Mwongozo Wa Nguu Za Jadi | KCSE Setbooks Guide
Sun
05
May
24

Mwongozo Wa Nguu Za Jadi

  2 hr, 20 min, 25 sec  140,568 reads 
BUY NOW Ksh. 200

Jalada, Anwani na Muhtasari

 

Katika jalada la riwaya ya Nguu za Jadi, kuna vitu anuwai vinavyoonekana, na vinaweza kuwa na fasiri mbalimbali kwa wasomaji tofautitofauti. Vitu vilivyopo kwenye mchoro wa jalada hilo ni: 

 

a) Picha ya mwanamume mzee anayemzungumzia mvulana. Kutokana na wanavyoonekana, ni wazi wamefunikwa kwa kiwango cha haja na giza. Hii inaweza kuchukuliwa kama ishara ya mtoto wa kiume ambaye ametanzwa na matatizo,  ambaye hajapewa hadhi anayostahili katika jamii, kama inavyoonekana baadaye kwenye riwaya yenyewe. 

 

b) Mbele ya picha ya mwanamume anayemzungumzia mvulana kuna uwanja usiokuwa  na mimea, pengine kutokana na uharibifu wa mazingira, jambo ambalo pia linajitokeza ndani ya riwaya. 

 

c) Mbele huko kuna miti ambayo imefunikwa na giza kiasi, ambayo inaweza kuchukuliwa kuwakilisha matumaini yaliyonyimwa nafasi ya kujitokeza vizuri. 

 

d) Nyuma ya miti kuna mlima mkubwa ulio na vilele (nguu) ambavyo vina mwangaza  juu. Hii inaweza kuchukuliwa kuwa ishara ya matatizo (mlima) na suluhu  inayopendekezwa na mwandishi ya kukabiliana na nguu (vikwazo) za tangu jadi zinazotatiza maendeleo ya jamii. 

 

e) Nyuma ya mlima kuna mwanga hafifu unaojitokeza. Mwanga huu unaweza kuchukuliwa kuwa kiwakilishi cha matumaini mapya kwamba jamii iliyokumbwa na matatizo mengi kwa muda mrefu hatimaye inapata mwanga, kama inavyofanyika kwenye riwaya Lonare anapochaguliwa kuwa mtemi, jambo linaloipa nchi ya Matuo  matumaini mapya ya mabadiliko chanya. 

 

Ufaafu wa Anwani: Nguu za Jadi

 

Nguu ni vilele vya milima. Katika riwaya hii, neno hili limetumiwa kisitiari, kuwakilisha vikwazo au matatizo yanayokumba jamii inayozungumziwa. Kwa hivyo, Nguu za Jadi ni vikwazo ambavyo vimekuwepo kama desturi au kanuni za maisha, na ambavyo vinadumaza maendeleo ya jamii. 

Mifano ya vikwazo hivyo kutoka katika riwaya ni:

✔ Mila ambazo zinawadunisha wanawake na kuwanyima uhuru wa kujiendeleza.  Mifumo ya uongozi mbaya inayosababisha ufisadi, ukabila, utabaka, ubinafsi, hali ya kutowajibika, ufujaji wa mali za umma, uharibifu wa mazingira, ukiukaji wa haki za watoto, ukatili na wizi wa mali ya umma. 

✔ Mifumo wa ubabedume uliokolea taasubi ya kiume wenye kudhalilisha wanawake na watoto wa kike. 

✔ Mila zinazomnyima mtoto wa kiume nafasi ya kujiendeleza. Mila hizi zimemtelekeza mtoto wa kiume kwa kutothamini elimu na maendeleo yake. 

✔ Umaskini uliokithiri. 

✔ Matumizi na ulanguzi wa dawa za kulevya. 

✔ Changamoto za ndoa na ukahaba. 

 

Riwaya ya Nguu za Jadi kwa Muhtasari

Riwaya inapoanza, mhusika mkuu, Mangwasha, yuko na wanawe wawili, Sayore na Kajewa,  katika kanisa fulani, ambapo wanajificha. Nje ya kanisa hilo, wapo watu wengine wa kabila la Waketwa, waliokimbilia usalama hapo baada ya makao yao katika eneo la Matango  kuchomwa. 

 

Kuna fununu kwamba jamii ya Waketwa inafurushwa kutoka makwao kwa sababu kuna watu  fulani wanaotaka ardhi ya Matango kwa nguvu. 

 

Mtemi Lesulia, kiongozi wa nchi, anachukia kabila la Waketwa kwani yeyeanatoka katika kabila la Wakule. Waketwa na Wakule Wana uhasarna wa tangu jadi. Lonare, ambaye ni kiongozi wa Waketwa, ana urnaarufu mkubwa nchini. Katika uchaguzi mkuu uliopita,  alitekwa nyara na kwa namna hiyo, Mtemi Lesulia aliishia kuchaguliwa bila kupingwa. 

 

Mangwasha ni mwanamke mwenye bidii, na anafanya kazi ya uhasibu katika afisi ya Chifu  Mshabaha. Chifu huyu ni rafiki mkubwa wa Mtemi Lesulia, naye pia anawachukia Waketwa.  Hivyo, anapanza kuwadhulumu Waketwa, jambo ambalo Mangwasha analifahamu kutokana na kufanya kazi naye. Chifu Mshabaha pia ni rafikiye Sagilu, mzee anayetaka kumuoa Mangwasha licha ya kwamba anajua msichana huyu ana mchumba, Mrima, na wanapanga ndoa. Siku ya harusi ya Mangwasha na Mrima, Sagilu anamtuma kimada wake, Sihaba,  akiwa na bomu lililofungwa kama zawadi kwa maharusi. Kwa bahati nzuri, watu  wanamshuku na maafa aliyokusudia kufanya hayafanyiki. Sagilu anamnyemelea Mrima na kumzuga kwa kutumia pesa kiasi kwamba Mrima anaisahau familia yake, huku akimwachia Mangwasha jukumu la kuwalea wana wao wawili. 

