiga kura ili kumteua kiongozi wao.
Ni mshawishi. Anamsisitizia Machoka kuwa wanafaa kumchagua kiongozi kutoka kabila lao. Anapokataa wanazozana.
Ni mkabila. Ananuia kuteua kiongozi kutoka kabila lake. Hajali iwapo kiongozi huyo ni mzuri au mbaya, amesoma au la.
Ni mvumilivu. Ni mmoja wa wale wanaosubiri ujio wa Sugu Junior katika sherehe za kuapishwa kwake. Anaunguzwa na jua na kusubiri, hata hina mikononi na wanja machoni unaanza kuyeyuka lakini anangoja hadi kiongozi anapofika.
Ni mkakamavu. Anapofanya uamuzi hatetereki. Anakata kauli kumteua kiongozi kutoka katika kabila lake. Anangoja hadi kiongozi anapofika katika sherehe za kuapishwa kwa Sugu Junior.
Umuhimu wa Zuhura.
Anadhihirisha jinsi raia wanavyochangia katika matatizo yanayowakumba kwa kuwachagua wasiofaa. Ni kiwakilishi cha ukabila na mchano wake katika kuiangusha jamii.
Kupitia kwake, mgawanyiko wa kijamii kwa misingi ya kiuchumi unadhihirika. Ni kiwakilishi cha matatizo wanayopitia raia wa kawaida katika nchi.
Sugu Junior
Ni fisadi. Anawaacha wananchi waliompa wadhifa kutaabika wala hajali maslahi yao. Anatwaa uongozi kwa njia za kifisadi kwani siye chaguo la wananchi
Ni mbadhirifu. Anatumia visivyo hela za jimbo la Matopeni. Anawalipia nauli viongozi wa majimbo jirani kuja katika sherehe za kuapishwa kwake, sherehe ambazo hata hawaji.
Ni mwenye tamaa. Ana tamaa ya uongozi. Anatumia kila njia kuhakikisha kuwa ametwaa uongozi japo siye chaguo la wananchi.
Ni mnafiki. Wakati wa kampeni, anajinasibisha na watu na hata kuwa karibu nao ili kupata kura zao. Anapopata mamlaka, anajitenga nao kama mbingu na ardhi.
Umuhimu wa Sugu
Ni kiwakilishi cha viongozi wasiojali maslahi ya umma uliowachagua.
Kupitia kwake, hali ya mvutano katika uongozi inadhihirika na jinsi hali hiyo inavyoathiri maendeleo Ni kiwakilishi cha unafiki wa viongozi wengi katika jamii
Ni kiwakilishi cha ukoloni mamboleo katika jamii ya sasa.
Fumo Matata
Ni mkakamavu. Anapoamua kuwania uongozi, harudi nyuma licha ya kufeli. Anafeli mara mbili lakini bado yuko debeni kwa mara ya tatu.
Ni mwenye bidii. Anazunguka kote Matopeni akiimarisha kampeni zake na kutwaa wafuasi wengi.
Ni mwenye maono. Watu wanapendezwa sana na mipango yake aliyoweka ya kuwaboreshea maisha na wako tayari kumchagua kwa ajili hiyo.
Umahimu wa Fumo
Ni kiwakilishi cha viongozi wanaojaribu kwa kila hali kupigania maslahi ya wananchi wanaoteseka. Kupitia kwake, hali ya ukoloni mamboleo inadhihirika ilivyokita mizizi katika jamii
Anadhihirisha mizozo iliyopo ya uongozi na athari yake katika jamii.
Ni kiwakilishi cha imani na tumaini la usawa wa kijamii katika siku zijazo.
Mbinu za Uandishi. Tashbihi
Maisha kati ya makundi haya mawili, yaani mpiga kura na mpigiwa kura, yametengana kama mbingu na ardhi.
Anasimama pale kama kigingi
Zuhura na Machoka walikuwa kama fahali wawili-hawakai katika zizi moja.
Maisha ya Wanamatopeni yalikuwa kama mchezo wa karata, hawajui leo wala kesho.
Wanamatopeni walipotathmini hali zao, walijifananisha na panya walionaswa kwenye mtego wa uhitaji. Fumo aliona hali ya Matopeni kama kisa cha msitu na shoka.
Wakishapata walichokitaka, walijitenga na umma kama wagonjwa wa ukoma.
Semi
zimegonga mwamba- zimekosa kufanikiwa kukodoa macho- kufungua macho yote
ndoto iliyozikwa katika kaburi la sahau- iliyosahaulika vinywa wazi- wameachama, kwa mshangao
kula halafa- kuapa/kuapishwa wakipiga doria- wakiimarisha ulinzi Methali
Punda akichoka, mzigo huutua. Lisilobudi hubidi
Wajinga ndio waliwao
Mzigo wa mwenzio ni kanda la usufi Ukistaajabu ya Musa, hujayaona ya Firauni Subira huvuta heri.
Majazi
Machoka-mhusika huyu amechoshwa na maisha ya umaskini. Ametoka kutafuta kibarua mchana kutwa huku amechoka. Yuko tayari kutua mzigo aliotwishwa, ambao umemchosha.
Zuhura- ni sayari ya pili kutoka kwenye jua. Anajiona kuwa karibu na jua(uongozi), eti kwa sababu kiongozi anatoka kabila lake. Yuko kwenye mstari wa mbele kupiga kura na pia katika sherehe za kuapishwa kwa Sugu Junior.
Matopeni-ni jimbo la watu wanaong’ang’ania maisha yao. Kumejaa tope la umaskini, ujinga, unyanyaswaji na ukabila, miongoni mwa mengine.
Sugu Senior. Sugu ina maana ya ‘siyoweza kubadilika kwa urahisi’, au ‘siyosikia dawa’. Mzee Sugu anatwaa uongozi na kuushikilia bila kutetereshwa na upinzani wa Zuzu Matata. Senior ni kuwa ndiye mkubwa kati ya Sugu wawili kwenye hadithi.
Sugu Junior. Mwanawe Sugu senior anayeendeleza ubabe wa babake dhidi ya mpinzani wake, Fumo Matata.
Zuzu Matata. Zuzu ina maana ya mjinga. Anapigania Sugu Senior kutolewa seli, na anapotolewa, anamnyang’ama uongozi. Hili linamletea matatizo mengi(Matata) hadi anapokufa bila kuonja ladha ya uongozi.
Fumo Matata. Ni mwanawe Zuzu Matata. Fumo ni aina ya mkuki unaotiwa kwenye upande mmoja wa mpini, au kiongozi wa kijadi. Ni mkuki wa Matopeni wa kuboresha maisha lakini hapati fursa hiyo. Pia ni kiongozi kwa kuwa anachaguliwa na raia lakini anapokwa nafasi yake.
Mamboleo. Ni uwanja anaofaa kuapishwa Sugu Junior. Hii ni shughuli ya kileo. Pia, viongozi wanafanya mambo kileo wanaposusia sherehe hizo. Wamechoshwa na wizi wa kura.
Kinaya
Wakati wa kampeni, serikali inajigamba ilivyoleta maendeleo. Ukweli ni kuwa haijaleta maendeleo yoyote.
Zuhura anamwambia Machoka kuwa wanafaa kumchagua mtu wao, awe mzuri au mbaya. Ajabu ni kuwa wao ndio wanateseka chini ya uongozi huo.
Zuzu Matata anampigania Mzee Sugu Senior kutolewa seli. Kinaya ni kuwa anapotoka, anapata umaarufu kumshinda na kutwaa uongozi. Wanaishia kuwa wapinzani badala ya kushirikiana.
Tunaambiwa kuwa pale Matopeni kupiga kura na kutopiga ni mamoja kwani uamuzi wa mpiga kura hauheshimiwi. Sasa kuna haja gani ya zoezi hilo basi? Shughuli muhimu ya kidemokrasia inageuzwa kuwa mzaha.
Uwanjani Mamboleo, sehemu ya viongozi imeimarishwa kwa hema, viti, vinywaji na ulinzi. Wananchi wanatelekezwa kwenye jua, hali ndio watoa ushuru.
Viongozi wa majimbo jirani wanasusia sherehe za kuapishwa kwa Sugu Junior hata baada yake kugharamia nauli yao ya ndege.
Kisengerenyuma/Mbinu Rejeshi
Machoka anapokinai matatizo ya maisha, anakumbuka shairi alilowahi kusoma la Malenga Mteule.
Machoka pia anakumbuka mambo yalivyokuwa wakati wa kampeni. Anakumbuka ahadi ambazo walipatiwa, jinsi serikali ilivyojisifia kuleta maendeleo huku upinzani ukikejeli kauli hiyo.
Anakumbuka pia kauli ya jirani yake Zuhura kuwa wanafaa kumchagua mtu wao, awe mzuri au mbaya, amesoma au la. Anakumbuka hali ya suitafahamu kati yake na Zuhura huyo kutokana na misimamo yao hiyo, hali iliyoyeyushwa na dhiki baada ya uchaguzi.
Tunarejeshwa kwa historia ya Matopeni baada ya kutwaa uhuru, huku Mzee Sugui Senior akiingia mamlakani baada ya kupiganiwa na Zuzu Matata kutolewa seli, upinzani wao katika safu ya uongozi hadi kufariki kwa Zuzu Matata bila kuonja ladha ya uongozi.
Takriri
Anawaza juu ya maisha yake. Maisha ya wasakatonge. Maisha ya wanaojiita ‘pangu pakavu’. Maisha ya wapiga kura. Maisha ambayo ni tofauti sana na maisha ya waliowapigia kura. Maisha kati ya makundi haya mawili…
“Wetu ni wetu, hata akiwa mbaya ni wetu… Awe amesoma au hajasoma, angali wetu.” Leo hii amebaki kujuta. Kujuta ghaya ya kujuta!
Tayari alikuwa amekwishafanya kosa. Kosa ambalo lilikuwa la kujitakia.
Hivyo ndivyo ari yake Zuzu Matata ya kuiongoza Matopeni ilivyogeuka kuwa ndoto. Ndoto inayosemekana ilizua uhasama mkubwa kati ya viongozi hawa wawili. Ndoto iliyomfanya Zuzu Matata kuwa mpinzani… Ndoto anayozidi kuiota akiwa mle kaburini. Ndoto iliyozikwa katika kaburi la sahau.
Ila kesho…kesho…kesho yote haya yatakuwa marehemu…
Zuhura amechukua nafasi yake kwenye sehemu ya pili…, sehemu ambapo jua kali lilipenyeza miale…,
sehemu ya wapiga kura… “Subira…subira…subira…ndugu zangu.” Tashihisi
Machoka anabaki kukodoa macho huku maonevu yakiihukumu nafsi yake. Kongole kwa ‘ushindi’ wako, ingawa ushindi huo huenda usione jua!
Ukumbini, viti vinamkodolea macho.
Hadithi ndani ya Hadithi
Tunasimuliwa kisa cha msitu na shoka. Miti katika msitu iliangamizwa na makali ya shoka huku ikifurahia eti kwa kuwa mpini wa shoka ulitokana na mmoja wao. Ilidhani shoka ni mwenzao. Kisa hiki kinafananishwa na Wanamatopeni wanaomchagua kiongozi kwa misingi ya kikabila ila anawadhulumu wakidhani ni mmoja wao.
Chuku
Taswira ya chumba chake ingeweza kumliza kipofu.
Hata hina aliyokuwa amejiremba Zuhura mikononi na wanja aliokuwa amejipaka imekwishaanza kudondoka kwa makali ya jua.
Ulinzi mkali ambao ungemzuia hata nzi kupita karibu naye!
Kejeli
Mzigo wa maisha haukuwatisha wala kuwakosesha usingizi viongozi wao Ndoto anayozidi kuiota akiwa mle kaburini!
Pale Matopeni, siku hizi hata wafu hupiga kura na kurejea maziarani!
Sherehe hii bila shaka imeigharimu serikali mabilioni ya pesa. Pesa za walipaushuru, kina yakhe kama Machoka na Zuhura.
Zuhura amechukua nafasi yake kwenye sehemu ya pili, palipoandaliwa kwa ajili ya watu kama yeye, sehemu ambapo jua kali lilipenyeza miale yake ya ghadhabu, sehemu ya wapiga kura, watozwa ushuru!
Koja
Tunaahidi kutengeneza barabara, kuimarisha sekta ya afya, kuinua kina mama wetu kwa kuwapa mikopo ya kuanzisha biashara…
…kaka, ndoto haifi ila vizingiti haviishi daima; kulimbikiziwa viongozi, udikteta, ukoloni mamboleo…
Mizani ya ubora wa kiongozi haitakuwa kabila lako, ukoo wako, familia yako, nani unayemjua, una hela ngapi…
Mbinu nyingine ni pamoja na Ushairi, Tabaini, Mdokezo, Maswali Balagha, Nidaa, Kuchanganya Ndimi, Tanakali, Lakabu na Ujumbe wa Simu.
Mapambazuko ya Machweo- Clara Momanyi Mtiririko.
Mzee Makucha na Mzee Makutwa ni marafiki, ambao wamestaafu na umri wao umesonga. Hata hivyo, urafiki wao uliokolea awali sasa umepungua, umebaki tu ule wa kujuliana hali. Mzee Makutwa anaonekana akizurura mtaani na gari lake baada ya kustaafu, wala hakuna ajuaye shughuli zake, hata Mzee Makucha. Anaonekana tu kila mara akiwabeba vijana garini, wala haijulikani anawapeleka wapi. Mkewe Makucha, Bi Macheo anamsaili mumewe kuhusiana na hili lakini hapati taarifa yoyote. Makutwa anajinaki kuwa hawezi kuishi maisha ya kutaabika hata kama amestaafu. Bi. Macheo anamshauri mumewe akomeshe urafiki na Mzee Makutwa, lakini mumewe anamweleza kuwa urafiki uliobaki kati yao ni wa salamu tu.
Mzee Makucha anauza vitafunio kwenye makutano ya barabara baada ya kustaafu kutoka kazi yake alipopigwa kalamu. Anafanya kazi na shirika la reli lakini linasambaratika baada yake kuachishwa kazi, hivyo juhudi zake kwenda mahakamani ni bure. Akiwa kazini kwake(kuuza vitafunio), anashangazwa na kazi anayofanya Makutwa, ambaye anatangamana na vijana kila uchao wala hana hata muda wa kuwasabahi wazee wenzake.
Mzee Makutwa anafika katika kazi ya Mzee Makucha na kutapakaza vumbi kwenye vitafunio vyake kwa gari lake akilipiga breki. Anamkejeli Makucha, akimwambia kuwa anafaa kujipumzisha nyumbani na kazi hiyo kuachia vijana. Lakini Makucha anamsisitizia kuwa yuko sawa nayo, kuliko yeye anayezurura mitaani na vijana. Anamdhihaki kuhusu bintiye aliyetoroshwa na Mhindi, huku akimkumbusha afurahie maisha licha ya matatizo. Mashaka ya Makucha kuhusu kazi afanyayo Makutwa yanazidi.
Vijana wawili, Dai na Sai wananunua kashata kwa Makucha na kuelezana kuhusu taabu za maisha baada ya kufuzu na kukosa kazi. Wanaamua kujaribu bahati yao na gari la probox linalozunguka likikusanya vijana. Makucha anajua bila shaka ni gari la Makutwa. Gari linapofika wanalipungia mkono na kuingia.
Linaendeshwa na kijana sasa hivi, sio Makutwa.
Makucha anamwita mkewe kuchukua vitu vyake na kuchukua teksi kulifuata gari lile. Wanasafiri hadi wanapoingia kwenye mgodi wa kisiri uliofichwa katika mazingira makavu. Anaingia kwenye mgodi na kushuhudia jinsi vijana wanavyodhalilishwa humo kwa kazi ya kutafuta madini. Anarudi tena na kuwadanganya walinzi kuwa anamtaka Mzee Makutwa, ambaye huku anaitwa Mzee Mamboleo.
Anawaaga akidai atamfuatilia nyumbani.
Anarudi mjini Kazakamba na kuripoti polisi, ambao wanaandamana naye hadi kwenye lile pango. Wanamkuta Mzee Makutwa akikagua mgodi. Anatokomea pangoni na kupotelea humo, hadi polisi wanapomrushia vitoza machozi. Anatoka akikohoa na kufungwa. Anamlaumu Mzee Makucha kwa kumwendea kinyume, lakini naye anamwambia haki ndio muhimu. Hatimaye anatupwa korokoroni kwa kosa la jinai.
Mzee Makucha anapokea zawadi ya hundi ya pesa kutoka kwa tajiri mmoja anayeendeleza miradi ya maendeleo kwa vijana. Anayaona haya kama mapambazuko mapya, licha ya maisha yake kuwa katika machweo.
Ufaafu wa anwani ‘Mapambazuko ya Machweo’.
Mapambazuko ni wakati wa asubuhi inapoingia na jua kuchomoza. Machweo nao ni wakati wa jua kutua na giza kuingia. Mada hii inaweza kufasiriwa kuwili; mapambazuko yanayotokea wakati wa machweo, au mapumbazuko yaliyo katika machweo. Dhana hizi, mapambazuko na machweo pia zimetumiwa kwa maana nyingine. Mapambazuko yanawakilisha wakati wa ujana, huku machweo yakiwakilisha uzee. Pia, mapambazuko yanaashiria mwangaza(fanaka) huku machweo yakiashiria giza(taabu/mashaka).
Makutwa anawashangaza wengi kwa kuwa anashinda na vijana kila wakati licha ya kuwa ni mzee. Hashirikiani na wazee wenzake hata kidogo. Anaonekana kama ujana wake umeingia akiwa mzee, yaani mapambazuko yake yanamjia akiwa katika machweo.
Mzee Makucha anafanya biashara ya kuuza vitafunio. Japo Mzee Makutwa anamkejeli, yeye anaiona kuwa ndio tumaini lake baada ya kufutwa kazi kwenye shirika la reli. Machweo yanaingia kwa kuachishwa kazi, na anaiona biashara hii kuwa mapambazuko yake.
Binti yake Makucha, Riziki, anaolewa na kigogo Mhindi baada ya kushindwa kuvumilia dhiki. Kutokana na machweo ya umaskini, anaonelea ndoa hiyo kama mapambazuko kwake.
Mzee Makucha anamweleza Mzee Makutwa kuwa siku moja, jua la macheo(Mapambazuko) litambishia mlango japo anaelekea machweo. Yaani, ipo siku atafanikiwa licha ya uzee wake.
Sai na Dai wanaeleza taabu ya maisha yao. Ni miongoni mwa vijana waliohitimu kutoka chuo kikuu na kukosa kazi. Wanazurura tu mitaani. Wako karibu kukata tamaa. Machweo yameanza kuwaingilia katika maisha hali bado wako wakati wa mapambazuko. Wanaona shughuli za probox ya Makutwa kama nafuu ya pekee, yaani mapambazuko ya kuwatoa katika machweo waliyomo.
Mzee Makucha anapofuata gari la Makutwa kwa teksi, linawaongoza hadi kwenye mgodi mkubwa, ambapo vijana na watoto wadogo wanafanya kazi ya kusaka vito vya thamani. Wanapata taabu nyingi, na wengi wao wanakosa hata fursa ya masomo. Machweo yameshaingia katika maisha yao hali wako katika mapambazuko.
Mzee Makutwa amewatesa vijana wengi kwa kuwaingiza katika machweo ya kumfanyia kazi ya kinyama ya kusaka vito. Hawana imani ya maisha bora. Kukamatwa kwake na polisi ni mapambazuko ya machweo, kwani uovu wake unafikia kikomo.
Mzee Makucha anapata zawadi ya hundi kutoka kwa tajiri mmoja anayeendeleza miradi ya kuwainua vijana kimaendeleo. Amekuwa akiishi kwa taabu kwa kuuza vitafunio kando ya barabara. Haya ni mapambazuko(mafanikio) ambayo yanamwangukia katika machweo ya maisha yake(uzee na taabu).
Dhamira ya Mwandishi
Kuelimisha kuhusiana na nafasi ya vijana katika kujenga na kuendeleza jamii
Anawasilisha hali ya maisha na pandashuka zinazohusika, pamoja na juhudi za waja kujikimu. Anadhihirisha namna biashara haramu zinavyoathiri jamii vibaya.
Anawasilisha mgogoro wa kiumri kati ya vijana na wazee unavyoathiri jamii. Anatoa tumaini kwa wanajamii wenye bidii kuwa siku moja mafanikio yao yatafika. Anaonya watenda maovu kuwa siku yao ya kunaswa itafika.
Maudhui Migogoro
Mzee Makucha na Mzee Makutwa wako katika mgogoro baada ya kustaafu. Makucha anafanya kazi ya kuuza vitafunio kando ya barabara hali Makutwa hajulikani kazi anayofanya. Anaonekana tu akizurura huku na huko na gari lake. Anaiona kazi ya Makucha kama ya kujiumbua lakini Makucha anaiona kuwa asili ya riziki yake. Anapopita na kumrushia vumbi, Makucha hafurahii tendo hili. Isitoshe, anamdhihaki Makucha kuhusiana na kazi yake na pia sababu ya bintiye Riziki aliyeolewa na Mhindi.
Bi. Macheo pia anajipata katika mgogoro na mumewe kuhusiana na Makutwa. Hapendi jinsi Makutwa anavyomfanyia stihizai mumewe, na kila mara anamtaka kukomesha urafiki kati yao. Hata hivyo, Makucha haoni neon lolote katika salamu wala haoni haja ya kutozipokea.
Mgogoro kati Makutwa na Makucha unaimarika Makucha anapojua kazi ambayo Makutwa hufanya ya kuwatumikisha vijana katika mgodi kutafuta vito. Anaamua kumwitia polisi ambao wanaenda kwenye mgodi huo na kumkamata Makutwa. Makutwa anamlaumu kwa tendo hili huku akimwita rafiki wa uongo, lakini Makucha anamwambia kuwa hawawezi kuwa marafiki na amtazame akihujumu taifa kwa kufyonza nguvu za vijana kiharamu.
Makutwa pia yuko katika mgogoro na sheria. Anaendesha biashara ya kimagendo ya kuwatumikisha vijana kutafuta vito katika mgodi wake. Hatimaye, polisi wanapata habari kutoka kwa Makucha na kumwahi katika mgodi huo. Hatimaye anafungwa jela kwa makosa ya jinai.
Nafasi ya Vijana Katika Jamii.
Vijana wamepatiwa nafasi changamano katika hadithi hii. Makucha anawachukulia vijana kuwa watumwa. Anawabeba na kuwapeleka katika mgodi wake kumfanyia kazi ya kutafuta vito vya thamani. Vijana hawa wanakosa nafasi ya kujiendeleza kielimu na kuyafurahia maisha yao pamoja na kutumikia jamii. Isitoshe, wanakumbwa na hali ngumu ya kimaisha, kwani huko wanakoishi hakuna hali nzuri.
Hewa si safi na kazi wafanyazo ni za sulubu.
Sai na Dai pia wanawakilisha hali ya vijana wengi katika jamii. Baada ya kuhitimu kutoka chuo kikuu, hawajapata kazi wala hawana matuamini. Wanashinda kuzurura mitaani. Dhiki inapowafika shingoni, wanaamua kujaribu bahati kwa Makutwa, bila kujua wanaelekea kujiuza kwa utumwa. Hata hivyo, Makucha anawaopoa kabla hawajazama huko.
Makucha anaamini kuwa vijana ndio raslimali kuu ya jamii. Baada ya kuwaokoa vijana wale kutoka mikononi mwa Makutwa, anawaonea imani. Anafahamu kuwa wengi wao wanafaa kuwa katika shule wakiandama elimu na hata wengine katika vyuo vikuu. Isitoshe, anapokea zawadi ya hundi ya pesa kutoka kwa tajiri mmoja ambaye anaendeleza miradi ya kimaendeleo kwa vijana. Bila shaka, anaelewa fika kuwa vijana wana jukumu kubwa katika jamii.
Kazi
Mjini Kazakamba, kila mmoja anajikaza vilivyo kujitafutia riziki kupitia kazi hii au nyingine. Mzee Makucha kila asubuhi anarauka kuuza bidhaa zake kwenye makutano ya njia akiwa na uhakika wa kunasa wateja wengi iwezekanavyo. Dhihaka za Mzee Makutwa hazibadilishi mtindo wake wa kujitafutia riziki. Mkewe naye anachuuza kaimati na vitumbua kwenye veranda ya nyumba yao.
Kabla ya kuanza kuchuuza vitafunio hivi, Mzee Makucha anafanya kazi na shirika la reli ambalo linamtimua kwa ajili ya kupunguza idadi ya wafanyakazi wake. Baadaye linasambaratika, hivyo anakosa marupurupu yake.
Makutwa naye anafanya kazi kama waziri hadi anapostaafu. Kazi hii inampa majivuno na anapostaafu, anadharau kazi ya Makucha ya kuuza vitafunio. Anajigamba na kazi yake anayofanya ambayo haieleweki, kwani anaonekana kila siku akiwabeba vijana huku na huko, wala hakuna ajuaye wanaenda wapi.
Baadaye tunafahamu kuwa ni kazi haramu ya kuwatumikisha kwenye mgodi.
Sai na Dai wanawakilisha vijana wengi wanaopata elimu hadi vyuo vikuu lakini wanakosa kazi. Vijana hawa wanaishia kuwa wakizurura mitaani na hatimaye kupata kazi za kidhuluma kama ile ya Mzee Makutwa ya mgodi.
Polisi wanafanya kazi yao ya kulinda sheria barabara. Wanapopashwa habari na Mzee Makucha kuhusiana na nyendo za Mzee Makutwa, wanaandamana naye hadi kwenye mgodi na kumkamata. Hatimaye, anafikishwa mahakamani na kuhukumiwa kwa kosa la jinai.
Umaskini
Mzee Makucha anaanguka kwenye lindi la umaskini baada ya kuachishwa kazi katika shirika la reli bila marupurupu, kwani shirika hilo linasambaratika pia. Analazimika kuchuuza vitafunio kando ya barabara kujipatia riziki. Mkewe naye anauza kaimati na vitumbua kwenye veranda ya nyumba yao.
Umaskini unawazidi kiasi kwamba binti yao wa pekee, Riziki, anawatoroka na kuolewa na Mhindi ili kuepuka urumo. Hata hivyo, umaskini huo unaondoka baada ya kitendo cha kishujaa cha Makucha kinachowaletea hundi ya pesa kutoka kwa tajiri mmoja anayethamini tendo lake.
Vijana maskini wanajipata taabani mikononi mwa Mzee Makutwa. Anawasomba kwenda kuwafanyisha kazi ya kusaka vito vya thamani katika mgodi wake. Wanafanya kazi hii katika mazingira mabovu na kufungiwa mle ndani, wasiwe na nafasi ya kutokea.
Uzalendo
Makucha anadhihirisha umuhimu wa uzalendo kupitia tendo lake la kuokoa vijana wanaotumikishwa na Mzee Makutwa. Anapojua shughuli anazoendesha, anawaendea polisi mara moja kuja kumkamata.
Anawaokoa vijana hao, anaowaona kama amali ya jamii.
Uzalendo wake unathaminiwa na tajiri mmoja anayeendesha miradi ya kuwainua vijana kimaendeleo. Anamtuza hundi ya pesa kutokana na ushujaa wake. Tajiri huyu pia anadhihirisha uzalendo kupitia miradi yake ya kujenga taifa, hasa vijana.
Makutwa, kwa upande mwingine, amekosa kabisa uzalendo. Analipoka taifa nguzo yake muhimu kwa kuwachukua vijana mabarobaro na kwenda kuwatumikisha katika mgodi wake. Vijana hawa wanafaa kuwa wakiendesha shughuli nyingine muhimu za kujenga jamii.
Ukoloni Mamboleo
Ukoloni huu unaendelezwa na Mzee Makutwa baada ya kustaafu uwaziri. Makutwa anaonekana akizurura huku na huko na gari lake huku akiwabeba vijana kutoka mitaani wala hakuna anayejua shughuli ambazo anaendeleza wala anakoelekea, hadi Makucha anapofuata gari lake kwa teksi likiendeshwa na kijana mwingine. Anafika kwenye mgodi wa Makutwa wanakofanya kazi vijana hawa.
Wanateremka bonde ambalo limejificha kabisa, hata miale ya jua haionekani. Wanaingi a kwenye tambarare kubwa lenye vuduta vya mchanga ambapo vijana kadhaa, ikiwemo watoto wadogo
wanafanya kazi. Wanadondoa vijiwe vidogovidogo vinavyong’aa. Wanasimamiwa na wanyapara wanaowaamrisha kwa sauti za kutisha.
Makucha anapoingia ndani ya pango, anapata taa za vibatari za kuzuia giza lililomo. Vijana wanachimba madongo ya mchanga na kuyatia ndani ya mikokoteni. Wamelowa jasho kutokana na upungufu wa hewa ndani ya mgodi huo.
Usiku, wanalala katika mabanda yaliyojengwa kigugu. Wanaoingia humo hawaruhusiwi kutoka. Makazi hayo yamezungushiwa ua wa stima na pia yana mabawabu katili na majibwa makubwa ya kuwazuia
vijana wale kutoroka. Makutwa ni kiwakilishi halisi cha ‘mkoloni mweusi’.
Maudhui mengine ni kama vile Ndoa, Utabaka, Udhalimu, Malezi, Uwajibikaji, Mabadiliko na
Mazingira.
Wahusika: Sifa na Umuhimu. Mzee Makucha
Ni mwenye bidii. Baada ya kufutwa kazi, anarauka kila asubuhi kuuza vitafunio kando ya barabara kuhakikisha kuwa amepata riziki.
Ni mpelelezi. Anashangaa kazi anayofanya mwenzake na kuamua kumpeleleza. Anasikiliza kwa makini mazungumzo kati ya Dai na Sai wanapotaja gari la Makutwa. Wanapoingia, anapanda teksi na kuwafuata hadi anapofahamu kazi anayoendeleza Makutwa ya kuwatumikisha vijana kwenye mgodi.
Ni mzalendo. Anapojua biashara anayoendeleza Makutwa ya kuwadhulumu vijana, anaamua kuwaita polisi kumkamata na kuwaokoa vijana wale ili waweze kuhudumia taifa.
Ni mjanja. Anafaulu kuingia katika pango la mgodi licha ya kuwa na walinzi wanaomzuia. Tunaambiwa kuwa anawachenga na kuingia ndani ya pango.
Ni mwerevu. Anapowapata walinzi wakiwahangaisha vijana wa teksi aliokuja nao kwa maswali, anawaambia kuwa alikuwa akimtafuta Mzee Makucha na kwa kuwa hajamwona, ataondoka tu. Hili linawazuia kujua mikakati yake ya kuwaita polisi.
Mwenye hamaki. Mkewe anapomzungumzia kuhusu Makutwa, anamjibu kwa hasira kuwa ataishia kuwa kidhabu. Matendo na maneno ya Makutwa anapofika anapouzia na gari yake yanamuudhi, hasa maneno kuhusu binti yake Riziki.
Umuhimu wa Makucha
Ni kielezo cha umuhimu wa uzalendo na utetezi wa haki katika jamii.
Ni kielelezo cha bidii na tumaini katika jamii na jinsi vinavyoweza kuleta mafanikio. Ni kiwakilishi cha dhiki zinazowakumba wananchi wa kima cha chini kiuchumi.
Kupitia kwake, umuhimu wa ndoa na mchango wake katika kujenga jamii vinadhihirika. Anadhihirisha aina za migogoro inayopatikana katika jamii.
Makutwa
Ni mwenye dharau. Anamsemesha Makucha kwa dharau licha ya kuwa anajidai kuwa rafiki yake. Anamkejeli kuhusiana na kazi yake duni ya kuchuuza vitafunio na bintiye mtoro.
Ni mnafiki. Anajitia urafiki na Makucha lakini hawezi kumfaa. Makucha anasema kuwa hajawahi kumfaa akiwa waziri, licha yake kumtaka Makucha amsafirishie shehena bila kulipa.
Ni dhalimu. Anawakusanya vijana na kuwapeleka katika mgodi wake kufanya kazi katika mazingira duni. Aidha, hawaruhusiwi kuondoka pale. Wamefungiwa kwa ua wa stima na kuwekewa walinzi wenye mbwa wakali.
Ni katili. Anapiga gari lake breki na kutapakaza vumbi kwenye vitafunio anavyouza Makucha bila haya. Hana imani kamwe na vijana anaowatumikisha.
Ni jasiri. Polisi wanapomjia, anawakimbia na kuingia kwenye mgodi. Anakataa kabisa kusalimu amri hadi pale wanapomtoa ndani kwa kumrushia vitoza machozi.
Ni mkakamavu. Baada ya kustaafu kama waziri, anaamua hawezi kuishi maisha ya kimaskini katu. Anaamua kufanya kazi ya mgodi na kuwatumikisha vijana ili kukimu hali yake ya kiuchumi.
Ni mwenye majivuno. Anajishaua mbele ya Makucha kuwa yuko kazini na gari lake na kuipuuza kazi yake ya kuuza vitafunio kando ya barabara.
Umuhimu wa Makutwa
Ni kiwakilishi cha marafiki wanafiki ambao wanalenga tu kujifaidi kutokana na marafiki zao bila wao kuwafanyia lolote la haja.
Kupitia kwake, matendo ya kihuni katika jamii yanadhihirika kupita kazi yake ya mgodi
Anadhihirisha jinsi wenye nafasi ya hali hutumia hali ya umaskini miongoni wa vijana kuwakandamiza.
Bi. Macheo
Ni mdadisi. Anamzungusha mumewe kichwa kwa maswali. Anamsaili kuhusu rafikiye Makutwa anakopeleka watoto anaowapakia kwenye gari, kwa nini aendeleze urafiki wake naye na kwa nini amkaribishe kwake.
Ni mwenye makini. Anashuhudia kila tukio baina ya mumewe na Mzee Makutwa. Anamwona akipakia vijana kwenye gari lake asijue aendako. Pia, anagundua jinsi Makutwa anavyomdhihaki mumewe.
Ni mshauri. Anampendekezea mumewe kukomesha uhusiano wake na Makutwa kutokana na shughuli zake zisizoeleweka na pia kwa jinsi anavyomkosea heshima.
Ni mwenye bidii. Anamsaidia mumewe pakubwa katika kuzumbua riziki. Anauza kaimati na vitumbua kwenye veranda ya nyumba yao.
Umuhimu Wake
Ni kiwakilishi cha wanawake wenye bidii na wanaowasaidia waume zao katika shughuli za kuzumbua riziki.
Kupitia kwake, umuhimu wa ndoa katika jamii unabainika na nafasi yake kwa wahusika kujengana. Anawakilisha changamoto za maisha kwa jumla na jinsi ya kuzikabili.
Anawakilisha nafasi na majukumu ya mwanamke katika ndoa na jamii kwa jumla.
Mbinu za Uandishi Semi
kujitanua kifua- kujigamba
unayepakwa mafuta kwa mgongo wa chupa- unayehadaiwa/unayedanganywa wasio na mbele wala nyuma- wasio na lolote la maana, wasio na thamani alipigwa kalamu- alifutwa kazi
kumpa kisogo- kumwacha, kumtenga kuponda raha- kujivinjari, kujifarahisha
iliwapiga chenga- iliwazidi maarifa, iliwakwepa kujiendea shambiro- kujiendea huku na huku ovyoovyo alitega sikio- alisikiza kwa makini
hoi bin taabani- katika hali mbaya
akiwa na moyo mzito- akiwa na hisia nyingi
Istiara
Sinema hiyo ya kikatili ilijibainisha mbele yao… “Maajabu ya Firauni ndiyo haya!...”
Aliyedhani ni rafikiye kumbe alikuwa mbwamwitu aliyevaa ngozi ya kondoo. Ndani ya pango, mbio za paka na panya zilishamiri
Kinaya
Mzee Makutwa anasemekana kuwa anashinda tu kujumuika na vijana, hata wazee wenzake hana muda wa kubarizi au kuongea nao.
Makutwa anaposimamisha gari kwenye biashara ya Makucha, anamwambia kuwa hakukusudia kumwudhi. Tendo la kutapakaza vumbi kwenye bidhaa zake na kejeli kuhusu bintiye ni wazi kwamba ananuia kumwudhi.
Makutwa anamwambia kuwa atawarejesha vijana wale katika kazi hiyo katika uwepo wa askari. Tayari ana makosa na anaongezea mengine.
Makutwa anamwambia Makucha kuwa alidhani ni rafiki wa dhati. Ni kinaya kwa kuwa Makutwa mwenyewe si rafiki wa dhati hata kidogo. Hakumsaidia akiwa waziri na kila mara humkejeli.
Sadfa
Shirika la reli analofanyia kazi Mzee Makucha linamfuta kazi. Wakati akitafuta haki, shirika lenyewe linasambaratika. Anakosa hata marupurupu yake.
Mzee Makucha anawazia nyendo za Mzee Makutwa za kuwabeba vijana katika gari lake kila mara. Wakati huo huo, anashtukia Makutwa mwenyewe amepiga breki mbele yake.
Mzee Makucha anapowazia kazi aliyofanya Makutwa, Sai na Dai wanakuja na kununua kashata kisha kuanza kuzilia hapo. Wanaanza kuzungumzia gari la Makutwa, na kumtia Makucha shaka zaidi.
Huku vijana hawa wawili wakiendelea kuwasiliana, gari la Makutwa wanalozungumzia linawasili. Kisadfa, mara hii si Makutwa analiendesha bali kijana machachari. Inakuwa rahisi kwa Makucha kuliandama.
Inasadifu kuwa Mzee Makucha anapofika kwenye mgodi wa Makutwa, mwenyewe hayupo. Anaweza kufahamu jinsi anavyotesa vijana, na kuwa anatumia jina bandia la Mamboleo.
Mzee Makucha anapowachukua polisi na kwenda nao mgodini, inasadifu kuwa Mzee Makutwa amerudi, na hivyo wanafaulu kumkamata.
Methali
Ujana ni moshi
Jambo usilolijua ni usiku wa giza. Mwomba Mungu hachoki Tashbihi
Machungu yaliyompata ni sawa na yale ya kupigiliwa msumari wa moto kwenye kidonda kibichi. Matarajio yake ya kuwa na maisha mema yakaporomoka kama jabali la barafu juani.
Hawa walikuwa wakidondoa vijiwe vidogovidogo vyenye kung’aa ungedhani walikuwa wakitenga ndume kwenye mchele.
Usiku walilala kwenye mabanda yaliyojengwa kigugu mfano wa mazizi ya ng’ombe. Alisimama mahali alipokuwa kama sanamu.
Mzee huyo…baada ya kufungwa kama mbuzi anayepelekwa kichinjioni.
Majazi
Makutwa. Ina maana mbili, mchana mzima(kutwa) au kupatikana. Mzee Makutwa anazurura na gari lake mchana kutwa kwa shughuli ambazo hazieleweki. Pia, anakutwa katika uhalifu wake na kutiwa ndani.
Makucha. Ina maana mbili pia, usiku mzima au kupambazuka(kucha), na pia kucha kubwa. Kila kuchapo, yuko mbioni kunogesha biashara yake. Pia ana ‘Makucha’, yaani uwezo mkubwa wa kupata atakacho.
Makucha yake yanadhihirika kupitia bidii zake. Anatafuta haki anapofutwa kazi na pia kumnasa Makutwa.
Macheo. Ina maana ya wakati wa jua kuchomoza, ishara ya matumaini. Ni ‘macheo’ katika maisha ya mumewe. Anamsaidia kuzumbua riziki na kumshauri panapohitajika.
Riziki. Ni bintiye Makucha anayetoroka kuolewa na Mhindi. Neon hili lina maana ya uwezo wa kujikimu au baraka kutoka kwa Mungu. Anaamua kusaka riziki yake kupitia kuolewa na Mhindi na pia anapata baraka za mume.
Kazakamba. Mji wanakoishi kina Makucha. Kila mtu huku amekaza kamba, yaani kujitolea, ili kuboresha maisha. Kuna wanaochuuza bidhaa na wanaofanya uhuni.
Sai na Dai. Sai ina maana ya kuudhi au kuwa mshindani. Dai nalo lina maana ya kutoa maoni au kupendekeza jambo. Sai anajibu maswali ya Dai kwa ushindani huku naye Dai akimtolea pendekezo la kupanda kwenye gari la Makutwa.
Tashihisi
Maneno ya mkewe yalimtwanga kichwa Mzee Makucha.
Ujana ulikwisha kumpa kisogo lakini alikuwa akiukimbiza. Alikuwa akiufukuza na kujaribu kuukamata. Magari hayo yalianza kuteremka kwenye bonde kubwa ambalo lilificha kabisa miale ya jua.
Jazanda
Shirika la reli alilohudumia tangu macheo ya maisha yake. Tayari alikuwa katika magharibi ya maisha yake
Huu sio wakati wa kujenga kichunguu bali wa kustarehe ndani ya kichunguu. Heri wewe unayestaladhi katika machweo ambayo sasa ni mapambazuko kwako.
Ukiumwa na nyuki, hauna haja ya kujitwika jukumu la kuharibu mizinga yote ya asali. Hujui faida ya nyuki ulimwenguni? Uliamua kurina asali ya nchi.
Magharibi ikamkuta akigaragara kwenye sakafu baridi huku akisubiri kufunguliwa mashtaka. Mkono wa sheria nao ukamsukuma kuyakabili machweo ya maisha yake kifungoni.
Ingawa nimefikia magharibi ya maisha yangu, sudi hii imenipa tumaini la mapambazuko mapya maishani. Nahisi kwamba jua la asubuhi limeniangazia miale ya matumaini mapya, hata kama machweo yako karibu!
Dayolojia
Mazungumzo kati ya Makucha na mkewe kuhusiana na urafiki wake na Makutwa.
Mazungumzo kati ya Makutwa na Makucha katika biashara ya Makucha kuhusiana na hali zao na kazi zao.
Mazungumzo kati ya Sai na Dai kuhusiana na maisha na jinsi ya kuishi baada ya kuhitimu wanapokuja kununua kashata kwa Makucha.
Mazungumzo kati ya Makutwa na Makucha kwenye mgodi baada ya Makutwa kukamatwa na polisi.
Uzungumzi Nafsia/Monolojia
Kwa nini niendelee kumstahi mtu asiye na fadhila kama yule? Aliwaza.
“Kazi? Kazi gani hii ya kubebana na vijana mchana kutwa? Maajabu haya!”
Gari aina ya probox? Mzee Makucha aliwaza. Hilo silo la Mzee Makutwa? Ndiye pekee Aliya na gari la aina hiyo hapa mjini. Kwani kipi kinaendelea?
Mzee Makucha…aliendelea kujismemea, Utumwa mamboleo ndio huu. Ubedui uliogubikwa ndani ya ukawaida wa kisasa ndio huu.
Balagha
“Sasa mtu akija kwako kukujulia hali umfukuze? … Je, alinisaidia alipokuwa waziri?...”
“Sasa mbona wamkaribisha humu mwako nyumbani kila anapobisha? Anapokukebehi na kututafishi hapa mbona unamvumilia?... Mbona hunielewi?”
Kwa nini niendelee kumstahi mtu asiye na fadhila kama yule? “Huchoki kukaa hapa ukichuuza akali ya vitu kama hivyo?…”
“Aliolewa au alitoroshwa? Mbona unaniuliza swali unalojua jibu?” “Kazi? Kazi gani hii ya kubebana na vijana mchana kutwa?”
Hilo silo la Mzee Makutwa? … Kwani kipi kinaendelea?
“Kwa nini nisilipie? Mnadhani mashaibu kama sisi ni mafukara hohehahe hatuna hata pesa mfukoni?”
Taswira
…alishtukia kumwona Mzee Makutwa amepiga breki karibu na pahali alipoketi. Vumbi la hudhurungi lilitapakaa na kutulia juu ya vitanufaji alivyokuwa akichuuza.
Mzee Makutwa alitamka na kuondoka kwa kasi huku akitifua vumbi liliofunika gari lake na kufanya wingu kubwa hewani.
Gari la probox liliacha barabara kuu na kupenya kwenye barabara ndogo ya mchanga... lilifuata taratibu kutokana na mashimo yaliyowatatiza madereva hao... walijikuta wanaingia ndani ya gongo la mwitu.
Kulikuwa na miti mikubwa iliyofanya kivuli pande zote ungedhani jua la kutwa limewasili.
Magari hayo sasa yalianza kuteremka kwenye bonde kubwa ambalo lilificha kabisa miale ya jua.
Mteremko ulikuwa mkali… Walikaribia mahali ambapo palikuwa na tambarare kubwa lililopambwa kwa viduta vidogovidogo vya mchanga. Upande wa kulia wa tambarare hilo, kulikuwa na umati mkubwa wa vijana waliokuwa wakiupepeta mchanga na kuugawa mafungu…walikuwa wakidondoa vijiwe vidogovidogo vyenye kung’aa …Walisimamiwa na wanyapara waliokuwa wakiwaamrisha kwa sauti za kutisha.
Humo pangoni, mlikuwa na taa za vibatari zilizowekwa kandokando ya njia ili kuondoa utusitusi
uliokuwa mle. Mzee huyo alipishana na vijana… wakichimba madongo ya mchanga na kuyatia ndani ya mkokoteni. Walikuwa wameloa jasho kutokana na uhaba wa hewa mle ndani.
Mavulia waliyovaa ni yale yaliyouzwa majiani… Usiku walilala humo katika mabanda yaliyojengwa kigugu… Ua wa stima uliozungushiwa makazi haya pamoja na mabawabu katili wenye majibwa makubwa…
Taharuki
Kazi ya Makutwa inatia kila mmoja taharuki. Anaonekana kila mara akibeba vijana mitaani kuelekea kusikojulikana. Hata hana muda wa kuzungumza na kukaa na wazee wenzake. Tunashangaa kipi hasa kinachomweka ukaribu na vijana, hadi hatimaye tunapojua biashara anayofanya.
Bintiye Makucha, Riziki, anashindwa kuvumilia umaskini na kuolewa na Mhindi. Hatujaambiwa hali ya maisha anayokumbana nayo huko.
Makucha anasikiliza mazungumzo ya Sai na Dai na kujua wanasubiri gari la Makutwa waende nalo. Hapo hamu yake ya kujua inazidi. Anapanda teksi na kuwafuata. Hamu ya kujua afanyalo Makutwa inapanda.
Mazingira wanayopita Makucha wanapofuata gari la Makutwa yanatia taharuki. Wanaingia kwenye gongo la mwitu na kupitia barabara yenye mashimo kisha kupata tambarare kubwa. Tuna hamu ya kujua mambo yanayoendelea huku.
Mbinu nyingine ni pamoja na Kuchanganya ndimi, Nidaa, Takriri, Mbinu Rejeshi, Chuku, Utohozi, kejeli
na Koja.
Harubu ya Maisha- Paul Nganga Mutua Mtiririko
Utulivu wa mazingira unamsahaulisha msimulizi(Kikwai) mpito wa wakati hadi anapopokea simu ya Mama Mercy(mkewe) akilalamika kuwa mtoto atalala. Anagundua ni saa nne kasorobo usiku na kufunga kazi na kuondoka ofisini.Hakuna msongamano wa magari. Anapofika Kenyatta Avenue, anagundua simu inaita. Ni mamake amepiga. Haipokei bali anaamua kumpigia akifika nyumbani.
Anapofika nyumbani, analakiwa na malalamishi ya bintiye, Mercy, ya njaa. Mama Mercy anamwambia kuwa hapendi mambo ya kukopa na ndio maana hakupika, kwani ndani ya nyumba hamna chakula.
Analalamika kuwa alikuja likizo lakini Kikwai hana muda wake.Kikwai anamweleza kuwa ni hali kazini ilivyo, haimruhusu kuwa naye. Mercy anashtakia njaa tena na hapo Kikwai anaelekea kwa Vaite.
Anamkopesha unga na mayai mawili.
Kikwai anamlisha Mercy na kuelekea kulala, kwani hataki kula hali mkewe hali. Mama Mercy analalamikia mapuuza ya Kikwai kwenye malazi. Kikwa anamweleza kuwa wako katika shughuli za kuandaa vitabu vya kuwasilisha kwa baraza. Hawajalipwa miezi miwili. Anaahidi kusema na Bosi siku inayofuata. Anamwambia aende na Mercy kazini lakini anapinga kuwa hilo haliwezekani.
Anapotega majira ya kuamka kwenye simu, anakumbuka kumpigia mama. Anapokea na kumweleza hali yao ngumu, akitaka msaada. Anamweleza kuwa fundi wa nyumba anatishia kutwaa mali yao kufidia malipo yake yaliyochelewa mwezi mzima. Kikwai anamwomba kuzungumza naye asubiri, anaahidi kuwakumbuka akipokea malipo.
Asubuhi, anaamshwa na kilio cha Mercy ambaye anamshtakia njaa. Anamwahidi kumnunulia kitu ale, kisha anaamka kujiandaa kwenda kazini. Anakumbuka awali. Alikuwa na mshahara mdogo lakini uliwakimu, hadi Mama Mercy alipokuwa mja mzito na kujifungua. Mercy naye akawa na mataizo yaliyowagharimu, na hata sasa anahitaji vitu vya shule. Kazini nako mshahara umeanza kucheleweshwa na kufanya mambo kuwa changamano zaidi.
Anapofika kazini, Bosi anampigia simu kumwita ofisini. Anamwuliza kuhusu mwenzake, Nilakosi, ambaye anaandaa ripoti ya tathmini ya mswada fulani. Bosi anasema mkataba wake wa miezi miwili huenda ukakatizwa kwa kuwa hali si nzuri. Anaahidi kutoa jibu kuhusu kadhia ya Nilakosi, ambaye ametishiwa na mpangishaji kumfungia nyumba. Anaomba advansi, angaa elfu tano alipe kodi.