 

Nchi ya Matuo inakumbwa na matatizo mengi. Kuna matatizoya kiuchumi yanayosababishwa na uongozi mbaya na ufisadi uliokithiri. Mtemi Lesulia anaendeleza ubaguzi dhidi ya Waketwa na vijana wengi walio na elimu hawapati kazi za kujiendeleza kimaisha. Kwa mfano, uteuzi wa wagombea nafasi za uongozi ukiwa umekaribia, machifu  wanalazimishwa kuwahamisha Waketwa kutoka Matango ili viongozi wanaopendelewa na mtemi wasipate upinzani, na yeye Mtemi Lesulia asishindwe na mpinzani wake mkuu wa kisiasa, Lonare. Sihaba anatumwa kwenda kuhakikisha kwamba makazi ya Waketwa yameteketezwa, 

 

Anawatumia vijana ambao wanatumia petroli kuchoma makazi hap. Lonare na wafuasi wake wamepeleka kesi mahakamani, na akiwa na wenziwe, kama vile Ngoswe, wanawashawishi watu kurudi katika mako yao ya zamani kule Matango ambako wanajenga mahema. Hata hivyo, siku ya tatu, vijikaratasi vinasambazwa kuwataka watu watoke kwenye ardhi hiyo  ambayo, inabainika, imetwaliwa na kupewa Nanzia, mkewe 

 

Mtemi Lesulia, na rafikiye mtemi, Mbwashu. Hawa wanataka kujenga jengo la kibiashara katika ardhi hiyo ya Matango. Watu wanaokuja kuanza ujenzi wanafukuzwa na Waketwa walioamua kuitetea ardhi yao kwa vyovyote vile. Baada ya kuona kwamba mpango wao umetibuka, Mtemi Lesulia anamtumia Sagilu kumpa Mrima pesa nyingi pamoja na  ahadi kwamba atapewa kazi serikalini, ilimradi amfanyie Mtemi Lesulia kampeni na kuwaendea kinyume Waketwa. 

 

Kipindi kifupi kabla ya uteuzi wa watakaopeperusha bendera za vyama mbalimbali, Sagilu  anatofautiana na mwanawe, Mashauri, baada ya mwanawe kugundua kwamba babake ana uhusiano wa kimapenzi na mpenzi wake, Cheiya. Mtemi Lesulia naye anakosana na mwanawe, Ngoswe, wakati anapanga njama ya kuvuruga zoezi la uteuzi ili kuwaharibia wapinzani wake nafasi za kuteuliwa. Ngoswe anaona kwamba hatua ya babake inaongozwa na ubinafsi wa kujitakia uongozi na kutojali kwamba baadhi ya watu huenda wakapoteza maisha yao katika vurugu anazopanga. Sagilu anashindwa katika uteuzi na inakuwa wazi kwamba Mtemi Lesulia atakuwa na upinzani mkubwa katika uchaguzi mkuu ujao. Kwa ushawishi wake, Chifu Mshabaha anafutwa kazi na mtemi anaamua kumwondokea Sagilu  ambaye sasa anaandamwa na sheria kwa ufisadi alioendesha nchini. Awali, tunaona Mangwasha akipoteza kazi yake katika afisi ya Chifu Mshabaha kwa kujitokeza kama mpinzani wa serikali kwani anamfanyia Lonare kampeni, kando na kwamba mara zote,  hakumkubalia Sagilu ombi la kumtaka awe kimada wake. Sihaba anatiwa mbaroni kwa kuendesha biashara haramu ya ukahaba inayosababisha wasichana wengi kuharibika lakini anaachiliwa kutokana na ushawishi aliokuwa nao serikalini. Mikasa hii inawaathiri wahusika wengi vibaya. 

 

 

Sagilu anapatwa na kichaa na mkewe mtemi, Nanzia, anaugua baada ya jengo lake la kibiashara la Skyline Mall kutwaliwa. Baada ya kulazwa hospitalini kwa muda, anafariki. 

 

Kwa mara nyingine, Lonare anatekwa nyara kabla ya uchaguzi lakini anafaulu kutoroka na kupata matibabu. Uchaguzi mkuu unafanyika na Lonare anachaguliwa kuwa mtemi. Rafikiye Sagilu anashindwa na Mwamba anayechaguliwa kuwa mbunge wa Matango. Lonare anawahutubia wananchi wa Matuo na kuahidi kuufufua uchumi wa nchi na kukabiliana na ufisadi serikalini. Anaahidi pia kwamba serikali yake itashughulikia tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana na kuhakikisha kwamba pana usawa wa kijinsia, akisema kwamba Matuo  imesambaratishwa na ubabedume. Anawaomba wananchi wenzake kujiepusha na ukabila na kuwahimiza kukataa na kufichua maovu yanapofanyika nchini. Lonare anachagua kutolipiza kisasi dhidi ya mahasidi wake wa kisiasa. 

 

 

Sura ya Kwanza

 

Mangwasha yuko na wanawe katika kanisa fulani ambapo yeye na watu wa kabila lake la Waketwa wamekimbilia usalama baada ya kuchomewa nyumba zao katika mtaa wa Matango, jijini Taria. Kuna fununu zinazosema kwamba pana watu fulani waliotaka kuitwaa ardhi ya Matango kwa nguvu. Inabainika pia kwamba mjini Taria, kuna jamii mbili ambazo  ni mahasimu wa tangu jadi, Wakule na Waketwa. Mtemi Lesulia, kiongozi wa nchi, anatoka katika jamii ya Wakule na anawachukia Waketwa. Lonare ni kiongozi wa Waketwa lakini ana umaarufu mkubwa nchini kote kwani katika uchaguzi mkuu uliopita, alikuwa na sera bora zaidi. Hata hivyo, kabla ya kufanyika kwa uchaguzi, alitekwa nyara na Mtemi Lesulia kuchaguliwa bila kupingwa. Mangwasha anafanya kazi ya uhasibu katika afisi ya Chifu  Mshabaha. Anajua kwamba Chifu Mshabaha, ambaye pia anawachukia Waketwa, anafanya mpango wa kuwadhulumu Waketwa. Kwa sababu hii, anapanga kumwona kiongozi wake,  Lonare, ili kumweleza njama zinazopangwa dhidi ya watu wake. 

 

Juhudi za Mangwasha, hata hivyo, zinatatizwa na hali kwamba jamii haimthamini mwanamke, na anashangaa kama atasikilizwa. Anaamua atafanya tu alilokusudia, liwe liwalo. 

 

Masuala makuu yanayojitokeza katika Sura ya Kwanza

 

✔ Uhasama wa kikabila na kisiasa unajitokeza kwani Waketwa wanabaguliwa na kupokwa haki zao za kumiliki ardhi na kuishi kwa amani. Waketwa wanalaumiwa hata kwa mambo ambayo hayako katika uwezo wa binadamu kudhibiti, kama vile maradhi sugu  yanapowashinda madaktari. Kiongozi wa Waketwa, Lonare ameepuka kifo mara nyingi,  kifo kilichopangwa na Wakule. 

✔ Ukabila ulioshamiri Matuo unawafanya Waketwa wengi kuwa katika tabaka la chini,  huku wakiwa na viongozi wachache sana serikalini. 

✔ Mfumo wa ubabedume unawanyima wanawake nafasi ya kujiamini kama wahusika sawa katika jamii. Mwanamke asiyekuwa na cheo au pesa hawezi kusikilizwa (uk. 8).  ✔ Ufisadi umeshamiri katika jamii. Ardhi ya Waketwa inapotwaliwa, Chifu Mshabaha anaangalia kando kwani ameshapokea mlungula (uk. 9). 

✔ Maudhui ya bidii yanajitokeza kupitia kwa mhusika Mangwasha ambaye msimulizi anasema alifunzwa kuuambaa uvivu (uk. 12). 

 

 

Sura ya Pili

 

Mangwasha ni msichana mwenye bidii kazini, katika afisi ya Chifu Mshabaha. Anakutana na Mrima, ambaye pia ni mwenye bidii, na kuchumbiana. Wanafanya mazoea ya kwenda kula chakula katika mkahawa unaomilikiwa na Sagilu, mzee ambaye ni rafikiye Mtemi Lesulia.  Sagilu anamtaka Mangwasha kimapenzi na anapomkataa, anaweka kisasi dhidi yake. Chifu  Mshabaha pia anamchukia Mangwasha kwa kumchumbia mwanamume asiyekuwa na pesa na kumkataa rafikiye, Sagilu, ambaye ni tajiri. 

Siku ya harusi ya Mangwasha na Mrima, Sagilu anamtuma Sihaba, kimada wake, na bomu  ambalo linalipuka na kusababisha watu waliohudhuria sherehe kutawanyika. Baada ya miaka kadhaa katika ndoa na kuwa na watoto wawili, Mrima anabadilika. Anaitelekeza familia yake na kuingilia ulevi. Mangwasha anateseka sana na anapoamua kufuatilia mumewe ili ajue ni nini kilichomfanya abadilike, anagundua kwamba anapewa pesa nyingi na Sagilu, ambaye ni adui wa ndoa yao. 

 

Masuala makuu yanayojitokeza katika Sura ya Pili

 

⮚ Mangwasha, mhusika mkuu, anajitokeza kama mwanamke jasiri na aliyejikomboa kiakili.  Hathamini tamaduni zilizopitwa na wakati, kama vile kulazimishiwa ndoa kwa misingi ya mali. Kwa msingi huu, anamkataa Sagilu ambaye anatumia ushawishi wa hela kumtaka awe mwanamke wake. Yeye ni mwenye mapenzi ya dhati, haliinayomfanya kumjali mumewe na kufuatilia ili ajue ana tatizo gani linalomfanya kuingilia ulevi na kuitelekeza familia yake. 

 

⮚ Sagilu anasawiriwa kama mtu katili, anayehodhi bidhaa na kuziuza kwa bei za juu wakati kuna uhaba wa bidhaa hizo. Aliwahi kuagiza maziwa ya watoto ambayo yalihatarisha maisha yao. Kwa kuwa ana uhusiano wa karibu na Mtemi Lesulia, sheria hazikumfuatilia katika suala hili, ishara ya ufisadi. 

 

⮚ Chifu Mshabaha anajitokeza kama mbaguzi na mpyaro. Anasema kwamba Waketwa hawana akili (uk. 20). 

 

⮚ Ufisadi unajitokeza kwani polisi hawajishughulishi kumtia mbaroni mwanamke anayekuwa na kilipuzi kwenye harusi ya Mangwasha. 

 

⮚ Sagilu ana kisasi na familia ya Mangwasha. Kwa sababu hiyo, anatumia pesa ili kumtokomeza Mrima na kwa namna hiyo, kumsababishia Mangwasha na wanawe mateso. 

 

⮚ Taasubi ya kiume inajitokeza kupitia mhusika Mrima ambaye anamwambia Mangwasha kwamba hamzuii kuoa mke mwingine (uk. 41). 

 

 

Sura ya Tatu

 

Waketwa ni watu wenye bidii. Hata hivyo, wengi wao wanaishia kufanya kazi duni na wanabaguliwa kwa kila hali kwani utawala wa Mtemi Lesulia ni fisadi na unaendeleza ubaguzi dhidi yao. Kuna matatizo ya kiuchumi yanayotokana na uongozi mbaya; vijana waliosoma hawana ajira na wengi wao hawasomi kutokana na umaskini uliokithiri. Pia, kuna uharibifu wa mazingira kutokana na mapuuza na kutojali kwa serikali. 

 

Uhalifu pia umeongezeka na maadili kuwakimbia watu, hasa vijana. Lonare anamtembelea Mangwasha. Tunafahamu kwamba machifu wamelazimishwa kuwahamisha Waketwa kutoka Matango ili Mtemi Lesulia asipate upinzani katika eneo hilo, na Lonare asichaguliwe, kwani wafuasi wake wengi wanaishi huko. Baadaye, Sagilu anamtembelea Mangwasha usiku na kutaka kumhonga kwa pesa ili amkubali. Mangwasha anamfukuza na kukataa Pesa zake.  Usiku huo anapolala, anaota kwamba jinyama hatari linamfukuza na mbele anakokimbilia anakabiliwa na moto mkubwa. Anapoamka, anatanabahi kwamba Matango inateketezwa kwa moto na watu wanahangaika ovyo. 

 

Masuala makuu

 

a) Maudhui ya bidii na kutobagua kazi yanasisitizwa katika sura hii. Waketwa hawakuchagua kazi kama walivyofanya Wakule. Walifanya hata zile zinazofikiriwa kuwa duni (uk. 43). 

b) Ufisadi unajitokeza kwani watu wengi, hasa wa jamii ya Wakule, wanapata kazi hata bila kuhitimu, jambo ambalo lina madhara makubwa, kama vile vifo vinavyofanyika hospitalini ambako watu wasiosomea udaktari wanaajiriwa kufanya upasuaji wa kimatibabu. Viongozi wa kijeshi pia wanatoka katika jamii ya Wakule (uk. 44). 

c) Uchafuzi wa mazingira pia umeangaziwa. Wananchi wanaathirika kiafya kutokana na uchafuzi wa mazingira (uk. 46). 

d) Umaskini unawafanya baadhi ya vijana kutopata elimu ya haja, huku wasichana wakipata mimba za mapema na kukosa kuendelea na masomo (uk. 48-49).  e) Lonare anajitokeza kama kiongozi bora kwani anapigania elimu ya wasichana na anataka kuongoza Matuo si kwa sababu ya mshahara tu bali kwa kuwa anawapenda wananchi wenzake, kuonyesha kwamba yeye pia ni mzalendo. 

f) Mwandishi ametumia jazanda ya jinyama na moto. Jinyama linalomkimbiza Mangwasha ni Sagilu ambaye ni mzee asiyekuwa na maadili, nao moto ni kiangazambele cha moto unaowachomea Waketwa makazi yao huko Matango. 