Anaitwa na Bosi tena, akimtaka aende kwake(Bosi) akampeleke mwanawe aliyeugua hospitali. Anamweleza kuwa hakuja kwa gari alilokabidhiwa na kampuni kwa kukosa mafuta. Bosi anakasirishwa na hili na kumtaka kurudi kazini. Siku inayofuata, Bosi haji. Wanapofunga kazi na Nilakosi, wanatembea. Anawazia hali ya familia yake. Tatizo lake kubwa ni Mercy, kwani hawezi kuelewa hali.
Langaoni la kuingia kwake, anapata bango la wazazi wanaotafuta kurithi mtoto wa kike. Anamwazia Mercy, jinsi anavyotaabika kumkimu na uhusiano wake na Mama Mercy ulivyoathirika vibaya.
Anapofika, anajulishwa kuwa Mercy alishindwa kula ugali wenye ladha na harufu ya mafutataa, alibahatika tu na ndizi mbili kutoka kwa shangazi yake aliyewatembelea. Anamtembelea Bishop wake, ambaye anamsaidia kwa chakula cha siku hiyo.
Kikwai anafika ofisini. Anapata arafa ya Nilakosi kuwa hatafika kazini kwani hali ni ngumu. Bosi anaingia ofisini na kumpigia simu afike humo mara moja. Anataka amweleze sababu ya kutofika kazini na gari la kampuni. Anapokea simu na kueleza kuwa mwanawe yuko salama. Kikwai anamweleza kuwa alikosa pesa. Bosi anadai kuwa Kikwai anaweka pesa mbele ya maslahi ya kazi. Anamwagiza amwone mhasibu kupokea mshahara wake kisha arejeshe vitu vya kampuni. Anapitia duka la Tuskys na kununua chakula na vitu vya kutumia na kwenda nyumbani. Baada ya kuandaa chakula na kula, anapumzika kidogo, kisha kuchukua kipakatalishi kuipiga msasa tawasifu kazi. Mercy anaingia na mara hii kushtakia shibe.
Ufaafu wa anwani ‘Harubu ya Maisha’.
Harubu ina maana ya taabu anayopata mtu. Maisha yamejaa harubu katika hadithi hii. Simu ya Mama Mercy ndiyo inamtoa Kikwai ofisini, huku akilalamika kuwa mtoto atalala. Ni wazi kwamba mambo si mazuri upande huo. Anapofika, anapata kuwa Mama Mercy hajapika kwa kuwa hataki kukopa. Mercy anamshtakia njaa mfululizo.
Mama Mercy anamzidishia Kikwai harubu kwa malalamishi yake kila mara. Analalamika kuwa Kikwai anamtelekeza na kuwa hawajibikii wajibu wake. Anasema kuwa yeye alikuja likizo hali mambo yako hivyo, hawapati muda wa kuwa pamoja. Hata anamtaka mumewe aandamane na Mercy kazini.
Kikwai analazimika kulala njaa kwa kuwa mkewe hajala. Haoni haja ya kula mkewe akiwa humo humo hali yeye hali. Isitoshe, chakula chenyewe kina ladha ya mafutataa. Wanaendelea kuzozana kwenye kitanda.
Kikwai anapokumbuka kumpigia mamake, anampasha taarifa ya harubu walio nayo, angaa awasaidie. Anamweleza kuwa fundi wa nyumba anatishia kutwaa mbuzi wao ili awauze ajilipe deni ambalo
limecheleweshwa karibu mwezi mzima. Hii ni harubu nyingine kwa upande wa Kikwai, kwani hana la kuwafaa, ila anaahidi kumtumia hela mwisho wa mwezi akipata mshahara.
Kikwai anaamshwa na kilio cha Mercy asubuhi, ambaye analalamikia njaa. Anajiandaa kwenda kazini huku akikumbuka harubu alizokuja nazo Mercy. Mahitaji mengi, mara mafua na meno, mara atie punje za mahindi sikioni au puani na kulazimu kiadi na daktari, hadi sasa anapohitaji sare za shule, kalamu, madaftari, karo na mengine.
Kazini, Nilakosi pia ana harubu yake. Mkataba wake wa miezi miwili unafupishwa kuwa mmoja, na pia anapata matatizo ya nyumba. Mpangishaji wake anatisha kumfungia nyumba kwa kuwa hajalipa kodi, anadhani anataka kumlaghai. Japo Bosi anatoa ahadi kutoa jibu, hafanyi hivyo.
Bosi analalamika kuwa Kikwai hafai kuacha gari la kampuni, ilhali hana pesa za kulitia mafuta. Anamtaka pia kwenda kwake kupeleka mtoto wake hospitalini kwa gari hilo. Siku inayofuata, haji kazini. Kikwai na Nilakosi wanalazimika kutembea kwani hawana hela za kupanda gari. Tatizo kuu la Kikwai ni Mercy ambaye hawezi kuelewa hali ilivyo.
Kikwai anafika nyumbani na kuambiwa kuwa Mercy alikataa kula ugali wenye ladha ya mafutataa. Alibahatika tu kupata ndizi mbili kutoka kwa shangazi yake aliyekuja kuwatembelea. Yanapomzidia, anaamua kwenda kwa Bishop ambaye anawaauni kwa chakula cha siku hiyo.
Nilakosi anazidiwa na kushindwa kabisa kufika ofisini. Kikwai anapofika anapata wito wa Bosi kufika ofisini mwake. Bosi analalamika kuwa anajali pesa kuliko kampuni, eti sababu haji kwa gari la kampuni kwa kukosa pesa za mafuta. Hivyo, anaafutwa kazi na kulipwa mshahara anaodai.
Huu unaondokea kuwa mwisho wa harubu ya maisha, lakini ukawa mwanzo wa nyingine. Analazimika kuishughulikia tawasifu kazi yake ili kuanza kusaka ajira mpya.
Maudhui Kazi
Kikwai anatia kila juhudi katika kazi yake ili kujipa riziki. Anapopigiwa simu na mkewe, bado yuko ofisini akiendelea na kazi, saa nne kasorobo. Anapopanda kitandani, anamweleza mkewe hali ilivyo kazini.
Anamwambia kuwa wanaandaa vitabu vya kuwasilishwa kwenye wizara. Haikosi anafanya kazi katika kampuni ya uchapishaji. Isitoshe, anamweleza kuwa hawajalipwa mshahara kwa miezi miwili sasa.
Anatega majira ya kuamka kwenye simu ili awahi kazini.
Anapoamshwa na kilio cha mwanawe, halali tena bali anajiandaa kwenda kazini. Anakumbuka awali jinsi kazi ilivyomkimu na mkewe, licha ya mshahara kuwa mdogo. Baadaye anakuja Mercy na mahitaji yake yanayonyonya pesa vilivyo. Isitoshe, kazini nako mishahara inaanza kucheleweshwa. Hali hii inasababisha matatizo ya kutoelewana kati yake na mkewe.
Kazini, yupo Nilakosi anayefanya kazi kwa kandarasi(contract) ambayo inatarajiwa kuisha baada ya miezi miwili. Hata hivyo, inpunguzwa hadi mwezi mmoja kutokana na upungufu wa mauzo. Kwa sasa, yuko katika harakati za kuandaa ripoti ya tathmini ya riwaya fulani aliyofanya. Kazi hii ndiyo inamkidhia mahitaji an kutokana na kuchelewa mshahara, anaanza kutishiwa kufungiwa nyumba kwa kuwa hajalipa kodi.
Bosi anawahangaisha wafanyakazi vilivyo. Anaahidi kutoa jibu la suala la Nilakosi lakini hasemi lolote. Pia, anamtaka Kikwai kwenda kwake kumpelekea mwanawe hospitali akidai magari ya kampuni ni ya dharura kama hizo. Anakosa kufika kazini siku inayofuata. Nilakosi na Kikwai wanalazimika kusafiri kwa miguu kwani hawana hela.
Siku inayofuata, Nilakosi anashindwa kufika kazini, hali ni ngumu. Kikwai naye anaitwa na Bosi na kupigwa kalamu kwa kisingizio cha kuthamini pesa Zaidi ya kampuni kwa kuwa haji na gari la kampuni, sababu hana pesa za kulitia mafuta. Analipwa mshahara wake na kuagizwa kurudisha mali ya kampuni. Maisha lazima yaendelee. Anaanza kushughulikia tawasifu kazi yake ili kutafuta kazi nyingine.
Migogoro
Usemi wa Mama Mercy anapompigia simu Kikwai una ladha ya mgogoro. Anamwuliza sababu ya kutofika hali mtoto aelekea kulala. Anapofika nyumbani, mgogoro wao unaonekana wazi. Anamweleza kuwa hajapika kwa kuwa hakutaka kukopa. Wanapoenda kulala, Mama Mercy analalamika kuwa mumewe hatimizi wajibu wake, na hata kumtaka kuandamana na Mercy kazini.
Mama anamweleza Kikwai mgogoro kati yao nyumbani na fundi wa nyumba. Wamemcheleweshea malipo yake kwa karibu mwezi mzima na sasa anatishia kutwaa mbuzi wao na kuku kuuza ili kujifidia malipo hayo.
Kikwai anagongana na Bosi baada ya kuacha gari la kampuni nyumbani kwa kukosa mafuta. Bosi anadai kuwa linafaa kuwa katika kampuni kila mara ili kutumika wakati wa dharura. Mgogoro huu ndio hatimaye unatumika kama kisingizio cha kumwachisha kazi, eti kwa kuwa anathamini pesa zaidi ya maslahi ya kampuni.
Nilakosi pia ana mgogoro na mpangishaji(landlord) wake, kwani mwezi unaisha na hali hajalipa kodi.
Landlord huyu anahofia kuwa Kikwai anataka kumlaghai.
Umenke.
Ni hali ambapo wanawake huwadhulumu wanaume katika jamii; kinyume cha ubabedume. Hali hii inadhihirishwa na Mama Mercy kwa jinsi anavyomtendea Kikwai, mumewe. Anampigia simu na kumlazimu kuondoka ofisini akilalamika kuwa mtoto yuko karibu kulala. Hata anapofika nyumbani, hamlaki kama mume bali anatulia tu kwenye pembe ya kochi.
Kikwai anampata Mama Mercy hajapika kwa kuwa hamna chakula. Anasema kuwa hapendi mambo ya kukopa. Kikwai analazimika kwenda kwenye duka mwenyewe kukopa. Anaporudi nyumbani, anaandaa chakula na kumlisha mwanawe, kasha anaelekea kitandani.
Mama Mercy analalamika kuwa mumewe anawaacha pale na kurudi tena jioni bila chochote. Hataki kusikiliza kuwa hajalipwa na pia anajaribu awezavyo kukidhi mahitaji yao. Anamfokea na hatimaye kumtishia kuwa ataenda na Mercy kazini. Anadai kwamba alikuja likizo ili aweze kujistarehesha. Hafanyi lolote kumsaidia mumewe kusaka riziki.
Kikwai anaeleza hali ilivyokuwa awali. Mshahara wake mdogo unawakidhia mahitaji yote, hadi Mama Mercy anapohimili na kujifungua Mercy. Anayaleta mahitaji mengine yanayomhangaisha Kikwai. Mama mercy anaathiriwa sana na mabadiliko ya kazini ya kuchelewa kwa mshahara wa mumewe.
Baada ya kulipwa na kuachishwa kazi, anaeleza kuwa anapita kwenye duka na kununua chakula na vitu vya nyumba na kurudi nyumbani. Ajabu ni kuwa anapofika, bado ndiye anaandaa chakula, wanakula, kisha anaingia kwenye kipakatalishi chake kuipiga msasa tawasifu kazi yake.
Ndoa
Kuna ndoa kati ya Kikwai na Mama Mercy inayodhihirisha misukosuko tele. Wanapooana, mambo yamenyooka kwani mshahara wa Kikwai unawakimu japo ni mdogo. Kisha Mama Mercy anapata mimba na kujifungua Mercy, anayekuja na mambo yake. Mafua, meno na kutia punje za mahindi kwenye pua na masikio. Sasa anahitaji karo, sare, madaftari na kalamu.
Mama Mercy anaanza kumlalamikia mumewe kila mara baada ya suala la kuchelewa kwa mishahara. Anamlaumu wala haamini anapomweleza hali ilivyo. Anasusia kupika kwa kuwa hakuna chakula wala hapendi kukopa. Kikwai analazimika kumshughulikia mtoto wao, Mercy, mwenyewe.
Ndoa hii pia inadhihirisha umenke. Mama Mercy anashinda nyumbani mchana kutwa lakini Kikwai anapotoka kazini, analazimika kuja kupika. Mama Mercy pia anamfokea kila mara, baada yake kufokewa na Bosi huko kazini.
Malezi
Kikwai na mkewe wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kumlea mwana wao, Mercy. Awali, mambo yako sawa hadi anapozaliwa Mercy. Anakuja na mahitaji ya hapa na pale ambayo yanamhanagaisha Kikwai. Mara ana mafua na matatizo ya meno, kasha atie punje za mahindi kwenye pua na masikio na kulazimu miadi na daktari. Sasa anahitaji sare, karo, madaftari na kalamu.
Mama Mercy anamtoa Kikwai ofisini akimweleza kuwa mtoto karibu analala. Analazimika kuacha kazi kwenda kumshughulikia. Anapofika, anamshtakia njaa. Analazimika kwenda kukopa chakula na kuja kumpikia. Anamlisha na kumpeleka kulala. Mercy anamwamsha tena asubuhi kwa kilio kingine cha njaa. Anamwahidi kumnunulia kitu huku akijiandaa kwenda kazini. Anaporudi, anaambiwa kuwa alikula ndizi mbili tu kutoka kwa shangazi, baada ya kukataa ugali wenye ladha ya mafutataa.
Kikwai anamkimbilia Bishop kwa msaada wa chakula kulisha familia yake. Siku inayofuata, anapigwa kalamu, lakini analipwa mshahara wake wa awali. Ananunua chakula kingi na kurejea nyumbani.
Anapikia familia yake na wanapokula, anaanza kuipiga msasa tawasifu kazi, tayari kutafuta ajira nyingine kukidhi mahitaji yao.
Ukengeushi/Mkengeuko
Ni tabia ya Waafrika kufuata maadili ya kimagharibi na kutupilia mbali maadili ya nyumbani. Unadhihirika kupitia kwa Mama Mercy. Anamfokea mumewe kila mara akilalamikia hali ya maisha licha ya kuwa anajitahidi. Hata anamtaka kuandamana na Mercy kazini. Isitoshe, mumewe ndiye anapika kila mara hata baada ya kuchanika kutafuta chakula chenyewe. Haya ni mambo ambayo hayafai kulingana na jamii ya Kiafrika. Anafaa kumheshimu mumewe na kumtumikia.
Maudhui mengine ni pamoja na Njaa na Umaskini, Mazingira, Dhiki na Usaliti.
Wahusika: Sifa na Umuhimu.
Kikwai
Ni mwenye bidii. Anajitoa na kujituma katika kazi yake. Anagutushwa saa nne kasorobo na simu ya mkewe, bado akiendelea na kazi ofisini mwake. Hata anapokosa mafuta ya gari, anaamka mapema ili kutembea kwenda kazini.
Ni mwajibikaji. Anafanya kila linalotarajiwa kutoka kwake, nyumbani na kazini. Anaikimu familia yake kwa kila hali licha ya ugumu wa maisha uliopo. Anafika kazini kwa wakati kila siku.
Ni mwenye Imani/tumaini. Kila mara anaamini kuwa maisha yatakuwa bora. Anamsisitizia Mama Mercy kuwa hali waliyo nayo ni ya muda tu. Anapoachishwa kazi, anaanza kuipiga msasa tawasifu kazi yake kwa matumaini ya kupata ajira mpya.
Ni mkakamavu. Anamsisitizia Mama Mercy kuwa anashughulika kila mara ili kuboresha maisha yao. Anakataa katakata kuandamana na Mercy kazini. Anapitia dhiki nyingi lakini anazikabili kwa ukakamavu.
Umuhimu wa Kikwai
Ni kiwakilishi cha mashaka ya maisha kwa jumla, hasa kwa watu wanaoishi mijini. Ni kielelezo cha bidii katika utendakazi na umuhimu wake katika maisha.
Ni kiwakilishi cha dhuluma za kindoa zinazotekelezwa dhidi ya mwanamume.
Ni kielelezo cha mwanandoa na mlezi mzuri na nafasi yake katika kuimarisha maisha ya familia yake.
Mama Mercy
Ni mbishi. Kila mara anazozana na mumewe kuhusiana na suala la kazi. Japo Kikwai anamweleza kuwa hali iko hivyo, hataki kumwelewa.
Ni mkakamavu. Anapofanya uamuzi, harudi nyuma. Anakosa kupika kwa kuwa hataki mambo ya mikopo. Anamzoza mumewe na hata kumtishia kuwa ataenda na Mercy kazini.
Ni mwenye mapuuza. Anampigia mumewe simu na kumweleza bintiye yuko karibu kulala. Hajapika wala kumlisha mtoto. Kikwai anapofika, amejikunyata kochini wala hata hamsabahi.
Amekengeuka. Anamtelekeza mumewe na kumgombeza kila mara. Mumewe anatoka kazini na kuja kupika yeye akiwepo tu wala hajali chochote.
Ni mstaarabu. Anahiari kutopika badala ya kukopa. Pia, Vaite anamwambia Kikwai kuwa amemkopesha kwa heshima ya mkewe, ambaye si mmbea kama wanawake wengine pale.
Umuhimu wake
Kupitia kwake, matatizo ya ndoa yanadhihirika wazi.
Ni kiwakilishi cha wanawake wa kisasa wanaowatumikisha waume zao bila shukrani
Ni kielelzo cha wanawake wanaojiheshimu, ambao hawajihusishi na umbea wa mitaani. Ni kiwakilishi cha migogoro katika jamii
Bosi
Ni dhalimu. Anawahangaisha wafanyakazi wake ikiwemo Kikwai na Nilakosi. Anamtaka Kikwai kwenda kwake kupeleka mwanawe hospitali akidai ni dharura. Suala hilo halihusiani na kampuni. Anamfuta kazi kwa kisingizio cha kuthamini pesa zaidi ya kampuni.
Ni mbishi. Anadai kuwa kwa vyovyote vile, Kikwai anafaa kuja kazini kwa gari la kampuni, licha yake kumweleza matatizo anayopata kuhusu mafuta. Hatimaye, anatumia hilo kumfuta kazi.
Ni mwenye mapuuza. Haoni sababu ya Kikwai ya kutofika kazini na gari la kampuni licha ya kuwa hana pesa. Anamfuta kazi bila habari, wala hajali atakakokwenda.
Ni mbinafsi. Anajali maslahi yake tu. Kila mara anamwitaita Kikwai ofisini kumpa majukumu lakini hajali maslahi yao. Anamtaka akampeleke mwanawe hospitalini. Anaahidi kuangazia suala la Nilakosi ila siku inayofuata haji kazini.
Ni mwenye dharau. Anamwambia Kikwai kuwa anathamini pesa zaidi ya kampuni, na hivyo anataka kumpumzisha kwa kumwachisha kazi, ili asiwe na bughudha ya kufanya kazi na kucheleweshwa mshahahara.
Umuhimu wa Bosi
Ni kiwakilishi cha udhalimu unaotekelezwa katika sehemu za kazi Anadhihirisha baadhi ya migogoro inayoshuhudiwa katika jamii. Kupitia kwake, uhusiano kati ya kazi an familia unadhihirika.
Nilakosi.
Ni mwenye bidii. Anafanya kazi yake kwa bidii. Amemaliza kutathmini riwaya, yuko katika harakati za kuandaa ripoti.
Ni mwajibikaji. Anatimiza wajibu wake kama mfanyakazi wa kampuni na kuwasili kazini hali inaporuhusu.
Umuhimu wa Nilakosi
Anadhihirisha hali ya mazingira ya kazi na uhusiano baina ya wafanyakazi unavyofaa kuwa. Kupitia kwake, taabu za maisha, hasa ya mjini zinabainika.
Bishop
Ni mfadhili. Anamkaribisha Kikwai kwake na kumsaidia kwa chakula.
Ni mcha Mungu. Ni mhubiri, na pia anamsisitizia Kikwai kuwa Bwana amekuwa mwaminifu.
Ni mwaminifu. Kikwai anakumbuka akisema kuwa kwake chakula hakiwezi kukosa. Anapomwendea kwa msaada wa chakula, hakika anakipata.
Ni mwenye utu. Anamsaidia Kikwai kwa chakula na hata kukataa rai yake ya kumfanyia kazi.
Umuhimu Wake
Kupitia kwake, nafasi ya dini katika jamii inabainika.
Ni kiwakilishi cha utu katika jamii.
Anasaidia kuonyesha uzito wa dhiki zinazomkumba Kikwai katika maisha yake.
Mbinu za Uandishi Balagha
“Saa ngapi? Si wajua mtoto angali anakusubiri?...”
Lakini mtu anawezaje kula chakula mkewe akiwa na njaa, tena hapo hapo katika chumba kimoja? “Sasa unataka nifanye nini?... Na mishahara? Sasa miezi miwili imetimia…”
“Hivi, kwani huko kazini wanasemaje? Si karibuni itatimia miezi miwili; miezi miwili bila malipo! Wanafikiri mnakula nini?”
Sasa kuna hili jipya la kucheleweshwa mishahara. Kisa na maana? … Ukosefu wa hiyo nafuu kazini umemwathiri Mama Mercy… Au pengine alikuwa anatii kanuni ya maisha ya mabadiliko?
“Aah, brother! Mpaka unifanyie kazi?...”
“Hilo linahusu nini wajibu wako? Tuseme wewe uliamua kususia kuja na gari kama njia ya kuonyesha kuchoshwa kwako na hali ya sasa?... Unatoa mfano gani kwa wenzako kazini?”
Uzungumzi Nafsia
Nitampigia nikifika nyumbani
Kama hatanikopesha huyu Vaite leo, basi nitaona moto, … Amejuaje hilo? Atapokea simu majira kama haya?
Hapatakalika hapa,
Si aliwahi kunieleza kuwa hapo kwake hapawezi kukosa chakula? Hapo ndipo ilipo riziki yangu leo.
Kuchanganya Ndimi
Barabara ya Waiyaki Way haina msongamano… ilinichukua dakika chache kuyafikia makutano ya Uhuru Highway na Kenyatta Avenue.
“Hili, Mama Mercy, ni kile tunaita bad coincidence…”
Kesho nitasema na Bosi. Akiwa katika mood nzuri huenda akanipa kitu kidogo…
“…katika hali kama hii, it is virtually unsustainable kuwa na wafanyakazi wengi. Contract yake inaisha lini?”
“Landlord anatishia kumfungia nyumba…”
“Nashukuru…eeh. He’s now stable. Out of danger…absolutely. Yes… asante sana…”
Dayolojia
Mazungumzo kati ya Kikwai na mkewe kabla Mercy hajawakatiza kuhusu suala la upishi. Kikwai anapomsaili, mkewe anamweleza kuwa hakupika kwani hakuna chakula na hapendi kukopa.
Mazungumzo kati ya Kikwai na mkewe, Mama Mercy, akimweleza jinsi hali ilivyo ngumu, na kuwa anafaa kuvulia, mambo yatakuwa mazuri. Inatuonyesha ugumu anaopitia Kikwai, migogoro na matatizo ya ndoa.
Kuna mazungumzo kati ya Kikwai na bintiye, Mercy, anapomwamsha asubuhi kwa kilio. Anamshatakia kuwa analia sababu ya njaa, naye anamwahidi kumnunulia kitu ale. Dayolojia hii inatuonyesha matatizo ya malezi na dhiki za maisha ya Kikwai.
Mazungumzo kati ya Kikwai na Bosi kuhusu Nilakosi na kandarasi yake inayokamilika, na pia kuhusiana na gari la kampuni, anapomtaka aende nalo kupeleka mwanawe hospitali, hali ameliacha nyumbani.
Inaonyesha migogoro, udhalimu na matatizo ya kazini.
Mazungumzo kati ya Kikwai na Bishop anapoenda kumwomba msaada wa chakula, wakijuliana hali na Bishop kumkidhia haja. Yanaonyesha nafasi ya dini katika jamii na umuhimu wa utu.
Mazungumzo kati ya Bosi na Kikwai anapomfuta kazi, akilalamikia mazoea yake ya kuacha gari la kampuni nyumbani. Anasema kuwa atamwondolea taabu ya kucheleweshwa mshahara kwa kumwachisha kazi. Yanadhihirisha migogoro na udhalimu kazini.
Semi na Nahau
nikajikaza kiume- nikajikaza kabisa kuchapa kazi- kufanya kazi kwa bidii kuuponda wa fisi- kutembea kwa miguu
shingo upande- bila kupenda, kwa kujilazimisha au kulazimishwa tu. Aliyekula kiapo- aliyeapa, aliyetoa ahadi
Mikono mitupu- bila chochote Sina budi- inanibidi, sina lingine Kinaya
Mama Mercy anampigia Kikwai simu kulalamikia mwana yuaelekea kulala. Amehiari kumweka Mercy na njaa hadi babake arudi, badala ya kukopa.
Bosi anamwambia Kikwai kuwa gari la kampuni linafaa kuwepo kwa ajili ya dharura kama inayomkumba ya mwanawe kuwa mgonjwa. Ukweli ni kuwa hii ni shughuli ya kibinafsi.
Bosi anamwambia Kikwai kuwa haoni kwa nini haji kwa gari la kampuni, licha yake kumweleza kuwa hana pesa za mafuta. Anadai kuwa anathamini pesa zaidi ya kampuni, pesa ambazo hata hana!
Bosi anamwambia Kikwai atamwondolea taabu kwa kumwachisha kazi ili asikumbwe na suala la kucheleweshwa mshahara. Ukweli ni kuwa anamweka katika taabu ya kutafuta kazi nyingine.
Tashihisi
Tuweze kusukuma siku…
Kwa sababu nisiyoweza kubaini, uliniparamia mpapo wa moyo nikisubiri simu kupokelewa upande wa pili.
Methali
Kila msiba huandamana na mwenziwe.
Istiara
Niliipokea kwa kasi ya mama anayechupa nje ya nyumba kumfuata mtoto mtundu asiyefahamu hatari iliyoko barabarani anakokimbilia.
Na kuongeza msumari wa moto kwenye kidonda kibichi, chakula kina harufu na muonjo wa mafutataa. Mbinu nyingine zilizotumika ni kama vile Utohozi, Mdokezo, Takriri, Sadfa, Nidaa na Koja.
Sabina- Winnie Nyaruri Ogenche Mtiririko
Ni Jumapili ya mwisho kabla ya mtihani wa kitaifa kuanza. Sabina anawazia mtihani pamoja na ufadhili wa shule ya bweni unaomsubiri iwapo atafaulu. Hata hivyo, anashangaa itakuwaje akifeli. Anakumbuka maneno ya mwalimu kuwa mizizi ya elimu ni michungu ila matunda ni matamu. Anagutushwa na wito wa Yunuke, na hapo anainuka haraka. Anagundua jua linatua na hivyo kuharakisha kuendea ng’ombe malishoni kuja kuwakama. Anawafunga zizini na kuanza kuandaa chajio. Jumatatu, anaamka na kukama ng’ombe, kupeleka kisonzo shambani na kwenda sokoni kuuza maziwa. Anatoka saa tatu unusu na kuelekea shuleni kwa maandalizi ya mtihani.
Sabina ana umri wa miaka kumi na minne, japo anaonekana mkubwa kutokana na dhiki. Mamake, Nyaboke, alijifungua akiwa kidato cha pili na kukatiza masomo. Janadume lililomtia uja uzito lilimtelekeza. Sabina anaanza shule katika darasa la kwanza akiwa na miaka saba na anapata matokeo bora. Akiwa darasa la nne, mamake anaugua ugonjwa wa ajabu unaoanza na kipele shingoni. Kinapozidi anapelekwa kwa mganga anayedai kipele hicho ni cha laana. Baadhi ya watu wanasema ni ya babake kwa sababu ya kujifungua nyumbani na kukataa posa ya wanaume, huku wengine wakimshuku Ombati, nduguye kwa kukosa mahari ya dadake. Hatimaye Nyaboke anafariki.
Sabina anatia bidii masomoni ili kuwafaidi bibi na babu, lakini hao wanafariki akiwa darasa la tano baada ya kujifungia ndani ya nyumba na jiko la makaa likiwaka. Watu wanaanza kuambaa familia yao, na analazimika kuishi kwa mjomba wake, Ombati, na mkewe, Yunuke. Hapa anatwikwa majukumu kama
kukama ng’ombe, kuzoa kisonzo, kuuza maziwa, kuwapeleka ng’ombe malishoni na majukumu mengine ya nyumba. Hata binamu zake hawamsaidii bali kumwongezea dhiki, ila Mike anayeandamana naye malishoni hata baada ya kuadhibiwa. Licha ya kazi zote, bado anaibuka wa kwanza darasani kwao.
Siku ya maandalizi, Sabina anafika amechelewa na kujiunga na wenzake. Mwalimu anawaambia kuwa wanafaa kuwa kwenye chumba cha mtihani saa mbili kasorobo. Atakayechelewa hataruhusiwa kufanya
mtihani. Sabina anatikisa kichwa kama kwa kupinga. Mwalimu mkuu anamwita ofisini na kumwuliza sababu ya kufanya hivyo na pia kuchelewa. Anamweleza majukumu aliyo nayo, na hapo mwalimu anamwandikia barua fulani. Anaporudi nyumbani, Yunuke anamvamia kwani saa mbili zimepita tangu wanafunzi wengine watoke shule. Anamweleza ni barua ilimkawisha huku akijiopoa na kutoroka. Yunuke anamtukana, akidhani ni barua kutoka kwa mwanamume.
Jumanne saa mbili kasorobo, Sabina yuko ukumbini akisubiri mtihani, hayuko sokoni Itumbe kuuza maziwa. Anafanya mitihani ya siku hiyo kwa furaha na tumaini. Anapofika nyumbani, Yunuka anamkabili kwa kutouza maziwa, lakini anasema aliyauza na kumkabidhi pesa. Yunuke anamtuma shambani kutapakaza kisonzo. Anaporudi anajaribu kusoma kwa mwanga wa kibatari, lakini Yunuke anakizima akimkashifu kwa matusi.
Ombati anafika nyumbani kwa likizo ya Disemba ili kumwandaa Mike kwa ajili ya shule ya upili, na kumwoza Sabina. Matangazo ya mtihani yakifanywa, Sabina yuko shambani naye Ombati ana mkutano na wanaomwoa Sabina. Maripota wanapofika wakiimba nyimba za kumsifu Sabina, hawaelewi yanayotukia. Wanapomwulizia Ombati mwanawe aliyefanya vyema, anamwita Mike, lakini wanasema wanamtaka Sabina. Sabina anafika kutoka shambani na rinda lake kuukuu. Wanambeba juu juu na kumshangilia. Ombati anawafurusha waliokuja kumwoa Sabina na mifugo wao, huku akijiunga naye kuhojiwa. Anampa hongera na kuwakaribisha kwa vyakula.
Sabina anakumbuka ugumu wa maisha yake, na shughuli zilizomwandama wakati wa mtihani wa kitaifa. Anakumbuka hisani ya mwalimu kuwaandikia wapishi barua ili Sabina awaletee maziwa badala ya kuyauza sokoni. Anauona huo kama mwanzo wa ufanisi wake. Yunuke na Ombati hawataki kumwacha. Mvua inawatawanya na habari za ufanisi wake zinabaki mada kijijini kwa takriban wiki nzima.
Ufaafu wa Anwani ‘Sabina’
Mada hii inatokana na jina la mhusika mkuu wa hadithi hii. Ndiye kitovu cha hadithi yenyewe na matukio yote katika kisa hiki yanamzunguka yeye. Inahusu maisha ya Sabina kwa jumla tangu kuzaliwa kwake, kulelewa na mamake Nyaboke hadi anapofariki, kuachwa tena na babu na bibi na hatimaye kudondokea kwenye familia ya Ombati na Yunuke. Huku anapitia dhiki tele na kujikakamua hadi anapofanikiwa hatimaye.
Dhamira ya mwandishi
Anasawiri matatizo yanayowakumba watoto yatima katika jamii kwa kukosa mtetezi
Kuonyesha jamii inavyomdhulumu mwanamke na jinsi yake kujiendeleza ili kushinda udhalimu huu. Anadhihirisha umuhimu wa bidii katika mambo tufanyayo na matunda yake.
Kuwaonya walezi wanaowadhulumu watoto yatima, kwani watoto hao wanaweza kuwa na vipaji vya kipekee vinavyoweza hata kuwafaidi walezi hao.
Anadhihirisha nafasi ya elimu katika kujenga na kuendeleza jamii.
Maudhui Elimu
Jamii hii ina imani katika usemi wa kuwa elimu ndio ngao ya maisha. Kila mzazi/mlezi anatia bidii kuvumisha elimu katika maisha ya mwanawe. Wanaamini kuwa mwenye elimu atapata mafanikio katika maisha.
Nyaboke, mamake Sabina, anasoma hadi kidato cha pili anapoambulia uja uzito. Analazimika kuacha masomo kuingilia ulezi. Hatua hii inawakera wazazi wake na kuwakatiza tamaa, kwani waliamini atasoma ili awe mtu wa maana maishani.
Sabina anadhihirisha nafasi ya elimu kwa kutia bidii za mchwa katika masomo. Yuko katika darasa la nane akijiandalia mtihani wa mwisho. Licha ya kazi nyingi anazofanya, bado analazimika kufika shuleni na kuendelea na masomo. Kwa sasa, anajiandalia mtihani, akijua kwamba akifaulu atapata ufadhili katika shule ya upili ya bweni.
Sabina anaanza masomo katika shule ya msingi ya Utubora katika darasa la kwanza akiwa na miaka saba kwa sababu ya ushupavu wake. Anaongoza katika darasa lake kwenye mitihani yote. Licha ya kufiwa na mamake, bibi na babu yake, halegezi kamba masomoni. Analazimika kuishi na Yunuke, mke wa mjomba ambaye anamtesa lakini anazidi kufana masomoni.
Binamu zake Sabina wanasoma katika shule ya upili ya Golden Heart. Wanaonana na Sabina wakati wa likizo tu. Ombati na Yunuke wanaona juhudi za Sabina kuwa kazi bure, lakini hakati tamaa. Nia yake kuu ni kujiunga na shule ya upili ya bweni.
Mwalimu mkuu anamsaidia Sabina kwa kuwaandikia wapishi barua wapokee maziwa yake. Anapata nafasi ya kufika katika mtihani kwa wakati na kuufanya bila tatizo. Matokeo yanapokuja, ndiye wa nane bora nchini. Ombati na Yunuke hawataki kujitenga naye wakati maripota wanapokuja kuwahoji. Kijiji kizima kinajaa habari za ufanisi wake kwa takriban wiki nzima.
Dhuluma/Udhalimu
Sabina anapitia dhuluma kadhaa katika maisha yake. Hapati muda wa kubarizi. Japo anasubiri mtihani wa kitaifa, analimbikizwa kazi nyingi na Yunuke. Anapoketi chini ya mparachichi kupumzika, anamwita kwa fujo. Analazimika kuinuka haraka kwenda malishoni kuwaleta ng’ombe ili awakame kisha kuanza
shughuli ya kuandaa chajio. Asubuhi siku inayofuata, analazimika kuamka mapema, kuwakama ng’ombe, kupeleka kisonzo shambani na kuuza maziwa. Anafika shuleni saa tatu u nusu.
Udhalimu unamkumba Sabina tangu akiwa darasa la tano, umri wa miaka kumi na mmoja anapoanza kuishi kwa Ombati. Hatimaye anazoea majukumu yote. Hata binamu zake hawamsaidii wanapokuja likizo bali kumwongezea dhiki. Lao ni kukaa kubarizi huku akitekeleza majukumu yote, lao kumtumatuma. Mike tu ndiye anamsaidia.
Sabina anapochelewa kwa mwalimu mkuu, Yunuke anamvamia japo anamwambia ni barua imemchelewsha. Anamtukana akidhani ni barua ya mwanamume na kumcharaza bakora. Hata siku za mtihani, bado anatakiwa kwenda kuuza maziwa kabla ya kwenda kwenye mtihani. Anaporejea siku ya kwanza, Yunuke anamkabili kuhusiana na maziwa, lakini anajiokoa kwa kumpa hela alizoyauza, lakini mara hii shuleni kwa hisani ya mwalimu mkuu.
Ombati anapanga kumwoza Sabina katika umri mchanga ili kupata mahari aliyokosa kwa mamake. Anapokuja likizo ya Disemba, anakutana na wakwe watarajiwa. Bado udhalimu unaendelea, kwani wakati huu Sabina yuko shambani akitapakaza kisonzo. Hata hana habari ya matokeo na ufanisi wake.
Utamaduni
Jamii inategemea ufgaji na kilimo ili kujiendeleza kimaisha. Sabina analazimika kukama ng’ombe wa mjomba wake, kuwapeleka malishoni na kuuza maziwa sokoni kabla ya kwenda shule. Pia anatakiwa kutapakaza kisonzo shambani. Hata maripota wanapofika kumhoji, yuko kazini kwenye shamba.
Anarejea bado akiwa na harufu ya samadi.
Kuna imani katika uganga na laana. Nyaboke anapopatwa na kipele shingoni, anapelekwa kwa mganga anayesema kuwa kimeletwa na laana. Hasemi ilikotoka. Watu wanakisia ni babake aliyemlaani kwa kuzaa kabla ya ndoa na kukataa wanaume wanaomposa wote. Wengine wanaamini ni Ombati kwa kukosa mahari yake. Hata Nyaboke anapofariki na hatimaye wazazi wake kumfuata, watu wanaanza kuambaa familia hiyo wakiamini wamelaaniwa.
Tamaduni za ndoa pia zimesawiriwa. Nyaboke anakataa posa ya wanaume wanaomtaka. Wanawake wanachukuliwa kama raslimali za kuzalisha mahari. Ombati anashukiwa kumlaani Nyaboke kwa kumkosesha mahari anapokataa kuolewa. Isitoshe, Ombati anaamua kumwoza Sabina baada ya mtihani kutokana na visingizio vya Yunuke vya uzinzi. Wakwezewatarajiwa wanakuja na kuleta mifugo, huku wakiandaa sherehe za kumlaki bi arusi wao. Wameandaa mapochopocho lakini yanakatizwa na mjo wa maripota.
Usaliti
Nyaboke anawasaliti wazazi wake kwa kuambulia uja uzito akiwa katika kidato cha pili. Wamejitolea kwa kila hali kumsomesha huku wakiwa na matumaini yake kuwafaa, yanayowatoka mara anapohimili na
kukatiza masomo. ‘Babake’ Sabina naye anamsaliti Nyaboke kwa kumtelekeza baada ya kumpa uja uzito.
Yunuke anamsaliti Sabina. Badala ya kumtunza licha ya kujua ni yatima, anamtesa na kumdhalilisha.
Anamlazimisha kukama ng’ombe, kupeleka kisonzo shambani na kuuza maziwa kabla ya kwenda shule. Anamfanyisha pia kazi zote za nyumba. Anapojaribu kusoma usiku, anamzimia kibatari anachotumia.
Anapofanya makosa madogomadogo, anamcharaza bila huruma na pia kumtukana vibaya, kila mara akimkumbusha kuwa yeye ni ‘kiokote’.
Ombati anamsaliti Sabina na Nyaboke pia. Kama mjomba, ni jukumu lake kumlinda na kumtunza Sabina. Badala yake, hafanyi lolote la kumfaa. Anaambia mwalimu mkuu kuwa nyumbani hakuna kazi zozote hali Sabina anatumikishwa sana. Anapanga njama ya kumwoza ili kufidia mahari aliyokosa kutoka kwa mamake, Nyaboke. Huu ni usaliti kwa Nyaboke, ambaye ni dadake. Anafaa kumtunzia mwana.
Binamu zake Sabina pia wanamsaliti. Wanapokuja likizo, wanamzidishia majukumu badala ya kumsaidia. Wanakaa tu na kubarizi huku wakimtumatuma, isipokuwa Mike anayejitolea kwenda naye machungani hata baada ya kuadhibiwa.
Nafasi ya Mwanamke
Anachukuliwa kama chombo cha kumstarehesha mwanamume. Nyaboke anatiwa uja uzito na janadume ambalo baadaye linamtema na kumwachia mzigo wa malezi peke yake.
Mwanamke anachukuliwa kama raslimali ya kuleta mapato kupitia kwa mahari. Nyaboke anapougua kipele kinachosemekana kuwa laana, Ombati anakisiwa kumlaani kwa kumkosesha mahari baada ya kukataa kuolewa. Ili kufidia mahari hayo, anaamua kumwoza bintiye, Sabina, baada ya kukamilisha mtihani. Tayari mifugo wameletwa na sherehe kuandaliwa, lakini zinakatizwa na mjo wa maripota baada ya Sabina kufaulu katika mtihani.
Mwanamke pia anachukuliwa kuwa mlinzi wa boma. Ombati anayoyomea mjini na kumwacha mkewe, Yunuke, nyumbani kuwa mlinzi wa mali yao. Yunuke naye anamtumia Sabina kutekeleza majukumu yote ya nyumba kabla ya kumruhusu kwenda shule.
Ndoa
Ndoa kuu katika hadithi ni ya Ombati na Yunuke, ambao wamejaliwa wana, Mike na wengine. Wawili hawa wanaishi kwa maelewano kama wanandoa kwa kiwango cha kuridhisha. Ombati anachuma riziki kama mume, huku Yunuke akibaki nyumbani kutunza boma kama mke wa boma hilo.
Nyaboke anaambulia uja uzito nje ya ndoa na kukataliwa na janadume lililomtia mimba. Hapo anapoteza imani na ndoa na kukataa posa za wanaume wote wanaokuja kumwomba awe mke wao. Hatimaye anafariki bila kuolewa.
Ombati anapanga ndoa ya mapema ili kujinufaisha kwa Sabina. Ndoa hii inachukuliwa kama kitega uchumi, ili ajipatie mifugo na hela. Sherehe za kumchukua bi arusi tayari zimepamba lakini zinatibuka maripota wanapokuja na taarifa za kufaulu kwake katika mtihani.
Kifo/Mauti
Nyaboke anaaga dunia baada ya kuugua kipele shingoni, ambacho kinatunga usaha na kuvimba. Juhudi za mganga wa kijijini anayepelekwa kwake hazizai matunda. Kifo chake ni pigo kubwa kwa Sabina, ambaye anabaki yatima. Anahisi kama amepoteza baba na mama baada ya ‘babake’ kutoweka.
Babu na bibi wa Sabina wanafariki kutokana na hewa ya sumu inayotokana na jiko la makaa. Wanajifungia ndani ya nyumba huku jiko likiwaka pembeni, na kupatikana asubuhi wakiwa wafu. Hili ni pigo lingine kwa Sabina, kwani ndio anaotegemea baada ya mamake kufariki. Anadondokea kwa mjombake anapokumbana na dhiki tele.
Maudhui mengine katika kazi ni pamoja na Mabadiliko, Migogoro, Utabaka, Familia, Malezi, Ukatili, Tamaa, Uzinzi na Utu.
Wahusika: Sifa na Umuhimu Sabina
Ni mwenye bidii. Anatia bidii katika masomo na pia katika kazi za nyumbani anazofanya. Kabla ya
kwenda shuleni, anatakiwa kukama ng’ombe, kutapakaza kisonzo shambani na kuuza maziwa. Licha ya yote haya, anafaulu vizuri katika masomo yake.
Ni mtiifu. Anafuata maagizo ya Yunuke na kumtii bila maswali. Anatapakaza kisonzo shambani anavyoagizwa na kukama ng’ombe na kuuza maziwa kabla ya kwenda shule. Anapoitwa na Yunuke, anatoka alipo upesi na kuelekea malishoni kuwaleta mifugo.
Ni mkakamavu. Anajitolea kwa kila hali kutimiza azma yake katika elimu. Baada ya kumaliza kazi zake, anatumia mwanga wa kibatari kusoma japo Yunuke anakizima. Licha ya kazi zote, bado anafaulu katika masomo yake.
Ni mwerevu. Akiwa katika umri wa miaka saba, anaungana na wenzake wanaotoka chekechea kwa wepesi wake wa kuelewa mambo. Baada ya matokeo kutoka, ndiye mwanafunzi wa nane bora nchini.
Ni mwenye maono. Hata baada ya mamamke kufariki, anaazimia kutia bidii ili kuwasaidia babu na bibi. Azma yake kuu katika siku za usoni ni kuwa daktari.
Umuhimu wa Sabina
Ni kiwakilishi cha dhiki ambayo watoto yatima hupitia katika maisha baada ya kuachwa na wazazi wao. Kupitia kwake, umuhimu wa bidii na matunda yake yanabainika.
Ametumika kuonyesha umuhimu wa elimu na nafasi yake katika kujenga jamii. Kupitia kwake, nafasi ya wazazi katika malezi na maisha ya wanao inadhihirika. Yunuke
Ni katili. Anamtumikisha Sabina bila huruma. Anamlazimisha kukama ng’ombe, kupeleka kisonzo shambani na kuuza maziwa kabla ya kwenda shule. Anapokawia kwenye ofisi ya mwalimu mkuu, anamvamia na kumtandika kwa bakora.
Ni mpyaro. Kinywa chake kinadondoka kila aina ya matusi bila haya. Anamwambia Sabina anaandama wanaume kama mamake na anajua matokeo yake. Anamwita mjalaana na baradhuli. Kila mara anamkumbusha kwamba yeye ni ‘kiokote’.
Ni dhalimu. Anatumia uyatima wa Sabina kumtumikisha nyumbani. Sabina anafanya majukumu yote ya nyumba huku yeye ameketi tu na kufurisha shingo. Hata wanawe wanapokuja likizo, hawamsaidii bali kumzidishia dhiki.
Ni mfitini. Anamwambia mumewe kuw Sabina ameanza kuwa na tabia za uzinzi na kumfanya kuandaa mipango ya kumwoza katika umri mchanga.
Umuhimu wa Yunuke
Kupitia kwake, udhalimu unaotendewa matoto mayatima katika jamii unadhihirika. Ni kiwakilishi cha nafasi ya mwanamke katika jamii.
Anadhihirisha nafasi ya ndoa na umuhimu wake katika kujenga na kuendeleza jamii
Kupitia kwake, watesi wa wasiojiweza wanapata funzo kuwa wanaowatesa wanaweza kufanikiwa na kuwafaa watesi hao.
Ombati
Ni mwenye tamaa. Ananuia kujinufaisha kutoka kwa dadake kupitia kwa mahari yake. Anapoyakosa, anaamua kutumia bintiye, Sabina, kwa kumwoza baada ya darasa la nane ili kupata mifugo.
Ni mtamaduni. Anaendeleza mifumo ya kijamii kama vile ubidhaaishaji wa wanawake. Anataka kupata mahari kupitia kwa Nyaboke na anapoyakosa, anaamua kumwoza bintiye, Sabina, katika umri mchanga na kumwandalia sherehe. Anasemekana kumlaani Nyaboke kwa kumkosesha mahari.
Ni kigeugeu. Maripota wanapofika kumhoji Sabina, anaungana naye huku akijisifia jinsi alivyomlea na alivyo mwerevu, licha ya kuwa awali anamtelekeza. Anawafukuza waliokuja kumposa Sabina na mifugo wao.
Ni mwongo/mzandiki/mnafiki. Anamhadaa mwalimu mkuu kuwa Sabina anapata muda wa kutosha kujiandaa kwa ajili ya mtihani. Anadanganya kuwa Sabina anapenda kazi za shambani hali analazimishwa.
Umuhimu wa Ombati
Anadhihirisha nafasi ya ndoa katika kujenga na kuendeleza jamii.
Kupitia kwake, tunaonyeshwa hali ya utamaduni na nafasi yake katika jamii. Ni kiwakilishi cha tamaa katika jamii na madhara yake.
Anadhihirisha nafasi ya mbaidiko wa kijinsia katika jamii.
Nyaboke
Ni mwenye bidii. Baada ya kujifungua, anaacha shule na kujikaza kumtunza mwanawe. Anaweza kumlisha na hata kumpeleka shule bila matatizo.
Ni mzinzi. Anaachia masomo katika kidato cha pili baada ya kuambulia uja uzito.
Ni mwenye msimamo thabiti. Anapoachwa na babake Sabina, anakosa imani na wanaume na kukataa posa zote anazoletewa na hakuna anayeweza kubadili msimamo wake.
Ni mlezi mwema. Anamkimu mwanawe peke yake. Anamlisha, kumvisha na hata kumpeleka shule.
Umuhimu wa Nyaboke
Kupitia kwake, changamoto zinazowakumba vijana katika juhudi za kuandama elimu zinadhihirika. Ni kiwakilishi cha nafasi ya mwanamke katika jamii na matatizo yanayomkumba.
Ni kielelzo ch malezi bora kwa wazazi hata kama kwa taabu kubwa.
Kupitia kwake, masuala ya kitamaduni kama laana, dhuluma na ubidhaaishaji wa wanawake yanadhihirika.
Mwalimu Mkuu
Ni mwenye makini. Anapohutubu ukumbini, anaweza kubaini Sabina anavyosumbuka akisikia kuhusu sheria za kuchelewa, licha ya kuwa kuna wanafunzi wengi darasani.
Ni mwajibikaji. Anatekeleza wajibu wake katika shule. Anawapa wanafunzi maagizo ya mtihani. Anamwita Sabina kujua linalomsumbua. Pia, anafuatilia kujua iwapo anapata nafasi ya kudurusu kutoka kwa Ombati.