 

 

Sura ya Nne

 

Sura hii inaanza asubuhi baada ya watu kukesha nje ya kanisa. Hii ni baada ya kufurushwa kutoka Matango. Mangwasha na Mbungulu wanakutana na wanawake wengine ambao  wanaelezea kwamba usiku walipochomewa nyumba walikutana na vijana. Hawa walikuwa na mageleni yaliyohanikiza harufu ya mafuta ya petroli. Vijana hao waliingia kwenye gari jekundu lililoendeshwa na mwanamke fulani ambaye hawakuweza kumtambua. Mkurugenzi wa ardhi mjini Taria anakuja mahali pale akiandamana na Chifu Mshabaha na mwanamke aitwaye Mbwashu. Anawaahidi watu chakula, mablanketi na mahema ya msaada. Watu  wanakasirishwa na hatua ya kuwachukulia kama wakimbizi lakini mkurugenzi huyo anasema kwamba chanzo cha moto uliowachomea makazi yao hakijulikani kisha anaondoka. Watu  wana hasira, hawataki kuishi mahali hapo; wako radhi kwenda kukita mahema huko  Matango. 

 

 

Siku ya tatu baada ya kurudi Matango, vijikaratasi vinasambazwa kuwataka Waketwa watoke sehemu hiyo. Watu wanakuja hapo kutaka kujenga ua ili kuzingira ardhi ya Matango lakini wanafukuzwa na wenyeji, ambapo Sihaba anajeruhiwa. Huyu ndiye aliyesambaza vijikaratasi vya kuwataka watu wahame eneo la Matango. Sagilu naye ameshaonywa na Mtemi Lesulia kuhakikisha kwamba jalada halisi la ardhi ya Matango halipatikani, kwani ardhi hiyo sasa ni mali ya Nanzia, mkewe mtemi, na Mbwashu. 

 

Baadaye, Sihaba anamtembelea Chifu Mshabaha. Anamwachia barua zenye taarifa kuhusu  jengo la kibiashara ambalo linanuiwa kujengwa Matango. Kuna barua kutoka kwa Mtemi Lesulia inayoeleza kwamba kipande hicho cha ardhi ni mali ya Nanzia na Mbwashu.  Mangwasha anazirudufisha barua zote na baadaye zinatumiwa kama ushahidi mahakamani katika kesi inayohusu ardhi ya Matango. Mwamba, mwanasheria anayewakilisha Waketwa katika kesi hiyo anashinda kesi kwa ushahidi huo. Mpango wa Mtemi Lesulia, Sagilu na Chifu Mshabaha wa kuwafurusha Waketwa kutoka kwenye ardhi ya Matango unakosa kufaulu. 

 

Mtemi Lesulia anapanga njama nyingine. Kupitia kwake Sagilu, wanampa Mrima pesa nyingi pamoja na ahadi ya kumpa cheo serikalini ikiwa atamfanyia kampeni Mtemi Lesulia na kuwaendea kinyume Waketwa. Mangwasha anapata pesa hizi pamoja na barua yenye ahadi alizopewa Mrima na anamtaarifu Lonare, Mwamba, Sauni na Sagura. Wanakutana na Mrima na kufanikiwa kumweleza ukweli kwamba anatumiwa tu kisiasa, na kwamba Mtemi Lesulia na Sagilu hawana mpango wowote wakumfaa. Wanakubaliana kurudisha pesa alizohongwa nazo kwa Sagilu, ambaye wanamkuta akiwa kwenye mkutano pamoja na wafuasi wake. 

 

Masuala makuu

 

⮚ Mangwasha na Lonare wanajitokeza kama wahusika waadilifu, wanarudisha pesa zilizotumiwa kama hongo kwa Sagilu kutoka kwa Mrima. Aidha, ni wenye mapenzi ya dhati kwa nchi na kwa watu wao. Wanamwokoa Mrima kutoka Majaani ambako  amedhoofikia kiafya. 

 

⮚ Chifu Mshabaha, Mbwashu, Sagilu, Mafamba na Mtemi Lesulia wanajitokeza kama wahusika fisadi na katili kwani hawajali athari za vitendo vyao vya kifisadi kwa wananchi. Mtemi Lesulia analinganishwa na mjusikafiri anayekula chakula cha mchwa na mchwa wenyewe. Maelezo haya yanajenga jazanda ya utawala dhalimu  unaowaangamiza wananchi wake. 

 

 

Sura ya Tano

 

Nchi ya Matuo inakaribia uteuzi wa viongozi. Sagilu, aliyekuwa na matumaini makubwa ya kupata uteuzi wa kugombea uongozi wa Matango anapata msururu wa mapigo. Ana uhusiano  wa kimapenzi na mpenzi wa mwanawe, Mashauri, aitwaye Cheiya. Mashauri anapogundua jambo hili anamchukia babake hata kumkana. Zaidi ya hayo, anajiunga na kundi linalomuunga mkono Lonare na Mwamba, ambao wanawania kiti cha mtemi na uongozi wa eneobunge la Matango mtawalia. Mashauri ni rafikiye Ngoswe, mwanawe Mtemi Lesulia.  Ngoswe anafahamika zaidi kama mlanguzi mkubwa wa dawa za kulevya, kando na kukusanya ushuru kutoka katika mashamba yånayomilikiwa na wazazi wake. Cheiya anatoka katika familia ya kimaskini lakini baada ya elimu yake na kukutana na Mashauri,  anakengeuka na kuanza kuhusudu pesa, na hii ndiyo sababu anashawishiwa na Sagilu kwa urahisi. 

 

Baada ya mtemi Lesulia kujua kwamba mwanawe Sagilu anamuunga mkono Lonare,  anapanga njama ya kuzua vurugu wakati wa uteuzi ili Lonare asipate kuteuliwa akaishia kushindana naye. Anafanya hivi pia ili Sagilu achukue uongozi wa Matango. Ngoswe hamuungi babake mkono katika azimio lake. Anashangaa ni kwa nini babake yuko radhi watu wapoteze maisha yao ili yeye na rafiki yake watwae uongozi. Yeye pia anaasi na kujiunga na Mashauri katika kumuunga mkono Lonare. 

 

Baada ya uteuzi kufanyika, Sagilu anashindwa na mpinzani wake, Mwamba. Jambo hili linamuudhi Mtemi Lesulia ambaye anaamua kuacha sheria ifuate mkondo wake, kwani mara zote amekuwa akiwalinda marafiki zake dhidi ya sheria, hasa Sagilu ambaye ni fisadi mkubwa. Kufuatia hili pia, Chifu Mshabaha anafutwa kazi na waziri anayehusika na masuala ya utawala. 

 

Mangwasha anafutwa kazi kwa kuwa anamuunga mkono Lonare ambaye ni mpinzani wa Mtemi Lesulia. Analazimika kujiunga na mumewe katika kuendeleza biashara kwenye duka lao. Mangwasha anamwonea huruma mtoto wa kiume kwani ameishia kutelekezwa huku  jamii ikimwangazia zaidi mtoto wa kike. Hivyo, kwa msaada wa mashirika mbalimbali,  anafungua afisi mjini Taria ili kuwashughulikia vijana hao, ambao aliona wanaendelea kuangamia taratibu. 