Ni mwenye utu. Anamsaidia Sabina kuwahi chumba cha mtihani kwa kumwandikia barua alete maziwa shuleni badala ya kwenda kuyauza sokoni asubuhi.
Umuhimu Wake
Ni kiwakilishi cha nafasi ya walimu katika maisha ya wanafunzi wao.
Anawakilisha utu na ubinadamu katika jamii na umuhimu wake katika kuiendeleza. Kupitia kwake, maudhui ya elimu yanadhihirika.
Mbinu za Uandishi Tashbihi
Alianza kwa kuachia tabasamu pana mithili ya msafiri aliyefika salama. Maswali haya yalimliza yakamwacha akisinasina kama mgonjwa wa mafua.
Hakuthubutu kumwendea…kwani alijua kufanya hivyo ni kama kujipeleka kinywani mwa simba mwenye njaa.
Yunuke alikuwa amejikunjia pembeni huku amefurisha shingo kama kiboko. Alikimbia kama mwehu hadi nyumbani,
Aligutuka kama mtu aliyebumburushwa kutoka ndotoni… Sabina alinyanyuka mara moja kama askari kanzu.
Miguu ya Sabina ilikufa ganzi, akabaki amesimama kama kisiki.
Kila mtu alijua kuwa kuitwa ofisini mwa mwalimu mkuu kulikuwa sawa na sungura kuitwa pangoni mwa simba.
Semi
Alipigwa na butwaa- alishangaa na kuduwaa. walikata tamaa- walikosa matumaini. alijifunga kibwebwe- alitia bidii kutekeleza. akatangulia mbele za haki- akafariki, akafa.
kulaza damu- kuzembea, kukaa bila kufanya chochote. haukutiwa doa- haukuathiriwa, haukuwekwa kasoro yoyote. ilikufa ganzi- ilipoteza hisia.
najipalia makaa- najiletea balaa. kuchana mbuga- kukimbia,kutoroka.
nyota ya jaha- bahati nzuri.
Kinaya
Sabina anapowazia kuhusu mtihani, kwanza anaachia tabasamu pana, kisha baada ya hayo, machozi yanaanza kumtiririka.
Mwalimu mkuu anasema kuwa Ombati alimwambia wanampa Sabina wakati wa kutosha kujiandalia mtihani. Ukweli ni kuwa hapati muda huo. Analimbikizwa kazi zote nyumbani na hata anapothubutu kudurusu, Yunuke anamzimia kibatari.
Sabina anaporudi nyumbani baada ya siku ya kwanza ya mtihani, Yunuke anamuuliza kama aliona kuraukia shule ndio muhimu kuliko kuuza maziwa. Kwake, kuuza maziwa ni muhimu kuliko shule!
Sabina anapodurusu, Yunuke anamzimia kibatari huku akisema hana akili za masomo. Ajabu ni kuwa Sabina mwenyewe anaibuka nambari moja darasani.
Ombati anasema kuwa anashukuru kuwa bintiye amefaulu masomoni. Ajabu ni kuwa awali, hamchukulii kama bintiye. Anadai kuwa anapenda kazi za shamba, hali ni kulazimishwa analazimishwa.
Yunuke na Ombati hawataki kumwachilia Sabina hata kwa sekunde baada yake kufaulu katika mtihani. Awali, hawana shughuli naye hata kidogo bali umuhimu wake mkuu ni kutumika nyumbani.
Kisengerenyuma/Mbinu Rejeshi
Huku Sabina akiwazia mtihani anaosubiri, tunarejeshwa kwa asili yake, ambaye ni mwana wa pekee wa Nyaboke, anayempata akiwa katika kidato cha pili. Anaachia masomo hapo na kuanza kumlea hadi anapofariki kutokana na kipele shingoni.
Baada ya mama kufariki, Sabina anatia bidii ili kuwasaidia bibi na babu akikua. Wawili hao pia wanafariki kutokana na hewa ya sumu kutoka kwenye jiko la makaa. Hatimaye anaishia kwa familia ya Ombati, mjomba wake.
Sabina anatwikwa mzigo wa kutekeleza majukumu yote ya nyumba na anayatekeleza hadi anapozoea. Binamu zake wakija likizo kutoka shuleni hawamsaidii ila Mike tu. Bado anaendelea na ubabe wake katika masomo licha ya ujakazi huo.
Wakati akihojiwa, Sabina anakumbuka jinsi Yunuke alivyoishi kumkumbusha kuwa yeye ni ‘kiokote’ kila mara. Pia, anakumbuka hisani ya mwalimu mkuu ya kumwandikia barua awapelekee wapishi shuleni maziwa badala ya kuyauza, iliyomsaidia kufanikiwa katika mtihani.
Maswali Balagha
Lakini, angefeli je?
Basi kapitia wapi shetani kuchukua roho zao?
Nitafanyaje nifike shuleni kabla ya saa mbili asubuhi? Kitanifika nini nikifika katika ukumbi huu baada ya mtihani kuanza?
“Uliona kuraukia shule ni muhimu kuliko kuuza maziwa,eh?”
62
“Tangu lini ukaanza kunihadaa…”
Taashira
Sabina alipata nafasi ya kumtapikia mwalimu mkuu masaibu yake…(neno ‘kumtapikia’ lina maana ya kumwambia au kumweleza)
Uvundo ulimtoka mwanamke huyo.(‘Uvundo’ hapa lina maana ya lugha chafu, matusi)
Istiara
Kichwa chake kidogo kilikuwa uwanja wa mawazo ainati… Chanzo cha laana hiyo kilibaki kuwa fumbo.
Ripoti za Yunuke kwa mumewe kuhusu Sabina alivyobadilika kuwa mumunye la kuharibikia ukubwani…
Methali
Mtaka cha mvunguni sharti ainame. Kulea mimba si kazi, kazi ni kulea mwana.
Ganga ganga za mganga humwacha mgonjwa na matumaini. Mtoto wa nyoka ni nyoka.
Kuwa mumunye kuharibikia ukubwani.
Tashihisi
Alipigwa na butwaa alipouona wekundu wa jua ukimezwa na vilima vya magharibi. Alikimbia…akavaa sare yake iliyoshiba viraka vya kila rangi…
Dunia iliamua kumnyesha shubiri pindi tu alipozaliwa. Alikizima kibatari kile na giza kuu likaivaa nyumba.
Chuku
Nyumbani, Yunuke alikuwa amechemka kwa hasira.
Kilio cha kwikwi kilimtoka na kuwafanya hata ng’ombe kumsikitikia.
Taharuki
Mwanzo wa hadithi unaibua maswali mengi. Tunaambiwa kuwa mtihani wa kitaifa unaelekea kuanza, naye Sabina ana hisia mseto na mawazo mengi. Tunataka kufahamu sababu ya haya yote, ambayo yanatanzuka polepole.
Nyaboke anafariki kutokana na kipele ambacho mganga anasema kuwa kimetokana na laana. Tunabaki na maswali mengi. Je, ni kweli kipele hicho kilitokana na laana? Na ni ya nani? Ni ya nduguye Ombati au wazazi wake?
Sabina anaitwa na mwalimu mkuu na kukabidhiwa barua, ambayo hatuambiwi ni ya nini. Keshoye, yuko miongoni mwa wanafunzi walioketi kwa wakati kusubiri mtihani. Anaporudi nyumbani, anamkabidhi Yunuke pesa za maziwa na ndoo, japo Yunuke aliambiwa hakuonekana sokoni. Tunapata jibu hili mwishoni, Sabina anapokumbuka hisani ya mwalimu ya kumwandikia barua apelekee wapishi maziwa badala ya kuyauza sokoni.
Sadfa
Wakati matangazo ya mtihani yanapofanywa, Sabina yuko shambani. Familia nzima nayo iko katika harakati za kuandaa mapochopocho kwa ajili ya harusi ya Sabina. Hivyo, hakuna anayepata taarifa za kufaulu kwa Sabina.
Wakati Ombati na wakwe watarajiwa wa Sabina wanasherehekea ndani ya nyumba, maripota wanawasili na umati ukimwimbia sifa Sabina. Wote wanashindwa kufahamu kinachoendelea.
Ripota mmoja anamwulizia Ombati mwanawe naye anamwita Mike. Mwalimu mkuu anaingilia kati kumwuliza aliko Sabina. Kabla ya kujibu, wakati huo huo anafika Sabina na rinda kuukuu huku harufu ya samadi bado imemtapakaa.
Uzungumzi Nafsia
Nitafanyaje nifike shuleni kabla ya saa mbili asubuhi? Kitanifika nini nikifika katika ukumbi huu baada ya mtihani kuanza?
Jazanda
Baada ya sherehe na shmra shamra za ushindi wa Sabina, mvua kubwa inaanguka na kuwatawanya watu. Mvua ni kiwakilishi cha baraka.
Mbinu nyingine ni pamoja na Nidaa, Utohozi, Mdokezo, Dayolojia na Koja.
Mzimu wa Kipwerere!- Yussuf Shoka Hamad Mtiririko
Mzimu wa Kipwerere unatisha sana. Mzimu wenyewe ni wa kichaka kidogo kilichojaa aina tofauti ya miti iliyobanana na kusabababisha kiza kinene cha kutisha. Kitisho cha kwanza ni kichaka hicho kuitwa mzimu. Pili, kichaka hicho kiko kwenye kiwanja kipana kilichozungukwa na nyumba za wanakijiji. Jina Kipwerere linatokana na jamaa wa Bw. Msa, aliyesemekana kumpata shetani aliyefichua damu enzi za ujinga. Alipofariki alizikwa hapo, kisha kichaka hicho kikaota. Hivyo, kinaaminiwa kutokana na mzimu wa mwanamama huyo aliyejaa nguvu za kimiujiza.
Kabla ya kufikia ‘mzimu’ huo kutoka pande zote, kumezungukwa na makaburi ya watu maarufu, ambayo lazima uyapite. Nayo pia yanasemekana kuwa na vizuu na mizuka. Pia kuna miiko kuhusu msitu huu.
Mtu haruhusiwi kupita hapo saa sita mchana au majira ya usiku ila wazee wa msitu huo, vinginevyo atatolewa kafara. Usiku kunaonekana taa ikiwaka. Msimulizi anapoulizia, anaambiwa ni shetani anawapa watoto wake chakula. Hili linamtia udadisi. Pia, wanapita huko na watoto wakicheza na kusikia sauti ya mwanamume na mwanamke kutoka humo msituni, hasa nyakati za usiku mchanga. Wanapouliza wazee wanaambiwa shetani wa mzimu ana mke, na huzungumza watoto wakilala. Majibu haya yanamtia kiu
64
zaidi. Wakati mwingine wanasikia harufu ya mihadarati kama vile sigara na tumbaku. Wazee wanasema baadhi ya mashetani hutumia mihadarati.
Salihina ni kiongozi wa kijiji na pia mzimu. Anaongoza shughuli zote na kuomba ruhusa kwa mzimu kama vile tohara, arusi na shughuli. Ndiye anasemekana kujua siri za mzimu. Pia anasimamia maadili ya vijana. Anawakataza kutangamana wavulana na wasichana hata katika michezo. Wakati mmoja, msimulizi anapokea adhabu ya viboko kumi kwa kusimama karibu na msichana baada ya kucheza.
Utumiaji wa mihadarati ni hatia na pia unasemekana kupigwa marufuku na mizimu. Hata hivyo, mji wa watawa bado unaongoza kwa usambazaji na utumiaji wa dawa hizi, zinakotoka hakujulikani. Suala la mzimu badala ya kumtia woga msimulizi, linamtia udadisi na ujasiri. Anaazimia kujua siri za mashetani. Anajisogeza karibu na msitu huo kila kuchao hadi siku moja anapoamua kuukaribia. Anapolala karibu na mzimu, anausikia wimbo ambao husemekana lazima utumiwe kama ufunguo wa kuingia humo.
Unaimbwa na mwanamume na kujibiwa na mwanamke upande mwingine, kisha anaingia mzimuni. Baada ya muda, harufu ya tumbaku inamjia na sauti zile za chinichini. Baada ya saa tatu, wawili wale wanaondoka, kila mmoja njia yake. Msimulizi anaondoka, tayari kurejea keshoye kuingia mzimuni.
Keshoye magharibi, msimulizi anafika huku amevaa guo jeupe lililomfunika kabisa. Anaimba ule wimbo na kuingia. Kuna giza totoro, hivyo anawasha tochi. Anamulika na kuona marobota ya bangi, makasha ya tumbaku na unga wa kilevi, pia chang’aa kwenye pipa. Kuna kitanda cha besera kilichopambwa kwa maua juu na mvunguni. Anasikia sauti ya mwanamume ikiimba wimbo wa mzimu. Anazima tochi upesi na kuingia mvunguni. Baada ya wimbo, wale watu wawili wanaingia. Anajawa na hofu anapogundua sauti ya Salihina.
Wanaanza kwa kutumia vileo. Bishoo, yule mwanamke, anamweleza Salihina mbinu mpya ya kusambaza mzigo. Wanachukua ndoo na kusema wanaenda kuchotea shetani wa mzimu maji. Hakuna anayewasumbua, hata polisi. Ndoo hizo zinajazwa mihadarati badala ya maji. Salihina anakubali wazo hilo. Bishoo anamweleza kuwa ana haraka ya kurudi nyumbani kumwuguza mumewe anayeumwa na jino. Anamwambia kuwa hawatakaa sana. Salihina anaanza kuimba akimwelekea Bishoo. Bishoo anasogea na kuchukua kiberiti kuwasha kibatari. Kwa hofu ya kuonekana, msimulizi anachomoka na kuwashtakia kuwa amewakamata.
Bishoo anaanguka na kuzirai pale pale. Salihina anatoka mbio lakini mti unamzuia kwa kushika kanzu lake jeupe la bafta. Anamwomba msimulizi msamaha na radhi akidhani ndiye amemshika. Msimulizi anaondoka na kuwaacha hapo. Salihina analilia kitawi kile hadi asubuhi, wanakijiji wanapofika na kushuhudia siri ya mzimu waliouogopa kiasi cha kuuabudu.
Ufaafu wa Anwani ‘Mzimu wa Kipwerere’
Neno ‘Mzimu’ lina maana mbili. Kwanza, sehemu ambapo hufanyiwa matambiko na ambapo huaminika roho za waliofariki huishi, na kivuli cha mtu aliyeaga ambaye huwatokea walio hai. Kipwerere ni jina la mwanamke wa enzi za ujinga anayeaminiwa kuwa na nguvu za kimiujiza.
Jina hili linapatiwa msitu ulio katika kijiji hiki. Kwanza, msitu huo umezungukwa na makaburi pande zote. Lazima uyapite kabla ya kuufikia. Makaburi haya yanazikwa watu maarufu. Ndipo mizimu yao inaishi.
Msitu huu unapatiwa jina la mzimu kutokana na kutisha kwake. Una miti mikubwa iliyokua na kubanana, ikafanya kiza kikubwa. Unaaminika kuwa ulichipuka baada ya Kipwerere kuzikwa hapo. Mwanamke huyu aliaminiwa kuwa na nguvu za miujiza.
Msitu huu pia unaaminika kuwa makao ya mashetani na mizimu. Hivyo, watu hawaruhusiwi kupita hapo saa sita mchana na usiku. Wanaopita hapo wanatishiwa kuwa watatolewa kafara na kuondokea kuwa chakula cha Mzimu wa Kipwerere.
Mzimu huu(msitu) una maajabu yake. Usiku huonekana mwanga wa taa, na pia husikika mazungumzo ya watu. Isitoshe, harufu ya tumbaku na vileo vingine hutoka huko. Majibu ya masuala haya ni kuwa mashetani huzungumza, na pia hutumia mihadarati kama binadamu.
Salihina ndiye kiongozi wa mzimu. Kila kitu kuhusiana na mzimu lazima ahusishwe. Anasemekana kuwa ndiye anaweza kuwasiliana na mizimu. Wakati wa tohara, matambiko na arusi ndiye hutoa maombi kwenye msitu ili mizimu ikubali masuala hayo yaendelee.
Kuingia mzimuni pia kuna masharti yake. Kuna wimbo ambao yasemekana ndio ufunguo wa kuingia humo, na ambao lazima uimbe ndipo mashetani wakukubalie kuingia. Msimulizi anausikia kutoka kwa Salihina na Bishoo wanapoimba na kuingia.
Mwishoni, msimulizi anagundua kuwa Salihina ndiye ‘Mzimu wa Kipwerere’! Ndiye anazungumza huko usiku na mshirika wake, Bishoo. Ndio wanaowasha taa na kuvuta sigara. Wanatumia msitu ule kufanya biashara haramu ya usambazaji wa dawa za kulevya. Sheria zote na imani kuhusiana na msitu huo ni hila tupu.
Dhamira ya Mwandishi
Anawasilisha mila na tamaduni zilizopitwa na wakati na imani za kijinga, na jinsi zinavyoweza kutumika kuendeleza uhalifu.
Anadhihirisha unafiki unaotumiwa na viongozi kutekeleza uhalifu na kujinufaisha binafsi. Anasawiri uozo uliokithiri katika jamii kama vile unafiki na ulaghai, uzinzi na mengine.
Anatoa onyo kwa wanaotumia ujanja kutekeleza uhalifu kuwa siku yao ya kunaswa itafika tu. Anadhihirisha migogoro iliyopo katika jamii, hasa kati ya wazee na vijana.
Anadhihirisha umuhimu wa kuwa na udadisi na ujasiri kuhusiana na masuala tata ya kijamii.
Maudhui
Itikadi na Ushirikina
Ni imani potovu kuhusiana na masuala ya ramli, uchawi, mizimu na masuala ya aina hiyo. Watu wengi wanatishwa na Mzimu wa Kipwerere kutokana na imani za kishirikina. Inaaminika kuwa msitu huo ulikua baada ya Kipwerere kuzikwa hapo, mwanamke anayesemekana kupata shetani aliyefichua damu.
Yasemekana baada ya kuzikwa hapo, mzimu huo unakua. Pia, anaaminika kuwa alikuwa mwanamke wa miujiza.
Mzimu wa Kipwerere pia una miiko yake. Watu hawaruhusiwi kupita pale muda wa jua mtikati au jua likishatua. Pia, hakuna anayeruhusiwa kuingia humo ila wale waitwao wahenga. Yeyote ambaye angefanya hivyo, basi anasemekana kuwa chakula cha mizimu, na atatolewa kafara.
Watu pia wanaamini kuwepo kwa mashetani na mizimu. Watoto wanapochezacheza nja ya msitu ule, wanasikia sauti za chinichini za watu wakiongea. Wazee wanawaeleza kuwa shetani ana mke na mara nyingi wanapozungumza, watoto wao huwa wamelala. Taa inayowaka inahusishwa na mashetani hao, sawa na mnuko wa tumbaku na mihadarati mingine.
Msimulizi anajawa na udadisi kuhusiana na mashetani hawa wanaozungumziwa kila mara. Anaamua kujaribu kuingia msituni na hata ikiwezekana kuwaona kwa macho! Kwake, ni kweli kwamba mashetani hawa wapo. Kuna wimbo unaoaminiwa kuwa ufunguo wa kuingia mzimuni. Anausikia kutoka kwa Salihina na kuuimba kisha kuingia. La kushangaza ni kuwa hamwoni shetani yeyote anavyotarajia.
Anagundua kuwa Salihina ndiye anaendesha shughuli zote wanazoshuhudia msituni humo.
Salihina na Bishoo wanatumia itikadi na imani potovu kuchuuza mihadarati. Bishoo anamweleza mpango wake wa kusafirisha dawa hizo kwa kubeba ndoo wanazodai kuwa wanaenda kuchotea shetani wa mzimu maji. Hata polisi wenyewe wanawaruhusu! Ndoo hizo hatimaye zinajazwa ‘mzigo’; mihadarati.
Mazingira
Hali ya mazingira imengaziwa kwa njia ya kipekee. Mandhari yanaonyeshwa kwa uwazi wa kupendeza. Mzimu wa Kipwerere una miti ya aina tofauti, ambayo imemea kwa ukaribu na kufanya kichaka cha kutisha. Mshonano huo wa miti unafanya muhali kwa miale ya jua kupita au maji ya mvua na kuzua giza totoro mle ndani ya msitu huo.
Kichaka hiki kiko katikati ya iwanja chenye uwazi cha takriban eka moja. Pande zote, yanazunguka majumba ya wanakijiji wa hapo. Katikati ya majumba ya wanakijiji na msitu huo, kuna uwazi mkubwa ambao hautumiwi kwa shughuli zozote za kilimo ila umehifadhiwa kwa ajili ya kuzikwa kwa watu wenye utukufu katika jamii. Hivyo, kabla ya kuingia msituni lazima upite makaburi hayo.
Msimulizi anapoingia kwenye msitu, anakumbana na kiza totoro. Anamulika na kuona kitanda cha besera kilichotandikwa vizuri. Juu yake kuna asumini na maua ya mlangilangi yanayonukia mahaba. Chini ya kitanda, kuna chetezo kilichojaa udi wa mawaridi. Msimulizi anapowashtua washirika wa mzimu, Bishoo anazirai naye Salihina kutoroka lakini anakamatwa na kitawi cha mti, kinachomzuia kukimbia.
Ulaghai
Salihina anaaminiwa na kuheshimiwa na watu kama mzee wa kijiji na kiongozi wa mzimu. Anawahadaa wanakijiji kwa kujifanya mtu mzuri mwenye maadili lakini ukweli ni kwamba ni mtu mbaya.
Anamcharaza msimulizi kwa sababu ya kusimama karibu na msichana tu. La ajabu ni kuwa yeye mwenyewe anazini na mke wa mtu kwenye Mzimu wa Kipwerere.
Salihina anatumia woga wa watu kuhusiana na Mzimu wa Kipwerere kujinufaisha. Anawafanyia maombi na kuongoza matambiko yote ili yakubalike na mizimu. Anatoa sheria kali za mizimu ili kuwazuia watu kuingia msituni humo. Anautumia kuendeleza uzinzi na kuficha shehena za dawa za kulevya.
Uvutaji sigara na dawa za kulevya ni marufuku katika kijiji hiki. Hata hivyo, kijiji hiki kinaendelea kuongoza kwa masuala haya. Haijulikani zianakotoka dawa hizi. Viongozi kama Salihina ndio wanafaa kuwa katika msitari wa mbele kuwinda wahalifu. La kusikitisha ni kuwa Salihina mwenyewe ndiye anaendeleza ulanguzi wa dawa hizi kwa ujanja wa kutumia Mzimu wa Kipwerere.
Bishoo anampa Salihina mpango wa kilaghai wanaotumia kulangua dawa zile za kulevya. Wanakusanya wanawake na kuwapa ndoo wakidai kuwachotea maji shetani wa mzimu. Watu hawasaili chochote wanaposikia haya, hata polisi. Ndoo hizi badala ya kujazwa maji zinajazwa mihadarati.
Bishoo anamwacha mumewe ambaye anaumwa kuja kuzini na Salihina na kuendeleza biashara zao. Anamwambia Salihina kuwa alimuaga mumewe kuwa ameenda kumwona mtoto wa jirani mgonjwa. Anataka wamalize biashara zao upesi arudi nyumbani.
Ulanguzi/Biashara Haramu
Matumizi ya mihadarati yamepigwa marufuku katika kijiji hiki. Hata hivyo, bado kinaongoza kwa matumizi yake. Ni suala ambalo linawachanganya wengi, kwani kule zinakotoka dawa hizo ni kitendawili kikubwa.
Msimulizi anapoingia kwenye Mzimu wa Kipwerere, anapata marobota ya bangi, makasha kwa makasha ya tumbaku na mapipa ya chang’aa. Anagundua biashara haramu ambayo Salihina na washirika wake huendeleza katika msitu huu kwa kisingizio cha mashetani.
Kwa kuwa ni ulanguzi, Bishoo analazimika kutumia ujanja kusambaza dawa za kulevya. Wanachukua ndoo wakidai kuchotea shetani wa mzimu maji na kuzijaza shehena ile. Hata hivyo, hatimaye wanafumaniwa na wanakijiji wanajua siri kubwa iliyomezwa na msitu ule.
Utamaduni
Kuna usimulizi wa visa katika jamii. Jina ‘Mzimu wa Kipwerere’ linatokana na kisa cha mwanamke aitwaye Kipwerere, anayeaminika kuishi enzi za ujahiliya, jamaa ya Bwana Msa aliyepata shetani aliyefichua damu. Inaaminika kwamba anapozikwa ndipo msitu ule unamea. Ndio sababu unaaminika kuwa makao ya mizimu na shetani na kuogopwa sana.
Jamii hii ina mtindo unaotumika kutekeleza matambiko fulani fulani katika jamii. Salihina ni mtendaji mkuu wa shughuli za kimila kijijini. Watoto wanapotaka kutahiriwa, huletwa kando ya mzimu ili Salihina awape Baraka. Kukiwa na arusi, lazima apatikane aombe ruhusa kwa mizimu ili shughuli ziendelee.
Salihina anakataa katakata watoto wa kiume na kike kutangamana, hata wakati wa kucheza. Yeyote anakaribia jinsia nyingine anapata adhabu kali. Msimulizi wakati mmoja anajipata amesimama karibu na msichana baada ya mchezo wa mwajificho. Salihina anapopata habari anampa viboko kumi.
Jamii hii pia ina nyimbo zinazotumiwa katika mazingira tofauti. Msimulizi amewahi kusikia kuwa ili kuruhusiwa kuingia mzimuni, lazima mtu aimbe wimbo fulani ndipo mizimu imruhusu kuingia. Akiwa kando ya msitu, anausikia wimbo huo ukiimbwa na mwanamume, na baada ya muda unajibiwa na mwanamke. Anaukariri wimbo huo na hatimaye kuuimba kesho yake kabla ya kuingia mzimuni.
Maudhui zaidi katika hadithi ni pamoja na Unafiki, Uzinzi, Ujinga, Migogoro, Jinsia na Ulevi.
Wahusika: Sifa na Umuhimu Msimulizi
Ni mdadisi. Kina anapopata sifa mpya ya Mzimu wa Kipwerere, lazima aulizie kwa wazee. Anaulizia sababu ya kuona taa huko usiku, harufu ya tumbaku kutoka huko na sauti za chini kwa chini zinazosikika.
Ni jasiri. Badala ya kuogopa kutokana na sifa za Mzimu wa Kipwerere, yeye anataka kujua zaidi kuhusu mzimu huo, hata ikigharimu maisha yake! Yuko tayari hata kukutana na shetani wa mzimu ana kwa ana!
Ni mpelelezi. Kila mara ana nia ya kujua kuhusu mzimu unaoogopwa na wanakijiji. Anaukaribia kila mara na kutafuta mbinu za kuingia huko wakati mmoja ili kujua kilichopo. Anakaribia na kuujua wimbo unaodaiwa kutumika kama ufunguo. Hatimaye anaingia msituni akiwa na tochi kuona kilichomo.
Ni mkakamavu. Haachi nia yake ya kuwaona shetani wa mzimu. Licha ya yote anayoambiwa na wazee na imani zinazowaogofya, anashikilia msimamo wa kuingia humo hadi anapotimiza azma yake.
Ni mwenye akili pevu. Anawaza kwa haraka na kutekeleza mawazo. Anaposikia watu wakija mzimuni, anazima tochi na kujificha chini ya kitanda. Anajua hawawezi kutarajia yuko humo. Bishoo anapoelekea kuwasha taa, anatokeza na kupiga ukemi, akijua wazi atawashtua.
Umuhimu wa Msimulizi
Ni kielelzo cha ujasiri na umuhimu wake katika jamii.
Anadhihirisha migogoro kati ya watoto na wazee hasa kuhusiana na masuala ya utamaduni. Kupitia kwake, mchango wa watoto katika kujenga na kuboresha jamii unadhihirika.
Anadhihirisha umuhimu wa upelelezi katika kuwafichua wahalifu.
Salihina
Ni mnafiki. Anajitia uzuri wa kiuongozi kumbe ni kazi bure. Anaongoza matambiko ya kijamii na kuwaombea watu Baraka kwa mizimu. Upande mwingine, analangua mihadarati na kufanya uzinzi kwenye mzimu.
Ni laghai. Anatumia nafasi yake kama kiongozi kulangua mihadarati. Anawajaza watu imani ya kuwepo kwa mizimu ili wasiingie msituni, ambamo anaficha shehena za mihadarati.
Ni dhalimu. Anawakataza watoto wa kiume na kike kutangamana katika michezo. Msimulizi anapokezwa viboko kumi bila kuambiwa kosa lake, eti kwa sababu tu alisimama karibu na msichana.
Ni mwenye tamaa. Tamaa inamsukuma kulangua dawa za kulevya ambazo ni marufuku katika kijiji hiki. Pia ana tamaa ya kumlaza Bishoo licha ya kujua ana mume.
Ni mzinzi. Anakutana na Bishoo msituni ili kupanga mikakati ya ulanguzi. Zaidi ya hayo, wana ajenda yao ya ‘kusakata rumba’. Hata wana kitanda mle msituni wanachotumia kutimiza ashiki yao.
Ni msaliti. Anasaliti wanakijiji wanaomwamini na kumheshimu kwa kuwaendea kinyume. Anasaliti utamaduni wa jamii kwa kuutumia kuendeleza uhalifu. Anamsaliti msimulizi kwa kumpiga bila hatia.
Umuhimu wa Salihina
Ni kiwakilishi cha uozo uliokithiri katika jamii.
Kupitia kwake, uhalifu unadhihirika na ujanja unaotumiwa kuuendeleza.
Ni kiwakilishi cha mila na itikadi zilizopitwa na wakati na jinsi zinavyoangamiza jamii. Kupitia kwake, utapeli wa viongozi na watu wanaoaminiwa katika jamii unadhihirika. Kupitia kwake, mgogoro kati ya watoto na wazee na pia ujadi na usasa unabainika wazi. Bishoo
Ni laghai. Anamuaga mumewe kuwa anaenda kumwona mtoto wa jirani ambaye ni mgonjwa, lakini ukweli ni kuwa anaenda kumwona Salihina.
Ni mjanja. Anatumia ujanja kulangua dawa za kulevya kwa kudai kuwa ni shughuli za kuwachotea shetani wa mzimu maji.
Ni mzinzi. Licha ya kuwa ana mume, anahusiana kimapenzi na Salihina kwenye Mzimu wa Kipwerere.
Ni mwoga. Msimulizi anapochomoka chini ya kitanda na kupiga kelele, anaanguka na kuzirai.
Umuhimu wa Bishoo
Kupitia kwake, uhalifu katika jamii unadhihirika na jinsi unavyoendeshwa. Ni kiwakilishi cha wanawake na nafasi yao katika kuporomosha jamii.
Kupitia kwake, uozo katika jamii unadhihirika kwa mapana.
Mbinu za Uandishi. Tashbihi
Mzimu wa Kipwerere ukitisha kama samba.
Alikuwa mkubwa…na mkali mithili ya simba jike anayenyonyesha watoto wake.
Kwa bahati mbaya, kuingia kwenye mzimu ule hakukuwa rahisi kama kucheza ngoma ya vanga, mduara au mchiriku.
Nilivaa guo jeupe lililonigubika gubigubi kama maiti. Nikawa kama dubu tu.
Kisha…nikajivurumisha mvunguni mwa kitanda kile chenye matendegu marefu kama miguu ya punda kirongwe. Nikakaa kimya na kutulia tuli kama ninyolewaye!
Masikio yangu yalivuka kichwa kwa kumwogopa bwana yule, yakawa kama masikio ya sungura aliyeiba mazao shambani.
Imani yake kali ilimvuka kama hondowea iliyokatika mpira kwenye mwendo.
Nilijitokeza mle mvunguni na maguo yangu meupe kama maiti nikaangua mwangwi mkali mfano wa parapanda siku ya kiama.
Maneno yale yalikuwa kama mkuki kwa watu wale wawili niliowashika ugoni.
Istiara
Yaani kile kitendo cha kichaka kile kuitwa mzimu tu kilikuwa homa ya jiji na shetani tosha. Na hapo…ufike majumbani ambako guo la hofu, hatimaye litakuvuka.
Yakaja kunifika makubwa ya mgeni kuacha chai akanywa masimbi ya chai.
Pia nilitaka nihakikishe kuwa hakuna shetani yeyote kati ya wale wawili, atakayeiona sura yangu…
Semi na Nahau
kukata kiu- kumaliza hamu.
alikuwa mstari wa mbele- alisisitiza zaidi, alikuwa wa kwanza. Alikataa katakata- alikataa kabisa.
yamepigwa marufuku- yamekataliwa, yameharamishwa. hatua kwa hatua- kwa utaratibu.
Nikaupiga moyo wangu konde- nikajipa ujasiri, nikaamua. Kufa au kupona- kwa vyovyote vile, lije litakalokuja.
ana kwa ana- kuonana kwa macho. nitatiwa nguvuni- nitakamatwa.
kwa mapana na marefu- kwa kiwango kikubwa.
Kinaya
Salihina anampiga msimulizi viboko kumi anapopata habari alisimama karibu na msichana. Ajabu ni kuwa yeye mwenyewe anashiriki uzinzi, tena na mke wa mtu.
Katika kijiji hiki, yasemekana kuwa kileo chochote aina ya tumbaku ni marufuku na kinaweza hata kugharimu maisha ya mtu. Kubwia unga na kunywa pombe pia ni makosa ya jinai. Ajabu ni kuwa kijiji chenyewe bado kinaongoza kwa uingizaji, usambazaji na utumiaji wa dawa hizi za kulevya.
Visa vya mizimu na mashetani vinaenea kijijini na kuwatia watu woga. Kinyume ni kuwa, msimulizi anaingiwa na udadisi badala ya woga, na hata yuko tayari kukutana na mashetani hao ana kwa ana!
Baada ya wale watu wawili wanaoimba kuingia mzimuni, harufu ya tumbaku inatokea. Msimulizi anasema kuwa hana shauku kwani anajua shetani huvuta sigara. Ajabu ni kuwa uvutaji huu ni marufuku. Swali kuu ni je, mbona shetani wa mzimu wavute tumbaku hali watu wanakatazwa kuvuta?
Salihina anapoambiwa na Bishoo mpango wa kubeba mihadarati kutoka msituni, anasema kuwa watu watafanya kazi hiyo takatifu kwa uadilifu. Kinyume ni kuwa si kazi takatifu bali uhalifu na ulaghai.
Maswali Balagha
Sasa ikiwa kichaka hiki kilipata sifa na cheo cha kuitwa mzimu wenye giza nene ndani, kwa nini kitishe kiasi hicho?
Je, kwa hali hiyo, mtu wa kawaida kichwa mchungwa, ataacha kuogopa?
Kwa nini mashetani wa mzimu wawe wanaogopwa na kila mtu ilhali hawawezi hata kujenga nyumba ya miti na udongo ya kukaa?
‘Rhumba bila kulewa, utalichezaje rhumba?’
Chuku
Woga ambao ukiweza kukupata hapa kwa kujitia hamnazo au kujitia ujabari wa kujipitisha haukuishia kwenye moyo tu, bali ulikuwa woga ulioweza kukutia maradhi hata ya senene,…
Kwa umbile lake hili, ilikuwa yumkini kuamini mle ndani ya kichaka mlikuwa na giza nene kuliko lile giza la kaburini.
Butwaa ambalo kwa hakika liliifanya akili yangu isimame kufikiri kwa muda wa sekunde kadhaa. Hapo masikio yangu yalivuka kichwa kwa kumwogopa bwana yule…
Taharuki
Mwanzo unatutia hamu ya kujua zaidi. Tunaambiwa kuwa Mzimu wa Kipwerere unatisha kila mtu, hata wenye ujasiri. Tunapata hamu ya kujua huu mzimu ni upi, tena kwa nini utishe kiasi hicho.
Msimulizi anapojibiwa kuhusu sifa za shetani, yeye anaingiwa na udadisi na kutafuta upenyu wa kuingia msituni. Ni hamu kuu kujua iwapo atafanikiwa na iwapo atakutana na shetani hao. Pia, tuna hamu ya kujua iwapo ni mashetani na mizimu wa kweli walio mle msituni.
Katika kijiji hiki, tunaambiwa kuwa matumizi ya mihadarati ni marufuku. Hata hivyo, bado kinaongoza kwa matumizi hayo. Anayesambaza hajulikani. Tuna hamu kuu ya kujua anayeshiriki haya.
Msimulizi anausikia wimbo ukiimba wakati yuko nje ya msitu. Mwanamume anaanza na kujibiwa na mwanamke. Tuna hamu kuu ya kujua hawa ni kina nani na wana uhusiano gani na mizimu na mashetani.
Mwishoni pia, tunabaki na maswali kadhaa. Ni hatua gani ambayo wanachukuliwa Salihina na washirika wake. Anasema kuwa hayuko peke yake katika hilo. Anashirikiana na nani? Mumewe Bishoo naye anamchukulia hatua gani, na mengine.
Sadfa
Inasadifu kuwa watoto wanacheza karibu na msitu wanaposikia sauti za chini kwa chini.
Wakati msimulizi yuko kando ya msitu, anawazia jinsi ya kujua wimbo unaosemekana kuwa ufunguo wa kuingia msituni. Kisadfa, wakati huo huo anausikia ukiimbwa na watu wanaoingia humo baadaye.
Msimulizi hatimaye anafaulu kuingia msituni na kushuhudia yanayotukia humo. Wakati anapomulikamulika mvunguni mwa kitanda, anausikia wimbo na kujua watu wanakuja.
Wakati msimulizi akiwa mvunguni mwa kitanda, Bishoo anachukua kiberiti tayari kuwasha taa. Hili linamlazimisha msimuliza kujitokeza kabla ya kupatikana.
Salihina anapotoroka, anakamatwa na tawi la mti kisadfa. Anafikiri kuwa ni msimulizi aliyemkamata na kuanza kupiga kamsa akimwomba radhi.
Methali
Lisemwalo lipo
Kamba hukatikia pabovu
Nyimbo
Wimbo wa Mzimu wa Kipwerere. Unaimbwa na Salihina na Bishoo kabla ya kuingia msituni. Unadhihirisha utamaduni wa jamii na pia ulaghai.
Wimbo wa kidumbaki anaoimba Salihina wa Rhumba. Wimbo huu unadhihirisha ashiki yake ya kimapenzi kwa Bishoo.
Koja
Msitu wenyewe ulikuwa wa kichaka kidogo cha miti mseto ikiwemo mibungo, mipera, mipendapendapo, mipo na miti lukuki ya makamo.
Kusini, mashariki, magharibi na kaskazini ya kichaka hiki…
Tabaini
Si mchana si usiku.
Hadithi Ndani ya Hadithi
Hadithi ya Kipwerere, anayesemekana kuwa jamaa wa Bwana Msa aliyepata shetani aliyefichua damu enzi za ujalihiya. Kisa hiki kinahusiana na Mzimu wa Kipwerere, kwani inaaminika alipozikwa ndipo msitu huo umemea.
Mbinu nyingine ni pamoja na Tashihisi, Utohozi, Kisengerenyuma, Dayolojia, Taswira, Takriri na
Mdokezo.
Kila Mchezea Wembe- Pauline Kea Kyovi Mtiririko
Hadithi ni barua kutoka Hospitali ya Uhai ni Neema inayoandikiwa Emmi na mpenziwe, Tembo. Nia kuu ni kuomba msamaha huku akimweleza mwenziwe yaliyomsibu, akikiri makosa yake. Bado yuko kitandani, japo ameimarika kidogo. Anaweza kusema kwa kulazimisha na chakula kinapita kooni, ila hajadiriki kuona. Maisha humo ni mazito upande mmoja na mepesi upande mwingine. Ni mazito kutokana na upweke na kejeli za wanaopita huko, ambao wanasema watafariki tu kama hao wengine. Ni mepesi kutokana na marafiki wa hospitalini kama muuguzi Nasir, anayemhudumia kwa utu, na Bwana Salim, mwathiriwa mwenzake anayempa tumaini kila uchao. Hata ndiye anamtia shime na kumsaidia
kuandika barua. Salim ameimarika haraka, anafikiri sababu ya mapenzi kutoka kwa aila yake ambao wanamiminika kumwona. Yeye(Tembo) amevunja muamala na watu sababu ya ulevi, hata wazazi wake.
Kaka na dada pia wanamtema baada ya kuleta vurugu katika mazishi ya mpwake. Anatamani angeweza kusema siku ya mwisho ya Emmi kumtembelea, na anakumbuka malalamishi yake aliyosikia kwa mbali. Anashangaa kwa nini hakubadili mienendo, kuacha pombe, tamaa na anasa licha ya kumwonya, kuitelekeza familia, kutowapa heshima licha ya kuonywa na majirani. Anamwona alivyojiponza, huku akimwomba talaka. Hata yuko radhi kuwalea wana. Tembo alisikia hayo tu, akatamani amwombe radhi lakini bila mafanikio. Anamwomba akivumilie kisa chake wanavyovumilia Salim, anayekiandika, na Mwanaheri, shemejiye ambaye ako tayari kupeleka barua hiyo kwa Emmi.
Siku ya maangamizi, aliamshwa saa nne na mkewe kuamsha kinywa. Baada ya kumaliza kiamsha kinywa saa sita, aliondoka bila kuaga mkewe, aliyekuwa jikoni akichoma mahamri. Alielekea mtindini, akapata walevi wamejaa japo mazingira ni mabovu. Walikunywa kwa kikoa. Ghafla, Moshi akaanguka na kuanza kufafaruka. Kila mtu akatoroka. Alipata taarifa Moshi alifia hapo hapo, na mama pima yu korokoroni.
Licha ya kujua pombe ya mama pima ni haramu, waliinywa sumu hiyo kwa hiari. Pombe hiyo ndiyo imempofusha na labda kumfanya hanithi. Uchunguzi umedhihirisha ilitiwa dawa ya kuhifadhia maiti. Mapipa hayo pia yalipatikana vitu kama panya wa kuoza, nyoka wafu, sodo na nguo za ndani.
Tembo na wengine walielekea kuzima kiu kwingine. Waliburudika kwa pombe ya watu wa kima cha chini na kuingia jukwaani. Msichana aliyejiremba alimjia Tembo na kumrai wacheze naye akakubali.
Aligutushwa na sauti nyembamba ikimwamsha huku akitikiswatikiswa. Akajipata na mwanamke aliyezeeka, mwenye sura ya kutisha. Hakuwa na mguu mmoja, tena kichwani kulikuwa vinyoya vyeupe vya kuhesabu. Walikuwa kwenye chumba cha udongo kilichoezekwa kwa mabati machakavu yenye matundu. Aliwaza jinsi ya kujiopoa lakini hakuwa na namna. Akasaili sababu yake kuwa hapo. Angeelika, au Anji kama alivyojiita akamwambia walikuja pamoja baada ya dance, tena yuko kwenye safe hands.
Alidai malipo kwa Tembo kwa ajili ya huduma aliyompa.
Aligundua amejifunga kanga. Akaendea suruali yake iliyoanikwa kwenye kamba, akatoa pochi, lakini halikuwa chochote. Akaunti ya simu pia haikuwa na kitu. Akachimbua kwenye soksi na kumtolea Anji salio la mshahara wake na kumpa. Aliondoka na kutembea kwa miguu hadi nyumbani. Baada ya kufika nyumbani, mkewe alimwamkua na kumwandalia kiamsha kinywa. Anatamani mkewe angemwuliza atokako wasawazishe mambo. Kwa kuhofia matokeo, aliamua kunyamaza. Anaamini unyende wa mkewe baada yake kuvua mavazi na kulala ndio ulimwokoa. Alipousikia, alijaribu kuinuka lakini akakosa nguvu. Emmi akaja ameshika nguo zake, alama za midomo Tembo hajui zilifikaje hapo. Mkewe aligundua hali yake ilihitaji dharura ya matibabu. Anamshukuru kwa kujasirika kuokoa maisha yake. Sasa anamhitaji ili kuwa mfano kwa wanaochezea pombe. Anapojitambua, anataka kujitoa uhai lakini kisa cha Salim cha mhudumu na mkufu kinamghairishia nia.
Tembo amejifunza mengi. Amejua ukatili wa dunia na jinsi inaweza kumtenda mtu. Hana hanani. Anamwachia mkewe shamba lake. Hajui iwapo mkewe hajatwaliwa na maharamia. Licha ya hali yake, anaamini ana thamani mbele ya wampendao wala hatakata tamaa. Anamwomba Emmi amsaidie, yuko radhi kubadilisha tabia. Anamwomba mkewe asalimie ndugu na watoto wao, na akiweza awalete awaone, afarijike. Anamalizia kwa kutaja anampenda.
Ufaafu wa Anwani ‘Kila Mchezea Wembe’
Ni ufupisho wa msemo ulio kwenye leso ya Bikizee kuwa ‘Kila mchezea wembe hujikata vyanda vyake’. Ina maana kwamba yeyote ambaye anachezea hatari huathirika kutokana na hatari hiyo.
Msimulizi yuko hospitalini, hata uwezo wa kuandika hana. Salim ndiye anamsaidia kuandika. Hana uwezo wa kuona. Bado mipira mikononi inatona maji japo ya pua ametolewa. Hana uwezo wa kuona. Hizi ni ishara za kujikata vyanda baada ya kuchezea wembe kwa kunywa pombe haramu. Salim pia ni mwathirika mwenzake.
Tembo anakumbuka wimbo wa watribu, ambao unasema kuwa janga la kujitakia halifanyiwi matanga. Ni muhimu kutia makini ili kuepuka vitimbi vya dunia. Maisha yanaweza kukupa fahari sasa, kesho yakakutema. Wimbo huu unaonya dhidi ya ‘kuchezea wembe’.
Tembo pia anachezea wembe kwa kutowaheshimu wanafamilia yake. Hana ukuruba na wazazi wake. Dada na kaka zake pia wanamtema anapozusha vurugu kwenye mazishi ya mpwa wake. Hali hii inamfanya kukosa watu wengi wa kumtembelea. Anaona kwamba Salim anaimarika vyema kwa kutembelewa na watu wengi wa familia wanaompa tumaini. Tembo anahisi anastahili pigo hili.
Tembo anakumbuka malalamishi ya mkewe anapokuja kumwona. Analalamikia tabia za mumewe ambaye anajitia bingwa wa ulevi, tamaa na anasa, hali ambayo inamletea madhara. Hata anataka ampe talaka aweze kupumzika. Yuko katika hatari ya kumpoteza mkewe kwa ‘kuchezea wembe’.
Moshi anachezea wembe pia kwa kubugia pombe haramu. Anaanza kufafaruka akiwa huko na hatimaye anaaga hapo hapo.
Mama pima anachezeawembe kwa kushiriki biashara haramu ya kuuza pombe. Imetiwa dawa ya kuhifadhia maiti na inaleta madhara. Hatimaye anaishia korokoroni.
Tembo anachezea wembe kwa kukubali kucheza densi na msichana kwenye baa. Anapogutuka, anajipata chumbani mwake Bikizee wa kutisha, kanga kiunoni. Analazimika kumpa salio la mshahara wake na kwenda nyumbani kwa miguu.
Emmi pia anachezea wembe kwa kuolewa na mlevi chkari. Anapitia mengi mikononi mwake. Analazimika kuwalea watoto peke yake na kumhudumia Tembo anayelewa kila mara na kuwatelekeza.
Dhamira ya Mwandishi
Kutoa onyo kwa wapiga maji haramu kuhusu madhara yanayoweza kuwakuta. Anadhihirisha matatizo ya ndoa na malezi yanayosababishwa na ulevi.
Anasawiri umuhimu na nafasi ya matibabu katika kuendeleza uhai kwenye jamii.
Anadhamiria kutoa tumaini kwa walio katika hali tata za kiafya na kijamii kuwa si mwisho wa maisha. Kudhihirisha umuhimu wa uhusiano/ukuruba mwema na watu wengine, hasa familia.
Kuonya kuhusiana na biashara haramu ambayo inaweza kumwangusha mhusika mikononi mwa sheria. Anadhihirisha nafasi ya mapenzi na ndoa kama asili ya tumaini kwa wahusika.
Anadhihirisha umuhimu wa kufaana hasa wakati wa dhiki.
Maudhui Migogoro
Nia kuu ya Tembo ni kumwomba msamaha mkewe kwa migogoro yao ya awali. Anakumbuka malalamishi yake mara ya mwisho anapokuja kumwona. Analalamikia tabia yake ya kupotea kila mara, tena hafanyi lolote kwa ajili ya familia yake. Hata anamwomba ampe talaka, yuko tayari kuwatunza watoto, kwani amezoea tayari. Tembo anatamani angepata uwezo wa kumwomba radhi wakati huo.
Anakumbuka siku ya maangamizi. Mkewe anamwamsha mwendo wa saa nne ilia apate staftahi. Anamaliza kuamsha kinywa saa sita. Anaambiwa mkewe anachoma mahamri jikoni lakini anaondoka bila kuaga. Anahofia kujibu maswali kuhusu wapi aendapo.
Walijipata tena kwenye mgogoro baada yake kurudi nyumbani siku iliyofuata. Mkewe anamwandalia chamcha, naye anavua mavazi na kujitupa kitandani. Anasikia ukemi wa mkewe, huku ameshika nguo zake zenye alama za rangi ya midomo. Anajua ana maswali ya kujibu lakini hali yake hairuhusu. Mkewe anamshughulikia kupata matibabu.
Tembo pia anajikuta kwenye mgogoro na Angelica kwenye chumba chake anapogutuka. Hajui kafikaje humo, tena Bikizee huyu anatakaje. Anatamani kutoroka lakini hana namna. Anji anadai malipo kwa huduma zake. Analazimika kuzoa salio la mshahara wake kwenye soksi na kumpa ili kujiopoa. Anji anasema atampeza lakini Tembo hanuii kuwahi kuonana naye tena. Analazimika kutembea hadi nyumbani, mwendo wa saa nzima.