 

Sihaba, ambaye anaendesha biashara ya ukahaba, anakamatwa na majengo anayoendelezea biashara hiyo yanafungwa. Miezi minne baada ya kushindwa katika uteuzi, Sagilu anapatwa na kichaa. Mkewe Mtemi Lesulia, Nanzia, naye anapatwa na msongo wa mawazo na kulazwa hospitalini, baada ya kupokonywa jengo la kibiashara la Skyline Mall. Ugonjwa wake unamsababishia kifo. Hata hivyo, kabla hajafa, anamweleza Ngoswe kwamba yeye ni mtoto  wa Sagilu, wala si mwanawe Mtemi Lesulia. Hali ya Sagilu inaendelea kuwa mbaya hospitalini. Mwishowe anamwomba mwanawe, Mashauri, msamaha kwa kumwendea kinyume. Mashauri anamsamehe. Mali ya Sagilu inatwaliwa na serikali kwani aliipata kwa njia ya ufisadi. Wakati huu pia inafahamika kwamba Cheiya alitumiwa kumtilia Lonare sumu  kwenye kinywaji chake. Anakamatwa na kupelekwa kwenye kituo cha polisi. 

 

Masuala makuu

 

a) Suala la ukengeushi linaangaziwa katika kisa cha Sagilu na Cheiya. Sagilu kuandamana na msichana wa umri wa Cheiya ni kuonyesha hali ya kutojiheshimu na kutojali maadili.  Cheiya, kwa upande mwingine, yuko tayari kujishusha hadhi kwa kuandama pesa.  Ukengeushi pia unajitokeza pale ambapo mmoja wa wasichana wanaofanya ukahaba kwa Sihaba anasema, za kutununulia chakula, nguo au hata vipodozi?" (uk. 142). Kauli hii inaashiria kwamba wasichana hawa wamekengeuka kiasi kwamba hawathamini kazi kama njia halali ya kujitafutia riziki. 

 

b) Suala la malezi mabaya pia linajitokeza katika sura hii kwani Ngoswe ni mwana kindakindaki aliyeengwaengwa na kudekezwa kupita kiasi (uk. 122). Yeye anaendesha biashara ya kulangua dawa za kulevya na babake, Mtemi Lesulia, anamlinda kiasi kwamba hata wakuu serikalini hawawezi kumkamata (uk. 122-123). Sifa ya Sagilu kama mtu fisadi inajitokeza. Anashirikiana na mwanawe kuifisidi nchi kwa kushiriki biashara ya vipusa na meno ya ndovu, na Mashauri anaposhtakiwa, kesi zenyewe zinazimwa kabla ya kuanza (uk. 127). 

 

c) Hatua ya Ngoswe na Mashauri kuungana katika kumpigia kampeni Lonare inaashiria uwezo wa vijana katika kuchangia mabadiliko chanya katika jamii. 

d) Ujasiri wa Mangwasha unaendelea kuonekana katika sura hii. Anapokabiliana na Chifu  Mshabaha baada ya kupoteza kazi yake, anamwambia chifu huyo kwamba yeye na wengine wanaotaka mabadiliko watazibomoa hisia zao za ukabila, ubinafsi na chuki (uk.  136). 

e) Tatizo la umaskini uliokithiri linawafanya watu kufanya mambo kinyume na maadili ya kijamii. Kwa mfano, baadhi ya wazazi wanawakubalia wana wao wa kike kushiriki ukahaba kama njia ya kujitafutia riziki (uk. 143). 

f) Kufutwa kazi kwa Chifu Mshabaha, kukamatwa kwa Sihaba, Nanzia kupoteza _jengo la Skyline Mall na hatimaye kufariki, na Mangwasha kuanzisha afisi ya kushughulikia mtoto wa kiume ni hatua muhimu katika ujenzi wa jamii mpya, jamii inayozingatia maadili na kuwajali watu. 

g) Kupitia mawazo ya Mangwasha, tunapata kuelewa falsafa ya mwandishi kuhusu maisha: kila mtu ni mhusika mkuu katika kisa cha maisha yake mwenyewe, na jambo la muhimu  ni mhusika huyo kuipa hadhira yake kitu cha kuwatia moyo maishani. 

 

 

Sura ya Sita

 

Siku chache kabla ya uchaguzi mkuu, Lonare anaripotiwa kupotea. Hata hivyo, wafuasi wake wanaamua watampigia kura, awepo au asiwepo. Hii ni licha ya Mtemi Lesulia kusema kwamba kiti cha mgombea nafasi ya mtemi katika Chama cha Ushirika kifutiliwe mbali kwani Lonare mwenyewe hayupo. 

 

Asubuhi ya siku ya uchaguzi mkuu, Lonare anapatikana ametupwa nje ya nyumba ya Mangwasha akiwa katika hali mahututi. Wafuasi wake waliokuwa wameishiwa na matumaini wanajitokeza kwa wingi kwenda kumpigia kura huku mwenyewe akipelekwa hospitalini.  Akiwa hospitalini, anamshauri Ngoswe kuacha biashara ya mihadarati kwani kwa kufanya hivyo, atakuwa anaokoa kizazi kizima kutoka katika maangamizi. Lonare anamshauri pia kuacha biashara nyingine haramu anazofanya na kujitanibu na mitandao inayoendesh  biashara hizo. Lonare anachaguliwa mtemi wa nchi ya Matuo. Baada ya ushindi huu,  anaihutubia nchi. Anaahidi kufufua uchumi wa nchi na kukata mirija ya ufisadi. Anaahidi pia kwamba serikali yake itashughulikia ukosefu wa ajira kwa vijana. Isitoshe, anaahidi kwamba atahakikisha kuwa kuna usawa wa kijinsia nchini huku akisema kwamba Matuo  imesambaratishwa na mfumo wa ubabedume. Anawaomba wananchi wenzake kuepuka ukabila na kufichua maovu yanapofanyika nchini. Anaamua kuwasamehe maadui wake wa kisiasa. 

 

Masuala makuu

 

✔ Ujumbe wa kutokata tamaa katika maisha unajitokeza katika sura hii. Licha ya kwamba Lonare amenyanyaswa sana na utawala wa

✔ Mtemi Lesulia, hakati tamaa. Wafuasi wake pia hawakati tamaa katika azimio lao la kumchagua kama mtemi. Hii ndiyo sababu wanaamua kumpigia kura tu, awepo au asiwepo. 

✔ Katika hotuba yake Lonare, ni wazi kwamba serikali atakayounda itakuwa serikali bora kwani ufisadi utamalizwa na umaskini kushughulikiwa, sawa na suala la Vijana na ajira.  Ni dhahiri kwamba mambo haya yakishughulikiwa, Matuo itakuwa nchi thabiti zaidi.

 

DHAMIRA

 

Dhamira ni shabaha au lengo kuu la kazi ya fasihi. 

1) Katika riwaya ya Nguu za Jadi, mwandishi anakemea ukabila uliosakini katika jamii na unaodumaza maendeleo ya nchi. Anadhamiria kutuonyesha pia jinsi ufisadi unavyoweza kubomoa asasi za kijamii na kufukarisha wananchi kiasi cha kutoweza kujiendeleza kimaisha. Mwandishi anatumia taswira mbalimbali kutuonyesha jinsi ufisadi unavyoweza kusambaratisha uchumi wa nchi hasa pale unapochangiwa na uongozi mbaya. 

 

2) Mwandishi anadhamiria kutoa tahadhari dhidi ya kuwapuuza na kutowashughulikia watoto na vijana ambao hasa ndio dirisha la matumaini ya nchi katika siku zijazo.  Utelekezwaji wa vijana na udunishwaji wa haki zao ni taswira inayojitokeza na kubainisha dhahiri dhamira ya mwandishi. 

3) Ugandamizwaji wa haki za wanawake na umuhimu wa asasi ya ndoa pia ni dhamira inayojitokeza katika riwaya hii mbali na ukombozi unaochochewa na uzalendo  miongoni mwa wanajamii. 

 

Falsafa ya Mwandishi wa Nguu za Jadi

 

Falsafa ni msimamo au mawazo yanayomwongoza mtu binafsi (kwa mfano, mwandishi)  katika maisha yake, na ambayo yanaweza kutumiwa pia kama nasaha kwa wasomaji au wasikilizaji wake, na jamii kwa jumla kupitia usomaji wa kazi fulani. 

Yafuatayo ni baadhi ya mawazo ambayo yanaweza kuchukuliwa kuwa falsafa au msimamo  wa mwandishi kuhusu mambo mbalimbali katika maisha. 

1) Mwandishi anaamini kwamba wanawake hawafai kufungwa na mila kiasi kwamba hawawezi kupata haki zao katika maisha. Mangwasha anamwambia Mbungulu kwamba mila isiyomruhusu mke kumtafuta mumewe kwenye starehe zake ni mila ya kishenzi (uk.  32). Hiyo ni kumaanisha kwamba wanawake hawafai kukaa na kusubiri tu mpaka pale mwanamume anapokuwa karibu ili wafanye maamuzi muhimu yanayohusu maisha yao. 

2) Mwandishi anapendekeza kwamba baadhi ya tamaduni za jadi zitupiliwe mbali kwani zimekwishapitwa na wakati. Miongoni mwa tamaduni hizo ni tamaduni zinazomtweza mwanamke kuonekana kama mtumwa wa mumewe. Badala yake, mwanamke katika ndoa anapaswa kuonekana kama mwenza (uk. 42). 

3) Mwandishi pia anaamini katika tabia ya kutochagua kazi, na mazoea ya kufanya bidii.  Kwa tabia yao ya kufanya kazi kwa bidii na kutochagua kazi, Waketwa wanapiga hatua sana kimaendeleo (uk. 43). 

4) Mwandishi anashikilia hoja kwamba fahari ya binadamu haitokani na kutoanguka katika maisha, bali inatokana na kuinuka kila anapoanguka (uk. 48). 

5) Mwandishi anaelekea kusema kwamba kwa uthabiti wa jamii, mtoto wa kiume anahitaji sana uwepo wa mzazi wa kiume pia ili mtoto huyo apate mafunzo muhimu 

yatakayomsaidia kukua na kujiendeleza inavyofaa (uk. 139). Mtoto wa kiume anaangamia kwa kutelekezwa kutokana na makini yote ya jamii kuelekezwa kwa mtoto  wa kike. 

6) Kupitia kwa mhusika Mangwasha, mwandishi anaelekea kusema kwamba binadamu  anapokuwa hai, ni muhimu kufanya jambo kwa faida ya jamii, kitu kitakacholeta matumaini katika maisha yao. Mangwasha anajishughulisha na kuboresha maisha ya mtoto wa kiume ambaye aliona kwamba mustakabali wake haukuwa na matumaini (uk.  164). 

 

 

MAUDHUI

 

Maudhui ni ujumbe wa jumla unaojitokeza katika kazi ya fasihi. Aidha, maudhui ni mafunzo  ambayo huweza kupatikana katika kazi ya kisanaa kama vile riwaya, na sehemu ya maana ambayo aghalabu huingiliana namada. Riwaya ya Nguu za Jadi ina maudhui mbaljmbali yanayojitokeza na ambayo yanajenga dhamira za mwandishi. Kutokana na hali kwamba riwaya hii ina maudhui changamano, ni vyema kwa msomaji kubaini maudhui mengine zaidi mbali na yale yaliyofafanuliwa humu. 

Ukabila

Ukabila ni hali ya kupendelea mtu, watu au Jamii fulani kutokana na misingi ya kabila.  Upendeleo huu huweza kuhusisha mambo mengi kama vile ajira, elimu, makazi, vyeo, na kadhalika. Katika riwaya hii,

1) Wakule ni jamii inayoonyesha ukabila; wao ndio wengi serikalini (uk. 43) kutokana na hali kwamba Mtemi Lesulia ambaye ndiye kiongozi wa nchi ya Matuo anatoka katika jamii hii. Wakule wengi hasa walio matajiri wanajibagua na kuishi katika mtaa wa Majuu  ambao ni mtaa linamoishi tabaka tawala. 

2) Kazi za madaraka ziliwaendea Wakule ilhali zile za daraja la chini kama vile kazi za mikono zilifanywa na Waketwa. 

3) Ukabila unasababisha ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana kutoka katika jamii ya Waketwa ambao ni wahitimu wa viwango mbalimbali vya elimu na taaluma.  4) Siasa za majina zinatawala (uk. 45) na ukabila unafanya watu wasiohitimu katika taaluma mbalimbali kuajiriwa na kusababisha maafa nchini. Watu wanaajiriwa kutokana na uchunguzi wa majina yao. Majina yanakuwa kigezo cha kupimia ajira.  5) Ukabila unamkolea mtemi kiasi cha kukosa imani ya kuajiri wanajeshi kutoka katika jamii nyingine. Kwa mfano, marubani wanaangusha ndege na manahodha wanapasua vyombo miambani kwa kukosa ujuzi (uk. 44). 

6) Dhuluma za Chifu Mshabaha kwa Mangwasha zinatokana na ukabila. Chifu  anadhihirisha hisia za kikabila anaposema "...Waketwa ni watu wasio na akili hata ya kuchagua wachumba." (uk. 20). 