Emmi anapomtembelea pia, analalamikia migogoro ya mumewe. Anapolewa anarudi nyumbani na maudhi, matusi na vipigo tu. Analalamika kuwa hawaheshimu yeye na watoto wake, wazazi wala wakwe, na hata majirani.
Tembo pia ana mgogoro na familia yake. Hana ukuruba na wazazi wake. Dada na kaka zake wanamtema anapozua vurugu kwenye maziara wakati wa mazishi ya mpwa wake. Hivi, hapati watu wa kumtembelea hospitalini kama rafikiye Salim.
Starehe na Anasa.
Emmi anashangazwa na tabia ya Tembo ya kujistarehesha kwa anasa za pombe. Anamkumbusha kuwa anasa za dunia hii hawezi kuzimaliza. Anajitia bingwa wa dunia na kusahau alikotoka, hali ambayo inamletea madhara na kumlaza hospitalini.
Siku ya kisanga kikuu, Tembo anaamshwa na mkewe kunywa staftahi. Anapomalizia saa sita, anamhepa mkewe na kuelekea kujistarehesha mtindini. Anawapata wenzake huko na wanakunywa kwa kikoa. Kila mmoja ana zamu ya kununua pombe.
Hata baada ya kituko cha Moshi, bado Tembo na wenzake wanaelekea kuzima kiu kwingine. Wanakunywa pombe ya kima cha chini wanayoweza kununua. Baadaye wanaingia jukwaani kusakata densi.
Tamaa ya anasa inamfanya kukubali rai ya msichana anayetaka kucheza naye, lakini anamgeuka baadaye. Kumbe ni Bi. Kizee aliyejipodoa. Anajipata mikononi mwake, ambapo anajinasua kwa kulipa salio la mshahara wake kwa ajili ya huduma alizopewa.
Mapenzi na Ndoa.
Ndoa kuu katika hadithi hii ni kati ya Tembo na Emmi. Inakumbwa na misukosuko kadha wa kadha. Wamejaliwa wana ambao hata Tembo hajui wanakula nini. Amewatelekeza kabisa. Mkewe hata anamwomba ampe talaka, yuko tayari kuwalea watoto wao pekee yake.
Tembo anaamshwa na mkewe asubuhi ya saa nne ili kupata kiamsha kinywa. Anapomaliza saa sita, anaondoka bila kumuaga, akihofia kuulizwa maswali kuhusu kule anakokwenda. Hana mapenzi ya dhati kwa mkewe wala hamjali.
Tembo anaporudi nyumbani kutoka kwenye mtindi, anavua nguo na kulala. Anagutushwa na ukemi wa mkewe. Amebeba nguo zake zenye alama za midomo. Kabla ya kumsaili, anagundua anahitaji dharura ya matibabu na hapo anamshughulikia mara moja. Tembo anamshukuru kwa hilo.
Dhamira kuu ya barua hii ni Tembo kumwomba msamaha mkewe. Anamwachia shamba lake lenye rutuba. Anahofia huenda amenyakuliwa na maharamia. Anahisi kwamba ndiye tu amebaki, akimwomba arejee kwake ili kumpa tumaini. Anamtaka kuwasalimia nduguze na wanawe, na hata awalete apate kuwaona afarijike. Anatamatisha kwa kusema anampenda.
Ulevi
Tembo amezama katika ulevi na ndio unamletea madhara yote aliyo nayo. Hana uwezo wa kuona. Yuko hospitalini hali hoi. Salim pia yuko hospitali hiyo hiyo, ni mwathiriwa mwenzake.
Anapoamshwa na mkewe, Tembo anakunywa staftahi hadi saa sita kisha kuondoka bila kumuaga mkewe anayechoma mahamri jikoni. Anahofia maswali ya wapi anaenda kwani anajua anaelekea kwenya anasa za ulevi. Anapofika huko anawapata wenzake wanaokunywa kwa kikoa, kila mmoja akichangia zamu yake. Mazingira wanapolewa yanatia kinyaa lakini kwao si hoja.
Pombe inasababisha mauti ya Moshi. Wakiendelea kunywa, anaanguka ghafla na kuanza kurusharusha miguu na kugaragara chini huku povu likimtoka. Hatimaye anafariki hapo hapo. Inagunduliwa kuwa pombe waliyokunywa ilitiwa dawa ya kuhifadhia maiti, tena ilikuwa na maajabu kama panya wa kuoza, nyoka wafu, sodo na nguo za ndani.
Tembo anakiri kwamba pombe hiyo, ambayo inapatiwa majina kama chang’aa, tear gas, moshi na mengine ni sumu, ambayo wanatoa pesa zao kuinunua, tena kwa hiari yao. Hana huruma kwa mama pima aliyetupwa korokoroni. Anaiona kuwa stahiki yake.
Licha ya kisanga cha Moshi, bado kiu ya pombe haiwaruhusu kupata hofu. Tembo anaandamana na wenzake kuzima kiu yao kwingine. Huko, wanalewa na kuanza kucheza densi. Anaanguka mtegoni wa Angelica, ambaye anamfyonza salio lake la mshahara kwa huduma za chumbani.
Kutokana na ulevi, hata hagundui kwamba nguo zake zina alama ya midomo, wala hajui zilifikaje huko. Anapomsikia mkewe akipiga ukwenzi, ndio kwanza anagundua, na anajua ana maswali ya kujibu. Hata hivyo, mkewe anagundua anahitaji dharura ya matibabu na kumsshughulikia. Haoni, magoti hayana
nguvu, mishipa ya damu nayo inazizima. Tembo anasema waliolala bila kuamshwa hawajaamka hadi leo, wengi wamefukiwa.
Majuto
Tembo anapoandika barua hii, yuko katika hali ya majuto makuu. Anakiri kwamba yeye ni mkosa na yuko tayari kuomba radhi, wala hana la kujitetea. Hajabanduka kitandani, hana uwezo wa kuona, bado anapigania uhai wake. Anayahisi maisha kuwa mazito kwa kukosa imani kwa watu wanaopita huko na kudai kuwa watajifia kama wenzao tu.
Anajuta pia kwa kukosa uhusiano mzuri na familia yake. Hapatani na mama wala baba yake, kutokana na utepetevu wake anapochapa mtindi. Kaka na dada zake pia wanamtema anapozua vurugu kwenye maziara wakati wa mazishi ya mpwa wake. Anaona aibu anapokumbuka haya. Anahisi alistahili pigo hili.
Anajutia ulevi wake. Anamwambia Emmi kwamba alikunywa sumu. Ndilo jina analoweza kuita pombe hiyo haramu. Licha ya kufahamu ni haramu, bado wananunua na kuinywa pombe hiyo, tena kwa hiari yao. Ndiyo inamwangusha katika hali aliyo.
Anajuta pia anapojipata kwenye chumba cha Angelica. Hajui alivyofika hapo, kwani alikuwa amelewa kabisa. Anatamani kutoroka lakini hawezi. Anajiokoa kwa kumpa salio la mshahara wake aliohifadhi kwenye soksi. Analazimika kurudi nyumbani kwa miguu.
Anajutia kufumbiwa kinywa na mke wake anapofika nyumbani. Anahisi kwamba ingekuwa afadhali kama angempa kisa hiki wakati huo, labda wangeweza kusawazisha mambo. Kwa kuhofia hatima yake, yeye alihiari kufumba kinywa.
Ulaghai
Mamapima anawalaghai wanywaji wa pombe yake. Anawaandalia pombe na kuitia dawa ya kuhifadhia maiti. Haijatajwa kwa nia gani. Pia kunapatikana kwenye mapipa yake panya wa kuoza, nyoka wafu, sodo na suruali za ndani. Inasababisha kifo cha Moshi na wengine na kumpofusha tembo.
Angelica pia anamlaghai Tembo. Anamwomba wacheze densi lakini baadaye, Tembo anagutuka kwenye makazi yake, huku amefungwa kanga kiunoni. Pochi lake halina hata ndururu. Analazimika kumlipa Anji kwa salio la mshahara wake alilohifadhi kwenye soksi. Pia, anaingia jukwaani huku amejiremba vilivyo ili kuficha sura yake ya kutisha.
Maudhui mengine ni kama vile Ufuska, Sheria, Uwajibikaji, Usaliti na Mauti/Kifo.
Wahusika: Sifa na Umuhimu. Tembo
Ni mlevi. Anaelekea kwenye mtindi kila mara na kumpuuza mkewe na wanawe. Ulevi ndio hatimaye unamlaza hospitalini na kumpofusha. Hata anahofia umempoka ujogoo wake.
Ni mgomvi. Anapolewa, anagombana na kila mtu na kuvuruga mahusiano yake na watu. Wazazi wake washamtema kitambo. Dada na kaka zake walimtema baada ya kuzua vurugu kwenye mazishi ya mpwa wake. Anagombana pia na mkewe na majirani.
78
Ni mvivu. Siku ya maangamizi, mkewe anaelekea kumwamsha kwa ajili ya kiamsha kinywa mwendo wa saa nne. Anamaliza kuamsha kinywa mwendo wa saa sita mchana.
Ni asiyewajibika. Anawatelekeza mkewe na wanawe wala hata hajui walacho. Mkewe anapomtembelea hospitali, anashangaa vipi anajidai kuwa na watoto hali hajui walacho. Hawajibikii matendo yake, jambo linalomletea mikasa.
Ni mwenye majuto. Anajutia matendo yake ya awali, ambayo yanamwathiri pakubwa. Anajutia uhusiano wake mbaya na familia yake, anajutia madhila yake kwa mkewe na kumwomba msamaha.
Ni mpenda anasa. Anapoamshwa na mkewe na kupata kiamsha kinywa, anaondoka kwenda kuvinjari kwenye mtindi. Anamhepa mkewe kuepuka maswali. Hata baada ya kisanga cha Moshi, bado wanaelekea mahali pengine kukata kiu. Wanalewa na kuingia ukumbini kusakata densi.
Umuhimu wa Tembo.
Kupitia kwake, madhara ya ulevi yanadhihirika.
Ni kiwakilishi cha wanaume wanaopuuza familia zao na kujizika katika ulevi na anasa. Ni kielezo cha watu wanaokiri makosa yao na kuomba msamaha wanapokosa.
Kupitia kwake, nafasi na umuhimu wa ndoa katika jamii unadhihirika. Kupitia kwake, nafasi ya matibabu katika kusaidia wanajamii inadhihirika. Emmi
Ni mvumilivu. Anavumilia vituko vingi vya mumewe bila lalamalalama. Kila mara, mumewe ni mlevi kupindukia wala hawajali. Analazimika kutunza watoto wao peke yake lakini anavumilia.
Ni mwajibikaji. Anatekeleza wajibu wake. Siku ya maangamizi, Tembo anakumbuka ndiye alimwamsha, tayari kamwandalia kiamsha kinywa. Akiondoka, Emmi alikuwa jikoni akichoma mahamri. Ndiye analea watoto mumewe anapozama kwenye pombe. Anapogundua hali ya mumewe, anamshughulikia kwa dharura.
Ni mwenye utu. Licha ya matendo yote ya mumewe, bado anamshughulikia kama mkewe. Anamlisha na kumtafutia matibabu na hata anapokuwa hospitalini, anakuja kumtembelea.
Ni mlezi mwema. Anasema kuwa mumewe hata hajui walacho au kuvaa wana anaowaita wake. Yeye amewalea kwa kila hali, na hata yuko tayari kuwalea iwapo atampa talaka.
Ni mwenye mapenzi ya dhati. Anampenda mumewe licha ya kuwa mlevi. Anamshughulikia kila anapohitajika kufanya hivyo. Anamtembelea hospitalini hali yake ikiwa taabani.
Umuhimu wa Emmi
Kupitia kwake, matatizo ya ndoa yanadhihirika.
Ni kielelezo cha wanawake walezi wema wanaojali wanao waume zao wanapozamia ulevi. Ni kiwakilishi cha nafasi ya mwanamke katika jamii.
Ni kielelezo cha uvumilivu katika maisha licha ya magumu mengi. Ni kiwakilishi cha migogoro katika jamii.
Salim
Ni mshauri. Anamsimulia Tembo kisa cha waumini na mkufu, ambacho kinampa tumaini jipya katika maisha. Anamwambia kuwa hali yake sio mwisho wa maisha na kumwonyesha sababu ya kutokata tamaa.
Ni mwenye utu. Anamsaidia Tembo kila anapohitajika. Hata barua ya kumpa mkewe, ndiye anamwandikia kwani yeye ameshapofuka.
Ni mfadhili. Anamsaidia Tembo kila mara anapohitaji msaada wake. Anamsaidia kwa ushauri na pia kuandika barua.
Ni mlevi. Tembo anaeleza kuwa Salim ni mwathiriwa mwenzake. Hata yeye alidhurika kutokana na pombe haramu.
Ni mwenye imani. Licha ya yote yaliyowakumba, bado anayaona maisha kwa mtazamo mzuri. Anaamini kuwa si mwisho wa maisha, imani ambayo anamjaza mwenzake, Tembo.
Umuhimu wa Salim
Ni kielelzo cha tumaini na imani katika maisha. Anawakilisha nafasi ya matibabu katika kujenga jamii.
Kupitia kwake, umuhimu wa kutokata tamaa licha ya matatizo unadhihirika.
Angalica/Anji/Angel/Bikizee
Ni tapeli. Anamlazimisha Tembo kulipia huduma zake, ambazo hakuagiza. Anampeleka kwake bila idhini yake na kumlazimisha kumlipa.
Ni mzinzi. Anamweleza Tembo kuwa yeye hatoi huduma za ubwete. Tembo anapoamka, amefungwa kanga kiunoni, na suruali yake kuanikwa kwenye kamba. Ni wazi kuwa ni mambo anayofanya Anji kila mara.
Ni mhadaifu. Ni vigumu hata kuamini msichana Tembo anayeona kwenye klabu ni yule yule anayepata kwenye chumba kile. Wa klabuni ni maridadi, tena aliyejiremba, lakini anayejikuta naye chumbani ni bikizee mwenye sura ya kutisha.
Ni mkakamavu. Hampi Tembo upenu wowote wa kutoroka. Anashikilia msimamo wake kuwa lazima amlipe. Hatimaye, anampa salio la mshahara wake alilohifadhi kwenye soksi.
Umuhimu wa Angelica
Kupitia kwake, ukware katika jamii unadhihirika.
Ni kiwakilishi cha wanawake matapeli wanaowafyonza wanaume pesa kwa kutumia ujanja. Anadhihirisha madhara ya ulevi kwa jinsi anavyoutumia kumnasa Tembo.
Anadhihirisha nafasi ya mwanamke katika jamii.
Mbinu za Uandishi.
Barua.
Hadithi hii imeandikwa kama barua kutoka kwa Tembo, aliye kwenye Hospitali ya Uhai ni Neema, kwa mkewe Emmi kwa ajili ya kumwomba msamaha.
Tashihisi
Baada ya hapo, akili yangu haikunakili kingine zaidi. Usiku nao ukawa waingia na kwenyewe kwanyunyuza.
Nimetambua kuwa dunia ni danganyifu. Inaweza ikakutia ugani ikucheze… ikakunyonyoa na kukuacha watetema. Ikakurarua ukawa tambara. Ikakufyonza ukabakia tepwetepwe. Ikakupora kila chote cha
kwako…
Japo maisha yangu yamekanyagwa na kutiwa najisi na tamaa yangu mwenyewe na ghiliba za ulimwengu…
Istiara
Naomba nikuite mpenzi…bado wewe ndiwe waridi la moyo wangu.
Naona heri kukiri makosa na kufanya toba kuliko kuwa mpishi mzembe wa kusingizia moshi apikapo mashendea.
Wingu la hofu, kutamauka, kushindwa na kujiuzulu linapoipamba mbingu yangu, ndiye anihimizaye. Mamapima naye yu korokoroni… Ziraili wao, watoaji roho za watu.
Nilikunywa sumu, Emmi.
Msuko wa filamu yangu hiyo ukaendelea kukunjuka aliposhuka kitandani bi kizee huyo.
Niliogopa kusema kitu labda nichokoze mzinga nishindwe kuyakabili makombora nitakayotupiwa.
Tashbihi
Kila siku saa ikiwadia utawaona kafurika wodi. Ni kama mchwa kichunguuni wanavyokizingira kitanda chake.
Tena kwa mbali kama ambaye niko katika njozi lakini kweli nilisikia malalamishi yako.
Jamaa mmoja almaarufu Moshi alianguka…viputoputo vya hewa vinamtoka kinywani na kufanya povu kama la sabuni ya unga iliyotiwa maji.
Anarusha mateke kama mwenye kuingiwa kifafa. Anafurukuta kama kuku anayetiwa bismilahi. Watu wakatawanyika kama siafu waliomwagiwa jivu la moto.
Rangi ni za kila nui na kila mahali… Kifani chake ni tausi. Kumbe kucheza na pombe ni sawa na kucheza na moto.
Tena meno yake ni rangi ya kahawia, utadhani hutafuna matawi kama twiga.
Hivi kichwani hakuwa na nywele, ni vinyoyanyoya vichache tu tena vyeupe kama chokaa. Anakwenda kwa kurukaruka kama kijizimwi kuelekea pembeni.
Inaweza ikakutia ugani ikucheze kama mpira.
Semi na Nahau
Niliponea chupuchupu- niliponea kibahati. yafisha moyo- yakosesha tumaini.
Ana moyo mkubwa- ana utu.
aliyenitia shime- aliyenihimiza, alinishinikiza. namwonea ghere- namhusudu, namwonea wivu. kupiga mafunda- kumeza kitu kiowevu.
kukutia macho- kukuona.
nikutake radhi- nikuombe msamaha.
atafanya juu chini- atafanya kila awezalo kutimiza jambo. kufungua kinywa- kula chakula cha asubuhi, kustaftahi. nilishika tariki- nilishika njia, nilianza safari.
moja kwa moja- kufululiza, bila kupinda popote.
kiguu niponye- kuondoka mbio sababu ya woga au hofu.
Maji ya kwake tuliyachapa kwa hiari- pombe yake tulikunywa kwa kujitakia. kusakata rhumba- kucheza ngoma.
nivunje kimya- niongee, nimalize kimya.
sikujua alfa wala omega zake- sikujua chochote kuzihusu. sina sinani- sina chochote.
Maswali Balagha
“Jamani mume wangu, hivi wewe huwezi kurekebisha tabia zako?... Hakuna starehe nyingine uliyoona ila kunywa pombe?...”
“Wajitapa una mke na watoto usiojua walacho wala wavaacho?... Majirani na marafiki wamekuusia mara ngapi uirekebishe tabia yako hii, uniheshimu mimi na watoto? Wazazi na wakwe zako pia uwape heshima? Waonaje sasa yaliyokufika kwa huko kujigeuza chachandu wa kujipalia makaa mwenyewe? Hivi wewe kumbe hukumbuki ulikotoka?...”
“Je, ni vipi tutoe pesa za jasho letu wenyewe tununue mauti? Jambo la starehe ligeuke kuwa maombolezo…”
Tangu lini mtu kahifadhiwa ali hai? Nisemeje mimi kama si mazingira haya? Nikashika mfukoni mwa suruali, lakini wapi?
Majazi
Hospitali ya Uhai ni Neema. Ndipo wanapelekwa Tembo na Salim baada ya kuponea kutokana na pombe haramu. Uhai kwao ni neema. Madaktari wanafanya wawezalo kuwasaidia. Wameponea baada ya kubugia pombe iliyowaua wengi.
Tembo. Ina maana ya pombe. Tembo ni mlevi kupindukia. Pia ina maana ya ndovu. Anajiona mwenye nguvu kama ndovu kabla ya upofu kumtuliza.
Moshi. Wingu linalotokana na moto. Hutoweka na kupotea bila kurudi. Moshi anaanguka na kufariki papo hapo, anatoweka kama moshi. Pia ni jina la aina ya pombe haramu, inayomwua Moshi mwenyewe.
Mwanaheri. Ni mwana mwenye heri. Tembo anasema kuwa amejaliwa maumbile mazuri na akili pevu. Pia, ana utu kwani anamwahidi Tembo kuhakikisha barua yake imefika.
Zawadi na Riziki. Wanawe Tembo. Zawadi ni tuzo, kitu anachopatiwa mtu kwa jambo zuri alilofanya. Ni tuzo la ndoa yao. Riziki ni baraka au mafanikio kutoka kwa Mungu. Mwana huyo ni riziki yao. Pia humaanisha mapato ya kumwezesha mtu kuishi. Anamtia mamake shime kutafuta riziki, ana riziki, yaani mahitaji yake yanakidhiwa.
Majengo. Sehemu anayoishi Angelica. Majengo ni wingi wa jingo, yenye maana ya banda au nyumba ya aina yoyote. Kuna jengo analoishi Anji, na haikosi kuna majengo mengine.
Methali
Kuvunjika kwa mwiko si mwisho wa upishi. asiye na mwana aeleke jiwe.
Kila mchezea wembe hujikata vyanda vyake.
Zimwi linijualo, halingenila kunimaliza(zimwi likujualo halikuli likakwisha) Asiyesikia la mkuu huvunjika guu.
Majuto kweli ni mjukuu huja kinyume.
Kinaya
Tembo anaeleza kuwa alizua zogo kwenye maziara wakati wa mazishi ya mtoto wa dadake. Ni kinaya kwake kuzua rabsha katika maziara wakati watu wanaomboleza.
Tembo anasema kuwa walikunywa pombe ya Mamapima kwa hiari, tena kwa pesa zao. Ni kinaya kuwa wanatoa pesa na kuzitumia kujidhuru kwa kupiga maji haramu yanayowaletea madhara.
Baada ya kisanga cha Moshi, ni kinaya kuwa bado Tembo na wenzake wanaelekea kuzima kiu ya pombe kwingine. Badala ya kujifunza kutokana na tukio hilo, haliwapigi mshipa.
Mamapima anasemekana kuwa alitia pombe dawa ya kuhifadhia maiti. Ni kinaya kuitia dawa hiyo kwa pombe itakayonywewa na watu walio hai.
Ulinganuzi kati ya Angelica wa klabuni na wa chumbani unadhihirisha kinaya. Wanapokutana na Tembo, amejiremba kwa marangi na maleba, anapendeza kweli. Anapogutuka kibandani mwake, anakabiliana na Bi. Kizee mwenye sura ya kutisha.
Angelica anasema kuwa watu wanamwita Angel, yenye maana ya malaika. Sura yake hata hivyo, ni kinyume cha jina hilo. Pia, anamwambia Tembo kuwa yuko katika safe hands. Hata hivyo, anamtapeli pesa zake, na pia mwonekano wake unatisha.
Tembo anapoondoka, Anji anamwambia kuwa anatumai watakutana hivi karibuni. Ukweli ni kuwa Tembo wala yeyote yule hawezi tamani kukutana naye tena.
Tembo anatamatisha barua yake kwa kumtaka mkewe awalete wanawe awaone. Ajabu ni kuwa tayari amepofuka, wala hana uwezo wa kuwaona.
Kejeli
Nafahamu fika kuwa ulistahili na unastahili maisha mazuri kuliko yale uliyoishi katika uhusiano wetu huu wa bahati nasibu.
“Hawa hawawezi kupona, watakufa tu hatimaye.”
“Wajitapa una mke na watoto usiojua walacho wala wavaacho?” Hivi sisi ni mizuka tu hatukustahili kuwa hospitalini bali kuzimu.
Kiumbe huyo angeitwa binadamu tu kwa kukosekana istilahi nyingine ya kuafiki sifa zake za kimaumbile. Ama kwa kweli nilikuwa kwenye mikono ‘salama’ si haba.
“pengine tukutane ahera, mwanga we!”
Takriri
Mimi sina neno kwa kuwa sina neno tu. Sina neno la kusema, sina neno la kujitetea wala neno la kulipia deni la neno unalonidai.
Mepesi kwa kuwa nimefanya marafiki humu humu hospitalini. Orodha huwa ndefundefu.
Niliogopa ungetaka maelezo marefumarefu ya kulikoni,…
Emmi… nastahili kuadhibiwa hata zaidi na zaidi.
Naomba uje unipunguzie dhiki, Emmi. Naomba uje unitoe kwenye lindi hili la majaribu , Emmi. Naomba nafasi ya mwisho moyoni mwako, Emmi. Njoo unipoze roho, Emmi. Njoo, ewe faraja yangu, njoo…
Chuku
Akili nyepesi masomoni yenye kunata mafunzo kuliko sumaku. Hali yangu ni kun faya kun. Ninatamani ahera ningali mzima.
Sijapata kumwona adinasi wa kutisha kama huyo. Laiti ungemwona, Emmi! Ungefikiri kuwa mbingu zimeteremka na kushusha viumbe kutoka mwezini au labda Mirihi imekosa falaki na kushuka duniani kumleta Bi. Kizee huyu.
Kiumbe huyo angeitwa binadamu tu kwa kukosa istilahi nyingine ya kuafiki sifa zake za kimaumbile. Tuliite ghofu la mtu. Mifupa yahesabika. Mishipa ya damu imechungulia kwenye ngozi yake chakavu iliyokunjana kama ya ndovu. Anapocheka ndio kabisa utataka ardhi ikumeze. Anafanya maji kukujaa tumboni.
Kwanza meno ni ya kuhesabu. Tena meno yake ni rangi ya kahawia… Harufu inayomtoka kinywani ni ya panya wa kuvunda.
Kama sura mbaya ingalikuwa ugonjwa, kinyanya hiki kingeishi kwenye chumba cha wagonjwa mahututi.
Kijumba ni cha udongo, kimeezekwa kwa mabati mabovu na kilango kina mianya ya kutosha kupita ngamia.
Na ndio maana ya kutamani mbingu ianguke na kunimeza mara moja. Dakika yoyote ile damu ingenikauka mwilini kwa woga. Tayari viungo vilikwisha nilegea. Nahisi mchanganyiko wa kichefuchefu na kizunguzungu.
Mwendo huo wa saa moja ulinichukua robo saa.
Nimetambua kuwa dunia ni danganyifu. Inaweza… Ikakunyonyoa ikakuacha watetema. Ikakurarua ukawa tambara. Ikakufyonza ukabakia tepwetepwe. Ikakupora kila chote cha kwako kwenye hazina.
Koja
Niliogopa ungetaka maelezo marefumarefu ya kulikoni, wendapi, warudi lini… Kuna wa kumi, wa tano, wa mkopo, almuradi…
Pana harufu ya uvundo, mikojo ya walevi, matope, fujo, yaani mchanganyiko maalum. Eti moshi, chang’aa, tear gas, sijui nini.
Rangi ni za kila nui na kila mahali: mdomoni, mashavuni, nyusini, kopeni na nyweleni halikadhalika.
Kuchanganya Ndimi
“Sweetheart, amka!
“I’m Angelica, huku wananiita Angel au Anji…”
“Ondoa wasiwasi mhibaka, you are in very safe hands. Usiulize maswali. It’s okay. Tulikuja sote jana baada ya dance, umesahau hivi?”
“Kama uonavyo, nyumba hii inahitaji maintenance…” “Thank you. U mteja wa kipekee…”
Tabaini
Si panya wa kuoza, si nyoka wafu, si sodo na nguo za ndani.
Hadithi Ndani ya Hadithi.
Kisa ambacho Salim anamsimulia Tembo. Hadithi ya mhudumu na mkufu anaoulizia waumini kama wanautaka, kisha wanaukimbilia hata baada ya kuuangusha, kuuvyoga huku akiusagasaga kwa kiatu na kuutemea mate. Hadithi hii inampa tumaini Tembo na kumwonyesha thamani ya maisha licha ya matukio yanayomkumba.
Kisengerenyuma/Mbinu Rejeshi
Matukio yote yanasimuliwa kwa mbinu rejeshi. Tembo anamwandikia barua mkewe akiwa hospitalini kumsimulia yaliyomkumba katika shughuli za ulevi.
Ushairi.
Tembo anamkumbusha mkewe ushairi(Wimbo) wa watribu wa umuhimu wa kuchunga mtima. Lau angefuata nasaha za wimbo huu, basi haya hayangemkumba.
Mbinu zaidi ni kama vile Nidaa,Utohozi, Jazanda na Mdokezo.
Kifo cha Suluhu- Dominic Maina Oigo. Mtiririko
Abigael na Natasha wanasimuliana masaibu yao yanayowalazimu kuwa kupe wa kunyonya wanaume. Wamekulia eneo moja na kupatana na hali ngumu ya maisha hadi wakakinai. Abigael yuko mwaka wa tatu na kapitia taabu tele. Ameomba na kutafuta misaada, hata kwa gavana lakini hapati. Natasha naye amesoma kwa zaidi ya miaka saba kutokana na ukosefu wa hela. Huku wakila chumbani wanamoishi pamoja, Natasha anamtolea Abigael wazo la kumtilia Suluhu, mpenzi wake wa sasa, dawa ya usingizi ili apate fursa ya kumpora.
Abigael anakutana na Suluhu kwenye chumba cha hoteli na anapomwandalia kinywaji, anamtilia dawa kwa maagizo ya Natasha na kumnywesha. Suluhu anawazia kumshawishi awe mkewe wa kando akipata njia ya kumwangamiza mkewe. Dawa inaanza kufanya kazi na hapo anavamiwa na usingizi mara moja. Abigael anatoa kisu cha makali kuwili kwenye mfuko aliozoea kubeba ambao alinunuliwa na Suluhu, tayari kummaliza. Anaamua kumpora kila kitu kabla ya kumwua. Anatoa kibeti na kupata noti za shilingi mia mbili mbili. Kuna vijikaratasi kadhaa. Kimoja kinasomeka vizuri. Anagundua ni barua na kuamua kuisoma.
Barua inatoka kwa Bi. Suluhu. Anasema anaamua kumwandikia mumewe kwa kuwa amemtenga kabisa. Anamkumbusha kazi yake ya kuuza makaa ilivyofika hatima ya ghafla, kisha akatwaa ubunge kwa mbinu azijuazo Bi. Suluhu. Anajua matendo ya mumewe; msichana wa chuo kikuu aliyemtunga mimba na kumwacha na hawara aliyepangia chumba mjini. Amevumilia kwa ajili ya watoto na kuwalea, na wa kwanza amekamilisha darasa la nane.
Anasisitiza jinsi anavyompenda, wala hajawahi kumwendea kinyume. Zaidi, anamwahidi kuwa hatasema maovu yake. Alimuua mama Abigael akihofia sheria baada ya kunyakua shamba lake. Haleti maendeleo kwa kuwa anawalipa wasichana wa vyuo vikuu baada ya kula nao uroda. Pia anatafuta pesa za kulipa Bwana Ngoma aliyefadhili siasa zake. Anamuasa akome tabia zake kwa kuwa hali yake ni bayana. Bi.
Suluhu yuko tayari kuaga. Anamshukuru kwa mema aliyomtendea kabla ya kubadilika, na yale aliyotendea wazazi wake kuwahadaa anampenda. Anamlaumu mumewe kwa kifo chake anahotarajia kutokana na kukosekana nyumbani na uzinzi, vinavyomletea msongo wa mawazo. Anakiona kifo cha suluhu iwapo kitamfanya mumewe arejee nyumbani kuwatunza watoto. Angeweza kumwua mumewe kwa kumtilia sumu lakini hakuhiari. Anamwomba amkome Abigael asimwambukize nakama. Anaahidi atazidi kumuasa siku alizosalia nazo hata asipomsikia.
Barua hii inamliza Aigael. Amejua kitendawili cha kifo cha mamake aliyepatikana ameuawa. Anakunja karatasi zile na kuzirudisha kibetini. Anajuta kuingilia ndoa ya Suluhu. Anaona kifo cha Suluhu hakitafaa lolote. Kifo kifaacho ni cha maovu na kupalilia utu. Anachukua kisu chake na kuondoka. Anachukua daladala kuelekea chuoni. Anafanya uamuzi wa kutia bidii kujipa riziki na kumwachia Mungu wajibu wa hukumu.
Ufaafu wa Anwani ‘Kifo cha Suluhu’.
Suluhu ina maana ya kusawazisha mambo ili yawe sawa. Pia inaweza kumaanisha kuwa na nguvu sawa. Mada ‘Kifo cha Suluhu’ inaweza kufasiriwa kwa maana tofauti.
Kwanza, kuna mhusika kwa jina la Suluhu. Mada hii inaweza kufasiriwa kurejelea kifo chake. Abigael ananuia kumwua Suluhu ili kulipiza kisasi kwa kumtumia kama tambara bovu na pia ampore pesa zake. Amebeba dawa ya kumtia usingizi na kisu cha makali kuwili kumwangamiza. Kifo hicho hakitukii kwani Abigael anaghairi nia. Anaona kuwa kifo hicho hakitakuwa na maana yoyote baada ya kusoma barua ya Bi. Suluhu. Anamwacha Suluhu usingizini na kuondoka kurudi chuoni.
Mada hii pia inaweza kufasiriwa kwa maana ya kifo cha kusawazisha mambo, yaani kifo cha kuleta suluhu. Natasha na Abigael wanakiona kifo cha Suluhu kuwa suluhu kwa tatizo lao la hela. Abigael anataka kumwua kisha kupora mali yake.
Bi. Suluhu anaona kuwa kifo chake kitakuwa kifo cha suluhu. Kwanza, kitakuwa kikomo cha tabu alizopitia maishani. Pia anasema ni suluhu iwapo kitamwezesha mumewe kurudi kuwashughulikia wanao.
Suluhu anapanga kumshawishi Abigael awe mkewe wa pembeni baada ya kuwazia jinsi ya kumwangamiza mkewe. Anakiona kifo cha mkewe kuwa cha suluhu kwa kuwa kitamwezesha kuwa na Abigael.
Abigael anaposoma barua ya Bi. Suluhu, anaona kuwa kifo cha Suluhu sio suluhu ya aina yoyote. Kifo cha kuleta suluhu ni kifo cha maovu yote katika jamii na waja kukumbatia utu.
Suluhu anamwangamiza mamake Abigael akihofia kuwa atamchukulia hatua ya kisheria baada ya kunyakua shamba lake. Kwa Suluhu, hiki ni kifo cha suluhu, kwani kitamwezesha kumiliki shamba hilo bila matatizo.
Mada hii pia inaweza kutoa maana ya suluhu yenyewe kufa, yaani nia ya kusawazisha mambo kufeli. Kwa mfano, wananchi wanamchagua Suluhu kuwasaidia. Wanamwona kama suluhu ya shida zao. Hata hivyo, kifo cha suluhu yao kinatokea Suluhu anapozamia uzinzi na kuwatelekeza.
Abigael anapania kumwua Suluhu na kupoka pesa zake, jambo analoliona kama suluhu ya shida zake. Hata hivyo, suluhu hii iliyopendekezwa na Natasha kwa shida zao inakufa baada ya Abigael kusoma barua ya Bi. suluhu, inayomfanya kughairi nia ya kumwua Suluhu.
Dhamira ya Mwandishi.
Kusawiri matatizo ambayo wanafunzi wa vyuo vikuu hupitia katika shughuli za masomo, hasa wale waliotoka familia maskini.
Anatoa onyo kwa watekelezao maovu kwamba siku yao ya kugunduliwa itafika.
Kudhihirisha viongozi wasiowajibika wanavyotekeleza maovu na kuwapuuza raia waliowachagua. Anadhihirisha matatizo ya ndoa, hasa ndoa za wakubwa zilizojawa na ufuska.
Kudhihirisha hali ya utabaka katika jamii kwa misingi ya hali za kiuchumi.
Maudhui
Elimu
Abigael na Natasha ni wanafunzi katika chuo kikuu kimoja nchini. Wanapitia hali ngumu kupata masomo kwa kuwa wametoka katika familia maskini. Inawabidi kuwa kupe kwa kuwanyonya wanaume ambao wanawapa uroda.
Wanaishi katika chumba kimoja ili kugawana gharama. Isitoshe, Natasha amesoma chuoni kwa zaidi ya miaka saba kutokana na hali yao ya kimaskini. Wanatamani pia kuwa na maisha mazuri kama wasichana wengine wanaowaona lakini hawana namna.
Abigael anapambana na hali yake si kwa maombi tu bali pia kwa kutafuta msaada kwa gavana wao. Juhudi zake zinagonga mwamba. Anakubali rai ya Natasha ya kumpora Suluhu ili wapate hela, japo anaghairi nia baadaye.
Bi. Suluhu pia anadhihrisha nafasi ya masomo katika barua yake. Anamweleza mumewekuwa amewasomesha wanawe na anajua mumewe atafurahi kuwa mwanambee wao ametamatisha masomo ya msingi.
Uzinzi/Ufuska/Ukware/uasherati
Abigael na Natasha wanawategemea wanaume kwa ajili ya kupata hela kutoka kwao huku wakiwapa uroda. Abigael anamwambia Natasha kuwa hana budi kuendelea hivyo, ili kukimu familia yake; babake na wadogo zake.
Abigael anamweleza Natasha kuhusu Suluhu. Anamnyonya hela na kumpa uroda akijua vyema ana mke. Mkewe anapata dhiki tele kutokana na ukware wa mumewe na hata kuonekana mzee kuliko alivyo.
Abigael anasema kuwa atazidi kumnyonya Suluhu hadi ajue kutulia katika ndoa yake.
Abigael na Suluhu wanapatana kwenye chumba kufanya uzinzi. Chumba hicho si kigeni machoni mwa Abigael, kwani Suluhu amemleta hapo awali ili kutimiza ashiki yake. Hata anapanga kumwangamiza mkewe ili Abigael awe mkewe wa kando. Mkoba anaobeba Abigael alinunuliwa na Suluhu kama kiwakilishi cha penzi lao la haramu.
Katika barua ya Bi. Suluhu, anaeleza ukware wa mumewe. Amemtia mimba msichana wa chuo kikuu na kumtelekeza. Amempangia chumba mjini mwanamke mwingine. Anamweleza kuwa hatasema kuwa anashindwa kuleta maendeleo kwa kufuja pesa akiwalipa wasichana anaokula uroda nao.Isitoshe, anasema kuwa uzinzi wa mumewe umemletea nakama. Anamtaka amkome Abigael asije akamwambukiza.
Ndoa
Katika hadithi, tunashuhudia ndoa kati ya Suluhu na mkewe ambayo imejaa misukosuko. Abigael anasema kuwa mkewe Suluhu hana amani katika ndoa yake licha ya mali tele ya mumewe. Anapigwa na maisha na kukonda, hata kuonekana mzee kuliko umri wake. Ana wasiwasi kuhusu aliko mumewe mara kwa mara.
Barua ya Bi. Suluhu inaonyesha uchungu wake katika ndoa isiyo na sitara. Suluhu anamwacha mkewe na kuandama anasa na wanafunzi wa vyuo vikuu. Hata watoto analazimika kuwalea peke yake. Bi. Suluhu anamkumbusha makubaliano yao wakati wa kufunga ndoa, ambayo mumewe anayapuuza.
Bi. Suluhu anaonyesha pia thamani ya ndoa ya kuweka siri kwa kumhakikishia mumewe kuwa hajawahi wala hatatoa siri zake anazojua. Hatasema kuwa alishindwa kuleta maendeleo kwa sababu ya kufuja pesa akiwalipa wasichana kwa ajili ya uroda, na pia kumfidia Bwana Ngoma hela alizomkopesha akifanya kampeni. Hatasema kuwa ndiye alimuua mama Abigael baada ya kunyakua shamba lake.
Bi. Suluhu anasema yuko tayari kufa na kifo chake kitahesabiwa haki. Amechoka na dhuluma za mumewe, ambazo zinamwumiza pamoja na wanawe. Anamshukuru kwa ghiliba kwa wazazi.
Aliwatendea mengi kuwahakikishia kuwa anampenda.
Isitoshe, anamwona Suluhu kuwa sababu ya kifo chake. Hili ni kutokana na upweke anaomwachia na mawazo mengi. Anapomtembelea daktari anaambiwa kuwa afya yake iko sawa ila mawazo tu.
Anamkumbusha anathamini mapenzi yao, ndio maana hakuwahi kumdhuru japo angeweza kumsumisha.
Anakiona kifo chake kuwa cha suluhu kwa kuwa kitamwezesha mumewe kurudi kuwatunza wanao. Anamtaka kumkoma Abigael asije akamwambukiza nakama. Anahisi kuwa muda wa kujuta kila mara unaelekea tamati. Barua hii inamfanya Abigael kujuta kwa kuingilia ndoa ya Suluhu na mkewe.
Nafasi ya Mwanamke
Mwanamke anachukuliwa kama chombo cha starehe. Abigael na Natasha wanawategemea wanaume kwa kila kitu, huku wakiwapa uroda. Bi. Suluhu analalamikia tabia ya mumewe ya kuwalipa wasichana wa vyuo vikuu baada ya kula nao uroda. Amemtia mimba msichana wa chuo kikuu na kumtelekeza.
Mwanamke anachukuliwa kama kiumbe dhaifu. Suluhu anamtelekeza mkewe, wala hana la kufanya. Analazimika kuvumilia na kumuasa mumewe kwa kuandika barua. Hata muda wa kuzungumza naye kama mkewe hapatiwi.
Mwanamke ni mlezi. Bi. Suluhu anawalea wanawe peke yake. Hata mumewe anamwambia kuwa wana hao ni wake pekee. Yule wa kwanza ametamatisha masomo ya shule ya msingi. Abigael naye analazimika kuwalea wanuna wake baada ya mamake kufariki. Hata babake anamtegemea!
Mwanamke ni muuaji. Natasha anampa Abigael dawa ya kumtia usingizi Suluhu ili aweze kumwibia. Anafika chumbani wanamokutana na Suluhu akiwa na kisu cha makali kuwili, tayari kumwangamiza. Isitoshe, tunaambiwa kuwa kila kijusi kinapotunga wanakitungua.
Mwanamke ni mwenye tamaa. Abigael na Natasha wana tamaa ya pesa, hali inayowasukuma kuwapa uroda wanaume. Wanafikia hatua ya kumtilia Suluhu dawa ili waweze kumpora.
Mwanamke ni mwenye bidii. Abigael na Natasha wanatia bidii kwa kila hali kufanikisha masomo yao. Mkewe Suluhu naye anajitolea kwa kila hali kuwakimu wanawe baada ya mumewe kumtelekeza.
Umaskini
Hali ya umaskini inawatia matatani Abigael na Natasha. Wanalazimika kuwavutia wanaume ili wapate hela za kukidhi mahitaji yao. Wamekulia katika eneo moja na kupigwa na upepo wa maisha vilivyo. Suala la kuwa na maisha bora kwao linabaki kuwa ndoto.
Abigael yuko mwaka wa tatu chuoni na amepitia taabu sana chuoni humo. Hajapata wa kumwauni. Anatamani kuishi maisha bora lakini uchochole wa wazazi wake unamzuia. Anatafuta msaada hadi kwa gavana lakini hapati wa kumfaa.
Natasha amesoma chuoni kwa miaka saba na bado hajahitimu, kutokana na umaskini. Wanaamua kupangisha chumba kimoja na Abigael ili kugawana gharama. Umaskini unawasukuma kumpangia maovu Suluhu.
Kabla ya kutwaa uongozi, Suluhu pia yuko katika hali ya umaskini. Biashara yake ya kuuza makaa inaenda kombo baada ya ukataji miti na kuchoma makaa kupigwa marufuku. Hata pesa za kupiga kampeni anakopeshwa na Bwana Ngoma.
Migogoro
Suluhu ana mgogoro na mkewe kutokana na kutowajibika kwake katika ndoa. Anamwachia mkewe jukumu la kuwalea wanao peke yake. Anamlalamikia kupitia barua ambayo Abigael anaipata kibetini na kusoma.
Abigael anagundua mgogoro kati ya mamake na Suluhu uliosababisha kifo chake. Suluhu ananyakua shamba lake na kumwua ili kujilinda kutokana na sheria. Anahofia kuwa huenda mamake Abigael akamchukulia hatua za kisheria.
Abigael pia ana mgogoro na nafsi. Anaondoka kwa nia ya kumuua Suluhu. Anapoisoma barua kutoka kwa mkewe, anakirihika na kumwacha Suluhu. Anaamua kumwachia Mungu suala la hukumu. Anajuta kwa kuingilia ndoa ya Suluhu.
Mauaji
Abigael amefiwa na mamake. Anagundua ukweli wa kifo chake kupitia barua ya Bi. Suluhu kwa mumewe anapomtaja mumewe kuwa muuaji wa mamake kwa kuhofia sheria, baada ya kunyakua shamba lake.
Bi. Suluhu anasema kuwa yuko tayari kufa kutokana na dhiki aliyopatilizwa na mumewe, Suluhu. Anasema kuwa kifo chake kitahesabiwa haki kwani kitaleta usawa katika familia yake. Anahisi kwamba mumewe ndiye sababu ya kifo chake.
Abigael na Suluhu wanhusiana kwa muda mrefu. Kila mara Abigael anapopata mimba, wanapanga mauaji kwa kutafuta mbinu murua ya kuangamiza kijusi. Suluhu vile vile anatafuta njia ya kumwangamiza mkewe ili Abigael awe mkewe wa pembeni.
Abigael ana nia ya kumwua Suluhu. Anafika kwenye chumba wanamokutana huku amebeba kisu cha makali kuwili. Anamtilia dawa ya usingizi kwenye kinywaji na kukitoa kisu. Kabla ya kumuua, anaona waraka kutoka kwa mkewe. Anapomaliza kuusoma, anaghairi nia.
Mabadiliko
Suluhu na Abigael wamekuwa wapenzi kwa muda mrefu. Wanapatana katika mambo mengi. Hata hivyo, Aigael anabadilika na kunuia kumwangamiza Suluhu. Suluhu hana habari kuwa Abigael anaweza kubadilika kiasi cha kutaka kumtoa uhai.
Suluhu anaponuia kumwoa mkewe, anajitolea kuwasaidia wazazi wake kwa kila hali. Anamfurahisha mkewe pia. Baada ya ndoa, anamtelekeza mkewe kabisa na hata kumwachia majukumu yote ya malezi. Anazurura huku na huku akila uroda na wanafunzi wa vyuo vikuu.
Hali ya Suluhu ya kiuchumi pia inabadilika. Awali, anapata riziki kwa kuuza makaa. Anabadilisha hali hii kwa kumkopa pesa Bwana Ngoma na kujitoma katika siasa na kutwaa uongozi. Anaanza kuishi kifalme.
Baada ya Abigael kusoma barua ya mkewe Suluhu, anaghairi nia ya kumuua Suluhu kama alivyodhamiria. Anaona kuwa kifo hicho hakitaleta mabadiliko yoyote, bali kifo kinachofaa ni kifo cha maovu katika jamii. Pia anaonelea kuwa hakimu wa kweli ni Mungu tu.
Kutowajibika
Suluhu hawajibiki katika ndoa yake kama mume. Anamtelekeza mkewe na kumwachia majukumu yote ya ulezi peke yake. Hali hii inamfanya mkewe kusongwa na mawazo kila mara akitaabika kuwazia aliko mumewe.
Suluhu pia anatelekeza wajibu wake kama kiongozi kwa kutojali maslahi ya wale waliomchagua. Anatumia pesa anazofaa kuwahudumia nazo kulipia uroda kutoka kwa wasichana wa vyuo vikuu na pia kumlipa Bwana Ngoma aliyemkopesha wakati wa kampeni zake.
Natasha na Abigael hawawajibikii ujana wao. Wanajinufaisha kutoka kwa wanaume kwa kuwapa uroda. Hali hii inawaweka katika hatari ya kupata magonjwa ya zinaa na ukimwi. Abigael anapohimili, anatungua mimba akishirikiana na Suluhu.
Unafiki
Abigael anamwendea Suluhu kwa upole katika chumba cha starehe wanamokutana. Anamnywesha kinywaji chake kama mtoto na kumfanya ajihisi kama mfalme. Ukweli ni kuwa ametia kile kinywaji dawa ya kumpa usingizi Suluhu ili aweze kumdhuru.
Suluhu ni kiongozi aliyechaguliwa na watu akiwaahidi kuboresha maisha yao. Hata hivyo, anatumia wadhifa huo kujistarehesha kwa kuwalipa wasichana wa vyuo vikuu wampe uroda.
Suluhu anataka kumwangamiza mkewe ili Abigael awe mkewe wa pembeni. Anajitia kumjali sana Abigael ilhali ndiye alimwua mamake baada ya kunyakua shamba lake.
Suluhu anaposhtakia nia ya kumwoa mkewe, anawafaa sana wazazi wake ili kuwatanabahisha kuwa anampenda mwanao. Hata hivyo, baada ya kumwoa, anamtelekeza kabisa katika ndoa wala hajali maslahi yake. Anajistarehesha na wanafunzi wa vyuo vikuu.
Maudhui mengine ni kama vile Uongozi, Tamaa na Ubinafsi, Ubabebdume/Taasubi ya Kiume, Usaliti, Ukatili, Dini na Udhalimu.
Wahusika: Sifa na Umuhimu.
Abigael
Ni mzinzi. Anawapa uroda wanaume ili aweze kuwanyonya hela zao. Anamwambia Natasha kuwa ataendelea kumnyonya Suluhu hadi atakapojua kutulia katika ndoa yake na kumthamini mkewe.
Ni muuaji. Anafika kwenye chumba wanamokutana na Suluhu huku amejihami na kisu, tayari kumwangamiza, japo anaghairi nia. Kila akipata uja uzito katika uhusiano wake na Suluhu, anakiangamiza kijusi.