7) Chifu Mshabaha anamfanyisha Mangwasha kazi nyingi hata zile zinazopaswa kufanywa na matopasi. 

8) Chuki ya Mtemi Lesulia kwa Lonare inatokana na ukabila hasa pale anapohujumu  biashara yake, kumwonea Lonare gere na hata kumpangia mauti (uk. 51-52, 171).  9) Maneno ya Sagilu pia yamebeba hisia za ukabila hasa pale ambapo anawachukua Waketwa kama watu wasioweza kufanya lolote. Anasema, "Ndege mliolelewa kizimbani nyie hamwezi kuruka. Mtawezaje kuruka ilhali mnaishi mkifikiria kwamba kuruka ni ugonjwa?" (uk. 176). 

10) Ukabila unafanya wenyeji wa Matango ambao ni Waketwa kuchomewa nyumba zao na kufurushwa ili wakati wa uchaguzi wa kisiasa wasimpigie mmoja wao kura.  11) Mtemi Lesulia anaendeleza hisia za ukabila anapowaita Waketwa panya (uk. 78).  12) Kufutwa kazi kwa Mangwasha pia kunatokana na ukabila (uk. 135-137) kwani tunaona anayeajiriwa kuchukua mahali pake ni Mkule. 

Utabaka

Utabaka ni hali inayosababisha jamii kujibagua katika makundi hasa mawili; matajiri na maskini au wenye mali na vyeo na wasio navyo. 

a) Utabaka unaonekana katika jumuiya inayozungumziwa (uk. 7). Nchi ya Matuo  inazingatia utabaka. Kuna tabaka la juu linalohusisha wakwasi, matajiri na wakuu wa serikali ambao pia wamejitenga na kuishi katika mtaa wa kifahari uitwao Majuu (uk.  7 na uk. 51). 

b) Wananchi wa kawaida wanaishi katika mitaa ya matabaka ya chini na yale ya kati kama vile Majengo, Matango na Majaani. Hawa wanahusisha wanaofanya kazi viwandani, mashambani, makarani, matarishi, matopasi au vibarua wanaofanya kazi za shokoa. 

c) Tunaarifiwa nchi ya Matuo ilishikilia utabaka (uk. 45), "...matajiri wakawa wenye nchi na wananchi wakasalia kuwa wana wa nchi". Maudhui ya utabaka yanaonyesha kuwa tabaka la juu ndilo lililomiliki nyenzo za uzalishaji mali na ndilo lililohujumu  dhamana na hawala za serikali. Tabaka hili linahusisha watu kama vile Mtemi Lesulia, Sagilu, Nanzia, Mbwashu, hata Ngoswe, mwanawe mtemi ambaye anaishi katika kasri la kifahari. 

d) Maudhui ya utabaka pia yanabainika kupitia mhusika Mangwasha anaposhangaa kumwona Mbwashu akiwasili pale kanisani kwa gari aina ya Land Rover kumaanisha kwamba hadhi yake haimruhusu kutumia gari kama lile (uk. 68). Aidha, mke wa Mtemi Lesulia naye anawasili pale kwa gari aina ya Pick Up (uk. 71). 

e) Tunamwona Cheiya akitamani maisha ya kifahari kutokana na utabaka uliokuwepo.  Anafanya usuhuba na Mashauri anayeishi mtaa wa Majuu naye akapata kuishi huko  (uk. 118). 

f) Maudhui ya utabaka pia yanaendelezwa na mhusika Mashauri anayesimulia kuhusu  kisa cha mfalme wa Ufaransa na malkia wake kwenye karne ya 18. Raia waliishi katika umaskini huku tabaka la mfalme likiishi maisha ya kitajiri (uk. 148-149). 

Uongozi mbaya

Maudhui ya uongozi mbaya yamegawika kuwili; uongozi mbaya serikalini na katika  familia.

1) Uongozi mbaya serikalini unaonekana kupitia kwa Mtemi Lesulia ambaye alitawala kwa mkono wa chuma na 'kauli alizotoa zilichukuliwa kama sheria za nchi' (uk. 7).  2) Mtemi anaonekana kuogopewa na raia wake na hili linabainika pale Mrima anapomkanya mkewe asijaribu kukutana na mtemi kumaanisha kwamba si mtu mzuri, na raia walimwogopa (uk. 8). Mtawala hapaswi kuogopewa na raia wake bali kuheshimiwa.  3) Uongozi mbaya pia unaonekana kupitia kwa kiongozi huyu ambaye anashirikiana na raia wake kuwanyanyasa raia wengine kwa kuwachomea makazi yao (Waketwa). Hii ni ishara 

ya uongozi mbaya wa kutenga na kubagua raia kwa sababu ya ubinafsi unaotokana na siasa za ubaguzi na chuki. 

4) Uongozi mbaya unaendelezwa pia na Chifu Mshabaha; kumnyanyasa Mangwasha kazini na kutojali kazi nyingi anazotekeleza katika afisi yake. 

5) Uongozi mbaya unaendelezwa pia kupitia kwa uteuzi mbaya wa viongozi katika serikali ya Mtemi Lesulia; Sagilu anapewa cheo kikubwa lakini kinamfaidi yeye binafsi ilhali mwanasheria, Mafamba, anayehudumia serikali anahujumu uchumi wa nchi kupitia kwa kesi zisizozingatia maadili na sheria za nchi. 

6) Maudhui ya uongozi mbaya yanaonekana kupitia kwa viongozi wa nchi wanaoruhusu  matendo maovu kama vile ufisadi na uporaji wa rasilimali ya umma ushamiri.  7) Uongozi mbaya unaonekana pale ambapo serikali haina mipango yoyote ya kuimarisha ajira kwa vijana wanaohitimu katika Shule na vyuo wala kuweka mikakati ya kuwakinga dhidi ya dhoruba za maisha. Wasichana wadogo wanahangaika mijini huku wakizalishwa wakiwa na umri mdogo na vijana wa kiume wakihangaika mijini bila ajira.  8) Ijapokuwa Mtemi Lesulia alikuwa ameshinda kiti cha mtemi wa nchi mara mbili,hakubadilisha sera za uongozi wala kuweka mikakati ya kushughulikia ukosefu wa ajira na kuimarisha uchumi au kutokomeza ufisadi nchini. 

9) Uongozi mbaya katika serikali unasababisha mafunzo hafifu ya wataalamu katika mfumo  wa elimu. Wataalamu wasiohitimu vyema kama vile marubani na manahodha wanasababisha maafa safarini kutokana na uongozi usiojali hitimu za watu. Serikali inawaajiri walimu na madaktari wasiohitimu (uk. 44) huku vijana waliohitimu wakikosa ajira. 