Ni katili. Anamkwamilia Suluhu licha ya kujua kuwa anamsababishia mkewe mateso. Anajua kuwa mkewe hana amani, hadi anaonekana mzee kuliko alivyo. Pia ana nia ya kumuua Suluhu.
Ni kigeugeu. Suluhu anampenda na kumkidhia mahitaji yake yote. Anamnunulia kifuko cha kubebea vitu, na hata yuko radhi kumwangamiza mkewe ili awe na Abigael. Abigael anamgeuka na kutaka kumwangamiza. Isitoshe, anatupilia mbali nia hiyo baada ya kusoma barua ya mkewe Suluhu.
Ni msomi. Ni mwanafunzi katika chuo kikuu, ambapo yuko katika mwaka wa tatu.
Umuhimu wa Abigael
Ni kiwakilishi cha matatizo yanayowakumba wanafunzi wa vyuo vikuu. Kupitia kwake, udunishwaji wa mwanamke katika jamii unadhihirika wazi.
Ni kiwakilishi cha wasichana wanaonyakua waume za watu na kuwasababishia dhiki wake zao. Anawakilisha unafiki na ukatili uliopo katika jamii.
Kupitia kwake, umuhimu wa kupinga maovu na kukumbatia utu unawasilishwa.
Suluhu
Ni mzinzi. Anamwacha mkewe na kwenda kula uroda na wasichana wachanga. Anampachika mimba msichana mmoja na kumwacha bila tumaini. Ufuska wake umemletea nakama.
Ni muuaji. Anamwua mamake Abigael asiwe kikwazo kwake baada ya kupoka shamba lake. Pia anadhamiria kumwua mkewe ili kumpa nafasi Abigael awe mkewe wa kando. Kila Abigael anapohimili, wanashirikiana kuangamiza kijusi.
Ni msaliti. Anamsaliti mkewe kwa kumwendea kinyume licha yake kumpenda kwa dhati. Anamsaliti Abigael kwa kumwua mamake. Anawasaliti raia kwa kutojali maslahi yao.
Ni asiyewajibika. Anamtelekeza mkewe na kumwachia jukumu la malezi ya wanao. Mkewe anamwambia kuwa hata wanawe wanajua matendo yake. Anamwambia mkewe kuwa wana ni wake(mkewe) peke yake. Anaponda raha na wasichana kwa hela za kuwahudumia wananchi.
Ni mnafiki. Anawasaidia wazazi wa mkewe ili kuwatanabahisha kuwa anampenda na kumjali. Anapomwoa, anamtelekeza na kutojali maslahi yake. Anawahadaa wananchi kumpa kura, kisha kutumia wadhifa huo kujistarehesha. Anajitia kumjali Abigael hali alimwua mamake.
Ni fisadi. Ananyakua shamba la mamake Abigael na kumuua ili kujikinga dhidi ya sheria. Anapangia msichana mmoja wa chuo kikuu kuhitimu kabla ya wakati wake ili ampe uroda.
Ni katili. Anamuua mamake Abigael baada ya kunyakua shamba lake. Anapanga pia kumwangamiza mkewe. Anawatelekeza wananchi kama kiongozi na kuzidi kuponda raha.
Umuhimu wa Suluhu.
Ni kiwakilishi cha viongozi wasiojali maslahi ya wananchi na kuwajibikia nyadhifa zao baada ya kukwea mamlakani.
Kupitia kwake, uozo katika jamii unabainika kwa uwazi.
Ni kiwakilishi cha matatizo yanayokumba ndoa kutokana waume wasiowajibikia majukumu yao. Ni kiwakilishi cha ukatili katika jamii, hasa unaopelekea mauaji ya watu wasio na hatia.
Bi. Suluhu
Ni mvumilivu. Anapitia mengi katika ndoa yake lakini anavumilia yote. Mumewe hajali maslahi yake hata kidogo, na hata wanawe anawalea pekee.
Ni mlezi mwema. Mumewe anamtelekeza na kumwambia wanao ni wake peke yake. Anajitolea kuwalea wanawe kwa kila hali, na yule wa kwanza ametamatisha masomo ya msingi.
Ni mwaminifu. Anamweleza mumewe kuwa hajawahi kumwendea kinyume hata mara moja katika ndoa yao.
Ni mwenye mapenzi ya dhati. Anampenda mumewe kiasi kwamba hata yuko tayari kumfia. Licha ya kumtelekeza, bado anatimiza wajibu wake. Anamwambia kuwa hakuwazia kumwangamiza licha nafasi tele za kufanya hivyo kujidhihirisha.
Ni msiri. Anamhakikishia mumewe kuwa atatunza siri zake anazojua hata katika mauti. Anamweleza kuwa hataambia yeyote kuwa ndiye alimuua mamake Abigael, kuwa anashindwa kuwahudumia raia kwa kula uroda na wasichana kwa hela za kuwahudumia na pia kumlipa Bwana Ngoma aliyemkopesha wakati wa kampeni.
Ni mwajibikaji. Anawajibikia wajibu wake kama mke licha ya vitimbi vya mumewe. Anamtunza mumewe na kuwalea wanawe peke yake.
Umuhimu wa Bi. Suluhu
Ni kiwakilishi cha udhalimu unaoendelezwa dhidi ya wanawake katika jamii. Anawakilisha matatizo yanayowakumba wanandoa, hasa wanawake.
Ni kiwakilishi cha wanawake ngangari wanaosimama wima kuzihudumia familia zao licha ya kutelekezwa na waume zao.
Ni kielelezo cha uvumilivu katika masaibu ya maisha.
Natasha
Ni mzinzi. Anashirikiana na Abigael katika shughuli za kuwapa uroda wanaume ili kupata hela za kukidhi mahitaji yao.
Ni mshauri. Anampa Abigael mpango kabambe wa kumpora Suluhu baada ya kumtilia dawa ya kumpa usingizi.
Ni mkakamavu. Hakati tamaa ya masomo licha ya umaskini wake. Amesoma kwa miaka saba na bado hajahitimu na yuko tayari kuendelea na masomo yake.
Ni mwenye tamaa. Anamweleza Abigael jinsi ya kumpora Suluhu kwani tatizo walilo nalo ni pesa tu. Ana tamaa ya kupata hela kwa haraka.
Ni rafiki wa dhati. Yeye na Abigael wamekulia katika kijiji kimoja na kupitia mengi katika maisha yao. Anashirikiana na Abigael chuoni kwa kila hali. Wanaishi chumba kimoja na kupambana na dhiki za maisha pamoja.
Umuhimu wa Natasha.
Ni kiwakilishi cha dhiki na matatizo ya wanafunzi katika vyuo vikuu.
Kupitia kwake, ukware unadhihirika katika jamii, hasa miongoni mwa wanafunzi wa vyuo vikuu. Ni kielelezo cha marafiki wa kweli wanaofaana katika dhiki na faraja.
Ni kielelezo cha ukakamavu katika kuandama azma zetu maishani.
Mbinu za Uandishi
Tashbihi
…wakazungushwa kama pia. Bila kufanya ajizi…, alimwamsha na hapo akaanza kumnywesha kinywaji kama mtoto mdogo. Alijiona kama mfalme.
…basi nirudishie mfuko kama ishara ya kutupa penzi kama jongoo na mti wake. Umejibaidi nami kama ardhi na mbingu.
Sitachoka kukuasa hata ikiwa ni mfano wa kumchezea mbuzi gambusi.
Abigael alimaliza kusoma waraka ule huku machozi yakimbubunjika kama maji kwenye maporomoko.
Kisa cha mke wa Suluhu kilikuwa kama msumari wa moto kwenye kidonda kibichi… Akahisi kama mwiba wa kujidunga usioambiwa pole.
Tashihisi
…wakapigwa na upepo wa maisha, wakazungushwa kama pia na hatimaye kutapikwa na dunia yenyewe bila simile.
“Mtazame mkewe Suluhu alivyochakaa na kupigwa na dunia.”
Hapo alijituliza… akili yake ilizidi kumsuta kwa kuoa kijanajike ambacho hakikujua maana ya kumpenda. Moyo ulimpapa na woga ukamvamia.
Mara alichomoa kibeti kilichokuwa kimetuna na kushiba.
Juu ya kitanda, kisu chake kilimkodolea macho kana kwamba kinamwuliza, “Umesahahu kilichokuleta humu.?”
…matumaini yangu ni kuwa utabadilika kabla ya siku yako kubisha hodi. Aliyaacha machozi yamtoke shibe yake kwani asingeweza kujizuia.
Barua ile ilimfichulia siri si haba.
Kisu chake kilikuwa pale pale juu ya kitanda kikiendelea kumkejeli na kumcheka Abigael.
Istiara
…wakapigwa na upepo wa maisha. Lakini hilo lilibakia kuwa ndoto.
Jitihada… pandashuka za maisha zikawa kibwagizo cha maisha yake.
Ukiongezea wasiwasi wa mara kwa mara kuhusu aliko mumewe, hapo unamwongezea shubiri kwenye ladha kali ya maisha yake.
Bwana Suluhu, naomba ujirudi ewe kiziwi hapo ulipo.
Kila mtu sasa anazungumzia kuabiri kwako garimoshi ambalo dereva wake unamjua sawasawa. Imekuwa safari ndefu yenye pandashuka...
Sina budi kukushukuru kwa yale mema uliyonitendea kabla ya wewe kujigeuza na kuwa mumunye.
Kitendawili cha kifo cha mamake aliyepatikana ameuawa na watu wasiojulikana kilikuwa kimeteguliwa katika barua hii.
Maswali Balagha.
Ni nani angemsaidia Abigael na kumwondolea ukungu njiani? “Kwa nini nisiitumie fursa hii angalau name mtu? Kwa nini?...”
Ingewezekana vipi wakati wamekaa katika uhusiano wao kwa zaidi ya mwaka na kila kijusi kilipotunga, njia bora za kukiondoa zilitumiwa?
“Umesahau kilichokuleta humu?”
Kwa nini unataka kujitia hamnazo kuhusu ahadi ulizotoa? Umesahau namna tulivyohangaika… na hatimaye tukabandikwa majina ya ajabu? Umesahau, Mume wangu? Umesahau namna kazi yako ya kuuza makaa ilivyofikia hatima ya ghafla baada ya serikali kupiga marufuku ukataji wa miti katika eneo la Dafrau? Ama cheo chako… kimekulevya na kukufanya usahau familia yako?
…wajua kwamba yule binti wa chuo kikuu uliyepanga ahitimu kabla ya wakati wake alinieleza ulivyoishia kumtunga mimba na kumwacha bila tumaini? Na je, wajua kwamba hata yule hawara mwingine uliyeishia kumpangia chumba kule mjini ili nisijue alinieleza kila kitu?
Semi na Nahau
Sina budi- sina lingine, inanibidi
sikuitia bahari chumvi- sikusababisha jambo hili. hatuna be wala te- hatuna chochote.
ndoto ya alinacha- ndoto isiyoweza kutimia. kupiga hatua- kutekeleza jambo la maana. amejaribu juu chini- amejaribu kwa kila hali. kugonga mwamba- kukosa kufanikiwa. chungu nzima- tele, -ingi.
amevuna kuwili- amefaidika mara mbili kwa tendo moja. kujitia hamnazo- kujipurukusha, kupuuza ukijua.
kupiga marufuku- kukataza, kuharamisha.
kwenda segemnege- kwenda kombo, kuharibika kwa mambo. Akamtupia jicho- akamwangalia mara moja. Takriri
Lakini hilo lilibakia kuwa ndoto. Tena si ndoto ya hivi hivi tu bali ndoto ya alinacha.
96
Takriri
Umesahau namna tulivyohangaika…? Umesahau, mume wangu? Umesahau namna kazi yako ya kuuza makaa ilivyofikia hatima ya ghafla… naamini umesahau!
Nimevumilia kwa miaka mingi kwa ajili ya wanetu. Nimevumilia madhila yako kwa muda mrefu… Kwa muda wote nilioishi nawe… Kwa muda wote tuliokaa pamoja…
Sitawaambia kuwa ulishindwa kuleta maendeleo… Sitawaambia. Narudia, sitawaambia!
Usidhani kuwa sikuwa na uwezo wa kukomesha vitendo vyako viovu. Usidhani sikuwa na uwezo wa kukutilia sumu kwenye chakula na kukuangamiza. Usidhani sikuwa na uwezo wowote.
Abigael aliona sasa kifo ambacho kilihitajika ni kifo cha dhuluma…
Methali
Jitihada ikabakia kutoondoa kudura(Jitihada haiondoi kudura) Amlaye nguruwe huchagua aliyenona.
Ukitaka kumuua nyani usimtazame usoni. Yaliyopita si ndwele tugange yajayo.
Afriti hafichiki
Alihisi kama mwiba wa kujidunga usioambiwa pole(mwiba wa kujidunga hauambiwi pole)
Kinaya.
Abigael anasema kuwa babake anamtegemea kwa kila kitu. Ni kinyume baba kumtegemea mwanawe, tena mwana anayesoma. Ndiye anatarajiwa kumsaidia mwanawe.
Abigael anasema kuwa mkewe Suluhu hana amani kutokana na mali ya mumewe. Ni ajabu mali ya mumewe kumkosesha amani badala ya kumfariji.
Ni kinaya kuwa Suluhu anatafuta njia ya kumwangamiza mkewe, ambaye anafanya kila awezalo kumvumilia. Ndiye analea watoto wao peke yake. Anamtunzia siri zake nzito. Ajabu ni kuwa Abigael, anayemfanya kuwazia haya ananuia kujinufaisha kutoka kwake, hata yuko radhi kumwua.
Bi. Suluhu analazimika kumwandikia mumewe barua kumpasha ujumbe wake. Ni kinaya kuwa hana muda wa kuwasiliana na mume wake.
Suluhu anamkodishia kimada wake nyumba mjini ili mkewe asijue, ila kimada mwenyewe anamweleza mkewe kila kitu.
Ni kinaya kwa Suluhu kumwambia mkewe watoto ni wake peke yake. Wanaume hutarajiwa kuonea fahari watoto zaidi ya wake zao. Isitoshe, Bi. Suluhu anasema kuwa anajua mumewe atafurahi kuwa mwanao wa kwanza amekamilisha masomo ya msingi, ambayo Suluhu mwenyewe hajachangia!
Bi. Suluhu anasema kuwa kifo chake kitahesabiwa haki. Ajabu ni kuwa amepitia mengi mikononi mwa mumewe hadi kuhiari kufa. Kwa hakika, kifo chake hakiwezi kuwa haki.
Abigael anagundua kuwa Suluhu ndiye aliyemwua mamake kupitia kwa barua ya mkewe. Ajabu ni kuwa badala ya ukweli huu kumtia machungu zaidi kumwua, unamfanya kughairi nia na kumwacha hai.
Barua
Bi. Suluhu anamwandikia mumewe barua kumweleza uchungu anaomsababishia. Mumewe ametengana naye na hapati fursa ya kuzungumza naye. Barua hii inaanguka mikononi mwa Abigael. Inadhihirisha kero anazopitia Bi. Suluhu na ukatili wa mumewe, ikiwemo kumwua mamake Abigael. Inamwonyesha Abigael anavyomsababishia mateso na hata hatari anayojiweka kuhusiana na Suluhu aliyebeba nakama. Inamfunza umuhimu wa utu na kumfanya kughairi nia ya kumwua Suluhu.
Majazi
Suluhu- Anaondokea kuwa suluhu kwa Abigael kwa kumkidhia mahitaji yake baada ya kumpa uroda. Anafanyia suluhu ugomvi wake na mama Abigael kwa kumwua akihofia sharia.
Dafrau- Ina maana ya kumbo. Ni eneo ambalo Suluhu anauzia makaa kabla ya ukataji miti kuharamishwa. Biashara yake yake inapigwa dafrau.
Bwana Ngoma. Anafadhili kampeni za Bwana Suluhu. Anamsaidia kunogesha ngoma ya siasa.
Taharuki
Abigael anapotaka kumwua Suluhu, anatoa kibeti na kuona karatasi ambayo ni barua. Tuna hamu naye kujua ni nini kilichomo.
Mwishoni mwa hadithi, tunabaki na maswali kadhaa. Kwanza, Abigael hajatimiza maangano yake na Natasha. Atamwelezaje akifika chumbani?
Hatujaambiwa iwapo Suluhu ameisoma barua kutoka kwa mkewe au la. Na je, akiamka pale ataweza kujua yaliyotukia? Atachukua hatua gani?
Abigael sasa amejua Suluhu ndiye alimwua mamake. Je, atamchukulia hatua za kisheria au atamwachia Mungu suala lote la hukumu?
Abigael anaamua kutia bidii kujiandalia riziki. Je, ataacha tabia ya kuwanyonya wanaume kwa kuwapa uroda?
Kuchanganya Ndimi
“You know what darling, I bought this watch at ten thousand dollars…” “Take this, my love. Ni ishara ya penzi letu ambalo linaanza kuchipuza…” Koja
…mabinti hawa wawili waliokulia eneo moja, wakapitia tabu tumbi akidi, wakapigwa na upepo wa maisha, wakazungushwa kama pia na mwishowe wakatapikwa…
Abigael aliona sasa kifo ambacho kilihitajika ni kifo cha dhuluma, unyonyaji, udanganyifu, wivu, kinyongo, tamaa, chuki, wizi na kutowajibika.
Tadmini
98
Bi. Suluhu anasema mumewe amemzidi Mfalme Suleimani kwa kujitwika hadhi na kusahau kila kitu kina mwisho wake. Mfalme huyu, katika Biblia, alijizidisha hadhi yake kuliko Mungu.
Bi. Suluhu analinganisha mateso yake na yale Mtume Paulo aliyopitia gerezani. Anamwandikia mumewe kama Paulo alivyomwandikia Timetheo kumjuvya hayo mateso. Anahisi kama Paulo, amevipiga vita vyema na ana taji mbinguni.
Anamalizia waraka wake kama Paulo alivyomalizia nyingi za nyaraka zake kwa kumwambia mumewe Amani ya Mungu iwe naye.
Dayolojia.
Mazungumzo kati ya Natasha na Abigael chumbani mwao. Yanatusaidia kuelewa dhiki wanazopitia na mikakati yao ya kupambana nazo. Inadhihirisha pia elimu yao katika chuo kikuu na misukosuko wanayopitia.
Kisengerenyuma/ Mbinu Rejeshi
Abigael anakumbuka kuwa amewahi kuwa chumbani waliko awali. Anakumbuka kauli za Suluhu kuhusu saa yake aliyodai alinunua dola elfu kumi. Anapochukua dawa ya kumtilia kwenye kinywaji, anakumbuka maagizo ya Natasha.
Tunaambiwa kuwa Suluhu na Abigael walikuwa wamekaa katika uhusiano wao kwa mwaka na kila kijusi kilipotunga walikiondoa. Anapotoa kisu kwenye mfuko wake, anakumbuka ulinunuliwa mfuko huo na Suluhu kama ishara ya penzi lao, pamoja na agizo la kuurudisha mapenzi hayo yakifa.
Bi. Suluhu pia anamkumbusha mumewe kule walikotoka. Alikuwa akiuza makaa na biashara ikasambaratika baada ya ukataji miti kupigwa marufuku. Anamkumbusha binti wa chuo kikuu aliyemtia mimba na kumtelekeza na hawara aliyempangia chumba mjini.
Isitoshe, anamkumbusha kuwa alimuua mamake Abigael baada ya kunyakua shamba lake, na pia Bwana Ngoma alimkopesha pesa za kampeni anazolipa na kusahau raia wake. Pia hasahau kumshukuru kwa wema wake kabla hajabadilika kuwa mwovu. Anamshukuru kwa msaada aliowapa wazazi wake kuwatanabahisha anampenda.
Sadfa
Abigael anatoa kibeti cha Suluhu ili kupora hela zake. Kisadfa, anakutana na karatasi ambayo anagundua kuwa ni barua na kuamua kuisoma.
Katika barua ya Bi. Suluhu, ametaja maovu ya mumewe aliyoweka siri, ikiwemo kumwua mamake Abigael. Barua hii inaanguka mikononi mwa Abigael kisadfa na kumsaidia kutegua kitendawili cha kifo cha mamake.
Mbinu nyingine zilizotumika ni pamoja na Nidaa, Mdokezo na Utohozi.
Ahadi ni Deni- Rayya Timammy Mtiririko
Fadhumo anajiunga na shule nzuri ya upili. Anapelekwa na babake mjini na kumnunulia kila anachohitaji. Wanaagana baada ya Fadhumo kumsisitizia atatia bidii na kufaulu. Babake anamuaga akisema anarudi kwa raha akijua atatia bidii kwa ajili yake mwenyewe na familia. Yanaondokea kuwa maneno ya mwisho ya babake. Wanapanga akae kwa binamu ya babake mjini kupunguza gharama. Mwishoni mwa muhula wa tatu, babake anaaga kwa ajali. Kabla ya mwaka wa pili kufika katikati, mamake naye anaaga.
Fadhumo anatamatisha muhula wa pili tu. Anaacha shule kuwa mlezi wa nduguze kama mwanambee. Anatafuta jamaa wa kumsaidia. Mjombake anakubali kumlipia kakake karo. Jamaa mwingine anataka kumsaidia ila Fadhumo awe kimada wake, lakini anakataa.
Anaolewa na Adan, ambaye anaahidi kuwakimu nduguze. Anajiahidi kuwa atatamatisha masomo siku moja. Baada ya miaka sita, anajaliwa wana watatu na kuona haja ya kurejea masomoni. Anamkumbusha Adan ahadi yake kumsaidia kusoma. Kiu yake ya elimu iko juu sana. Adan alidhani ni utoto tu, na anampenda mkewe ambaye anampa furaha katika maisha. Yuko tayari kutimiza.
Anapata mwalimu wa kumfundisha nyumbani bila kuchelewa. Anafanya mtihani na kupata alama C-. Anajiunga na koleji ya kufunza watoto wadogo. Anapata astashahada na kupata kibarua cha kufundisha. Anaazimia kusomea stashahada. Watu wanaanza kumtia maneno kuwa mkewe hafai kusoma wala kwenda kazini. Anayemwudhi zaidi ni mjomba anyetuma ujumbe kuwa anataka kumwona. Anapoenda, anamwambia kwamba mambo ya mkewe kusoma hataki kuyasikia, kwani atakuwa mjeuri na huenda akamtoroka na hao walimu wake au wanafunzi wenzake. Anampenda na kumheshimu mjomba lakini hili hawezi kuridhia. Anajua mkewe hana nia mbaya na yuko tayari kumsomesha hadi atakapo. Anamtazama njomba kwa huruma na kuondoka, akijua uamuzi moyoni.
Ufaafu wa Anwani ‘Ahadi ni Deni’
Unapotoa ahadi kwa mtu, umejiweka katika deni ambalo utalipa kwa kutimiza ahadi uliyotoa. Fadhumo anatoa ahadi kwa babake kuwa atasoma kwa bidii kwa ajili ya kuboresha maisha yake mwenyewe na ya familia wanapoagana mjini. Mwishoni mwa muhula wa kwanza, babake hata hivyo, anafariki katika ajali ya barabarani. Mamake anapofariki pia, analazimika kuacha shule kukidhi mahitaji ya nduguze.
Fadhumo anakataa rai ya jamaa anayemtaka kuwa kimada ili aweze kumsaidia na wadogo zake. Anakubaliwa kuolewa na Adan ili awakidhi ndugu zake. Hata hivyo, moyoni anajiambia kuwa hata yeye ataandama elimu. Yuko tayari kutimiza ahadi yake kwa babake, hata ikipita miaka mingapi.
Baada ya kujaliwa watoto watatu baada ya miaka sita kwenye ndoa, anaona muda umefika. Anamkumbusha mumewe alipomwambia kuwa ana hamu ya kusoma, na kuwa hamu hiyo haijamtoka. Adan alifikiri kwamba ni utoto na hamu hiyo itaisha, lakini Fadhumo anamkumbusha yalikuwa maagano yake na babake, lazima alipe deni la ahadi aliyotoa.
Adan analazimika pia kutimiza ahadi yake kwa Fadhumo. Anawakimu nduguze na kuwapeleka shule baada ya kumwoa Fadhumo. Anapopata hamu ya kuendelea na elimu, yuko tayari kumsaidia kwa kila hali, ili kutimiza ahadi aliyompa.
Fadhumo anaanza masomo licha ya kuwa miaka imesonga. Licha ya changamoto tele anazopitia, anatia bidii. Anapata mwalimu wa kumfunza nyumbani ambaye wanashirikiana kwa karibu, hadi anapopata alama ya C- katika mtihani. Anajiunga na koleji ya kufunza watoto wadogo na kujipatia astashahada
100
inayomwezesha kupata kazi ya kufunza kwenye shule moja. Hatimaye anajiunga na masomo ya stashahada.
Watu wanaanza kutoa maneno kuhusiana na suala la Fadhumo kusoma na kufanya kazi. Wanamwambia Adan kuwa amemwacha mkewe kuzurura ovyo. Wengine wanasema kuwa mkewe hana haja ya kufanya kazi bali akae nyumbani na kutunza watoto. Hata hivyo, Adan hawezi kuwasikiza kwani yuko katika harakati za kutimiza ahadi aliyotoa.
Mjombake Adan, aliyemlea baada ya babake kuaga pia hatoshi kugeuza msimamo wake. Anamtumia salamu akamwone, na kumwonya dhidi ya mkewe kusoma na kufanya kazi, eti huenda akamkimbia na hao walimu au wanafunzi. Anamtaka akomeshe mambo hayo. Adan anajua hawezi kutimiza hilo.
Anamtazama kwa huruma tu, akijua lazima atimize ahadi yake kwa Fadhumo.
Fadhumo pia anatimiza ahadi ya moyo wake. Jamaa wa babake anapomtaka awe kimada wake ili aweze kumlipia karo anakataa. Hawezi kukubali kuuza utu wake. Anahiari kuolewa na Adan badala ya kuwa kimada, wala habadilishi ahadi yake kwa moyo wake anapoolewa. Anatimiza ahadi ya ndoa kwa kumzalia Adan na kumsaidia kubeba mzigo wa malezi.
Dhamira ya Mwandishi.
Anawasilisha changamoto wanazopitia wanafunzi katika juhudi za kupata elimu.
Anaonyesha umuhimu wa uvumilivu na kujitolea katika kutimiza azma zetu maishani na jinsi hali hiyo inavyoweza kuleta mafanikio.
Anasawiri matatizo yanayomkumba mtoto wa kike katika jamii iliyojawa na taasubi ya kiume. Anawasilisha matatizo yanayowakumba watoto mayatima katika jamii.
Anasawiri nafasi ya ndoa na umuhimu wake katika jamii.
Maudhui Elimu
Jamii hii inaaminia umuhimu wa elimu. Babake Fadhumo, licha ya umaskini wake, anampeleka bintiye mjini na kumnunulia vitu anavyohitaji kujiunga na shule ya upili ya kaunti. Anaachia masomo katika kidato cha pili, muhula wa tatu kwa kukosa karo na pia kuwatunza wadogo zake. Inamlazimu kuolewa, lakini anasema kuwa bado ataendelea na masomo.
Ili kunata moyo wake, Adan anamwahidi kuwasomesha ndugu zake, ahadi anayoitimiza. Baada ya miaka sita ya ndoa, anajiunga na shule tena kukata kiu yake ya elimu. Anapata mwalimu wa kumfunza nyumbani, ambapo hachelewi hata siku moja, hadi anapozoa alama ya C-.
Baada ya masomo hayo, anajiunga na koleji ya mafunzo ya kufundisha watoto wadogo. Anahitimu na kupata astashahada. Baada ya kupata kazi hiyo, bado anaandama cheti cha stashahada.
Watu wanajaribu kumtia maneno Adan kuhusiana na mkewe kusoma lakini hawasikizi. Wanamtaka amwachishe mkewe masomo. Mjombake anamwamuru asisikie maneno hayo lakini hamtilii maanani. Anaondoka kwake akijua hawezi kutimiza hilo.
Nafasi ya Mwanamke.
Jamii hii inaonekana kumkandamiza mwanamke, japo kuna matumaini ya maisha bora kwake. Mwanamke anawasilishwa kuwa msomi. Fadhumo anapelekwa na babake mjini kuandaliwa kujiunga na shule ya upili, anayoacha baada ya kufiwa na wazazi. Hata hivyo, anarejea masomoni miaka sita baadaye na kupata ufanisi mkubwa.
Mwanamke anachukuliwa kama chombo cha starehe. Jamaa ya babake Fadhumo anataka kujistarehesha na Fadhumo kimahaba ili kuwasaidia nduguze kupata elimu, lakini anakataa.
Mwanamke pia anachukuliwa kuwa mtumishi wa nyumbani. Watu wanamwambia Adan kuwa hafai kumwacha Fadhumo aendelee na masomo wala kazi bali anafaa kukaa nyumbani ili atunze boma. Mamake Fadhumo hahusishwi katika kumwandaa kujiunga na shule. Ni baba anayeandamana naye mjini.
Mwanamke pia anaonekana kama kiumbe dhaifu asiyestahili makuu. Mjombake Adan anamwambia kuwa hafai kumwacha mkewe azidi kusoma, kwamba amesoma vya kutosha. Anaona kuwa akizidi kusioma atakuwa mjeuri. Mjombake Fadhumo anakubali kumlipia kakake lakini si yeye.
Umaskini
Babake Fadhumo, Mzee Khalif ni maskini, lakini anajikakamua kumkidhia bintiye mahitaji yote ili ajiunge na shule ya upili. Anamtaka Fadhumo atie bidii katika masomo ili aweze kujifaa na kuifaa familia yao pia. Fadhumo anatakiwa kuishi kwa binamu ya babake mjini wakati wa likizo za mihula miwili ya kwanza kuepuka nauli.
Umaskini unamlemea zaidi Fadhumo wazazi wake wanapoaga. Analazimika kuacha masomo ili kukidhi mahitaji ya nduguze, kwani ndiye mwanambee, na pia kwa sababu ya kukosa karo. Hali hii inamfanya jamaa wa babake kumtaka awe kimada ili awakimu wadogo zake. Hata hivyo, umaskini haumfanyi kujidunisha kiasi hicho.
Umaskini ndio unamsukuma Fadhumo kuolewa katika umri mchanga, jambo ambalo hakutaka. Adan anapotokea kwa nia ya kumwoa, hana hila wala ujanja wa kujitoa. Anakubali tu Adan anapoahidi kuwasomesha wanuna zake.
Mapenzi na Ndoa.
Ndoa kuu katika hadithi ni kati ya Adan na Fadhumo. Anamwoa akiwa mchanga ili aweze kuwakidhi wadogo zake baada ya wazazi wao kuaga. Hata hivyo, anampenda kwa dhati na kumtunza ipasavyo.
Fadhumo na Adan wanajaliwa watoto watatu, na Fadhumo yuko tayari kwa zaidi. Wanaishi kwa kuelewana kama wanandoa na kusaidiana katika malezi ya wanao. Fadhumo anafanya suala la malezi kuonekana jepesi na Adan.
102
Adan anakubali kumsomesha mkewe baada ya miaka sita nje ya shule. Rai za watu kuwa anamtelekeza mkewe na huenda akamkalia hazimkatizi kumsaidia. Hata mjomba wake anaingilia kati kumtaka kukomesha mambo ya mkewe kusoma lakini hayuko tayari.
Mjombake Adan anaonelea kuwa mwanamume ndiye mwenye sauti kwenye ndoa. Anamtaka Adan akomeshe mambo ya mkewe mara moja kama mwanamume katika boma hilo.
Taasubi ya Kiume/Ubabedume
Mwanamume anaonekana kupaliwa makuu katika jamii hii huku mwanamke akidunishwa. Khalif anampeleka Fadhumo mjini kumnunulia vitu anavyohitaji kujiunga na shule ya upili. Mamake Fadhumo hahusishwi katika shughuli hii wala maamuzi kuhusu Fadhumo kwenda nyumbani likizoni.
Jamaa wa babake Fadhumo anamtaka kimapenzi; awe kimada wake ndiposa amsaidie kwa kuwasomesha ndugu zake wadogo. Suala la kufiwa na wazazi linampa upenyu wa kufuata mkondo huo lakini Fadhumo hampi nafasi.
Mjombake Fadhumo haioni haja ya kuelimisha mtoto wa kike. Anajitolea kufadhili masomo ya kakake mkuu, kwa kuwa anaona kuwa ndiye afaaye kusoma.
Fadhumo anapozidi kuandamana masomo, watu wanaanza kumtia Adan maneno. Wanamlaumu kwa kumwacha mkewe azurure huku na huko. Wanaona kuwa anafaa kumwamrisha atulie nyumbani ili kulea watoto na kutekeleza majukumu ya hapo. Wanaona kuwa hahitaji kufanya kazi.
Mjombake Adan anamtaka kukomesha suala la mkewe kusoma, kwani anaona kuwa litamfanya kuwa mjeuri asiyemsikiliza mumewe. Anasema kuwa kama mwanamume katika ndoa yao, Adan hapaswi kukubali upuzi kama huo kuendelea.
Familia na Malezi.
Fadhumo anajaliwa familia inayomwezesha kukua na kusoma. Babake anampeleka mjini kumnunulia vitu vya kujiunga na shule ya upili. Pia, binamu wa babake anakubali kuishi naye wakati wa likizo ya mihula ya kwanza miwili.
Wazazi wake wanapofariki, analazimika kuacha shule kuwakidhi nduguze kama mwanambee wa familia. Mjombake anafadhili elimu ya kakake. Jamaa wa babake anamtaka kuwa kimada ili awakimu lakini anakataa.
Fadhumo anapata familia yake mwenyewe anapoolewa na Adan. Anamwoa ili aweze kumsaidia kukidhi mahitaji ya wanuna zake. Wanajaliwa wana watatu na hata Fadhumo yuko tayari kupata zaidi. Anawalea wanawe kwa staha na kumfanya Adan ayaone malezi kuwa mepesi kama kanda la usufi.
Mjombake Adan anamwita anapohisi kama mambo hayaendi sawa. Anamtaka kumkomesha mkewe kusoma. Mjomba huyu ndiye amemlea Adan baada ya babake kufariki. Hivyo, Adan anamheshimu na kumsikiza, licha ya kuwa hayuko tayari kutekeleza matakwa yake wakati huu.
Kifo/Mauti.
Babake Fadhumo, Mzee Khalif anaangamia kwa ajali ya barabarani na kumwachia ukiwa Fadhumo. Yuko katika kidato cha kwanza wakati huu, na kifo hiki kinamhuzunisha sana.
Mamake Fadhumo pia anafariki akiwa katika kidato cha pili na kuwaacha wanawe yatima. Mauko ya wazazi hawa yanamletea matatizo. Analazimika kuacha shule kwa kukosa karo na pia kuwakimu nduguze wadogo. Hatimaye anaolewa na Adan.
Adan anapokwenda kwa mjombawe, anamsikiliza kwa makini kwa kuwa ndiye mlezi wake. Alimlea na kumsomesha hadi alipofika baada ya babake mzazi kuaga.
Maudhui mengine ni kama vile Uzinzi, Migogoro, Utamaduni na Mabadiliko.
Wahusika: Sifa na Umuhimu Fadhumo
Ni msomi. Anajiunga na shule ya upili maarufu kaunti nzima. Hata baada ya kuolewa, anarejea masomoni na kujipa vyeti vya astashahada na stashahada.
Ni mkakamavu. Anaamua kurudi masomoni hata baada ya miaka sita nje. Anakataa katakata rai ya kuwa kimada kwa jamaa anayemtaka kukidhi mahitaji ya nduguze.
Ni mwenye bidii. Hata baada ya kuwa nje ya shule kwa miaka sita, anarejea tena masomoni na kutia bidii. Anatafuta mwalimu wa nyumbani kumsomesha na kujiunga na koleji baada ya kupata alama C-.
Ni mwajibikaji. Anaacha masomo kuwakidhi wadogo zake wazazi wao wanapoaga. Anajaribu kila awezalo kutafuta jamaa wa kuwasaidia. Analazimika kuolewa kwa ajili yao. Anakidhi majukumu anayotakiwa katika ndoa.
Ni mwenye mapenzi ya dhati. Anampenda mumewe Adan na anamkidhia mahitaji yote kama mumewe. Anamwambia kuwa yuko tayari kumpa watoto zaidi.
Umuhimu wa Fadhumo.
Ni kiwakilishi cha elimu na umuhimu na nafasi yake katika jamii ya sasa.
Kupitia kwake, madhila yanayowakumba watoto mayatima, hasa wa kike yanadhihirika.
Ni kielelezo cha bidii na kujitolea katika kutekeleza azma na jinsi hali hiyo huleta mafanikio. Ni kiwakilishi cha nafasi ya mwanamke katika jamii iliyojaa ubabedume.
Ni kiwakilishi cha asasi ya ndoa na nafasi yake katika jamii.
Adan
Ni mwajibikaji. Anawajibikia suala la elimu ya mkewe. Anamsaidia kuandama elimu anayotamani hadi atakapo. Anatimiza wajibu wake kama mume na kupuuza maneno ya watu.
Ni mfadhili. Anajitolea kuwakimu nduguze Fadhumo baada ya kumwoa. Anawasomesha hadi wanapomaliza na kuingilia ya Fadhumo.
Ni mwenye msimamo dhabiti. Anapoamua kumsomesha Fadhumo, maneno ya watu hayamrudishi nyuma. Hata mjombake aliyemlea hatoshi kumbadilisha.
104
Ni mwadilifu. Anamsikiliza mjombake bila neno kutokana na heshima anayompa. Japo hakubaliani na matakwa yake, anaondoka bila neno kwa ajili ya adabu.
Ni mpenzi wa dhati. Anampenda mkewe Fadhumo na yuko radhi kumkidhia mahitaji yake yote na kumsaidia kusoma hadi popote atakapo.
Umuhimu wa Adan
Ni kiwakilishi cha ndoa na nafasi yake katika kujenga jamii.
Ni kielelzo cha wanaume wanaowathamini wanawake licha ya mitazamo hasi ya jamii. Kupitia kwake, migogoro katika jamii, hasa kwa misingi ya kijinsia inadhihirika.
Anadhihirisha nafasi ya familia na mahusiano yake katika jamii.
Kupitia kwake, umuhimu wa elimu na nafasi yake katika kujenga jamii inadhihirika.
Bwana Khalif(Babake Fadhumo)
Ni mwenye bidii. Licha ya umaskini wake, anafaulu kumwingiza bintiye katika shule inayofahamika kaunti nzima na hata kumpeleka mjini kumnunulia vitu anavyohitaji kujiunga na shule hiyo.
Ni mshauri. Anamsisitizia bintiye umuhimu wa kuandama elimu kwa bidii ili iweze kumfaa yeye binafsi na familia yake pia.
Ni mwajibikaji. Anatekeleza majukumu yake kikamilifu kama baba. Anampeleka Fadhumo shule na kumkidhia mahitaji yake huko na kumpa ushauri. Anamtafutia mahali pa kuishi likizoni kutokana na uhaba wa fedha.
Umuhimu wake
Kupitia kwake, nafasi ya wazazi katika maisha ya wanao inadhihirika.
Kupitia kwake, umuhimu wa elimu na nafasi yake katika kujenga jamii inadhihirika. Anawakilisha pigo la mauti katika jamii na athari zake hasa kwa mayatima.
Mjombake Adan
Ni mtamaduni. Anashikilia kuwa lazima mume awe mkuu wa familia na aweze kumpeleka mkewe anavyotaka kama kichwa cha uhusiano wa ndoa.
Ni mwajibikaji. Baada ya babake Adan kufariki, anamlea na kumkimu hadi utu uzimani.
Ni dikteta. Anapomwita Adan kwake, hampi nafasi ya kutoa habari yake bali anamwamuru akamkomeshe mkewe kusoma.
Ni mbaguzi. Anabagua kwa misingi ya kijinsia. Anasema kuwa mwanamke kama Fadhumo hafai kuachiwa kusoma, anafaa kukaa nyumbani na mume ndiye mwenye kusema katika ndoa.
Ni mwenye imani potovu. Anaonelea kuwa Fadhumo akiendelea kusoma atakuwa mjeuri kwa mumewe, au atoroke na walimu au wanafunzi wenzake.
Umuhimu wa Mjomba
Ni kiwakilishi cha ubabedume katika jamii na jinsi unavyomkandamiza mwanamke. Kupitia kwake, nafasi ya utamaduni inadhihirika.
Anadhihirisha matatizo yanayokumba ndoa kutokana na suala la jinsia. Ni kiwakilishi cha uwajibikaji kwa kumlea Adan baada ya babake kufariki. Anadhihirisha umuhimu na nafasi ya familia katika maisha.
Ni kiwakilishi cha migogoro kati ya vijana na wazee katika jamii.
Mbinu za Uandishi Tashbihi
Maneno hayo yalikuwa kama hirizi aliyoamua kuivaa ili yamwongoze …
…mawazo yalikuwa yanampitia akilini mzomzo kama picha kwenye kioo cha runinga. Masharti magumu aliyoyaona vigumu kuyakubali kwani ni kama kuuza utu wake kwa shetani. Miaka ilipita kama upepo…
Fadhumo… alionekana kama mtoto mdogo aliyekuwa akimtazama mamake kwa hamu kuona kama atakumbuka ahadi aliyotoa ya kurudi na pipi akitoka sokoni.
Basi hapo alifurahi na kama mtoto, akaanza kueleza kwa furaha…
Alishuhudia macho yake yalivyokuwa yanang’aa kama ya mtoto aliyepewa peremende.
Maswali Balagha
Kwa nini aambiwe wakati wa shule? Kama ni mengine basi si yangesubiri? “Utoto? Utoto? Lakini si nilikwmbia ni ahadi niliyompa babangu?” “Mambo mazuri? Unanifanyia utani ama nini?”
“Mjomba, mbona sikuelewi?...”
“Yapi haya nasikia mkeo anasoma? Akisoma, atasoma mpaka wapi? … Kwani nani anayevalia suruali
katika ile nyumba? Wewe au yeye? … Kwa nini wewe unakubali? Kwani umemuoa au amekuoa?...Wewe ni simba mwitu au simba wa sarakasi?”
Dayolojia
Mazungumzo kati ya Fadhumo na babake. Yanaonyesha hali yao ya kiuchumi na pia ushauri wake kwa Fadhumo kuhusiana na elimu. Mazungumzo hayo yanaondokea kuwa kumbukumbu za daima kwa Fadhumo.
106
Mazungumzo kati ya Fadhumo na Adan akimweleza nia yake ya kurejea shule, ambayo mumewe anaridhia. Yanadhihirisha ukakamavu wa Fadhumo na ufadhili wa mumewe pamwe na masuala ya ndoa.
Mazungumzo kati ya Adan na mjombake. Yanadhihirisha mitazamo yao tofauti kuhusu mwanamke. Pia yanadhihirisha migogoro iliyopo katika jamii.
Istiara
Alikuwa ndiye taa iliyomulika na kuchangamsha nyumba nzima.
…mwalimu mkuu aliweza kusoma wahaka usoni mwake.
Kwa bidii, alifanya ulezi na uzito wote wa ndoa uonekane kanda la usufi.
Semi
maisha ya kijungujiko- maisha ya kutaabika kukidhi mahitaji. moyo ulikuwa mzito- alikuwa na mawazo tele, aliemewa. roho ilimruka- alishtuka sana.
yameingia katika kaburi la sahau- yamesahaulika.
ndio mwanzo mkoko unaalika maua- ndio anazidi kuimarika. akawa roho si yake- akajawa na wasiwasi na kihoro.
Kisengerenyuma/ Mbinu Rejeshi
Fadhumo anakumbuka mazungumzo yake na babake, ambayo yanaishia kuwa maongezi ya mwisho kati yao. Anayaweka moyoni na kuyakumbuka kila siku.
Baada ya miaka sita katika ndoa, Fadhumo anamkumbusha Adan ahadi yake ya kumrudisha shule aliyotoa wakati wakifunga ndoa. Anamweleza kuwa hawezi kuacha hamu hiyo kwani ni ahadi aliyompa babake.
Adan anapomtembelea mjombake, tunarejeshwa malezini mwake. Ni mjomba aliyemlea baada ya babake kuaga.
Tashihisi
Lakini naona wakati ni huu, ukiuacha utakuacha. Adan alipigwa na mshangao.
Methali
Ahadi ni deni.
Asojua maana haambiwi maana.
Kinaya.
Jamaa wa babake Fadhumo anamtaka awe kimada wake ili amsaidie kwa malezi ya nduguze. Ni kinyume kwake kumtaka kimapenzi mtoto wa jamaa wake ili kumsaidia.
Watu wanamwuliza Adan kwa nini mkewe anaenda kazini hali hahitaji kufanya hivyo. Ni kinaya kwao kusema hivyo hali mkewe huyo amehitimu kwa ajili ya kazi hiyo.
Mjombake Adan anamwita na kumwamrisha akomeshe mkewe kusoma. Ni kinaya kuwa badala ya kumhongera kwa juhudi zake anamkwaza.
Mbinu nyingine ni kama vile Utohozi na Nidaa.
Toba ya Kalia- Douglas Ogutu. Mtiririko
Jack anapokea simu ya Kalia, babake Siri, rafikiye mkubwa tangu utotoni. Ujumbe ni kuwa Siri atakuwa hewani kwenye runinga ya Kikwetu, na ameagiza Jack na wazazi wake (Siri) wawepo. Anavaa shati alilolainisha kwa kuweka chini ya godoro na suruali ya khaki. Hali hii ni kwa kuwa anawekeza kujiendeleza kimasomo. Safarini, Jack anakumbuka baruapepe ya Siri akimweleza angetumia fursa hiyo kupitisha ujumbe aliotaka ulimwengu usikie. Siri huwasiliana na wazazi wake kupitia skype, na Jack ndiye huwasaidia kuunganisha mitambo, licha ya kuwa amekomea shule ya upili kimasomo.
Wanaketi ukumbini wa mahojiano na kukaribishwa kwa sharubati. Kiswahili cha binti mtangazaji kinamfurahisha Bi. Mshewa, mkewe Kalia kwani ni mwalimu wa Kiswahili. Jane Gatoni, mtangazaji, anawakaribisha watazamaji katika kipindi chao, Nyumbani ni Nyumbani na kuwatambulisha wageni, kisha kuwapa fursa kuwasabahi watazamaji. Picha ya Siri inatokea kwenye kiwambo. Gatoni anamshukuru kwa kuitikia wito baada ya mchango wake mwingi kupitia facebook na twitter.
Anamwuliza sababu ya ufanisi wake katika Kiswahili akiishi Uchina, na hata kukifundisha huko. Siri anaeleza kuwa hali hiyo ilichangiwa na tabia za Monika katika riwaya ya Z. burhani ‘Mwisho wa Kosa’, aliyeenda ughaibuni na kuiga kila kitu huko. Akaahidi moyo wake kuwa mzalendo. Hata Uchina, kuna waliojifunza lugha hiyo na huizungumza vyema kuliko watu wa nyumbani. Wanaenda mapumzikoni kwa furaha huku Bi. Mshewa akimwahidi Jack siku yake itafika, kwani shindano la awali wakiwa kidato cha nne lilitoa nafasi kwa mtu mmoja. Jack anaungulika kwa kupokwa nafasi yake.
Gatoni anamwuliza Siri historia ya ufanisi wake. Kalia anapatwa na wasiwasi, kwani kuna sehemu isiyofaa kujulikana. Anaenda msalani kumpigia Siri simu lakini hampati. Anarejea kupata Siri akiendelea. Anaeleza mashindano yaliyofadhiliwa na wahandisi wa Uchina, mshindi akiahidiwa ufadhili kufikia uzamifu katika Chuo Kikuu cha Uhandisi. Shule yao ilitoa miradi bora, Jack akiwa wa kwanza naye wa tatu. Anajuta kumhini Jack bahati yake. Katika sherehe za kutambua mshindi, Kalia anabadilisha orodha, Siri anapewa ushindi na Jack kupewa nafasi ya tatu. Wanashiriki chamcha na mawaziri na wazazi wao pamoja na walimu wa shule. Jack na Kembo, anayechukua nafasi ya pili, wanakabidhiwa hundi za shilingi elfu kumi. Kembo anawapa wazazi wake, naye Jack anampa Bi. Mshewa amhifadhie. Urafiki wao ukaendelea na kumaliza kidato cha nne, Jack bado akamshinda Siri kwa pointi tano. Kwa kukosa wazazi, akaanzisha biashara kwa zile elfu kumi, akilipa nusu ya faida kwa wazaziwe Siri, eti ni shukrani ya malezi.
Siri anakiri wazaziwe wangempeleka shule bila ufadhili. Waliahidi kumtunza Jack hadi kilele cha masomo yake, lakini alibakia kuuza viatu. Hakulalama, japo Siri anaumika. Anamwomba msamaha Jack na pia kwa
108
ajili ya wazazi wake. Amepata kazi, na anatoa mshahara wa mwaka wa kwanza kufadhili elimu ya chuo kikuu ya Jack. Anawataka watatazamaji wasidhulumu mayatima na maskini. Bi. Mshewa anamwomba msamaha Jack kwa yote waliyomtendea. Kalia anamsifia Siri kwa ujasiri na kumwomba Jack msamaha, akiahidi kushughulikia masomo yake. Jack anafurahi kuwa atarudi masomoni. Anamshukuru Siri na kuwasamehe wazazi wake. Anawashukuru kwa kumwezesha kuanzisha biashara, iliyomfunza mengi. Bi. Gatoni anatamatisha kipindi na kuwaaga. Njiani, kila mmoja yuko huru, huku wakichagua vyuo Jack angeweza kusomea.
Ufaafu wa Anwani ‘Toba ya Kalia’.
‘Toba’ ni majuto yanayotokana na kutenda maovu. Hivyo basi, mada hii inarejelea majuto ya Kalia kutokana na maovu aliyotenda. Ndilo tukio kuu katika hadithi hii.
Siri anampa Jack ujumbe kuwa amewaalika pamoja na wazazi wake katika kipindi cha Nyumbani ni Nyumbani kwenye runinga ya Kikwetu. Anamwambia kwamba ana ujumbe muhimu ambao angependa ulimwengu ujue, lakini asimwambie babake. Sababu ni kuwa unahusu uovu wa Kalia.
Siri anapoulizwa kuhusu safari ya mafanikio yake, Kalia anaenda msalani kumjulisha kuwa kuna sehemu ya historia hiyo isiyofaa kusikika na yeyote. Hii ni sehemu aliyompoka Jack haki. Hataki kukiri makosa yake na kuomba toba, hadi muda unapofika.
Siri anasimulia Jack alivyoshinda katika mashindano na kutwaa fursa ya kusomea Uchina, lakini Kalia akampoka nafasi hiyo na kumwekea mwanawe, Siri, aliye huko wakati huu. Anajuta sana kwa hilo, na anamwomba Jack msamaha, na pia kwa ajili ya wazazi wake. Jack anawasamehe.
Kalia anaomba msamaha pia kutokana na kitendo chake. Kuonyesha toba yake ni ya dhati, anaahidi kuyashughulikia masomo ya Jack hadi atakapo.
Kando na hayo, matendo ya Kalia yanastahili toba, kwani anamchukulia Jack nafasi hiyo, licha ya kuwa na uwezo wa kumsomesha Siri bila msaada. Anayepokwa nafasi hiyo ni yatima! Si hayo tu, Kalia aliahidi kumsomesha hadi atakapo baada ya wazazi wake kuaga.
Jack anapoanzisha biashara ya viatu, anaanza kuimarika na hapo wazazi wa Siri wanaanza kudai nusu ya faida yake, eti ni zawadi ya malezi. Hata hivyo, Jack anawasamehe wala hana kinyongo. Anaikubali toba ya Kalia.
Kitendo cha Siri kwa Kalia ni toba. Anamwanika kwenye runinga ya Kikwetu kutokana na matendo yake ya awali. Kisa cha Jack kinamwuma kiasi cha kutovumilia na kuamua kuuambia ulimwengu. Hawezi kuvumilia zaidi.
Dhamira ya Mwandishi
Anadhihirisha umuhimu wa mahusiano ya kimataifa katika kuendeleza nchi za Kiafrika. Anawasilisha teknolojia na umuhimu wake, hasa katika mawasiliano.
Anadhihirisha nafasi na umuhimu wa urafiki katika maisha.
Kutoa ushauri kwa wale wanaowatesa mayatima na maskini kukomesha tabia hiyo. Anawasilisha viongozi wanaotumia nyadhifa zao kujinufaisha kwa jasho la wengine. Anawasilisha umuhimu wa kukiri makosa na kuomba msamaha.
Maudhui Elimu.
Jack na Siri wanasoma katika shule moja ya upili ambayo ni maarufu nchini. Wanatamatisha elimu ya kidato cha nne pamoja, na Jack anampiku Siri kwa pointi tano. Inawawezesha kushiriki katika shindano linaloandaliwa na wahandisi kutoka Uchina na kuibuka katika nafasi tatu za kwanza.
Mashindano hayo yanamwezesha Siri kupata fursa ya kuendeleza elimu yake Uchina, japo ni Jack anayestahili nafasi hiyo. Jack anaandaa kazi ya kupigiwa mfano na hata fomyula zake zinaingizwa kwenye vitabu, japo kwa jina la Siri.
Jack pia akiwa Uchina anaendeleza elimu ya lugha ya Kiswahili kwa wakazi wa huko, na anasema kwamba baadhi yao wanapata umilisi hata kuliko wazungumzaji wa nchi yake ya nyumbani. Anaimarisha ujuzi wake wa lugha kwa kusoma riwaya mbili, tamthilia mbili na diwani ya amashairi kila mwezi.
Jack anapokamilisha masomo yake ya shule ya upili, anakosa namna ya kuendelea kwa kuwa wazazi wake waliaga. Anaanza biashara ya kuuza nguo lakini baada ya Siri kuanika matendo ya Kalia hewani, hali inabadilika. Anapata nafasi ya kujiunga na chuo kikuu kwa ufadhili wa Kalia.
Kando na hayo, Bi. Mshewa pia ameelika hadi kuwa mwalimu wa Kiswahili, sawa na Bi. Gatoni, mtangazaji na mwendeshaji wa kipindi cha Nyumbani ni Nyumbani katika runinga ya Kikwetu.
Teknolojia na Mawasiliano.
Hadithi inadhihirisha maendeleo ya teknohama katika jamii. Jack anapokea simu kutoka kwa Kalia, kumweleza kuhusu mwaliko wa Siri katika mahojiano kwenye runinga ya Kikwetu. Wakiwa njiani, Jack anakumbuka baruapepe aliyotumiwa na Siri kumfahamisha kuwa kuna siri alitaka kusema.
Tunaambiwa kwamba Siri huwasiliana na wzazi wake kupitia skype, na Jack ndiye huwaunganishia mitambo kuhakikisha mawasiliano yanafaulu vizuri. Wanapatana naye vyema akiwa Uchina.
Ukumbi wa mahojiano unadhihirisha hali ya teknolojia na mawasiliano kwa uwazi. Jack anaketi karibu na mtangazaji, huku mkabala mwa mtangazaji mna kiwambo kikubwa kama ukuta. Hapa ndipo picha ya Siri inatokea wakati wa mahojiano na wanaendesha shughuli nzima bila matatizo.
Kalia anapohisi hatari ya Siri kutaja yasiyofaa, anaelekea msalani kumkumbusha kuhusu hayo. Hata hivyo, mawasiliano hayakamiliki kwani simu ya Siri haipatikani kwa wakati huo.
Ndoa
Ndoa katika hadithi hii ni kati ya Kalia na Bi. Mshewa, wazazi wake Siri. Yaelekea kwamba ndoa yao ina fanaka, kwani wanaonekana kupatana na kuelewana katika masuala mengi. Wanakubaliana katika tendo la kumpoka Jack nafasi yake na pia kukubaliana wakati wa kuomba msamaha kwa hayo. Wamejaliwa mwana ambaye ni Siri, na ambaye wanashirikiana ipasavyo katika malezi yake.
Ulaghai
110
Kalia anatumia ulaghai kumtwalia mwanawe nafasi ya kusomea Uchina. Jack anatokea kuwa na kazi bora na kuchukua nafasi ya kwanza katika mashindano. Ndiye ana haki ya kwenda Uchina kwa ajili ya masomo ya juu. Hata hivyo, Kalia anabadilisha matokeo kumweka Siri nafasi ya Jack.
Bi. Mshewa anapoona biashara ya Jack imeimarika, anamwamrisha kutoa nusu ya faida yake kwao, eti ni shukrani ya malezi, hali hawajamsaidia kwa lolote. Hili linamfanya kukosa uwezo wa kujiunga na chuo.
Urafiki
Unadhihirika kupitia kwa Jack na Siri, ambao ni marafiki tangu utotoni. Wanaanza urafiki huo na unakua hadi kiasi cha watu kuwafikiri kuwa ndugu. Wanadhihirisha ukweli wa udugu kuwa kufaana sio kufanana, kwani wanafaana katika kila jambo.
Kuna uaminifu kati yao. Siri anamdokezea Jack kuwa kuna suala kubwa ambalo anatumai kuwasilisha katika mahojiano wanayoenda Jack na wazazi wake. Anamwambia asidokeze lolote kwa babake, kwani yanafaa kuwa siri. Ana imani naye kama rafiki kuwa atatunza siri yao, jambo ambalo Jack anatekeleza.
Hata baada ya babake Siri kumlaghai Jack nafasi yake, bado urafiki wao unabakia. Jack halalamiki na kimya chake kinamwuma Siri hadi kuamua kutoboa ukweli. Anaposema, hata machozi yanamlengalenga kutokana na uchungu. Anajitolea kufadhili masomo ya Jack yote kwa mshahara wa mwaka wake wa kwanza kazini.
Kazi
Siri anawaeleza wazazi wake na rafiki yake Jack kuwa amepata kazi. Amefanikiwa baada ya masomo ya uhandisi nchini Uchina kupitia nafasi aliyotwaliwa na Kalia kwa ulaghai. Ananuia kutumia kazi hiyo kumfidia Jack kwa kumfadhilia masomo.
Babake Jack pia anafanya kazi kama mmoja wa wanakamati wa Wizara ya Sayansi na Teknolojia nchini. Yuko katika sherehe za kuwatuza wanafunzi waliofaulu katika shindano. Anatumia nafasi yake hiyo kumfaa mwanawe.
Bi. Mshewa naye anafanya kazi kama mwalimu wa Kiswahili. Bi. Gatoni naye anatekeleza wajibu wake katika studio, akifanya kazi ya utangazaji. Ndiye anaendesha kipindi cha Nyumbani ni Nyumbani katika runinga ya Kikwetu.
Jack anapokosa namna ya kuendelea na masomo baada ya wazazi wake kuaga, anatumia elfu kumi alizopatiwa kama tuzo kuanzisha biashara ya kuuza viatu. Biashara hiyo inamwezesha kukimu mahitaji yake, na pia kuwekeza kwa ajili ya kuendeleza masomo yake.
Maudhui mengine ni pamoja na Dini, Ukatili, Tamaa na Ubinafsi, Udhalimu na Migogoro.
Wahusika: Sifa na Umuhimu. Jack
Ni msomi. Anasoma na kuhitimu katika masomo ya shule ya upili. Anakosa nafasi ya kujiunga na chuo kikuu kwa kukosa hela. Hata hivyo, anajiandaa kwa kuwekeza, na fursa inapojitokeza, yuko tayari kuendelea.
Ni mwerevu. Anawasilisha mradi bora zaidi katika mashindano. Anapata alama tisini na nane. Siri anaungama kazi ya Jack ilikuwa ya kipekee na hata ilizua fomyula zilizowekwa kwenye vitabu.
Ni rafiki wa dhati. Urafiki wake na Siri ni wa kipekee. Wanasaidiana katika kila jambo, hata baadhi wanawafikiri kuwa ndugu. Hata kuhiniwa fursa yake na kupewa Siri hakuwatenganishi.
Ni msiri. Anapata baruapepe kutoka kwa siri kumweleza kuwa ananuia kufichua jambo la siri. Jack hamwambii yeyote. Anatunza siri hiyo.
Ni mwenye bidii. Anapoanza biashara ya kuuza viatu, anaimarika mara moja, hadi kumtia tamaa Bi. Mshewa. Licha ya kutakiwa kulipa nusu ya faida yake, bado anashikilia kazi hiyo vizuri.
Ni mvumilivu. Anapitia mengi katika maisha yake lakini hakati tamaa. Anafiwa na wazazi wake. Wazazi wa Kalia wanamdhulumu lakini bado anawaheshimu na kuwapa nusu ya faida yake.
Ni msamehevu. Anawasamehe wote waliomkosea mwishoni. Anawaeleza wazazi wa Siri kuwa hana kinyongo nao kabisa.
Umuhimu wa Jack
Ni kiwakilishi cha vijana shupavu walio na akili pevu ya kupambanua mambo. Anawakilisha madhila yanayowapata yatima katika jamii mikononi mwa wasiowajali. Kupitia kwake, umuhimu wa urafiki unabainika.
Ni kielezo cha msamaha na upendo kwa waliotukosea.
Ni kielelezo cha bidii na umakinifu katika kutekeleza mambo. Kupitia kwake, nafasi ya teknolojia na mawasiliano inabainika. Siri
Ni msiri. Anamweleza Jack kwa siri kupitia baruapepe kuwa ananuia kutoa ujumbe fiche kwa ulimwengu kwenye mahojiano wanayoenda na wazazi. Anamwagiza kutunza siri ile, na wazazi wake wanafahamu wakiwa hewani.
Ni msomi. Anasoma hadi chuo kikuu, ambapo amepata ufadhili wa kusoma hadi shahada ya uzamifu katika Chuo Kikuu cha Uhandisi.
Ni jasiri. Anatoboa siri kubwa kuhusu ufanisi wake uliopokwa Jack kwenye mahojiano ya runinga bila kitete hata kidogo. Hata babake anamhongera kwa ujasiri huo.
Ni mzito wa hisia. Kimya cha Jack kinamchoma moyoni, hadi anapoamua kutoboa ukweli. Katika masimulizi yake, analengwalengwa na machozi.
Ni mzalendo. A naeeza kuwa alichukia tabia za Monica, mhusika wa riwaya ya Z. burhani, ‘Mwisho wa Kosa’, kutokana na kukengeuka kwake. Anakipigania Kiswahili na kukifunza Uchina.
Ni rafiki wa dhati. Urafiki wake na Jack ni wa kumpigiwa mfano tangu utotoni. Hata yuko tayari kutoa mshahara wake wa mwaka kumlipia karo ya chuo.
Ni mshauri. Mwishoni mwa kipindi, anawapa watazamaji wosia kuwa wasiwadhulumu mayatima na maskini.
Umuhimu wa Siri.
Kupitia kwake, nafasi na umuhimu wa urafiki unadhihirika.
112
Anawakilisha teknolojia na mawasiliano na umuhimu wake katika kuunganisha jamii. Kupitia kwake, umuhimu na nafasi ya elimu katika kujenga jamii inadhihirika.
Ni kielelezo cha watetezi imara wa haki na ukweli. Ni kielelezo cha ujasiri katika kutekeleza mambo.
Ni kielelezo cha uzalendo na umuhimu wake katika jamii.
Kupitia kwake, mahusiano ya kimataifa na umuhimu wake katika jamii unadhihirika.
Kalia
Ni laghai. Anamhini Jack nafasi yake ya kusomea uhandisi Uchina na kumkabidhi mwanawe, Siri. Anabadilisha orodha na kumweka mwanawe wa kwanza licha ya kuwa alikuwa wa tatu.
Ni mnafiki. Anatoa ahadi ya kumtunza Jack baada ya wazazi wake kuaga, lakini hatimizi bali anatumia wadhifa wake kumdhulumu.
Ni mwenye tamaa. Anapoka nafasi ya Jack na kumpa Siri, licha ya kuwa ana uwezo wa kumsomesha bila msaada wowote.
Ni mfadhili. Anaahidi kusimamia elimu ya Jack hadi atakapo badala ya Siri.
Umuhimu wa Kalia
Ni kiwakilishi cha wanajamii wanaotumia nyadhifa zao kujinufaisha na familia zao. Anawakilisha nafasi ya mzazi katika malezi ya mwanawe.
Kupitia kwake, madhara ya ulaghai yanadhihirika.
Ni kiwakilishi cha wanajamii wanaowadhulumu mayatima kutokana na hali yao.
Bi. Mshewa.
Ni msomi. Amesoma hadi kiwango cha juu na kuwa mwalimu wa Kiswahili.
Ni mwenye tamaa. Anakiri kuwa anapoona biashara ya Jack imeanza kuimarika, anapandwa na tamaa na kumtaka kuwa anawapa nusu ya faida yake.
Ni mwenye majivuno. Anafurahishwa sana na umilisi wa mwanawe katika Kiswahili, na kudai kwamba ni urithi aliomwachia, kwani yeye ni mwalimu wa Kiswahili.
Umuhimu wake
Kupitia kwake, madhara ya tamaa yanadhihirika.
Ni kiwakilishi cha ndoa na nafasi yake katika kujenga jamii. Anawakilisha nafasi ya mzazi katika malezi na makuzi ya mwanawe. Bi. Gatoni
Ni mwajibikaji. Anatekeleza wajibu wake kwa umma kama mtangazaji. Anawakaribisha studioni wageni waalikwa na kuwapa sharubati kisha kuendeleza kipindi.
Ni mwenye umilisi. Anazungumza kwa ufasaha mkubwa katika kuendesha kipindi kile.
Ni jasiri. Anasikiliza maneno ya Siri yanayotoa ujumbe mzito. Anawauliza Kalia na Bi. Mshewa usemi wao kuhusu madai ya mwanao.
Umuhimu wa Bi. Gatoni
Anadhihirisha nafasi ya teknohama katika kujenga na kuendeleza jamii. Ni kiwakilishi cha uwajibikaji katika utendakazi.
Kupitia kwake, nafasi na umuhimu wa vyombo vya habari katika jamii unadhihirika.
Mbinu za Uandishi Tashbihi
… na meno meupe mithili ya theluji…
Mkabala… kulikuwa na kiwambo kikubwa kama ukuta.
Tulizidi kufanya kazi kwa pamoja na kupendana kama ndugu wa toka nitoke.
…kuniruhusu kufanya biashara ni kama kuniingiza katika chuo cha maisha.
Majazi
Siri. Anaficha sababu kuu ya kuwaita wazazi wake katika mahojiano. Anamwambia Jack asiwadokezee kuwa ana ujumbe anaotaka kupasha ulimwengu. Hata hamwambii Jack jambo gani haswa ananuia kusema.
Kalia. Ina maana ya kukaa juu ya mtu au kitu. Hutumika pia kumaanisha kumdhulumu mtu bila hiari yake. Anamkalia Jack kwa kunyakua nafasi yake na kumpa Siri. Kwenye studio, anataka kumkalia Siri kwa kumwagiza asidokeze yasiyofaa lakini hampati kwenye simu.
Kikwetu. Jina ya runinga anayohojiwa Siri. Ni ya kikwetu, kwani inatumia lugha ya Kiswahili, na pia inahoji masuala ya kinyumbani kwa watu wa nyumbani.
Masumbuko. Jina la pili la Jack. Anasumbuka kwa kuhiniwa nafasi yake ya ufadhili, kushindwa kuendelea na masomo na kulazimishwa kulipa nusu ya faida yake kwa wazazi wa Siri. Analainisha nguo kwa kuiweka chini ya mto na kuvaa suruali ambayo haijakauka.
Kinaya
Tunaambiwa kuwa Jack ndiye anaenda kwa Kalia kuwaunganishia mitambo kuwasiliana na Siri. Ajabu ni kuwa licha ya kuwasaidia, hawamjali hata kidogo.
Siri anaeleza hali ya kinaya katika riwaya ya Z. burhani, ‘Mwisho wa Kosa’. Monika, mhusika mkuu, anapelekwa ng’ambo kusoma. Marejeo yake yanayotarajiwa kuleta furaha yanaleta huzuni.
Waliomsomesha na kumtunza anawaona kama hawana maana na kuwakebehi.
Siri anafundisha watu wa Uchina Kiswahili. Anasema kuwa baadhi yao wanapata umilisi zaidi ya watu wa nyumbani, waliolelewa na lugha hiyo!
114
Kalia anaenda msalani kumwambia Siri kuwa kuna sehemu ya ufanisi wake ambayo haifai kujulikana na mtu yeyote, seuze ulimwengu. Ajabu ni kuwa jambo hilo ndilo sababu kuu ya mahojiano haya. Siri anapanga kulisema kwa ulimwengu.
Kalia anampoka Jack nafasi ya kujiunga na chuo kikuu Uchina na kumpa Siri. Ajabu ni kuwa ana uwezo wa kumsomesha Siri bila msaada, na anayepokwa nafasi hiyo ni yatima! Isitoshe, alitoa ahadi ya kumkimu baada ya wazazi wake kufariki.
Bi. Mshewa anamwagiza Jack kutoa nusu ya faida yake kwao, eti ni shukran ya malezi. Ajabu ni kuwa hawajamlea kwa vyovyote, kwani walimhini fursa yake na kutogharamia masomo yake ya juu.
Semi
kuzungumza moja kwa moja- kwa kuonana, bila kupitia kwa mtu mwingine. akapiga funda la sharubati- akatia kiasi mdomoni na kumeza.
kupasua mbarika- kusema ukweli wa jambo lenye uzito. alimkazia macho- alimwangalia bila kupesa.
kazi ya Jack ilikuwa ya kupigiwa mfano- yenye ubora wa kipekee. alikuwa na kibarua kigumu- alikuwa katika hali ngumu.
Methali
Udugu ni kufaana, sio kufanana. Liwalo na liwe
Lisilobudi hubidi.
Chuku
Urafiki wao ulifana kiasi cha wao kujulikana na watu wengi kama ndugu. Makochi… yalipendeza mno kiasi cha kijana huyu kutoamini alifaa kuketi hapo. Kuchanganya Ndimi.
… Siri huwasiliana na wazazi wake kwa njia ya skype. Upande wa kushoto…, kulikuwa na nembo ya skype.
Ni kutokana na mchango wako kupitia twitter na facebook… “Nani hapo nchini asiyetambua Masu footwear?”
Tashihisi
Akachukua shati la kipekee… Lilikuwa limetii amri ya kunyooka baada ya kulaliwa…
…usifanye hivyo mbele ya macho na masikio ya dunia nzima. Hata hivyo, kimya chake hunihukumu mno.
Taswira
Urefu wa kimo rangi ya maji ya kunde na meno meupe mithili ya theluji ni baadhi ya sifa za Siri.
Ukumbi wa mahojiano ulikuwa mtulivu na ulisheheni usafi asiowahi kuona Jack. Makochi yenye rangi ya manjano yalipendeza… bwana Kalia na mkewe, Bi. Mshewa, waliketi kwenye kochi lililowasitiri vyema. Jack aliketi kwenye jingine karibu na alipokuwa mtangazaji. Mkabala na alipokuwa mtangazaji, kulikuwa na kiwambo kikubwa kama ukuta… Upande wa kushoto pembeni mwa kiwambo hicho, kulikuwa na nembo ya skype.
Maswali Balagha
“Nani hapo nchini asiyetambua Masu footwear?” Mtangazaji alikuwa na kibarua kigumu. Angesema nini? Uzungumzi Nafsia
Huenda huu ndio wakati wa kupasua mbarika! Siri, usifanye hivyo mbele ya macho na masikio ya dunia nzima, aliwaza Jack.
Hadithi ndani ya Hadithi
Jack anasimulia kuhusu hadithi ya Monika katika riwaya ya Z. Burhani , ‘Mwisho wa Kosa’. Anaeleza alivyochukizwa na tabia ya Monika kuwakebehi watu waliomfaa katika masomo baada ya kurejea kutoka ng’ambo. Ndiyo inampa motisha ya kuenzi asili yake, na kufundisha Kiswahili Uchina.
Mbinu nyingine ni kama Mahojiano, Nidaa na Utohozi.
Nipe Nafasi- Mzamane Nhlapo Mtiririko
Mamake msimulizi anaamka huku macho yamesharabu wekundu. Baba yao hawatumii pesa kutoka Afrika Kusini anakofanya kazi migodini. Mama anaamua waende Makongeni kwa jamaa ya baba badala ya kuwatazama wanawe wafe njaa. Wanaabiri basi kutoka Habelo, kijiji wanachoishi, mjini Mbote.
Wanafikia mwisho wa barabara na kushuka basi. Wanaipanda Milima ya Maloti huku wakianguka mara kwa mara kwa utelezi, nayo baridi ikiwapiga vilivyo. Mama anajisemea kuwa lazima arudi kufanya kazi kuwakidhi wanawe.
Baada ya kumaliza milima, mama anataka kumnyonyesha mtoto wao mdogo, Mkhathini, lakini amefariki. Wanalia kwa kite na kuendelea na safari. Wanafika kwa jamaa yake baba. Wanakaribishwa kwa furaha na huzuni sababu ya kifo cha Mkhathini. Mama ana ujasiri, kwani anajua lawama zinazomsubiri, kuwa haheshimu mumewe na amesababisha kifo cha mwanawe. Mama anasema amekuja bila ruhusa ya mumewe wala jamaa zake kwa kuwa alijua hawangempa, na pia kuokoa wanawe kufa njaa. Anataka waishi hapo mwezi au miwili akisaka ajira, hilo pia bila ruhusa.
Maongezi ya mama yanazua minong’ono miongino mwa wanaume, wanaohisi amewakosea heshima. Baadhi wanadai lazima arudi kwao Swaziland. Msimulizi anaisikia harufu ya kitunguu kwenye nyumba jirani na tumbo linanguruma, anatamani chakula. Mama Kazili, hata hivyo, anawaeleza wazi hana nia ya kurudi Swaziland, wala hatalazimishwa. Anasema kuwa anaielewa vyema Biblia, lakini hila za kumdhalilisha mwanamke zinatiliwa nguvu na serikali inayojidai imechaguliwa na wanawake, kwani wanaume wengi wako Afrika Kusini wakifanya kazi. Wanaume wanatoka nje mmoja mmoja kujadili suala hilo.
116
Msimulizi na nduguze wanapatiwa chakula. Wanaume wanadai lazima Kazili awaombe msamaha. Wanawake wa makamo wanamuunga mkono lakini wale wazee wanaona amekosa. Wa mwisho kuingia amebeba kifurushi cheupe, maiti ya Mkhathini. Matweba, kaka mkubwa wa Moshe, mumewe Kazili, anasema wana watabaki kwao kama wiki mbili, lakini mama atarudi Habelo keshoye wakazike Mkhathini. Kazili anasimama kupinga uamuzi huo, ambao huwa wa mwisho. Anaanguka na kuzimia katikati ya usemi wake. Richman(Msimulizi) na nduguze wanaondolewa kwa kupiga kelele wanapolia, huku mama akimwagiwa maji kichwani aamke. Mama anashikilia kuwa lazima aboreshe maisha ya wanawe. Mwishoni mwa mwaka huo, ni mwalimu wa shule ya msingi bila idhini ya yeyote. Anakidhi mahitaji ya wanawe.
Ufaafu wa Anwani ‘Nipe Nafasi’
Huu ni wito kutoka kwa wanawake, wakiongozwa na Bi. Kazili kwa wanaume. Mwanamke anataka kupatiwa nafasi, kwani amekandamizwa sana katika jamii hii. Mwanamke anapopata nafasi, anawajibika zaidi ya mwanamume.
Kazili anapoona mambo yakienda kombo, anaamua kuchukua hatua mwenyewe bila kumhusisha mumewe kama anavyotakiwa. Anawachukua wanawe na kufululiza hadi kwa jamaa mmoja wa mumewe wasije wakafa. Anapopata nafasi, anafanya busara na haki kinyume na mumewe.
Msimulizi anasikia usemi wa mamake wanapopanda Milima ya Maloti. Anajisemea kuwa atarudi kufanya kazi kuwakimu, na siku hiyo lazima wale chajio. Mumewe amekosa kuwajibika, hivyo yuko tayari kuchukua nafasi hiyo.
Mama Kazili anamwambia Matweba na wanaume wenzake kwamba aliondoka bila kuomba ruhusa kwa mumewe kwa sababu alijua hangekubaliwa. Anawajuza kuwa hawezi kukaa tu kuwatazama wanawe wakihangaika kwa njaa, amewaleta wanawe wakae hapo kama miezi miwili akitafuta ajira, bila ruhusa pia. Anafanya maamuzi mwenyewe.
Wanaume wanahisi kwamba Kazili amewatusi, na kwamba lazima arudi kwao Swaziland kwa kuwakosea heshima. Hatarajiwi kusema ukweli. Hata hivyo, anawakumbusha kuwa yeye ni raia halali wa Lesotho kupitia kwa ndoa, na hakuna anayeweza kumlazimisha kurudi Swaziland, hata mumewe.
Zaidi, anaeleza jinsi wanawake wanavyohiniwa nafasi na wadhifa katika jamii kwa kusingizia Biblia, kuwa mwanamke anafaa kuwa mnyenyekevu. Anachukuliwa kama mtoto ambaye anafaa kuomba ruhusa kwa kila kitu kutoka kwa mumewe. Hali hii inaendelezwa na chama tawala. Hata hivyo, yeye yuko tayari kuchukua nafasi ya kuboresha maisha yake na ya wanawe.
Maneno ya Kazili yanasababisha kimya, kwani wanaume hawaamini kwamba mwanamke anaweza kusema mambo kama hayo. Hajapatiwa nafasi kama hiyo. Isitoshe, wanaume wanaelekea kwenye kraal kutatua masuala hayo. Ni wanaume tu wanaoruhusiwa huko. Wanawake hawajapata nafasi hiyo.
Matendo ya Kazili yanalakiwa kwa maoni tofauti huko Habelo. Wanawake wazee wanaona kuwa amekosea wanaume heshima na anafaa kuomba msamaha, lakini wale wachanga wanaona kuwa amaesema ukweli mchungu. Wanafaa kupatiwa nafasi pia kuwa na usemi.
Maamuzi yanayochukuliwa kwenye kraal huwa ya mwisho yasiyoweza kubatilishwa kwa kuwa wanaume wametawazwa viongozi na Mungu. Kazili anaagizwa kuwa atarudi alikotoka na kuacha wanawe, kisha abebe maiti ya Mkhathini akasaidiwe kuzika. Wanaanza kufumukana lakini anapinga maamuzi hayo.
Wengine washaanza kutoka, kwani hawatarajii jibu au neno lolote kuhusu maamuzi yao, hajapatiwa nafasi hiyo, lakini anaichukua.
Richman(Msimulizi), anashangaa iwapo nia ya mamake ya kuboresha maisha yake na yao itatimia. Hata hivyo, mamake anatimiza hayo kwani mwishoni mwa mwaka, anaanza kufunza shule ya msingi, bila idhini kutoka kwa yeyote. Ametwaa nafasi hiyo.
Dhamira ya Mwandishi.
Kubainisha dhiki wanazopitia wanawake mikononi mwa wanaume katika jamii inayowadhalilisha. Anatoa mwelekeo kwa wanawake walio katika dhuluma kujikaza kujiondoa humo wenyewe.
Anaelimisha kuhusu nafasi ya wanawake katika familia na jamii kwa jumla. Anadhihirisha umuhimu wa ujasiri na ukakamavu.
Anawasilisha matatizo ya kijamii na jinsi ya kuyakabili ili kuyashinda.
Maudhui
Taasubi ya Kiume/ Ubabedume
Kazili anapata fununu kwamba mumewe ana mke mwingine migodini. Hata hivyo, inaaminika kwamba mwanamume ana uhuru wa kuwa na wake wengi atakavyo, lakini mke mwema hafai kulalamika. Mume mwenyewe hamtumii pesa na anapozituma kupitia kwa mamake hazimfikii mkewe.
Mama Kazili anapofika kwa Matweba, analaumiwa kwa kuondoka nyumbani bila ruhusa ya mumewe, wala hata kumwambia. Wanaona huko kama kumdharau mumewe. Anapotaka ajira, wanasema kuwa hapaswi kuifanya bila idhini kutoka kwa mumewe.
Kazili anaeleza jinsi wanaume wanavyojitukuza kwa kusingizia Biblia, inayosema wanawake wawe wanyenyekevu kwa waume zao. Wanatakiwa kuwaomba waume zao ruhusa kufanya kila kitu, hata kutembelea familia na marafiki zao.
Wanaume wanaposikia maneno ya Kazili, wanabaki kinywawazi kwa kutoamini. Wanadai kwamba anafaa kurudi kwa wazazi wake Swaziland kwa kuwakosea heshima. Wanawake wazee wanaamini kuwa amewakosea heshima wanaume. Wamepandishwa wadhifa sana kiasi cha kuruhusiwa kuwadhulumu wanawake watakavyo.
Wanaume pia ndio wanaopatiwa wadhifa wa kusuluhisha matatizo ya familia. Ni wao tu wanaoruhusiwa kwenda kwenye kraal kufanya maamuzi kuhusiana na masuala ya familia. Wanadai kwamba Mungu aliwapa wadhifa wa uongozi.
Maamuzi yanayotolewa kwenye kraal yanachukuliwa kuwa sheria wala hayafai kubadilishwa. Matweba anapotoa habari za yale waliyoamua, watu wanaanza kufumukana kwani wanaamini kwamba hiyo ndiyo sheria wala haifai kupingwa.
Msimulizi anaeleza tukio la kijijini Habelo, baada ya mwanamke mmoja kumwambia mumewe ni mzembe kandamnasi. Wanaume wanaanza kukutana kuelezana jinsi mwanamke huyo alivyokosa heshima. Anatoweka kijijini na watu wanafikiri aliamriwa kurudi kwao, hadi mbwa wanapofukua mwili wake kondeni mwao. Mumewe alimuua na kumzika.
Migogoro
118
Msimulizi anashuhudia migogoro kati ya wazazi wake. Babake anafanya kazi migodini Afrika Kusini, hali mamake anaishi kijijini Habelo. Ana mke mwingine huko, na pia hamtumii mama pesa, na anapotuma hazimfikii. Japo anajua hili, anadai kwamba ameshindwa kuishi na mke anayeshinda kulalamika. Mama anaamua kuondoka kwenda kwa jamaa ya babake.
Mama na wanawe wanapofika kwa Matweba, mgogoro unazuka. Mama analaumiwa kwa kuondoka bila ruhusa, lakini anadai kwamba hangekaa tu wanawe wakihangaika, na pia alijua hangeruhusiwa.
Anaeleza kwamba yuko tayari hata kutafuta kazi, kinyume na taratibu.
Kazili pia anazua mgogoro miongoni mwa wanwake. Wale wazee wanaona kwamba amekosa heshima kwa wanaume, lakini wake wachanga wanahongera juhudi zake.
Maamuzi ya wanaume kwenye kraal yanawazulia mgogoro mwingine na Kazili. Hakubaliani na maamuzi yao wala hayuko tayari kuyafuata. Wanajiandaa kufumukana lakini anasema maoni yake kwa ujasiri.
Anaanguka na kuwalazimu kummwagia maji. Mwishoni mwa mwaka, amekuwa mwalimu wa shule ya msingi bila ruhusa kutoka kwa yeyote.
Msimulizi anaeleza mgogoro uliotukia Habelo miaka miwili awali, baada ya mwanamke mmoja kumwita mumewe mzembe kandamnasi. Wanaume wanasemezana jinsi alivyokosa maadili kwa wanaume.
Hatimaye anatoweka, na baadaye kubainika mumewe alimuua na kumzika kondeni mwao.
Usaliti
Moshe anamsaliti mkewe na wanawe. Anamwacha nyumbani peke yake na watoto bila kutuma pesa za matumizi. Anapotuma zinapitia kwa mamake lakini hazimfikii mkewe. Licha ya kujua haya, hafanyi lolote kumsaidia. Anasemekana kuwa na mke mwingine migodini anakofanya kazi.
Serikali tawala pia inawasaliti wanawake. Licha ya kuwa ndio wanaoiweka mamlakani, kwani waume wengi wanafanya kazi mbali na nyumbani, serikali hiyo inaendeleza mifumo ya dhuluma dhidi ya jinsia ya kike. Inaendeleza siasa za wanawake kuwanyenyekea waume zao, ambao wanawadhulumu.
Matweba anamsaliti Kazili. Badala ya kumliwaza kwa kufiwa na mwanawe, anamkemea akidai kuwa ndiye sababu ya kifo chake, kwa kuwa hakumheshimu mumewe. Anasema kuwa lau angesalia nyumbani, kifo hicho hakingetokea. Anamtaka kuondoka keshoye na kimba hicho kwenda kukizika.
Baadhi ya wanawake wanamsaliti Kazili. Anajitolea kwa kila hali kuwapigania kutokana na dhuluma za wanaume, lakini baadhi wanadai kwamba amewakosea heshima wanaume na anafaa kuomba msamaha. Wako tayari kuendelea kudhalilishwa!
Familia
Uhusiano wa kifamilia hauchukuliwi kwa uzito. Mumewe Kazili anatuma pesa kwa mamake, ambazo hazimfikii mkewe. Wanawe wanazidi kutaabika mikononi mwa mama yao. Msimuliza anaeleza kuwa nyanya yao ndiye anapata pesa na hampi mama, ila baba anajua hili. Hata hivyo, anasema kuwa inamwia vigumu kuishi na mke anayeshinda kulalamika.
Kazili anapoona mambo hayaendi vizuri na wanawe wako hatarini kafariki kwa njaa, anaamua kwenda kwa jamaa ya babake anayeishi Makongeni. Anaona kwamba huko wanaweza kupata auni ya chakula. Msimulizi anasema kuwa jamaa ya baba yao anafurahia kuwaona lakini taswira ya Mkhathini aliyefariki inamtia wasiwasi.
Matweba anataka majibu ya maswali kutoka kwa Mama Kazili kuhusiana na safari yake kuja huko. Anataka kumkumbusha kwamba hakuolewa kwenye ukoo wa Belo kuua watoto bali ‘kuwatengeneza’. Matweba ako tayari kusimama mahali pa nduguye aliye kazini Afrika Kusini.
Utamaduni
Japo Kazili anajua kwamba mumewe ana mke mwingine huko migodini anakofanya kazi, hatarajiwi kulalamika kwani utamaduni unamruhusu mume kuwa na wake wengi. Ndiye pia anatakiwa kufanya kazi na kukidhi familia yake.
Msimulizi anasema kuwa kama mama hangekuwa makini, angekumbushwa kuwa hakutolewa Swaziland aje kuwaua watoto bali kuwatengeneza. Mwanamke anachukuliwa kuwa kifaa cha uzazi. Anatarajiwa kuvyaa watoto wengi iwezekanavyo na kuwatunza. Anatarajiwa pia kuomba ruhusa kutoka kwa mumewe kabla ya kufanya lolote.
Matweba na wanaume wenzake wanamsikiza Kazili. Tunaambiwa wanasikiza kwa kimya kama kile kinachokuwa katika mahakama yao ya kitamaduni. Wanaume pia wana sehemu ambayo wanatumia kutoa maamuzi kuhusiana na masuala ya kifamilia kama hayo inayoitwa kraal. Hapo wanawake hawaruhusiwi. Maamuzi wanayotoa wanaume yanachukuliwa kuwa sheria.
Tunaambiwa kuwa Matweba na wenzake wanajitahidi kulinda tamaduni za jamii. Matweba anadai kuwa wanaume ambao hawajapata kazi kwenye migodi wana jukumu la kuhakikisha kwamba familia haisambaratiki. Wanafaa kuhakikisha kuwa wanawake wanawaheshimu waume zao.
Msimulizi anaeleza kisa cha mwanamke aliyesema mumewe ni mzembe. Hayo yalionekana kuwa matusi makubwa. Ilisemekana kuwa amerudi kwa wazazi wake au kuwa ngalile, mwanamke aliyerudi kwa wazazi wake. Wanagundua baadaye kuwa aliuawa na mumewe na akamzika kondeni mwao. Hata mama Kazili anapobisha kauli ya wanaume, wanawake wazee wanahisi kwamba anafaa kuomba msamaha.
Msimulizi na ndugu zake wanaandaliwa chakula kitamu cha papasane(aina ya mboga za mwituni) na nyama ya kondoo. Anasema kuwa jina lake la kupanga, Richman, linatokana na bwana mmoja wa jamaa ya Belo aliyefuga kondoo wengi. Isitoshe, anasema kuwa anawasikia ng’ombe wakikoroma kwenye kraal. Ni baadhi ya shughuli za kiuchumi zinazoendeshwa.
Kazi
Moshe, babake msimulizi anafanya kazi katika migodi huko Afrika Kusini. Anatakiwa kutumia kazi hiyo kuikimu familia yake. Anatuma pesa kwa mamake muda kwa muda. Wanaume wengine pia wanafanya kazi katika migodi hiyo hiyo na kuwaacha wake zao nyumbani.
Kazili anamweleza Matweba na wenzake kwamba yuko tayari kutafuta kazi ili kukimi mahitaji yake na ya wanawe. Mwishoni mwa mwaka, anapata kazi kama mwalimu wa shule ambayo msimulizi anatumaini kuwa itawaboreshea maisha.
Mazingira
Kati ya Makongeni na Habelo, ni umbali wa kilomita arobaini. Msimulizi, mamake na nduguze wanaabiri basi uchwara mjini Mbote. Wansafiria basi hilo kwa kilomita thelathini. Kufikia hapo, haliwezi kuendelea na safari kutoka hapo, ndio mwisho wa barabara.
Wanalazimika kutembea kwa miguu safari ngumu. Wanakabiliana na majabali na hatari ya utelezi milimani Maloti. Ni milima mikubwa na myeupe, na theluji imetapakaa kila mahali. Zaidi, baridi kali
120
inawapiga. Naposeka, dadake msimulizi anaanguka mara kwa mara na kulowesha nguo zake kwa theluji. Msimulizi anambeba mgongoni. Wanaanguka pamoja mara kwa mara. Mama pia anaanguka mara mbili tatu. Wanazidi kupambana huku vipande vya theluji bado vikiwapiga nyusoni.
Hali ya mazingira inasababisha kifo cha ndugu yao mdogo, Mkhathini. Isitoshe, hali ya mazingira inawawezesha wanawe kupata hifadhi. Kutokana na theluji, Matweba anasema kuwa atawaruhusu wana kukaa kwa wiki mbili tatu hivi, kisha watarudishwa Habelo. Richman na nduguze wanapata chakula chenye mboga aina ya papasane, inayohimili baridi ya kipupwe. Inafanya vizuri katika mazingira haya.
Ukombozi
Mwanamke yuko katika vita vya kujikomboa kutoka kwa dhuluma za mwanamume na utamaduni unaomdhulumu na kumdhalilisha. Kazili ndiye anaongoza vita hivi. Anapoona mumewe amemdhalilisha vya kutosha, anaamua kuondoka. Hajali kuomba ruhusa kama anavyotakiwa. Anachotilia maanani wakati huu ni maslahi yake na ya wanawe. Wanapanda milima kwa bidii hadi wanapofika nyumbani kwa Matweba, kakake mumewe.
Kazili anasimama kidete kupinga dhuluma za wanaume kwa wanawake kwa kusingizia Biblia na utamaduni. Anasema kwamba anataka kuwa mfano kwa wanawake kwamba wanafaa kuchukua hatua wanapoona waume zao hawawajibiki. Wanawake wa makamo wanakubaliana na rai ya Kazili, licha ya wale wazee kuchukulia haya kuwa madharau na kumtaka kuomba msamaha. Wako tayari kubadili mkondo huu wa dhuluma dhidi yao.
Mama Kazili anakana maamuzi ya wanaume kwenye kraal ambayo awali yanachukuliwa kuwa sheria isiyoweza kupingwa. Vitisho vyao kuwa atarudi kwao Swaziland havimshtui. Anawakumbusha yeye ni raia halali wa Lesotho kupitia kwa ndoa. Anawaambia kuwa atarudi nyumbani kupambana kuboresha maisha yake na ya wanawe. Mwaka huo ukiisha, anafanya kazi ya ualimu bila ruhusa kutoka kwa yeyote, na wanawe wanapata chakula kila siku.
Mabadiliko
Mama Kazili anaondoka Habelo bila ruhusa kutoka kwa mumewe kama anavyotakiwa. Yuko tayari kupigania hali yake na ya wanawe. Hayuko tayari kutawaliwa na mwanamume kama jamii inavyotaka. Anawajuza haya wazi wazi Matweba na wanaume wenzake.
Wanapomaliza kupanda Milima ya Mailoti na Mkhathini kufariki, mama anaangua kilio. Wanapofika nyumbani kwa Matweba, hata hivyo, anajua hali inayomkabili. Sasa yuko makini na uso wake umejaa ujasiri. Anapozungumza baadaye kupinga maamuzi ya kraal, amerejea sautu ile ile ya milimani.
Kazili anapobisha kauli za wanaume, wanashtuka sana kwani hawajazoea hali hii. Wamezoea wasemalo ni sheria. Mwamko wake unaleta msisimko miongoni mwa wanawake wa makamo wanaohisi kwamba hatimaye amesema ukweli unaostahili kusemwa. Wanahisi kwamba ni wakati wao kusimama kidete kupinga mzigo mzito wa kiuchumi uanowalemea.
Msimulizi anakumbuka usemi wa mama kuwa ataboresha maisha yake na ya wanawe, jambo ambalo anashangaa kama linawezekana. Hii ni kwa sababu hili linawaziwa kuwa jukumu la wanaume. Hata hivyo, anaamini mwishoni mwa mwaka, mamake anapopata kazi ya kufunza shule ya msingi, kwani hawakosi chakula.
Kifo/Mauti
Baada ya kumaliza kupanda Milima ya Maloti, mama anamchukua mtoto wake mchanga, Mkhathini, akinuia kumnyonyesha. Hata hivyo, mwili wa mtoto huyu umekakamaa, wala hapumui. Anaangua kilio na kuemdelea na safari huku amebeba maiti hiyo hadi nyumbani kwa Matweba.
Msimulizi pia anakumbuka kisa cha mwanamke wa Habelo aliyetoweka baada ya kumwambia mumewe kandamnasi kwamba ni mvivu. Hatimaye, anagunduliwa amefariki baada ya mbwa kufukua mwili wake ulioanza kuoza kondeni mwake.
Maudhui mengine ni kama vile Nafasi ya Mwanamke, Dini, Ukatili, Udhalimu, Uwajibikaji na Malezi.
Wahusika: Sifa na Umuhimu. Mama Kazili
Ni mkakamavu. Anapoamua lake, harudi nyuma. Anaamua kuondoka Habelo bila idhini ya yeyote. Anawachukua wanawe na kuondoka kuwatafutia chakula. Anamwambia Matweba kwamba atatafuta ajira bila ruhusa kuwakidhi wanawe na kweli mwishoni mwa mwaka huo, anakuwa mwalimu.
Ni jasiri. Anawakabili wanaume bila woga. Anawaambia wazi kwamba wanawadhalilisha wanawake. Anawaambia kwamba anataka kuwa mfano bora kwa wanawake kuwa wanafaa kusimama kidete kutetea maslahi yao. Msimulizi anasema kuwa walipofika kwa Matweba, uso wa mamake ulijaa ujasiri wa ajabu.
Ni mwenye bidii. Anatia bidii katika kusaka ajira hadi anapoipata na kuwa mwalimu wa shule ya msingi. Yuko tayari kufanya lolote kuboresha maisha yake na ya wanawe. Mwishowe, wanapata chakula kila siku.
Ni mwajibikaji. Anapoona mambo yanaenda kombo huko Habelo, anaamua kuondoka kwenda kwa jamaa ya mumewe Makongeni. Anaelewa kwamba akikawia huko wanawe watakufa njaa.
Ni mkombozi. Anajitolea kupigania haki za mwanamke katika jamii. Anaondoka bila ruhusa kwa mumewe na kwenda kwa Matweba kuwatafutia wanawe chakula. Anawaeleza wanaume waziwazi kuwa wanafaa kuwapa wanawake nafasi kujiendeleza. Anazua mwamko mpya miongoni mwa wanawake wa makamo.
Umuhimu wa Kazili
Ni kiwakilishi cha dhuluma za jamii dhidi ya jinsia ya kike.
Ni kielelezo cha wanawake jasiri wanaojitolea kwa kila hali kupigania maslahi yao. Anawakilisha migogoro inayoshuhudiwa katika jamii.
Ni kiwakilishi cha ndoa katika jamii na masaibu yake. Ni kielelezo cha ujasiri na ukakamavu katika maisha Richman(Msimulizi)
Ni mfadhili. Wanapofika kwenye Milima ya Maloti, dadake Nopaseka anaona ugumu kukwea kwani anaanguka mara kwa mara. Anajitolea kumbeba mgongoni, licha ya kuwa wanaanguka mara kwa mara.
122
Ni mwenye makini. Anagundua mzozo kati ya wazazi wake na mamake na mkwewe. Anagundua mabadiliko katika sura ya mamake wakiwa kwenye Milima ya Maloti na nyumbani kwa Matweba. Anagundua macho ya mamake yamesharabu wekundu kama alikuwa akilia.
Ni mwenye kujali. Anamjali sana mamake. Anapomwambia wanaondoka Habelo, anataka kujua wanaenda wapi na kwa nini. Anaposema mbele ya Matweba na wanaume wengine kisha kuishiwa na nguvu na kuanguka, Richman analia kwa kite akishangaa ikiwa mamake atafariki.
Umuhimu wa Richman.
Anawakilisha matatizo wanayopitia watoto katika ndoa yenye mizozo. Ni kielelezo cha watoto wanaowajali wazazi wao wakati wa matatizo. Ni kielelezo cha utu na ubinadamu katika jamii.
Kupitia kwake, madhara ya utamaduni hasa kwa watoto yanabainika.
Matweba
Ni mtamaduni. Anashikilia kwamba wanawake hawana uhuru wa kufanya maamuzi bila ruhusa ya waume zao. Anamwambia Kazili kuwa hatamruhusu kumdhalilisha Moshe. Tunaambiwa kuwa pamoja na wanaume wenzake, wanajitahidi kutunza utamaduni.
Ni dhalimu. Anataka kumrudisha Mama Kazili Habelo siku inayofuata, huku amebeba maiti ya Mkhathini mgongoni alivyombeba kumleta. Anataka kukaa na wanawe kwa wiki mbili tatu kisha kuwarudisha.
Ni mfadhili. Yuko tayari kukidhi mahitaji ya watoto wa kakake Moshe. Anawapa chakula cha kutosha. Anasema kuwa atakaa nao kwa wiki mbili kisha kuwarejesha kwa mama yao Habelo.
Ni katili. Hajali masaibu yaliyompata Kazili huko Habelo. Anataka kumtwika mzigo wa kurudi huko kumzika Mkhathini. Anamlaumu kwa kifo chake. Hamwonei huruma kwa kuwa amefiwa na mwanawe.
Umuhimu wa Matweba
Ni kiwakilishi cha wanaume wanaoendeleza unyanyasaji wa wanawake katika jamii. Anawakilisha utamaduni na nafasi yake katika jamii.
Anawakilisha nafasi ya familia katika kusaidiana maishani.
Moshe(Babake Msimulizi)
Ni mzinzi. Anamwacha mkewe nyumbani na kuoa mwingine kwenye migodi Afrika Kusini, anakofanya kazi.
Ni mwenye mapuuza. Anajua kuwa pesa anazotuma kwa mamake hazimfikii mkewe lakini hafanyi lolote. Anadai kwamba anachoshwa na mkewe kulalamika kila mara.
Ni mtamaduni. Anadai kwamba ameshindwa na mke ambaye anashinda kulalamika kila mara, hali anamdhulumu. Anaoa mke mwingine migodini kwa kuwa utamaduni unamruhusu.
Ni mwenye bidii. Anaondoka kwao Lesotho kwenda hadi Afrika Kusini kufanya kazi katika migodi ili kukidhi mahitaji ya familia yake.
Ni katili. Anamtelekeza mkewe na wanawe nyumbani na kuoa mwingine. Licha ya kujua hela hazimfikii mkewe, hafanyi lolote. Mkewe analazimika kuranda kwa jamaa kusaka msaada.
Umuhimu wa Moshe.
Ni kiwakilishi cha wanaume wanaodhulumu wanawake katika jamii. Ni kiwakilishi cha waume wasiojali aila yao.
Kupitia kwake, nafasi ya kazi katika kuboresha maisha inadhihirika. Anawasilisha matatizo na misukosuko iliyopo katika ndoa.
Mbinu za Uandishi.
Semi
alikata kauli- aliamua.
shughuli ya kuuma meno- shughuli ngumu, ya kung’ang’ana. baridi shadidi- baridi kali sana.
vilikufa ganzi- vilipoteza hisia sababu ya baridi. kumeza mafunda machungu- kuhisi uchungu mwingi. bumbuazi iliyowapiga- mshangao uliowapata. walikaa tuli- walikaa na kutulia.
kumtia mikononi- kumshambulia kwa vita.
Kumuunga mkono- kukubaliana naye, kusisitiza msimamo wake. walijishushia pumzi- walipumua kwa nguvu kisha kutulia. kusimama wima- kujitolea kwa moyo mmoja.
tuliangua kilio- tulianza kulia.
Tashihisi
Baridi ilizidi kututafuna kadri tulivyokazana kupanda Milima ya Maloti… Mashavu yetu yaliadhibika kwa upepo baridi huku vipande vya theluji vikitupiga kwenye nyuso zetu.
Tulijikaza zaidi kupambana na safari ile ya kilomita kumi. Ukimya uliotawala unaweza kumithilishwa…
…sauti yake ikisindikizwa na minong’ono kutoka kwa wanaume waliokuwa pale.
Kundi la ndege… huku wakiimba nyimbo zao kama kwamba hakukuwa na theluji tena. Sauti yake ilipenya masikio kwa udhabiti wa ajabu.
Kimya kilitawala nyumbani mle…
124
…mzigo mkubwa wa kiuchumi ulitishia kuwashinda kuubeba peke yao. Kimya chao kilitisha.
…akatuachia ulimwengu huu katili, usiojali.
Tashbihi
Ukimya uliotawala uliweza kumithilishwa na ule unaotarajiwa katika mahakama zao za kijijini wakati kuna kesi nzito ya kuamuliwa.
Sheria za jamii zinamchukulia mkwanamke kama mtoto anayefaa kuwa chini ya uelekezi na utunzaji wa mwanamume.
Kimya kilitawala nyumbani mle kana kwamba wote walikuwa wamekatwa ndimi. Mmoja baada ya mwingine… Kiza kiliwafanya kuonekana kama vivuli virefu.
Kinaya
Mosha anajua kwamba mkewe hafikiwi na hela anazotuma. Hata hivyo, hafanyi lolote, bali anamlaumu kwa kulalamika.
Matweba anamlaumu Kazili kwa kifo cha mwanawe badala ya kumfariji. Anadai kwamba angemheshimu mumewe na kusalia nyumbani, hayo hayangetokea. Ajabu ni kuwa huko walikuwa hatarini kufa njaa.
Anatakiwa kuomba ruhusa kwa mumewe na wakwe, ambao ndio kichocheo chake kuondoka.
Kazili anailaumu serikali kwa ajili ya mateso na dhuluma dhidi ya wanawake. Chama cha Taifa cha Basutoland kinachoendeleza haya kimechaguliwa na wanawake hao, kwani wengi wa waume zao wako kazini kwenye migodi, na wanashabikia chama kingine. Badala ya kuwatetea wanwake hao, kinawakandamiza.
Kazili analaumiwa kwa kuwakosea heshima wanaume, na kumdhalilisha mumewe kwa kuondoka nyumbani bila kumtaariifu. Ajabu ni kuwa anawaambia ukweli wasiotaka kusikia, na mumewe mwenyewe ndiye anamdhulumu kwa kumtelekeza na kumlazimu kuja huku.
Mama Kazili anapozirai, msimulizi na dadake wanaangua kilio. Wanaondolewa upesi wakisemekana wanatoa kelele zisizofaa. Ajabu, hawaoni kama hilo ni tukio la kusikitisha bali wanamwagilia maji kichwani ili aweze kuamka.
Kisengerenyuma/ Mbinu Rejeshi
Wanapofika kwa Matweba, msimulizi anaona mabadiliko katika sura ya mamake. Anasema kuwa hungejua ni yule yule ambaye muda mfupi uliopita alikuwa ameanguka mara kadhaa na wanawe kwenye theluji.
Msimulizi anakumbuka tukio la awali kijijini Habelo, wakati mwanamke mmoja alimwita mumewe mzembe kandamnasi. Baada ya muda, mwanamke huyo alitoweka na baadaye kufahamika aliuawa na kuzikwa mbwa walipofukua mabaki ya mwili wake ulioanza kuoza.
Msimulizi anapopatiwa chakula chenye nyama ya kondoo, anakumbuka kuwa jina lake la kupanga, Richman, lilisemekana kutokana na bwana mmoja aliyeishi Makongeni miaka ya 1890, ambaye alifuga kondoo wengi.
Mama anapoeleza msimamo wake akipinga maamuzi ya wanaume kwenye kraal, msimulizi anakumbuka kuwa sauti anayosema kwayo ni ile aliyokuwa nayo wakipanda Milima ya Maloti. Anapoanguka, anakumbuka anguko lake kwenye milima, tofauti ni kuwa wakati huu hataji jina la babake.
Msimulizi anakumbuka matukio ya siku waliyoenda kwa Matweba na maneno ya mamake. Anakumbuka hasa usemi wake kuwa kabla ya kufa, anataka awe amepata nafasi ya kuboresha maisha yake na ya wanawe.
Kejeli
…wangemkumbusha kuwa ndugu yao hakumuoa kutoka Swaziland kuwaulia watoto, aliolewa pale ‘kuwatengeneza’ watoto ili kuiendeleza familia ile.
“Na unafikiri unatoa mfano gani kwa wake wengine walioolewa katika familia ya Belo?” Sasa, nikiwa na nyama ya kondoo sahanini mwangu, niliona kuwa jina lile kweli liliniafiki.
…maamuzi hayo yalichukuliwa kuwa matakatatifu kwa maana wanaume walitakaswa viongozi wa familia na mwenyezi Mungu.
Utabeba maiti ya mtoto huyo mgongoni mwako, kama ulivyoibebea kuileta hapa.
…tulichukuliwa na kupelekwa kwenye ile nyumba nyingine kwa kusababisha kelele zisizofaa na kuwasumbua watu wazima waliokuwa kule.
Chuku
Hewa ilikuwa baridi shadidi, na iligandisha hata boho za mifupa mwilini… Matweba aliamuru kwa sauti ambayo ingemwogofya simba.
Tumbo langu lilinguruma na mate kunidondoka. Kwa miaka miwili nilikuwa sijapata kula nyama. Istiara
Ingawa waume zao walidinda kukiri hili, mzigo mkubwa wa kiuchumi ulitishia kuwashinda kuubeba… Mbegu aliyokuwa anapanda ilianza kuota mizizi.
Takriri
… kama inavyosema sheria. Sheria za kijamii…
Mmoja baada ya mwingine, walianza kutoka nje, kimyakimya. Harakaharaka, tulichukuliwa…
Maswali Balagha
“Na unafikiri unatoa mfano gani kwa wake wengine walioolewa katika familia ya Belo?” “Huyu mwanamke anasoma Biblia kweli? Atajifunza lini kutuheshimu?”
“Ndio. Anaiheshimu Biblia? Anatuheshimu kweli?”
Dayolojia
126
Mazungumzo kati ya msimulizi na mamake kabla ya kuondoka Habelo. Anamweleza mwanawe sababu ya kuondoka huko. Mazungumzo haya pia yanatuwasilishia matatizo anayopitia Mama Kazili na kujitolea kwake kuboresha hali yake na ya wanawe.
Mazungumzo kati ya Kazili na Matweba. Yanatusaidia kubaini nafasi ya mwanamke katika jamii na jinsi jamii inavyomdhalilisha na kumtukuza mwanamume.
Uzungumzi Nafsia
Niliyasikia maneno yake, Nitarudi na kufanya kazi ili niweze kuwakimu… leo lazima watapata chajio…
Tanakuzi
… kulikuwa na mchanganyiko wa furaha na huzuni.
Lakabu
Msimulizi ana jina la kupanga, ‘Richman’.
Mbinu nyingine ni pamoja na Tadmini, Mdokezo, Koja na Utohozi.
Nilitamani- Phibbian Muthama. Mtiririko
Tumaini(Msimulizi) yuko katika hali ya kutanga huku njaa imemzidi, kwani hajala tangu jana ila chai rangi aliyokunywa usiku, ila ana matumaini ya maisha bora. Ameondoka kwa Nina awali, anayemkaribisha katika nchi hii ya Wabongo na kuishi naye kama mwanawe kwa muda. Tumaini alimwacha mwanawe wa pekee na bibi yake, Farida. Nina anamtembeza, kumtunza na kumshauri kuepukana na Wabongo. Sasa anagundua alimwonea gere Nina kutokana na majaliwa ya mume mzuri na mali. Naye anatamani kuishi maisha mazuri kama Nina. Aliona hafai kugharamiwa na Nina, akaondoka kwake. Yuko kwenye stendi anapowaza haya. Anaamua kwenda Kariokoo kusaka kazi yoyote ya kumpa hela. Anasimamisha gari na kondakta anakubali kumbeba bure baada ya kumdanganya amepoteza kipochi chake.
Anashuka sokoni Kariokoo na kuanza kupitapita maduka ya Wahindi. Anahofia kuwa watamtambua kwa Kiswahili chake na sura ya ugeni, lakini ana imani. Machozi yanamtoka kwani hana wa kumwauni na hataki kumsumbua Nina. Anaona ofisi za mabasi ya Tahmeed, anayoyajua tangu Kenya na kwenda hapo. Anampata kaka mmoja anayemfaa kwa shilingi elfu tano za Tanzania na kumpa nambari ya simu, akimwahidi kumjuvya akipata kazi. Ananunua chakula na kumnunulia rafikiye, Jenifa matembele. Baada ya wiki tatu, anampigia jamaa huyu simu lakini hapatikani. Anabaki kumtegemea Mungu tu. Anaona Jenifa hana tabasamu tena, labda sababu yake kuwa kupe. Hataki kumsumbua Nina amsaidie japo anahitaji. Anawaza kurudi Kenya, lakini anaona hawezi kurudi mikono mitupu. Anaanza sasa kutaka, sio kutamani. Anataka maisha mema na mume mzuri.
Jumamosi moja, Nina anampigia simu kumjulia hali, kisha kwa hiari akamtumia pesa kiasi. Siku hizi hali nyumbani, anamdanganya Jenifa amekula alikokuwa kumpunguzia gharama. Anaamua kubarizi Coco Beach. Anaketi ufuoni kwenye pareo akiangalia bahari, baada ya kununua mihogo na soda. Anasikia mlio wa gari, na kando yake anasimama mwanamume mmoja. Anamwona kama aliyemtamani awe wake.
Sura yake inamvutia na anaamua kumsikiza. Mwanamume anadai kuwa aliwahi kumwona Westlands, nchini Kenya. Mwanamume yule anamwalika chamcha na kumshika mkono. Wanaondoka wakizungumza, na hapo anajua jina lake ni Romeo. Tumaini anamwona kuwa mumewe anayetarajia kwa
uzuri wake. Romeo naye anashtakia mapenzi kwake. Wanaelekea asikojua, ila tu anakisia ni kwenye migahawa mikubwa. Anamweleza atakavyomfanya tajiri kwa kumiliki mali yake tele. Kuwa Mbongo hakumfanyi kughairi nia ya kuolewa naye.
Ndani ya gari, hisia zinazidi kumsisimka Tumaini. Wanatabasamu wote. Romeo anampapasa na kumzulia msisimko mkubwa. Anamwita na kumwambia kwambe yeye(Romeo) si mtu wa kawaida, tena atakuwa mke wake katika dunia yao mpya. Alikoingia hawezi kutoka. Sauti yake ni nzito na kali. Tumaini anaanza kujuta. Anasikia simu ya Romeo ikiita na kusikia kwamba damu yake inatakikana! Romeo napoongea kwenye simu, Tumaini anafaulu kujifungua mkanda. Anajaribu kufungua mlango lakini umetiwa ufunguo. Anapita juu ya Romeo na kuponyoka mbio. Anakata misitu bila kujua aendako. Anatamani sasa kuwa nyumbani Kenya. Alitamani kupata mume mzuri, lakini si kwa njia hii. Vyote alivyotamani vimemponyoka.
Ufaafu wa Anwani ‘Nilitamani’.
Ina maana ya kuwa ‘nilitaka sana’. Hali hii ya kutamani ndiyo inamzonga msimulizi tangu mwanzo hadi mwisho. Kwanza, anaondoka kwao Kenya hadi nchi ya Wabongo kwa kutamani maisha mazuri. Licha ya mengi yanayomkumba, ana matumaini makuu kuwa atapata maisha bora.
Tumaini anaishi na Nina ambaye anamtunza vizuri kama mwanawe. Anamkidhia mahitaji yake yote. Anaona jinsi Nina alivyobarikiwa kwa mume mzuri na utajiri mwingi. Anatamani kuwa na milki kama hiyo ya Nina. Ndiyo mara ya kwanza anagundua kwamba alimwonea gere.
Anapohama kwa Nina, Tumaini ana matumaini ya maisha mazuri. Anaazimia kutafuta kibarua cha aina yoyote, almuradi aweze kutia tonge kinywani. Kwenye stendi alipo, anaamua kupanda basi kuelekea Kariokoo, akitamani kutafuta kibarua huko angaa apate hela kiasi.
Tumaini anapatana na kaka mmoja kwenye ofisi ya mabasi ya Tahmeed, ambaye anamwahidi kumtafutia kazi na kumpa nambari yake ya simu. Tamaa ya kupata kazi inamtuma kumpigia baada ya wiki, lakini anamkosa. Anabaki kutamani tu. Mambo yanazidi kuwa magumu kwake, lakini anabakia na matumaini kwamba ipo siku.
Anatamani pia kumtua Jenifa mzigo wa utegemezi, lakini hana namna. Anaona kwamba hana raha, na anakisia ni kwa sababu anatumia vitu vyake bure bilashi. Anahofia pia kumkopa Nina japo ana uhitaji. Kutamani kwake kunamtuma kumlilia Mungu, akiahidi kumtumikia milele akimpa ajira. Hakuna ibada inayompita.
Tumaini anatamani kurudi nyumbani lakini hana namna. Anashangaa jinsi bibi yake atampokea, na mwanawe Radhi. Hawezi kuwarudia hivyo tu. Anaamua heri kufia huku ugenini. Anazidi kutumaini kila uchao, na sasa anapanda ngazi kutoka kutumaini na kuanza kutaka. Anataka yaliyo mema na mazuri, maisha matamu.
Kutamani kwake kunajisisitiza kwa ushairi mawazoni. Anatamani kuwa na kasri afurahie, kazi ajikimu, na gari la kifahari. Anatamani kupata mume mwema wa ndoa, wapate watoto wema waadilike kwa dini, maisha yawe mepesi na kumpa burudani.
Tumaini anatumiwa pesa kiasi na rafikiye Nina na kuamua kwenda kubarizi Coco Beach. Anakutana na Romeo, mwanamume mtanashati ambaye anamshtakia mapenzi. Kwa tamaa yake, anamwona kama mwanamume aliyemwaza kwenye lile shairi lake. Wanaandamana huku akijidai kumpeleka katika mgahawa mmoja mkubwa.
Romeo na Tumaini wanavutana katika mapenzi kama sumaku. Hata hivyo, anagundua jinsi kutamani kwake kulivyomwingiza matatani. Romeo anamwambia sasa atakuwa mke wake katika dunia yake mpya, kwani yeye si binadamu halisi. Anagundua hatari aliyoko anaposikia Romeo akiitishwa damu yake.
Anaponyoka na kuchana mbuga mbio.
Anapasua misitu na kutoroka, asijue aendako. Japo alitamani kupata mume, si kwa njia hiyo. Anatamani kuwa nyumbani kwao Kenya ikiwezekana. Anakumbuka vyote alivyotamani bila mafanikio, ila tu mitihani inayomzonga. Alitamani lakini hajaweza.
Dhamira ya Mwandishi
Anawasilisha matatizo yanayowakumba raia wanaoazimia kujaribisha maisha katika nchi za kigeni. Anadhihirisha hatari ya kuwa na tamaa kupita kiasi.
Anaonyesha umuhimu wa kuthamini nyumbani, hata kukawa vipi kwani bado ni nyumbani. Anawasilisha matatizo yanayowakumba vijana katika harakati za kutafuta riziki.
Anasawiri dini na nafasi na umuhimu wake katika kujenga na kuendeleza jamii. Anaonyesha ulaghai wa kimapenzi na hatari zake kwa wahasiriwa.
Maudhui. Tamaa.
Tumaini ana tamaa sana katika maisha yake. Anatamani maisha mazuri na kuamua kuondoka kwao Kenya kwenda nchi ya Wabongo kufuatilia maisha hayo. Anatamani kuwa na mali kama Nina, anatamani kuishi kwa raha teletele na pia kupata kazi nzuri.
Tumaini anapanda kutoka kiwango cha kutamani na kuanza kutaka. Anataka maisha mazuri, anataka mume wake waoane na kupata watoto wazuri. Anapokutana na Romeo akibarizi Coco Beach, anahisi kwamba amepata mume aliyetamani. Romeo anashtakia mapenzi kwake, naye Tumaini anasalitika. Anamwona kuwa mtanashati zaidi duniani na kuamua kumkwamilia.
Tamaa ya Tuamaini inamgutua anapomaizi kwamba Romeo si binadamu wa kawaida bali jini. Anamwambia kuwa ashakuwa mkewe katika dunia yao mpya wala hawezi kutoroka. Anasikia waziwazi Romeo akiitishwa damu yake. Anafaulu kuponyoka na kutorokea vichakani.
Tumaini anajutia tamaa yake. Anakumbuka mambo yote aliyotamani maishani na ambayo hajafanikiwa kuyapata, bali amebakia tu kujipata kwenye mitihani. Sasa anatamani angekuwa nyumbani kwao Kenya ikiwezekana. Ametamani vingi, tena sana, lakini hajafanikiwa.
Utabaka.
Tumaini yuko katika tabaka la chini katika jamii. Anaishi kwa kupapatisha. Kila siku anahisi afadhali jana kwa jinsi matatizo yanavyomzidi. Anatamani kupata kazi ili ayaboreshe maisha yake lakini mambo hayawi mazuri hata kidogo. Mhudumu kwenye ofisi ya Tahmeed anamwahidi kumwitia nafasi ya kazi ikipatikana lakini baadaye anapiga nambari aliyompa na kumkosa.
Anatafuta kazi hapa na pale bila mafanikio. Anamtegemea rafikiye, Jenifa, ambaye anaonekana kukosa furaha. Anapofikiri amefanikiwa, anagundua kwamba ndio ameangukia pabaya, kwani anayedhani kuwa atamkweza upeo mwingine anaondokea kuwa hasidi. Anataka kumtoa kafara na analazimika kutoroka.
Jenifa anaweza kusemekana kwamba yuko katika tabaka la kati. Si tajiri mkubwa vile, lakini angalau ana uwezo wa kujikimu na kumsaidia Tumaini. Tumaini anajiona mzigo kwake kwa kumtegemea kwa vitu vya matumizi na kuamua kumtua. Mara kwa mara anamdanganya amekula ili kumpunguzia mzigo wa kumlisha na kukaa njaa.
Kwa upande mwingine, kuna walio katika tabaka la juu kama Nina na Romeo. Nina na mumewe wanamiliki mali tele hadi kumtia gere Tumaini. Anaazimia sana kuwa kama Nina na kumiliki mali aliyo nayo lakini hana namna. Anamkidhia Tumaini mahitaji yake yote bila matatizo hadi anapoamua mwenyewe kuondoka. Hata anamtumia Tumaini hela kwa hiari yake, kwani kwake si tatizo.
Romeo anakutana na Tumaini katika mkahawa wa Coco Beach, ambapo anajipumbaza kusahau matatizo yake. Ana gari aina ya Audi Q5 ambalo ni ishara ya hali yake ya kiuchumi. Anambeba Tumaini na kumzuga kwa namna atakavyomfanya tajiri na mmiliki wa mali yake tele.
Kazi
Ndiyo nguzo kuu ya kujiendeshea maisha. Tumaini anataka sana kupata kazi ili aweze kuwa na maisha bora. Ni moja kati ya sababu zake kuu kuondoka nchini kwao Kenya na kuhamia nchi ya Wabongo.
Anaona kuwa atapata kazi huko na kuyaboresha maisha yake, ya bibi yake na mwanawe.
Akiwa kwenye stendi, Tumaini anaamua kupanda basi kuelekea mjini kutafuta kibarua Kariokoo. Anaazimia kuwasaidiasaidia matajiri katika kuendesha biashara zao, labda hata awe mesenja. Hajali kazi atakayofanya, mradi tu aweze kupata hela kidogo za kukidhi mahitaji yake.
Anakutana na jamaa mmoja kwenye ofisi za mabasi ya Tahmeed, ambapo amefika kuulizia kibarua cha aina yoyote. Kijana yule anampa nambari yake akimwahidi kumpigia akipata nafasi ya kazi. Baada ya wiki tatu, anaamua kumpigia lakini anamkosa kwenye ile nambari. Bado ana matumaini ya kupata kazi, na anamwomba Mungu amjalie kila mara.
Urafiki
Tumaini anajaliwa marafiki wawili wa dhati, Nina na Jenifa. Anapofika nchini mwanzo, ni rafikiye Nina anamweka na kumkidhia mahitaji yake yote kama mwanawe. Anampa ushauri pia kuepukana na Wabongo, ambao ni wasanii, asije akajipata pabaya. Anamkidhia haja zote wala halalamiki, hadi Tumaini mwenyewe anapoamua kuondoka.
Nina anampigia simu kumjulia hali. Tumaini hana nia ya kumjuza kuhusu masaibu anayopitia, wala hawazii kurudi tena kwa Nina. Hata hivyo, Nina anajitolea kwa hiari yake kumtumia pesa kiasi kwenye simu yake, ambazo anaamua kujiburudisha kwenye mkahawa kando ya bahari.
Baada ya kuagana na Nina, Tumaini anaishi na rafikiye mwingine, Jenifa. Ndiye anakidhi mahitaji ya nyumba. Tumaini anahisi ugumu wa kumtegemea kwa kila kitu kwa kuwa hana kazi. Anahisi kuwa mzigo kwa kutumia chakula, sabuni, mafuta na vitu vingine vyake. Anaamua kumhadaa mara kwa mara kwamba amekula ili kuepuka hayo. Anapopata hela kutoka kwa kijana wa mabasi ya Tahmed, anamnunulia Jenifa matembele.
Mazingira
Tumaini anapendezwa na mazingira ya nyumbani kwa Nina anakoishi baada ya kufika nchi ya Wabongo. Anasema kwamba Nina na mumewe walimiliki mashamba ya misitu, magari ya usafiri na nyumba kama kasri. Kuna taa za kisasa, madirisha makubwa kama ya benki na miti ya manukato iliyozingira kama vile milangilangi na misumini.
Mazingira ya Coco Beach pia yanaonekana kuwa ya kuvutia sana. Tumaini ananunua kaukau za muhogo na soda ya pepsi kisha kutandaza leso chini na kukaa kuvinjari. Ni kwenye ufuo wa bahari na anaketi akiitazama. Inaashiria maisha yasiyokuwa na kikomo.
Romeo naye anapombeba Tumaini, anampeleka hadi kwenye ufuo wa bahari na kumwonyesha baadhi ya mali anayomiliki. Anamwonyesha majumba ya kifahari karibu na ufuo wa bahari, penye miti iliyoshika rangi ya kijani. Hata anapopata upenyu wa kutoroka, anakata katikati ya misitu na kukimbilia huko.
Ulaghai
Tumaini anamjulisha konda kwamba anaomba kubebwa bila hela. Anamdanganya kuwa amepoteza kipochi chake, lakini ukweli ni kuwa hana hela zozote. Ili kutilia mkazo ulaghai wake, anatumia sauti ya unyenyekevu na kuvaa wasiwasi usoni.
Tumaini anakutana na jamaa kwenye ofisi za mabasi ya Tahmeed, ambaye anamwahidi kumsaidia kupata kazi akipata yoyote mahali. Anampa nambari na kumwahidi kumpigia. Hata hivyo, Tumaini anapiga nambari hiyo baada ya kama wiki tatu hivi lakini anaambiwa kwamba haitumiki.
Romeo pia anamteka Tumaini kwa ulaghai. Anajitia kwamba amewahi kukutana naye mtaani Westlands, nchini Kenya. Hata hivyo, Tumaini anagundua baadaye kuwa kwao ni Zanzibar. Isitoshe, anamchochea kwa maneno ya mapenzi hadi kumteka mzima, bali ana nia tofauti ya kumtia mtegoni Tumaini. Anataka kumpeleka katika ulimwengu wake tofauti na huu wa binadamu wa kawaida.
Starehe na Anasa.
Tumaini anapotumiwa hela na Nina, anaamua kwenda kuvinjari kwenye Coco Beach, karibu na ufuo wa bahari. Ananunua kaukau za muhogo na soda ya pepsi na kuketi kwenye pareo kujiburudisha.
Anatazama maji ya bahari na kuyaona kama maisha yasiyo na mwisho.
Romeo anapokutana na Tumaini, anamteka kwa fikra kuwa anapelekwa katika migahawa mikubwa pale mjini. Anamwendesha hadi kwenye ufuo wa bahari na kumwonyesha majumba yake mengi pamoja na miti iliyoshika rangi ya kijani.
Ndoa.
Nina na mumewe wanaishi kwa staha na hali ya kumtamanisha yeyote kuwa katika ndoa. Mume mwenyewe ameumbika vizuri, na pia wanamiliki mali ya aina tofauti ambayo inafanya maisha yao kuwa ya raha mstarehe. Hata Tumaini anapoishi nao anaanza kuwaonea wivu na kutamani kuwa na mume kama huyo.
Tuamini yuko katika ndoa ya kisaikolojia. Anatamani sana kupata mume mzuri amwoe, waishi maisha mazuri. Anajiona akiwa ameolewa, huku wamejaliwa watoto ambao wanawalea kwenye misingi ya kidini na kuwakuza vyema.
Hata anapokutana na Romeo, mawazo haya ndiyo yanayomsukuma kwake. Anamwona jinsi alivyo mtanashati na kudondokea kwake. Romeo anamweleza mapenzi yake kwake na Tumaini anasalitika. Wanapofika ufuoni, Romeo anamwambia kwamba atakuwa mkewe kwenye dunia mpya, kwani yeye si
binadamu wa kawaida. Japo Tumaini anatamani kupata mume, si kwa njia hiyo. Anakataa na kutoroka mbio.
Maudhui mengine ni pamoja na Mabadiliko, Malezi, Kutowajibika, Umaskini na Dini.
Wahusika: Sifa na Umuhimu Tumaini
Ni mwenye tamaa. Anatamani kumiliki mali kama ya Nina. Anatamani kuwa mtu wa maana katika jamii, na kubadilisha hali yake ya maisha. Anatamani kuwa na mume mzuri na familia. Anapokutana na Romeo, tamaa inamwangusha mtegoni, nusura aishie dunia nyingine!
Ni mwenye tumaini. Licha ya hali ngumu, bado anaona kwamba mambo yatakuwa mazuri. Anasema kwamba anazidi kutafuta kazi kila uchao, akiamini kwamba siku yake itafika.
Ni mnafiki. Anapoona mambo yake yameenda kombo, anamgeukia Mungu na kumpa ahadi ya kumtumikia milele iwapo atamfungulia milango. Anakuwa mtu wa kanisa wala hakuna ibada inayompita.
Ni mwenye utu. Hataki kuwa mzigo kwa yeyote, na anafanya kila awezalo kutimiza hili. Baada ya kuishi kwa Nina kwa muda akimtimizia mahitaji yake, anaondoka. Anamdanganya Jenifa amekula alikokuwa ili kumpunguzia gharama. Anaposaidiwa hela mjini, anamnunulia matembele.
Ni mwongo/mdanganyifu/mhadaifu/mzandiki. Anamhadaa kondakta wa basi kwamba kipochi chake kimepotea na kutumia sauti ya unyenyekevu na kuvaa uso wa wasiwasi. Anamhadaa Jenifa kuwa amekula alikokuwa. Anamhakikishia Nina kuwa yuko sawa japo matatizo yamemjaa.
Ni mwenye bidii. Kila uchao anajituma kuhakikisha kwamba maisha yake yanakuwa bora. Anaazimia kupata angalau hela kidogo kuwaauni bibi yake Farida na mwanawe Radhi. Anazuru kila sehemu katika harakati za kusaka ajira ya aina yoyote.
Ni mkakamavu. Anapofanya uamuzi, basi. Anatoka kwao na kuhamia nchi ya Wabongo ili kusaka maisha mapya. Japo mambo huko ni magumu mno, anajikakamua na kupambana na hali. Anahiari kufia huko kuliko kurudi nyumbani mikono mitupu.
Ni mwoga. Anapofahamu nia haswa ya Romeo kwake, anagutuka kupata kwamba amejitabawalia.
Umuhimu wa Tumaini.
Kupitia kwake, masaibu yanayowakumba raia katika nchi za kigeni yanadhihirika. Ni kiwakilishi cha bidii na tumaini katika kusaka maisha bora.
Ni kiwakilishi cha matatizo halisi ya maisha hasa kwa maskini.
Kupitia kwake, madhara ya kuwa na tamaa iliyokinai yanabainika wazi. Ni kielelezo cha utu katika jamii.
Ni kionyeshi cha unafiki wa kidini, ambayo anaikwamia wakati wa matatizo.
Nina
Ni mwenye utu. Anampokea Tumaini ambaye ni raia wa nchi nyingine kwake na kumkidhia mahitaji yake yote bila lalama. Anamsaidia kujizoesha maisha yake mapya. Akiwa kwa Jenifa, anamtumia hela kwa hiari yake mwenyewe.
Ni mshauri. Anampa Tumaini ushauri dhidi ya Wabongo, ambao wana sifa za kisanii. Anamwonya ajihadhari nao wasije wakamwacha kwa mataa.
Ni mfadhili. Tumaini anapoishi kwake, anamfadhili kwa kila kitu wala hapati tatizo lolote hadi anapoondoka. Hata akiwa kwa Jenifa, anamtumia hela kwenye simu yake aweze kujifaa.
Ni mwenye kujali. Anamkidhia Tumaini kila kitu na kuhakikisha kwamba ako sawa katika hali zote. Anamshauri dhidi ya kuwaamini sana Wabongo asije akaingia matatani. Anamjulia hali mara kwa mara baada ya kuondoka kwake.
Umuhimu wa Nina.
Ni kiwakilishi cha utu na ubinadamu katika jamii.
Kupitia kwake, nafasi ya mwanamke katika jamii inadhihirika. Ni kiwakilishi cha utabaka na mipaka yake katika jamii.
Jenifa
Ni mfadhili. Anamkidhia Tumaini mahitaji yake yote anapoondoka kwa Nina. Tumaini anasema kuwa labda anamkera kwa kutumia vitu vyake kama sabuni, mafuta na vitu vingine vidogovidogo.
Ni mwenye shukrani. Anamshukuru Tumaini anapotoka mjini na kumletea matembele. Anamshukuru kwa hilo japo dogo tu.
Ni rafiki wa dhati. Anamsaidia Tumaini katika maisha kama rafiki yake. Anamlisha na kuishi naye kwake.
Umuhimu wa Jenifa
Ni kiwakilishi cha urafiki wa dhati wa kufaana katika dhiki. Ni kielelezo cha utu na ubinadamu katika jamii.
Kupitia kwake, tunajifunza kuwa na shukrani hata kwa ajili ya vitu vidogo.
Romeo
Ni laghai. Anamhadaa Tumaini kwa kisingizio cha mahaba, lakini ukweli ni kwamba anataka kumtumia kwa matambiko yake. Anamteka kwa ahadi nzito nzito zinazomfumba macho Tumaini.
Ni katili. Anamlazimisha Tumaini kuwa mkewe wa kipepo. Anamwambia kuwa ameshaingia katika ulimwengu huo na hawezi kutoka. Wenzake wanampigia simu kudai damu ya Tumaini.
Umuhimu wa Romeo
Kupitia kwake, ulaghai wa kimapenzi unadhihirika na hatari zake. Ni kiwakilishi cha uongo na utapeli katika jamii.
Ni kiwakilishi cha madhabahu ya kipepo yanayotumiwa kujilimbikiza utajiri.
Mbinu za Uandishi
Tashbihi
…viwanda na nyumba yao ya kuishi kama kasri la sultan vile.
…madirisha makubwa kama ya benki…
Nilitaka niufukuze ukata niliozaliwa nao. Niliuona kama laana. Mweupe, macho yake ya wastani meupe kama theluji lakini malegevu. Ngozi yake imetepekwa kama jejeta.
Tukaridhiana. Niliona kama mwezi umechukua nafasi ya jua kuniangazia mwanga. Siku niliyopata mume bila kutafuta, kama miujiza.
Tukawa kama pacha wa huba.
Maisha hapa ni tofauti na nilikoishi mimi. Maisha kama peponi. Nikamwangalia usoni, anametameta kama ana lulu ndani yake… Nilivyovitamani vyote nikavilaani. Niliona kama ndoto.
Tashihisi
Mara mawazo yanijia akilini na kuizonga nafsi…
…kuona miji tofautitofauti na kujua jinsi nitakavyotakabaliana na hali ya maisha katika nchi hii. Tabasamu nzuri iliyoficha pua yake ya kubabatana.
…maisha yanikubali nami niyakubali, tukubaliane na tufaane.
…nikaona bora niondoke nami nikapambane na maisha ya mjini.
Pale nikawa napita maduka ya Wahindi, nikawa nasema na moyo wangu. Jua …linafifia na kuleta rangi ya manjano na nyekundu. Machweo yanabisha. Maswali yalikuwa yanasema na akili yangu.
Tukafuata barabara kuu safi, sikumbuki ilikuwa inatuelekeza wapi… Maisha yalionekana kupumua hewa safi.
Maswali Balagha
Nifanyeje mimi mgeni?
Lakini nifanye nini? Nilipata tabu sana.
Lakini ningesemaje huko kwetu nirudipo? Ningerudi na nini hasa? Pesa gani, mali gani au na nani? Bibi angenipokeaje? Na mwanangu mpendwa je? Radhi wangu? Sijui.
Maisha ni kuishi leo. Wa kesho aishile?
Nikaanza kuvuta taswira ya maisha mapya, nifanyeje nipate nitakacho? Mbona mitihani inanizonga namna hii?
Majazi
Kigamboni. Ina maana ya vitani. Ni sehemu anakoishi Tumaini. Yuko vitani dhidi ya dhiki, njaa na umaskini.
Tumaini. Ni kuwa imani kuwa jambo litatokea. Ana tumaini katika maisha yake. Hakati tamaa kamwe. Ana tumaini la maisha mema, kupata kazi, mume na familia nzuri.
Nina. Lina maana ya mama. Anamkidhia Tumaini kama mama. Pia ina maana ya umiliki. Ana mali tele, mume mzuri na utu pia.
Romeo. Ni mhusika wa sinema ya kimapenzi ya Romeo and Juliet. Ameshamiri mapenzi motomoto kwa Tumaini, japo ni ya bandia.
Radhi. Ina maana ya neema au baraka. Ni baraka kwa Tumaini kama mwana. Pia ina maana ya msamaha. Tumaini hataki kumrudia mkono mtupu. Anafaa lolote la radhi.
Istiara
Nilihisi nimefika, kwamba nina ufunguo wa maisha niliyoyahitaji… na hapa nilihitaji mlango wa kufungua tu.
Ngao yangu ni imani tu.
Nilivuta subira, japo ulikuwa mtihani mgumu sana. Nilipanda ngazi kutoka kutamani na kuanza kutaka. Ile bahari iliashiria maisha yasiyokuwa na mwisho… Kifua nacho ni cha ngao.
Kila nikimtazama Romeo nampata naye ananitazama. Tumekua sumaku.
Semi
kusaka tonge- kusaka cha kujikimu kimaisha.
nikaze kamba- nitie bidii na kupambana, nisikate tamaa. nikakata kauli- nikaamua.
Sikukata tamaa- sikuacha kuwa na matumaini. bure bilashi- bure kabisa, bila sababu yoyote.
Niume jongoo kwa meno- nifanye jambo nisilopenda, linalotia kinyaa. Nikashika njia- nikaanza safari.
Moja kwa moja- bila kupinda au kubadilika. kupiga gumzo- kuzungumza.
Nikakimbia mguu niponye- Nikakimbia kasi sana kuepuka hatari.
Kinaya
Tumaini anasema kwamba Nina alimkirimia kama mama yake kwa kila kitu. Hata hivyo, anaamua kuondoka kwake, japo hana pa kuishi na kuishi kwa rafiki yake Jenifa. Ni ajabu kuwa anachoka kufadhiliwa hali hana hanani.
Tumaini anasadiki kwamba alimwonea gere Nina. Haya ni licha ya roho ya utu ya Nina, ambaye anamkidhia haja zake zote.
Tumaini anapopata hela kutoka kwa Nina, anaamua kwenda kudanganya moyo Coco Beach. Ananunua kaukau za mihogo na soda ya pepsi na kuketi akitazama bahari. Anavinjari kama mwenye vyake hali anateseka.
Tumaini anasema kwamba hapendi kusema na wageni lakini Romeo anaonekana kuwa mwungwana. Tunagundua baadaye kwamba si mwungwana hata kidogo. Sura yake pia ni kinyume cha uhalisia wake.
Tumaini anaiona Jumamosi hii anayokutana na Romeo kuwa ya fanaka maishani mwake. Hata hivyo, ni matata zaidi ambayo inamletea mikononi mwa Romeo.
Takriri
Sina namna ila nina matumaini. Matumaini ya kuyaishinda maisha… naona mwanga mpya, ukurasa mpya na matumaini kuzidi.
Alinifunza mambo ainaaina…
Niende mjini Kariokoo kusaka kazi hata kama ni kuwasaidiasaidia matajiri…
Nisingejali, almuradi nipate hela kidogo. Nipate kula. Nipate afua… niipate riziki yangu. Nahitaji chakula, nahitaji nauli kurudi Kigamboni, nahitaji ajira. Kila kitu nahitaji.
“…nifanye chochote nisife njaa, nisife wakati natamani… Nisaidie kakangu, ni…sa…i…di…e.” Ni nadra kumpata mwanamke wa namna yake mjini siku hizi, nadra sana.
Ni miezi sita tangu nigurie hii nchi, sina ajira, sina kibarua, sina hata kibanda. Maisha yalikuwa yashachukua mkondo mpya. Mkondo wa shida na dhiki.
Nilimpenda na kumpenda zaidi kila hatua.
Nikakimbia mguu niponye. Nilikimbia nisijue niendako. Nikakimbia.
Taharuki
Mwanzoni, tunabaki kujiuliza maswali kadhaa kuhusu msimulizi. Ni nani, yuko wapi na anasumbuka kwa nini. Haya yanatanzuka taratibu masimulizi yanavyozidi.
Tumaini anatuambia kuwa ana mwana, Radhi, ambaye amemwacha kwa bibi yake, Farida. Hatujajuzwa kuhusu wazazi wake, na mazingira aliyopata huyo mtoto, kwani ni wazi kuwa hana mume.
Jenifa ni rafiki ya Tumaini ambaye anamkidhia mahitaji yake ya kimsingi. Hatujaelezwa zaidi kumhusu, hususan usuli wake wala kazi anayofanya.
Tumaini anafikiri kwamba Romeo ni Mkenya, lakini anagundua baadaye kwamba asili yake ni Zanzibar. Romeo awali anamwambia kwamba alimwona Westlands, jijini Nairobi. Hatujui iwapo ni ukweli aliwahi kumwona au amejua ni Mkenya tu kwa mbinu nyingine. Tumaini mwenyewe anakana japo tunajua ni Mkenya.
Tumaini anapogundua nia ya Romeo, anafaulu kuponyoka kutoka garini mwake na kuyoyomea vichakani. Hatujui hatima yake ni gani.tunabaki na maswali tele. Je, atajua vipi njia ya kurudi Kigamboni? Ataendelea kusaka ajira au atahiari kurudi Kenya? Tuseme hatarudi nyumbani, Jenifa atachukua hatua gani? Na je, Romeo aliyemtoroka atamfuata au labda kumnasa kwa mbinu ya giza? Tamaa ya Tumaini itafika kikomo au ataendelea tu kutamani? Na maswali mengi mengine.
Methali
Maskini hachoki, na akichoka keshapata.
Usiende kwa wenzako mikono mitupu kwani hairambwi.(mkono mtupu haurambwi) Maisha ni kuishi leo, wa kesho aishile?
Chuku
Napunguza mwendo kwa kuishiwa na nguvu, tumbo limebanana na mgongo, usiseme njaa.
…kidevu kimenyolewa vizuri utadhani kimechongwa na kuacha uso kung’aa.
…na sasa kakutana na mwanamume mtanashati zaidi duniani.
Romeo akaanza kunipapasa taratibu. Nikahisi msisimko wa aina yake, kama mizuka inanipanda vile. Nikamwangalia usoni, anametameta… mara anageuka mweupe, mara mwekundu!
Taswira
Taswira ya mume wa Nina; …alivyokuwa na mume mzuri, mrefu kiasi, si mweusi si mweupe. Tabasamu nzuri iliyoficha pua ya kubabatana. Asiyekonda wala kuwa mnene. Miguu iliyojaa vizuri na kulainishwa na weusi wa malaika…
Taswira ya Tumaini pale Coco Beach; ufuoni nikanunua kaukau za muhogo na soda ya pepsi. Nikatandaza pareo yangu, nikakaa nikiangalia bahari… ile bahari iliashiria maisha yasiyokuwa na mwisho…
Taswira ya Romeo; Alikuwa wa asili ya Kiarabu. Mweupe, macho yake ya wastani meupe kama theluji ila malegevu. Uso wenye umbo la embe dodo, kidevu kimenyolewa vizuri utadhani kimechongwa na
kuacha uso kung’aa. Nywele za singa zinanukia udi hasa. Mwili wote unanukia riha ibura ya uturi. Mikono imechongeka vizuri kwa misuli ya wastani. Kifua nacho ni cha ngao. Usiseme maguu manene yaliyoketi vizuri kwenye kaptura lake la buluu.
Pale Romeo anapompeleka Tumaini; …Romeo aliegesha gari, akaanza kunionyesha majumba ya kifahari kwenye ufuo wa bahari, penye miti iliyoshika rangi yake ya kijani.
Kuchanganya Ndimi
Romeo na Tumaini wanapokutana katika Coco Beach, wanazungumza kwa lugha ya Kizungu. Mara ninaona Booking Office ya mabasi yaitwayo Tahmeed…
Nikashika njia mpaka Coco Beach.
Tukapiga selfie… Tukatifua vumbi la beach na kuondoka. Nakumbuka tu akiambiwa, “We need her blood, faster!” Kisengerenyuma/ Mbinu Rejeshi
Tumaini anakumbuka maisha yake ya tangu utotoni akiwa kwenye stendi alikoketi. Anakumbuka alivyotoka kwao Kenya, alivyoishi na Nina kwa muda akimkidhia mahitaji yake na baadaye kuhamia kwa rafikiye Jenifa.
Tumaini anapotembea mjini Kariokoo, anaona ofisi za mabasi ya Tahmeed. Anasema kuwa aliyajua mabasi haya tangu Kenya.
Koja
Ni miezi sita tangu nigurie hii nchi, sina ajira, sina kibarua, sina hata kibanda. Chakula, sabuni ya kuoga, mafuta na vitu vingine vidogovidogo.
Niliisubiri sana siku hii. Inifae, inikubali, iniridhie, inifanikishe mimi.
Tabaini
Alinifunza mambo ainaina; si upishi, si kuishi na watu kwa wema na kunitoa usungo.
Misimu
Bora uhai!- kauli ya kujipurukusha kutokana na dhiki. Konda- kondakta, anayekusanya nauli garini.
Mbinu nyingine ni pamoja na Mdokezo, Kejeli, Lahaja na Nidaa.
Pupa- F. M. Kagwa Mtiririko
Mwakuona amezaliwa na kulelewa katika mtaa duni na nduguze, ambapo amekumbana na dhiki si haba katika maisha yake. Wanapatwa na utapiamlo kwa kupungukiwa na chakula na kuwa na nywele za hudhurungi na miguu ya matege. Hata hivyo, bado ni mtiifu, mcha Mungu na anatia bidii masomoni.
Jioni moja akitoka shuleni, anamwona bibi fulani akimwangalia kutoka mbali na hatimaye kumsalimu anapomfikia. Anamwambia kuwa ni wakala wa kampuni fulani mjini ambayo inatafuta vijana wa kudhamini. Mwakuona anaona hii kama fursa yake ya kupata afueni, hasa anaposikia kuna masomo ya juu. Wakala huyu anavutiwa na sura ya Mwakuona anapomkagua. Yuko kidato cha tatu na amebaleghe na kuwa na umbo nzuri. Wanakubaliana, huku Bi. Mtego akiahidi kumtayarishia pasipoti na visa kwa muda wa wiki moja. Anampa kijisimu ili wawasiliane, lakini anaonywa kisionekane na yeyote, hata wazazi wake. Wataambiwa kila kitu kikiwa tayari.
Mipango inakamilika na Mwakuona anatoka nyumbani kisirisiri, akijiandaa kama anayeenda shuleni. Anapofika mjini, anabadilisha kwenye choo cha umma na kuvaa mavazi aliyopatiwa na Bi. Mtego baada ya kuvua sare. Anampigia Bi. Mtego naye anakuja kumchukua. Anapelekwa katika chumba maalum wanakolainishwa miguu, nywele na kulishwa vizuri na wenzake wanaopatana huko. Wengine wanaondoka kwa furaha. Wanaandaliwa kwa majuma sita na kubadilika kabisa na kutiwa vipodozi na mapambo. Mwinamo nako, ametafutwa kila mahali bila mafanikio. Wazazi hawana picha yake wala hela za kuwalipa polisi.
Anapoondoka matayarishoni, anakumbuka hajawahi kumwona tena Bi. Mtego wala kuwasiliana naye, na kisimu kilikwishachukuliwa. Anaendeshwa na dereva lakini kapewa nguo fupi. Anatarajia kupelekwa uwanja wa ndege, lakini gari linalenga asikojua. Anajipata kwenye jengo lililoandikwa Chenga-ways, anakopokelewa na watu wanaomjua kwa jina.
Anaona wanawake wanaotembea mbele ya wanaume nusu uchi, huku wanaume wakiwachagua na kuelekezwa vyumbani. Wanaume wanalipa na kuwafuata. Anaambiwa anayemchukua ameamuliwa na hapo anamfuata mwanamapokezi. Wanapita mapokezi mengine ambapo wasichana wananengua viuno mbele ya wanaume na kunyakuliwa. Analenga kuona kaunta ya wanaosafiri. Anakutana na msichana waliyekuwa pamoja matayarishoni. Anataka kumsalimu lakini mwelekezi wake anamzuia. Anaingizwa kwenye chumba na mlango kukomelewa.
Anampata mwanamume anamsubiri, akimwambia kuwa alimchagua na kumlipia pesa nyingi. Mwakuona anakumbuka matukio ya awali tangu Bi. Mtego, kutoroka nyumbani, matayarishoni, na sasa hapa alipo. Anajaribu kupinga hatua za yule mwanamume lakini inambidi kukubali madhara aliyojiletea mwenyewe. Anaporejeshwa chumbani walimo wenzake, Mashaka, aliyekaa pale kwa muda anamliwaza.
Anamweleza nia yake ya kutoroka, kutafuta haki na kurudi masomoni. Mwakuona anaapa kutoroka pale huku akiwalaumu wanaoendesha biashara hii, Bi. Mtego aliyemnasa na serikali iliyofumbia macho hali hii, baadhi ya wateja wakiwa maafisa wa serikali. Anajilaumu pia kwa kuhadaiwa kwa urahisi.
Ni miezi saba imepita na amepitia mengi. Leo yuko mbioni kutoroka, na nyuma anaandamwa. Alifaulu kwa kuomba ruhusa kwenda msalani akawa hajafuatwa. Anasikia sauti, ambayo inatolewa na bati lililobambatuka na kuacha mwanya. Anarusha viatu nje na kusikia mtu akikemea kisha vishindo vyake akitoroka. Anaruka na kufikia mtambaapanya, anapita na kujirusha nje licha ya bati kumkwaruza.
Anafuata njia yenye giza asionekane. Amekimbia kwa tahriban saa nzima na amechoka kabisa. Anashindwa kuendelea na kuketi kando ya kijia, kiatu mkononi tayari kujikinga.
Ana malengo matatu makuu. Kwanza, analenga kufika nyumbani, japo hajui kama watamkubali. Pili, ni kutafuta kituo cha polisi na kueleza yanayotukia huko Chenga-ways alivyoahidiana na Mashaka, ambaye hajui aliko. Tatu ni kwenda kwenye kituo cha habari na kusimulia yaliyompata ili watesi wao waanikwe, na labda kuchukuliwa hatua. Kutoka Chenga-ways, wanamsaka kila mahali baada ya kuona shimo alikotokea na alama za damu. Wengine wanachunguzwa wasiwe na nia ya kutoroka. Jua linapochomoza, anakuona nyumbani kwao, Mwinamo kwa mbali.
Ufaafu wa Anwani ‘Pupa’.
Ina maana ya papara au haraka katika kutekeleza jambo. Ina madhara mengi, mazuri na mabaya. Kuna methali isemayo kwamba mwenye pupa hadiriki kula tamu.
Mwakuona anapokutana na Bi. Mtego na kusikia nia yake ya kumpeleka ng’ambo kufanya kazi, anamezwa na pupa na kukubali masharti yake mengi bila kuyawazia sana. Anaiona hii kama fursa yake ya kuwa na maisha mazuri na kusaidia familia yake pia.
Bi. Mtego anampa simu ambayo anafaa kuificha na kuitoa faraghani. Haifai kuonekana na yeyote, hata msiri wake wa karibu zaidi wala wazazi wake. Anaificha kusikoweza kufikika na mikono ya ziada.
Anaposubiri kwa wiki, muda huu anauona kama mwaka kutokana na pupa aliyo nayo kwenda ng’ambo. Anahiari kuacha hata familia yake na masomo yake.
Mwakuona anaondoka nyumbani kwa pupa siku ya miadi kwa jitihada tele kufika mjini, anakofaa kukutana na Bi. Mtego. Anajifichaficha na kuwahadaa watu hadi hatimaye anapofika mjini. Anabadili
sare na kuvaa mavazi aliyopatiwa na viatu, kisha kumpigia simu wakala wake. Anashangaa kwa nini mhisani wake ndiye anamtumikia. Hata hivyo, pupa haimruhusu kuchunguza hilo. Anaona ng’ambo tu!
Katika matayarisho, anafanyiwa mengi. Anatengenezwa nywele na kukandwa kisha kulainishwa ngozi. Anahudumiwa kwa muda wa majuma sita pamoja na wenzake, huku wakilishwa vyakula vizuri. Huduma zote hizi ni za bure. Wanarembeshwa zaidi na kuvikwa mapambo ya kila nui. Haya yote hayamtumi kushuku anachoandaliwa, akili yake inalenga ng’ambo bado.
Muda wote wa matayarisho, hajamwona wala kuwasiliana na Bi. Mtego. Simu nayo ilikuwa keshachukuliwa. Hayo hayamtumi kuwa na maswali yoyote. Hata anapogundua kwamba amevishwa nguo fupi, anawaza labda ndio ustaarabu wa ng’ambo. Hata anabebwa na dereva wake peke yake. Anatarajia kuona uwanja wa ndege baada ya kutoka hapa.
Mwakuona anapofika Chenga-ways, anauliza kuhusu safari yake ya ng’ambo. Vicheko vya wanawake nyuma ya kaunta havimgutushi kuhusu shughuli za huku. Hata anapoitwa, anainuka kwa furaha na kiherehere kumfuata mwelekezi. Anatarajia kupelekwa kwenye uwanja wa ndege na kusahau shughuli za pale. Akilini, imejaa taswira ya ng’ambo.
Mwakuona anapambanukiwa na mambo anapojikuta ndani ya chumba mikononi mwa mwanaume, tena mlango ushakomelewa. Hana la kujinasua, bali inamlazimu kukubali matokeo. Sasa anagundua jinsi pupa ilivyomziba macho na kumweka hatarini.
Pupa ya kutoroka inampata Mwakuona, na inatiliwa mkazo na rafiki yake Mashaka, anayemweleza hali iliyomkumba. Wanakubaliana kuhepa kwa vyovyote vile na kusaka haki kwa ajili yao na pia kwa ajili ya wenzao. Anamlaumu Bi. Mtego, mwenye Chenga-ways na wateja wa pale, na pia serikali kwa kufumbia macho biashara kama hizi. Lakini anaapa jambo moja, chuma chao ki motoni!
Anakumbuka ushauri wa mwalimu wake Bw. Mpevu kuhusu kufanya maamuzi yanayofaa katika maisha yao. Anashangaa kwa nini hakufuata ushauri wake, msichana wa kidato cha tatu pale alipo, akadanganyika kwa urahisi hivyo. Anakiri kwamba ni pupa imemwingiza humu na kujilaumu, lakini anaamua kupambana kujitoa. Anashangaa iwapo wasichana walioandaliwa pamoja hakuna aliyejua yanayowasubiri. Haikosi nao pupa iliwaziba macho.
Pupa inamwezesha kutoroka Chenga-ways. Anaingia msalani usiku wa manane na kutoka kwa haraka kupitia kwenye tundu lililoachwa na bati lililobambatuka. Licha ya kufaulu, anakwaruza na kuvuja damu. Anatoka na kutafuta viatu alivyotangulia kutupa nje na kupata kimoja. Anakichukua na kutoka mbio.
Anapitia upembe wenye giza asionekane.
Japo wamemwandama, bado ana pupa ya kutekeleza maaganao yake na Mashaka. Anaazimia kufika nyumbani na kuomba msamaha, japo hajui iwapo watampokea. Anaazimia pia kutafuta kituo cha polisi kutafuta haki, na pia kituo cha habari kuwaanika wale mahasidi. Kunapopambazuka, anakuona mwinamo kwa mbali. Kuna tumaini.
Pupa pia ndiyo inamsukuma Bi. Mtego kumtendea Mwakuona unyama ule. Anamhadaa kwa ahadi za ng’ambo. Nia yake ni kunufaika kwa malipo kutokana na biashara hii haramu. Ana pupa ya kupata hela za haraka.
Wateja wa Chenga-ways pia wana pupa ya mahaba. Wanachagua wasichana kati ya wanaocheza densi mbele yao na hata kuwalipia kwa ajili ya huduma zao. Pupa inawatuma kuwaharibia maisha wasichana kwa kuwakatizia masomo na kuwadhulumu kimapenzi.
Dhamira ya Mwandishi
Ananuia kuonya dhidi ya pupa katika maisha na madhara yake.
Anawasilisha dhiki na matatizo yanayowaandama walio katika kimo cha chini kiuchumi. Anawasilisha ulaghai ulivyokithiri katika jamii na hasara zake.
Anawasilisha biashara haramu zinazoendeshwa katika jamii na kudhihirisha madhara yake. Anasawiri masaibu yanayoandama mtoto wa kike katika jamii.
Anawasilisha umuhimu wa kuwa na fikra pevu za kugundua dalili za hatari inapokuja.
Maudhui Umaskini
Mwakuona amezaliwa katika familia ya kimaskini. Wanaishi katika mtaa duni wenye nyumba zilizojengwa karibu kwa mabati makuukuu, udongo, mahema makuukuu na hata katoni. Zinajiinamia na kuwa na thamani ya chini kama wanaoishi huko. Wakazi wanazaa watoto wengi, huku wakiwa na imani mmoja akifanikiwa, atatoa familia katika umaskini.
Mwakuona anaona mengi katika maisha yake. Ana nguo moja ambayo anafua na kungoja ikauke avae. Wazazi wake wanataabika kuwalisha kila siku. Yeye na ndugu zakewakubwa wanalazimika kukwangura mabaki na ukoko ili wachanga wapate angaa tonge. Wanapatwa na utapiamlo na unyafuzi. Nywele zinageuka hudhurungi na miguu kufanya matege. Miguu isiyojua viatu inakaukiana na kujaa tekenya.
Bi. Mtego anatumia umaskini wa Mwakuona kama chambo cha kumnasia. Anamweleza kuhusu kampuni ambayo inafadhili safari za vijana kwenda ng’ambo na kuwafadhilia masomo. Hali hii inamtia Mwakuona hamu ya maisha na kuondoka umaskini. Anakubali rai yake. Anaona akilini mwake maisha mazuri, vyakula vya kifahari na nguo nzuri. Anaazimia hata kuhamisha familia yake hadi mtaa wa kifahari na kuelimisha nduguze.
Umaskini pia unakatiza juhudi na tumaini la wazazi wa Mwakuona kumpata. Hawajampigisha picha awali kutokana na hali yao. Isitoshe, hawana hela za kutosha kuwasaidia polisi kumsaka au kama
wanavyosema wao, ‘kuwatilia gari mafuta’ . Wanakata tamaa ya kumwona mwanawe. Mwakuona anapotoroka Chenga-ways, anashangaa iwapo watamkubali. Aliondoka maskini wa mali, sasa ni maskini wa kila kitu.
Tamaa
Tamaa ndiyo inamwuza Mwakuona na kumtumbukiza kwenye danguro. Anaelezwa na Bi. Mtego kuhusu kampuni ambayo inawafadhili vijana kufanya kazi na pia kuwagharamia elimu. Hali hii inamtia Mwakuona mshawasha wa kuishi maisha mazuri. Anaanza kujiona akiwa na maisha mazuri, akila vyakula vizuri na kuboresha maisha ya aila yake.
Shughuli zote kutoka Mwinamo, kupelekwa matayarishoni na kufanyiwa maandalizi zinaashiria wazi kwamba hakuna ng’ambo wanayokwenda. Hata hivyo, tamaa ya maisha mazuri haimpi nafasi Mwakuona kushuku yanyowasubiri.
Bi. Mtego pia anamnasa Mwakuona kutokana na tamaa. Anamtumia kama kitega uchumi kwa kumuuza kwenye danguro huko Chenga-ways. Anamhadaa ili kupata malipo yake. Anapoingia mtegoni, anamkabidhi na kuelekea kunasa mwingine.
Wateja wa Chenga-ways pia wamejawa na tamaa ya mapenzi. Wanawachagua wasichana miongoni mwa wale wanaocheza mbele yao na kisha kuwalipia kisha kwenda kujiburudisha nao. Wengine wananyakuliwa bila hiari kama Mwakuona na Mashaka. Bila shaka, mwenye huku amesukumwa na tamaa ya kupata pesa haraka.
Ulaghai
Bi. Mtego anamhadaa Mwakuona kwa ahadi ya kumpeleka kazini ng’ambo na kuyaboresha maisha yake. Anamwambia kwamba asiwaambie wazazi wake, kuwa watafahamishwa kila kitu wakati atakuwa tayari kuondoka nchini. Mwakuona anapatiwa simu. Bi. Mtego anamhudumia kwa kila hali hadi anapotimiza azma yake na kumpeleka matayarishoni.
Mwakuona anapofika kwenye maandalizi, anapatana na wasichana wenzake. Hapo, wanapata huduma za kipekee. Wanakandwa mwili na kulainishwa ngozi, huku wakilishwa vyakula vizuri. Wanafurahia huduma hizi za bure, wakiamini wanaandaliwa kwenda ng’ambo. Ukweli, hata hivyo, ni kwamba wanatayarishwa kuuzwa kwenye danguro.
Mwakuona anabebwa na gari lenye dereva akiwa pekee ndani. Anajihisi kama malkia, bila kujua yanayomsubiri.
Anapambanukiwa na mambo hatimaye anapojipata kule Chenga-ways, mikononi mwa mwanaume ambaye amemlipia tayari. Anaishi kule na kupitia mengi hadi anapofaulu kutoroka baada ya miezi saba.
Ufuska/ Ukware/ Uzinzi/ Uasherati.
Bi. Mtego anamtega na kumwingiza Mwakuona kwenye danguro. Mwakuona anajiandaa kwenda ng’ambo kama ahadi ilivyosema, lakini anapotolewa kwenye maandalizi, anaelekezwa Chenga-ways ambako biashara ya ufuska inaendeshwa.
Mwakuona anapofika, mwanamapokezi anamwambia kuwa kuna watatu wanaomng’ang’ania. Mwakuona anafikiri anarejelea waajiri. Anasikia vicheko nyuma ya kaunta. Hali halisi ni kwamba ni wanaume wanaomng’ang’ania ili wazini naye kwa kuwa ni mrembo sana.
Mwakuona anawaona wanawake ambao wamevaa nusu uchi wakitembea kwa madaha mbele ya wanaume huku wakiwakagua. Wanaume wanachagua wanaotaka, ambao wanaelekezwa katika chumba fulani. Wanaume hawa wanalipa na kuelekea kutimiza ashiki zao.
Anapoelekezwa kwenye chumba chake, anaona wanaume wamekalia viti kama huko alikotoka, wanachagua wasichana kati ya wanaonengua viuno mbele yao, huku wamevaa viguo vinavyoning’inia viunoni.
Mwakuona anapoelekezwa chumbani mwake, kuna wanume wanaokutana nao, ambao wanageuka tena kumwangalia. Anakutana na msichana waliyekuwa pamoja maandalizini. Anataka kumpiga pambaja lakini mwanamapokezi anamzuia. Msichana yule anamwambia kuwa atajulia huko mbele. Yeye ashayajua tayari.
Mwakuona hatimaye anafikishwa kwenye chumba, kuongozwa ndani na mlango kukomelewa. Anamkuta mwanamume ambaye anamsifia kwa urembo wake na kumweleza kwamba ameshalipa kwa ajili yake. Mwakuona anajaribu kubisha akisema yeye si kahaba, lakini tayari ashafika kichijioni, hana namna ya kujiopoa.
Mwakuona anapoondoka pale, machozi hayamkauki machoni. Mashaka anamweleza yaliyomkuta katika danguro hilo kwa miaka miwili aliyokaa humo. Wanakubaliana kujiopoa kutoka kwenye ufuska huu.
Mwakuona anaishi hapo kwa miaka saba na kupitia mengi katika danguro hilo japo hatimaye anafaulu kutoroka.
Nafasi ya Mwanamke
Mwanamke amesawiriwa kama bidhaa au kitega uchumi. Mwakuona anamezwa na tamaa ya maisha mazuri na kuishia kuanguka kwenye mtego wa Bi. Mtego na kuingizwa danguroni. Bi. Mtego anamtendea haya yote kutokana na tamaa ya kujipatia hela.
Mwanamke anachukuliwa pia kama chombo cha kumstarehesha mwanamume. Mwakuona, Mashaka na wasichana wengine wengi wananaswa na kuuzwa kwenye danguro ili kuwahudumia wanaume kimapenzi huko Chenga-ways.
Mwanamke pia anachukuliwa kama kifaa cha kumpandeza na kumburudisha mwanamume. Mwakuona na wenzake wanapelekwa katika matayarisho ili kuwapendeza wateja wao. Wanakandwa miili na kulishwa vizuri hadi wanapoimarika na kisha kupelekwa danguroni. Huko, anawapata wanawake wanaonengua viuno na wengine kujishaua mbele ya wanaume, ambao wanawanyakua wanaowapendeza.
Mwanamke anachukuliwa pia kama mtumwa, hasa wa kimapenzi. Mashaka anamweleza Mwakuona mengi aliyopitia katika maisha yake pale Chenga-ways, ambapo ameishi kwa miaka miwili. Alitwaliwa bila hiari yake, kama anavyofanyiwa Mwakuona, na bila shaka wasichana wengine wengi. Mwakuona anapobishana na mwanamume anayemsubiri, anamweleza kwamba hana hiari, yuko mikononi mwake.
Ufisadi
Wazazi wa Mwakuona wanapogundua kwamba ametoweka, wanamtafuta bila mafanikio na kuamua kupiga ripoti kwenye kituo cha polisi. Huko, hawapati msaada, kwani polisi wanawataka ‘kuwawezesha’ kumtafuta, yaani kutoa hongo au ‘kuwatilia gari mafuta’. Hali hii inazika juhudi zao za kumpata mwanao.
Mwakuona analaumu serikali kwa kufumbia macho biashara haramu kama inayoendeshwa huko Chenga-ways. Anasema kwamba baadhi ya wateja huko ni maafisa tajika serikalini. Kuna sehemu ya serikali ambayo inajua suala hili lakini haichukui hatua. Bila shaka, kuna wanaotumia biashara hii katika serikali kujinufaisha.
Migogoro.
Mwakuona anajipata kwenye mgogoro na mhudumu mmoja anayemwona akitoka msalani kubadilisha mavazi, anapokuja mjini kukutana na Bi. Mtego. Anataka kujua kwa nini yuko mjini bila sare badala ya kuwa shuleni. Mwakuona anamjibu kwa ufidhuli kuwa hayo hayamhusu.
Mwakuona yuko kwenye mgogoro na mwanamapokezi pale Chenga-ways. Anataka kujua wakati wa ndege yake kuondoka, kwani yeye anatamani kwenda ng’ambo. Anapokutana na msichana waliyekuwa pamoja matayarishoni, anataka kumpiga pambaja lakini mhudumu anamzuia. Anamwelekeza moja kwa moja hadi chumbani mwake.
Mwakuona pia anagombana na mwanamume anayemsubiri kwenye danguro. Anamsifia kwa urembo wake na jinsi alivyofanya chaguo bora. Mwakuona anajaribu kubisha akimwambia kwamba yeye si
kahaba, lakini mwanamume huyu anamfokea, akimkumbusha kwamba amelipa hela nyingi kwa ajili yake. Hana namna ya kumhepa.
Mwakuona anazua mgogoro kule Chenga-ways baada ya kutoroka. Wanajua ni hatari, na lazima wamtafute asije akamwaga mtama kwenye kuku wengi. Vyumba vyote vinapekuliwa kuhakikisha hakuna aliye na nia ya kutoroka. Wanamwandama kwa kila mbinu; kwa magari, kwa baiskeli na hata wengine kwa miguu. Mwakuona naye amejikunyata kando ya kijia, kiatu mkononi, tayari kujikinga. Azma yake kuu ni kufika kwa polisi kuripoti yanayoendelea huko na kuwaanika waovu wale kwenye vyombo vya habari.
Mwakuona pia yuko katika hali ya mgogoro na wazazi baada ya kuondoka bila taarifa. Sasa hajui iwapo watampokea, japo azma yake kuu ni kurudi nyumbani. Wazazi wake ni wacha Mungu, haoni kama watamkubali tena alivyo, tambara mbovu, maskini wa utu na mali.
Dini
Licha ya kuzaliwa katika familia maskini, tunaambiwa kwamba Mwakuona alikuwa mcha Mungu, kama alivyolelewa na kuelekezwa na wazazi wake. Hata anapoingizwa danguroni, anajuta sana kwa kuwa ni kibiritingoma wa kulazimishwa, anatenda dhambi bila hiari.
Mwakuona anapofaulu kutoroka, bado hajasahahu suala la dini. Anamkumbuka na kumwomba Muumba amwepushe na shari, afike asikokujua.
Mwakuona pia anapania kurejea kwao Mwinamo baada ya kufaulu kutoroka. Hata hivyo, linalomtatiza ni iwapo wazazi wake watamkubali tena, kwani ni wacha Mungu, naye tayari ni tambara mbovu.
Maudhui mengine ni pamoja na Udhalimu, Kazi, Familia na Malezi, Unafiki na Ushirikiano.
Wahusika: Sifa na Umuhimu. Mwakuona
Ni msomi. Kisa hiki kinapoanza, ni mwanafunzi wa shule ya upili, katika kidato cha tatu. Amesoma kwa taabu kufikia hapo, kwani amezaliwa katika familia ya kimaskini kwenye mtaa wa mabanda.
Ni msiri. Tunaambiwa kuwa anapopatiwa simu na Bi. Mtego na kuagizwa isionekane na yeyote, kuweka siri si jambo ngumu kwake. Anaitunza simu ile na kuificha kwa siku saba, isionekane na yeyote. Anafaulu kuondoka nyumbani bila yeyote kujua wala kushuku lolote.
Ni mwenye pupa. Anapodokezewa na Bi. Mtego kuhusu mpango wa kazi ughaibuni, anatekwa mara moja. Anakubali kwa haraka na kutii maagizo yote ya bibi huyu hadi anapojipata matatani.
Ni mcha Mungu. Tunaelezwa kuwa kama wakaazi wengine wa Mwinamo, Mwakuona ana imani ya kidini. Hata anapoingizwa danguroni, inamwuma kuwa anatenda dhambi bila hiari.
Ni mwenye mapuuza. Kuna dalili tosha kwamba Bi. Mtego anamhadaa, lakini anakosa kabisa kuzitia maanani. Bi. Mtego anamhudumia na kumtaka aweke mipango yote siri, kisha anapoingizwa matayarishoni, bibi huyo anatoweka. Anakumbuka ushauri wa mwalimu wake aliopuuza akiwa mashakani tayari.
Ni mkakamavu. Anaamua kwamba atatoroka kutoka Chenga-ways kwa mbinu zote, na anajikakamua hadi anapofaulu. Tangu alipoanza mipango ya kutoroka, anaapa kutafuta haki, jambo ambalo anaazimia kufanya.
Ni jasiri. Anafaulu kutoroka kwa ujasiri kupitia tundu kwenye msala. Hata sauti ya mtu anayosikia haimzuii kuhepa. Anaamua kupitia njia yenye giza, tayari kukumbana na lolote.
Umuhimu wa Mwakuona.
Kupitia kwake, dhiki ya maisha kwa vijana wanaozaliwa na kulelewa mitaa duni inadhihirika. Anawakilisha mashaka yanayomkabili mtoto wa kike katika maisha.
Kupitia kwake, ukiukaji wa haki unadhihirika na jinsi unavyoendeshwa.
Ni kiwakilishi cha pupa katika mambo na jinsi inavyoweza kuleta madhara.
Anawasilisha nafasi ya elimu na umuhimu wake katika kujenga na kuendeleza jamii, pamoja na wasomi binafsi.
Bi. Mtego
Ni laghai. Anamdanganya Mwakuona kwa kumwahidi makuu; kufanya kazi ng’ambo na kusoma. Anampa kisimu ili waweze kuwasiliana. Hatimaye, anakichukua tena baada ya kutimiza azma yake.
Ni mjanja. Anamwambia Mwakuona kuwa wazazi wake wataambiwa kila kitu mambo yakishakuwa tayari. Anafahamu vyema kuwa wakijua, mipango yake haitaenda vizuri.
Ni mnafiki. Anajitia urafiki na Mwakuona kama kwamba ananuia kumsaidia. Hata hivyo, nia yake ni kumwuza kwenye danguro ili kujinufaisha.
Ni msaliti. Anamsaliti Mwakuona kwa kumwingiza katika biashara ya uzinzi bila hiari yake, huku akimdanganya kuwa atampeleka kazini ng’ambo.
Umuhimu wa Bi. Mtego
Ni kiwakilishi cha wahalifu wanaojitia ufadhili ili kuendeleza maovu yao. Kupitia kwake, nafasi ya mwanamke katika jamii inadhihirika.
Kupitia kwake, tunabaini biashara haramu zinavyoendelezwa katika jamii.
Mashaka.
Ni mwenye huruma. Amamtuliza Mwakuona, ambaye ameemewa baada ya matukio ya Chenga-ways. Anamweleza kuwa amepitia mengi pale na kumtaka kunyamaza.
Ni mwenye utu. Licha ya kuwa amepitia mengi katika makao haya, bado hajapoteza imani. Anaona uwezekano wa wokovu na kumtaka Mwakuona wajinasue.
Ni mshauri. Anamshauri Mwakuona watie bidii na kujitahidi ili waweze kutoroka sehemu ile. Ananuia kuripoti kwa polisi na pia kutangaza kwenye kituo cha habari.
Umuhimu wa Mashaka
Ni kiwakilishi cha dhiki na matatizo wanayopitia vijana baada ya kutoswa kwenye biashara haramu katika madanguro.
Anawakilisha umuhimu wa urafiki, hasa katika nyakati za taabu. Anawakilisha nafasi ya mwanamke katika jamii.
Mbinu za Uandishi Tashbihi
Nyumba nyingi za kule zilijiinamia ovyo kwa uzee, kama zinazoomba msaada kwa yeyote aliyeziona. Ungetembea nyumbani kwao, ungedhani u shuleni kwa wingi wa watoto.
Mwakuona aliminywa na maisha mithili ya mjusi aliyebanwa na mchanja kuni katikati ya gogo na gome.
...miguu ikiwa myembamba kama ya korongo, Alikuwa msiri kama kaburi.
Japo aliziona siku hizo kama mwaka,
Nyumbani na shuleni alikuona kama jongoo na mti zilizofaa kutupwa pamoja.
Nauli aliyoachiwa pamoja na pesa za masurufu alizitunza kama mboni ya jicho lake,
Ili asionekane kama kuku mgeni mwenye kamba mguuni, Bi. Mtego alikuwa amempa viatu vya thamani kiasi na nguo alizoficha hadi sasa.
Mwakuona alifurahi ghaya kwa kuandaliwa kama malkia kamili.
...ngozi ikawa tepetepe kama ya mtoto mdogo,
...simu aliyopewa ilikuwa kama nguo ya kuazima isiyositiri makalio;
Walifuatana...amfuata mhudumu mfano wa kondoo amfuataye mchinjaji kuelekea kichinjioni. Kila neno alilosema lilikuwa kama msumeno ukatao kuwili,
...wakaona hali zao zalingana kama sahani na kawa.
“Dunia ni kama shamba la mahindi, huzaa mahindi na vizimwili.”
Chenga-ways kumwachilia ni sawa na kujitia kitanzi.
Alijikunyata pembeni kama kinda aliyenyeshewa kwa kuhofia kufumaniwa kabla ya kujibabadua,
...anahema kama njiwa aliyekimbizwa na mwewe. Anatetemeka kama kifaranga aliyenyeshewa.
Tashihisi
Nyumba nyingi za kule zilijiinamia ovyo kwa uzee, kama zinazoomba msaada kwa yeyote aliyeziona. Mwakuona aliminywa na maisha…
Si kwamba aliomboleza lakini yaliyomwandama hayakumkubali kutabasamu.
…hisani ya bibi yule ilimfunika macho, akaona kiwi, akajikuta amenasika.
Jengo la kifahari lenye jina Chenga -ways lilimkaribisha kwa taa za kumemetuka.
Haya yote yalijibiwa kwa micheko ya wanawake asiowaona nyuma ya kaunta. Ilimdhihaki na kuhanikiza kote.
Msichana yule…alipoona mwenzake anaelekezwa na wasiwasi umemwandama…
Mwakuona naye, sasa wasiwasi wautikisa mwili mzima, kajikunyata pale mlangoni, nyayo zimekataa kuelekea aliko yule mwanamume mgeni.
Kutokana na simanzi iliyomganda, machozi yamekataa kukauka… Fadhaa na jitimai zilimwandama Mwakuona usiku kucha,
Siku zimesonga, imetimia miezi saba.
Moyo wampapa, damu ikitaka kumsaidia kupambana na hali… Kule matlai, jua linachungulia, mchana wabisha hodi. Mbali huko, anakuona Mwinamo, bado kwainama mbele ya mitaa jirani ya kifahari.
Istiara.
Mwakuona alikuwa… mwenye heshima na bidii ya mchwa masomoni.
Mwakuona …akakubali bila masharti, naye mvuvi akajua amekwisha mnasa samaki mkubwa.
Bi. Mtego alipoona simu ya Mwakuona, akajua ndoano yake imenasa, chambo ki pale pale, angekitoa kinywani mwa samaki na kukitumia kunasia mwingine.
Bi. Mtego yu pale pale, nyangumi mzamisha madau.
Kila aliyetoka mle alikuwa kivuli cha aliyeingia, amekwishabadilika kabisa… Kwa Mwakuona, yote haya yalikuwa fumbo.
Alimwendea mgeni wake kwa kasi, kavaa tabasamu ya chui mchekesha swara,
Anakabiliwa na mwanamume ambaye ni wazi anatokwa na mate ya fisi, yeye ni kingugwa hasa, yu tayari kumhujumu!
Mwanamume Yule alilikaribia windo lake, akamwekelea mkono begani na kujaribu kumrairai… Bahati iliyoje kwetu sote kupatana! Mimi mtende, wewe thamani ya hela zangu!
Hana la kufanya… Ni jogoo hapo alipo, baada ya kurushiwa punje za mtama, akazifuata… Kwanza sharti turudi masomoni… tuwe ngome imara ya kuupinga udhalimu huu.
Maneno haya yaliyoleta dalili za mwanga gizani yalizibadilisha shake za Mwakuona zikabaki sinasina. Haya aliyaona kuwa maji yaliyokwisha mwagika, hayazoleki.
Hata kama anajihisi kuwa tambara bovu, ni tambara lao. Labada watalishona au hata walitumie kutandika mlangoni ua kupangusia nyayo.
Chenga- Ways nako, shughuli zote zimekwama. Bidhaa muhimu, mhimili wa biashara , umetoweka.
Semi
zilizojengwa kigugu- zilizojengwa kwa ukaribu.
kuzipa tabu kisogo- kuziacha tabu, kuzisahau au kuziondokea. akaona kiwi-akaona giza.
yalikuwa ya kumtoa nyoka pangoni- yalikuwa ya kuvutia. Hayakuhusu ndewe wala sikio- hayakuhusu kwa vyovyote vile. wakitembea mzofafa- wakitembea kwa kujishaua.
alipiga moyo konde- alijikaza, alijikakamua. asizozilalia wala kuziamkia- zisizomhusu hata kidogo. kumpiga pambaja- kumkumbatia.
kumtilia chambo- kumshawishi ili kumnasa. akiambua nyayo- akitembea kwa miguu. apige unyende- apige duru, atoe kelele. apige hatua- afanye jambo, afanye uamuzi. watapigwa kalamu- watafutwa kazi.
Methali
Kuzaa mwana si kazi, kazi ni kulea. Ng’ombe mkubwa ndiye hulalia miba, Usimwage mtama penye kuku wengi.
Nyumbani na shuleni alikuona kama jongoo na mti zilizofaa kutupwa pamoja(amtupaye jongoo humtupa na mti wake)
Ili asionekane kama kuku mgeni mwenye kamba mguuni(kuku mgeni hakosi kamba mguuni) Dau la mnyonge haliendi joshi.
Kuku wa maskini huliwa na kanu majirani wakiangalia.
Hayawi hayawi huwa.
Ilikuwa sawa na nguo ya kuazima isiyositiri makalio(nguo ya kuazima haisitiri matako) Cha kuzama hakina rubani
Kilichompata ngwena na kiboko ni chicho. Mbwa hafi maji aonapo ufuo.
Nyumbani ni nyumbani.
Ng’ombe akivunjika mguu malishoni hujikokota hadi zizini kufaliwa na wenzake wazima.
Maswali Balagha
…si mapya na ya thamani bora ameyakumbatia kiganjani?
Alimwendea alipokuwa, jambo lililomduwaza Mwakuona- iweje anayemsaidia ndiye anayemtumikia? Nani asingefurahia huduma hii ya kifahari, tena ya bure?
“Kuning’ang’ania?... mbona hamkufanya uamuzi mapema kuhusu mwajiri wangu? Ni wa nchi gani? Nasafiria ndege gani? Safari yangu ni ya saa ngapi? Mshahara wangu ni kiasi gani?”
“Hii ndiyo kazi ya ng’ambo niliyodanganywa naenda kufanya?”
Zingali tumboni wala hazimfai tena… kupigapiga mabawa kutamfaa nini?
“Dunia ni kama shamba la mahindi… Utakwendaje kuvuna ukakusanya vizimwili badala ya mahindi na kuvipeleka ghalani?”
Vipi yeye, mwanafunzi wa kidato cha tatu, asikumbuke ushauri wa shuleni, nyumbani na maabadini, akafanya uamuzi wa busara?
Mbele kuna pande mbili, wenye giza totoro na kwingine kuna mwangaza. Afuate njia ipi aepuke zahama?
Aelekee upande gani afike kule? Tena akifika, aila yake itampokea?
Bwana na Bi. Mtondo, wazazi wacha Mungu, watampokea mtoto ajaye akivalia kibiritingoma? Jamii itamkubali akija mkono tupu baada ya miezi saba?
Hata kama ni kazi ya ujakazi, aje bila chumvi mkononi, hana hata senti ya kusagia mkunguni?
Hadithi za mengi mabaya aliyopitia zitawafaa nini?
Walikuwa na mpango kabambe ila sasa mwenzake yu wapi?
Majazi
Mwakuona- Binti huyu anayaona mengi katika maisha yake. Anazaliwa katika familia ya kimaskini na kukabiliwa na matatizo chungu nzima. Hatimaye, anahadaiwa na kuingizwa danguroni. Anapotoroka, anaandamwa na kufikia tamati ya hadithi, hatujui anayaona mengine kiasi gani.
Mwinamo- ina maana ya kupinda kwenda mbele. Ni mtaa duni ambao una vyumba vibovu. Mtaa huu ‘umeinama’ kutokana na dhiki ya wanaoishi huko. Tunaambiwa kuwa Mwakuona, “…anakuona
Mwinamo, bado kwainama mbele ya mitaa jirani ya kifahari.”
Bwana na Bi. Mtondo. Mtondo ni siku baada ya kesho kutwa. Hawana matumaini ya kuimarika. Wanajishughulisha kupata lishe ya siku, ya mtodo hayawahusu. Fanaka yao haipo leo wala kesho, labda mtondo. Mwakuona wao anapopotea, matuamini yao pia hayapo leo wala kesho.
Bi. Mtego- ni mbinu inayotumika kunasa. Anamwekea Mwakuona mtego na kumnasa kisha kumtumbukiza kwenye uzinzi. Bila shaka anafanyia wengine hivyo. Anapomtia matayarishoni, anatoweka, bila shaka kuwawekea mtego wengine.
Chenga-ways- Maanake ni nia zisizo wazi. Wanaofikishwa pale wanafanyiwa hivyo kwa kuchengwa. Mashaka anatamani kutoroka lakini njia za kufanya hivyo zinaishia kuwa chenga sana kwake. Mwakuona analazimika kutumia chenga chenga kutoroka, lakini bado kuna chenga kwani anaandamwa kinyama.
Uwezekano wa kufaulu kutoroka bado ni chenga.
Kazamoyo- shule anakosomea Mwakuona. Ni shule ya watoto wa maskini ambao wanalazimika kukaza moyo katika maisha yao.
Mashaka- ina maana ya taabu anazopitia mtu katika maisha. Msichana huyu amepitia mengi pale
Chenga-Ways baada ya kutoroshwa kama Mwakuona na jitihada zake za kuhepa kutofanikiwa.
Bwana Mpevu- ni mwalimu wa Mwakuona. Ana mawazo mapevu kulingana na ushauri anaowapa. Anawataka wawe wapevu ili wafanye maamuzi ya busara.
Uzungumzi Nafsia
Sasa zahitaji tu kupelekwa saluni zioshwe kwa shampuu, zisingwe na kulainishwa kwa kitana moto. Miguu ikivishwa nguo za kazi na viatu vya mchuchumio, basi! Aliwaza yule wakala.
Masomo bila uwezo ni bure! Aliwaza.
Ila alijihimiza, “Chuma chao ki motoni!”
Pupa imenitumbukiza katika kisima nilichochimba, sasa naingia mwenyewe…
Mara kwa mara aliwakumbuka aliokuwa nao ‘matayarishoni’. Waliyajua haya au walikuwa mateka kama mimi? Mbona pasiwe na hata mmoja mwenye hekima atakuramshe, tutunge mbinu za kujinasua?
Koja
Mwakuona alikuwa mtiifu, mcha Mungu, mwenye heshima na bidii ya mchwa masomoni.
…hisani ya bibi yule ilimfunika macho, akaona kiwi, akajikuta amenasika.
Mwakuona aliposikia matumaini ya utajiri na masomo, alichanganyikiwa, akakubali bila masharti, naye mvuvi akajua amekwisha mnasa samaki mkubwa.
Msichana wetu aliona vyakula alivyotamani kama pizza, nguo za bei, rangi za kucha na za midomo, wanja machoni, kope na kucha za kubandika, mitindo ya kisasa ya nywele na urembo aina anuwai. Aliona mashangingi, akaona kasri, akaona ameheshimika katika jamii.
Kwa akraba yake, aliona akiwanunulia nguo za bei, vyakula aina aina, akaona akiihamishia kwenye mtaa wa kifahari, akiwaelimisha nduguze.
Asubuhi ya miadi ilikuwa na changamoto si haba- kujiandaa kama aendaye shuleni, chengachenga, kuvizia kwingi, kudanganya huyu na yule ili kufika mjini.
Kazi ikawa kula na kunywa vinywaji mzomzo, huku miguu ikisuguliwa kwa vifaa maalum vya kielektroniki, kutengenezwa nywele, kulainishwa uso kwa mvuke na mafuta ainaina kisha kusingwa na kukandwa mwili ili ulainike.
Kila aliyetoka mle…amekwishabadilika kabisa- mwili umelainika, ngozi ikawa tepetepe kama ya mtoto mdogo, nyusi zimenyolewa na kuchorwa upya na wasanii maalum wa urembu huku kope ndefu zimepandikizwa kwenye vikawa vilivyopakwa wanja uliofanana na rangi ya midomo.
Alimwendea mwenzake kwa kasi, kavaa tabasamu ya chui mchekesha swara, mikono kapanua, ataka kumpiga pambaja.
Mwakuona naye, wasiwasi sasa wautikisa mwili mzima, kajikunyata pale mlangoni, nyayo zimekataa kuelekea aliko mwanamume huyu mgeni.
Akili zake ziliupitia mzingile… tabu za nyumbani, masomo shuleni Kazamoyo, Bi. Mtego, ‘ng’ambo’,
chumba cha ‘matayarisho’, mapokezi ya pale alipo na hatimaye zikatua kwenye chumba alimokuwa sasa. Yule mwanamume… kuusifu urembo wake- umbo lake, urefu, ngozi, nywele na umri!
Ni jogoo hapo alipo, baada ya kurushiwa punje za mtama, akazifuata, akazidonoa, akazimeza kwa pupa, akanaswa. Zingali tumboni wala hazimfai tena, kisu chamwelekezea makali shingoni, macho kayatoa pima- kupigapiga mabawa kutafaa nini?
… walisimuliana hali zilizowaleta mle, wakapelekana utotoni, masomoni, wakona hali zao zinalingana…
…elimu inawasaidia kupata akili tambuzi, wachuje, watwae vifaavyo na kuacha vibaya.
Aliushika mtambaapanya, akavuta nguvu zake zote na kujinyanyua, akachupa hadi nje.
Amekimbia kwa muda wa takriban saa nzima, kalowa jasho chepechepe, anahema kama njiwa anayekimbizwa na mwewe.
Atatafuta kituo cha polisi, labda kwa msaada wa jamii yake, apige ripioti, asimulie yote yanayotendeka Chenga-ways. Aliamini polisi wangechukua hatua, wawanusuru maskini wenzake na kuiangamiza biashara ile haramu.
…alilenga kutafuta yalipo mashirika ya habari, asimulie yaliyomfika, wahalifu wale waanikwe.
Moyo unampapa, damu ikitaka kumsaidia kupambana na hali, autazame mstakabali wa maisha yake.
Kuchanganya Ndimi.
…aliona vyakula alivyotamani kama pizza…
Gari la kifahari lilimjia; atakuwa chauffer- driven, yeye pekee anabebwa back- left, afunguliwa mlango! “Kuna watatu wanaokung’ang’ania, you are a hotcake.”
“Kindly tell me, mbona hamkufanya uamuzi mapema…”
Kabla ya kuandama chaguo lake, mwanamume angeenda kulipa palipoandikwa Pay here.
Akasikia mmoja… akisema kwa sauti ya furaha, “Give me this beautiful queen of all slay queens… she’s wow!”
Alitaka kumsalimu ila mwelekezi wake akamwambia, “Not now!”
Taswira
Taswira ya mtaa wa Mwinamo, hasa majengo yake yaliyokaribiana yaliyojengwa kwa mabati makuukuu, udongo, mahema na hata katoni na karatasi.
Taswira ya watoto wa Mwinamo wenye utapiamlo na unyafuzi, nywele za hudhurungi, miguu myembamba yenye tekenya wala isiyovishwa viatu, iliyokaukiana na kuunga matege.
Taswira ya Mwakuona na wasichana wenzake wanapotoka matayarishoni. Wametiwa vipodozi na mapambo ya kila aina, na kubadilika kuwa wa kuvutia.
Taswira ya pale mapokezini ya wasichana wanaosakata densi huku wengine wakijishaua mbele ya wanaume wanaowateua watakao.
Taswira ya Mwakuona na mwanamume anapoingizwa chumbani na mlango kufungwa. Taswira ya mwanamume yule akimwendea na jinsi Mwakuona anavyomwambaa kwa hofu na jakamoyo tele.
Taswira ya Mwakuona anapotoroka kutoka Chenga-ways kupitia kwenye tundu msalani, kuvitupa viatu nje, changamoto anazopitia hadi hatimaye kufaulu kutoka humo.
Taswira ya Mwakuona akitoroka. Mbele yake anapata njia mbili, moja yenye giza na nyingine mwangaza na kuamua kupitia gizani. Anakimbia huku amelowa jasho na kupumua kwa nguvu.
Taswira ya Mwakuona tena mwishoni mwa hadithi; “Mwakuona angali anajikunyata nyuma ya kisiki. Baridi shadidi inamguguna. Anatetemeka… Moyo wampapa, damu ikitaka kumsaidia kupambana na hali… Kule matlai, jua linachungulia, mchana wabisha hodi. Mbali huko, anakuona Mwinamo, bado kwainama mbele ya mitaa jirani ya kifahari!
Kisengerenyuma.
Mwakuona anapokutana na Bi. Mtego anayempa habari za kampuni inayowaajiri vijana, anakumbuka tabu alizopitia maishani na kuona fursa ya kuziondoka.
Mwakuona anapotolewa matayarishoni, anakumbuka kuwa hajawahi kumwona Bi. Mtego wala kuwasiliana naye, kwa kuwa hata simu aliyopatiwa ilikuwa kanyakuliwa.
Mwakuona anapokabiliana na mwanamume katika danguro, anakumbuka matukio yaliyomfikisha hapo kuanzia tabu za nyumbani, masomo shuleni Kazamoyo, Bi. Mtego, ahadi za kwenda ng’ambo, matayarishoni na hatimaye alipo sasa.
Mwakuona na Mashaka wanapatiana hadithi za jinsi walivyotekwa na kutumbukizwa walipo na kuelezana waliyopitia maishani mwao, ikiwemo utotoni mwao na masomoni.
Mwakuona anajilaumu kwa kuanguka mtegoni mwa Bi. Mtego. Anakumbuka ushauri wa mwalimu wake, Bwana Mpevu kuhusu kufanya maamuzi ya busara na maonyo aliopatiwa shuleni, nyumbani na maabadini. Anawakumbuka pia wasichana aliokuwa nao matayarishoni na kushangaa iwapo walijua yaliyowasubiri.
Akiwa mbioni, Mwakuona anakumbuka makubwa aliyopitia Chenga-ways. Anakumbuka jinsi anavyotoroka baada ya kufaulu kuingia msalani bila kuandamwa, na kufaulu kutorokea kwenye tundu la msala. Anamkumbuka pia na Muumba wake na kumwomba amwepushe na shari.
Mwakuona pia anakumbuka maagano yake na Mashaka kuhusu kutafuta haki yao na wenzao kwa yeyote atakayefaulu kutoroka, jambo analoazimia kutekeleza.
Kinaya
Wakazi wa Mwinamo, licha ya kuwa wanazugwa na umaskini, wanakopoa watoto wengi. Wanaona kuwa wanaweza kupata wa kuwafaa kati yao. La ajabu ni kuwa hawawazii jinsi watakavyowalisha watoto hao kwa hali hiyo.
Rai ya Bi. Mtego kuwa Mwakuona asiwajuze wazazi wake haimpigi mshipa. Ni kinaya kwake kushikilia kuwa wazazi hawafai kujua hadi mipango inapotamatika. Kwa nini wasijue hali ni mwanao? Ni wazi kwamba huu ni unafiki lakini Mwakuona hatambui hilo.
Ni kinaya kuwa Mwakuona haoni dalili zote kuwa Bi. Mtego anamhadaa. Anayemsaidia bado ndiye anamhudumia, jambo ambalo halimpigi mshipa. Hata wanapofika kwenye danguro, bado akili yake inamwambia kuwa anaenda ng’ambo wala yanyotukia pale hayamhusu.
Mwakuona anamwuliza mhudumu kwenye kaunta kuhusu safari yake ya ng’ambo. Anashangaa kwa nini hawakuamua kuhusu mwajiri wake anapoambiwa kuna watu watatu wanaomng’ang’ania. Ni wazi
kwamba haya ni masuala tofauti na kazi ya ng’ambo. Hawazii haya angaa kujaribu kujinasua.
Ni kinaya kuwa kati ya wasichana wengi waliokuwa matayarishoni, hakuna hata mmoja aliyewaza kuhusu waliyokuwa wakiandaliwa, licha ya dalili kuwa wazi.
Mwakuona anaondoka nyumbani kwa matumaini makuu ya kuiboresha hali yake na ile ya aila yake. Ajabu ni kuwa badala yake, anarejea akiwa maskini zaidi, wa mali na utu!
Sadfa
Mwakuona anakutana na Bi. Mtego kisadfa akitoka shuleni bila kumtarajia.
Mwakuona anapomfuata mwelekezi kuelekea asikokujua, anakutana kisadfa na msichana waliyekuwa pamoja kwenye ‘matayarisho’ japo hawapatiwi fursa ya kuwasiliana.
Mashaka na Mwakuona wanakutana kisadfa, baada yake kuhujumiwa kule danguroni. Wanaishia kuwa na kisa kinacholingana na kuwa marafiki wa kutiana moyo.
Mwakuona anafaulu kutoroka kisadfa. Anaenda msalani usiku wa manane bila kuandamwa, kinyume na taratibu. Isitoshe, inasadifu kuwa choo hicho kiko pembeni na kina bati lililobambatuka, linalompa mwanya wa kuhepea.
Wakati wa kutoroka, anamsikia mtu upande wa pili akikemea kisha vishindo vyake akitoroka. Hakutarajia kumpata yeyote pale wakati huo.
Mwakuona anatoroka usiku wa manane na kujaribu kutafuta njia ya kurudi kwao Mwinamo asiijue. Kunapopambazuka na jua kuchomoza, anakuona Mwinamo kwa mbali.
Taharuki
Kulingana na maelezo ya Bi. Mtego, ni wazi kwamba anamdanganya Mwakuona wala hakuna ng’ambo anakompeleka. Tunaachwa na hamu ya kujua ni wapi hasa ananuia kumpeleka baada ya hadaa zote.
Wazazi wa Mwakuona wanakosa tumaini la kumpata mwanao kwa kukosa mbinu ya kumtafuta na msaada wa polisi kukosekana. Hatujui iwapo wanaendelea kujaribu kumsaka au wanamwacha tu.
Baada ya kutolewa kwenye ‘matayarisho’, anatarajia gari lielekee kwenye uwanja wa ndege lakini linalenga asikokujua. Kama Mwakuona amwenyewe, tunasalia na hamu ya kujua wanakoelekea.
Mwakuona anapokumbana na mwanamume anayemsubiri, anasema kuwa alimchagua yeye kati ya wengi. Hatujaelezwa vipi alimfahamu, kupitia kwa Bi. Mtego au wakati wa maandalizi. Isitoshe, mhudumu anasema kuwa kuna watu watatu wanaomng’ang’ania. Hatujui hao wengine ni wepi, na mbinu gani inatumiwa kuamua atakayemchukua.
Mwakuona akiwa katika harakati za kutoroka, anasikia sauti inayomtia kiwewe. Baadaye tunafahamu inatokana na bati lililobambatuka. Hata hivyo, hatujafahamishwa kwa uwazi ni nani aliyesonya na kutoroka baada yake kutupa viatu nje, tena alikuwa akifanya nini hapo wakati kama huo.
Mwishoni, tunabaki na maswali tele. Je, rafikiye Mwakuona, Mashaka, bado yuko kule danguroni? Atafaulu kutoroka? Na je, Mwakuona anarejea nyumbani? Wazazi wake na wakazi wengine wanampokea vipi? Wanamkubali katika jamii yao? Watamhurumia na kumfariji au kumlaumu na kumfokea? Na je, anafaulu kutimiza maagano yake na Mashaka? Iwapo atafaulu kufika kituo cha polisi na hata cha habari kutoa taarifa, wahalifu wale watachukuliwa hatua? Mashaka, Mwakuona na wenzao watapata haki? N.k
Jazanda
Dau tokomevu aghalabu humshawishi mpiga kafi kuelekea kwenye mawimbi. Dau linapopigwa na dhoruba, kujaribu kuyakumba maji huwa jitihada isiyo na mazao. Kuangamia hakuwi mbali. Papa na nyangumi husubiri azamaye azame, wamtie kinywani.
Ni jogoo hapo alipo, baada ya kurushiwa punje za mtama, akazifuata, akazidonoa, akazimeza kwa pupa, akanaswa. Zingali tumboni lakini hazimfai tena, kisu chamwelekezea makali shingoni, macho kayatoa pima- kupigapiga mabawa kutamfaa nini? Kuna kufa na kupona na kuliwa na kingugwa.
“Dunia ni kama shamba la mihindi, huzaa mahindi na vizimwili. Utakwendaje kuvuna ukakusanya vizimwili badala ya mahindi na kuvipeleka ghalani?”
Mbinu nyingine ni kama vile Nidaa, Mdokezo, Tanakali, Takriri na Dayolojia.