10) Maudhui ya uongozi mbaya pia yanaendelezwa kupitia kwa mtemi wa nchi pale anaposhirikiana na wezi wa mali ya umma, walafi na wabinafsi kuihasiri nchi. Katika uk.  78, kwa mfano, Mtemi Lesulia anamwambia Sagilu ahakikishe jalada la ardhi halipatikani anaposhirikiana naye kuwapoka Waketwa ardhi yao. 

11) Tunaarifiwa pia kwamba mtemi hakutafakari ili kujua maana ya uongozi kwa raia wake.  Nyenzo za uongozi wa nchi tunaona zikimilikiwa na matajiri wachache wanaoshabikia wizi wa mali ya umma. "Uchumi wa nchi ulikuwa ukisambaratika kwa kasi kutokana na uongozi mbaya wa Mtemi Lesulia." (uk. 51). 

12) Maudhui ya uongozi mbaya pia yanaendelezwa kupitia kwa Mtemi Lesulia na familia yake. Hakuweza kumpa mwanawe, Ngoswe, uongozi aliostahili katika malezi yake. Hii ndiyo maana Ngoswe anashiriki ulevi, ufuska na kujihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya. Maudhui ya uongozi mbaya pia tunayaona kupitia kwa familia ya Mrima.  Hakuweza kuwaongoza vyema watoto wake kutokana na ulevi hadi wakamsahau kama mzazi wao. 

Ufisadi

Ufisadi umejitokeza kwa njia mbalimbali kupitia kwa baadhi ya wahusika na unachukua sehemu kubwa katika riwaya hii. 

1) Kutozingatia ujuzi, maarifa au taaluma ya mtu katika ajira kunasababishwa na ufisadi.Serikali ya Mtemi Lesulia inawaajiri watu wasiokuwa na ujuzi wala maarifa huku walio na uwezo huo wakiachwa (uk. 44). Tunaambiwa ajira zinatolewa kibubusa na kwa kujuana hasa katika misingi ya ukabila. Hali hii inasababisha hujuma katika uajiri na kuzorotesha uchumi wa nchi. 

2) Ufisadi unasababisha ukiukaji wa maadili ya kifamilia kwani tunaona mauaji ya kifamilia yakikita mizizi. "Mume anamgeukia mke na kumchinja, naye mke akafanya vivyo hivyo." (uk. 47). 

3) Taasisi na mashirika ya serikali yanamilikiwa na mitandao ya wezi na hivyo kuipoka nchi hadhi yake (uk. 47). Rasilimali ya nchi inafujwa na watu walioshabikia wizi.  4) Polisi nao wanaendeleza ufisadi pale wanapowatoza madereva wa Lonare faini zisizoeleweka; pale Lonare anapohangaishwa na polisi kwa makosa madogomadogo; kupokonywa leseni, na kadhalika. 

5) Maudhui ya ufisadi yanajitokeza pale kundi la mabwanyenye linapohujumu dhamana na hawala za serikali. 

6) Upokeaji hongo unaonekana pale watu waliotumwa kumkatizia Lonare maisha walipomjia na kumwonyesha pesa walizopewa na maadui zake ili kumuua.  7) Kitendo cha Sagilu kujaribu kumhonga Mangwasha kwa pesa ili afaidi penzi lake pia ni kitendo cha ufisadi (uk. 60). 

8) Kauli ya Mtemi Lesulia ya kuamuru jalada la ardhi ya Matango kufichwa inadhihirisha ufisadi (uk. 78). Alitaka kuwaondoa Waketwa wasimpigie kura Lonare au Mbaji wakamshinda yeye au Sagilu. Alitaka pia kufyeka uwanja ili 

9) Nanzia na Mbwashu wamiliki ardhi hiyo huku wakisema ardhi hiyo ilikuwa imetengewa ujenzi wa soko. Hivi vyote vinaashiria ufisadi. 

10) Ufisadi unaonekana pale Sagilu na Sihaba wanapojaribu kumshawishi Mbaji kwa kila njia ili asimfanyie Lonare kazi (uk. 98). 

11) Maudhui ya ufisadi yanaendelezwa na mtemi na jamaa yake pamoja na marafiki zake wanapojaribu kuwapoka Waketwa ardhi ya Matango kwa njia zisizo halali. Hongo  inatolewa kwa Chifu Mshabaha, Sagilu na Sihaba katika mchakato huo. 

12) Kitendo cha.kuwachomea wenyeji wa Matango nyumba na kuwafurusha kinatokana na ufisadi kwani kuna vijana waliohongwa kutekeleza uhalifu huo. 

13) Sihaba anapotumiwa na Sagilu kusambaza vijikaratasi kuwataka Waketwa wahame kutoka Matango ni hujuma inayotokana na ufisadi. 

14) Maudhui ya ufisadi pia yanaendelezwa na taasisi ya magereza kwani tunaona milango  ya gereza ikifunguliwa ili wahalifu kama vile Sihaba watoke (uk. 85). 

15) Ufisadi pia unaendelezwa kupitia wahusika kama vile Mbwashu na Sagilu wanaotumia njia haramu kuagiza bidhaa ghushi nchini na kukataa kulipa ushuru mbali na kutoa mlungula bidhaa hizo ziliposhikwa na maafisa wa forodha (uk. 68). 

16) Tashbihi inayotolewa ya kumlinganisha Mtemi Lesulia na mjusikafiri juu ya kichuguu  inapiga mwangwi ufisadi uliokuwepo katika serikali yake (uk. 93). Utawala wake unafisidi pato la nchi linalotokana na jasho la raia wake. 

17) Maudhui ya ufisadi yanaendelezwa pia na mwanasheria Mafamba. Huyu anashiriki ufisadi pale anapoficha siri za watawala kwa kutoa habari za uongo mbele ya korti kuhusu vyeti ghushi vya ardhi iliyomilikiwa na wenyeji wa Matango. Ufichuzi wa mwanasheria Mwamba unaweka bayana ufisadi unaohusishwa na ardhi ya Matango (uk.  95). 

18) Ulevi wa Mrima unatokana na upotovu wa maadili ambao chanzo chake ni Sagilu.  Kupitia kwa hila za Sagilu, Mrima anatoweka nyumbani kushiriki ulevi kwa kupewa pesa ili aiharibu ndoa yake na Mangwasha. 

19) Mrima anapokea mlungula kutoka kwa Sagilu ili kuhujumu kampeni ya Lonare na kumuunga mkono Mtemi Lesulia (uk. 105-114). 

20) Ufisadi unabainika Lonare anapomwambia Sagilu, "Nimekuja kukukabidhi mlungula huu uliokuwa umempa Mrima." (uk. 116). 

21) Maudhui ya ufisadi yanaendelezwa na mhusika Ngoswe anaposhiriki katika biashara haramu ya dawa za kulevya ambazo 'zilisambazwa nchini kwa siri' (uk. 123). Ijapokuwa sheria kali zilipitishwa nchini kuhusu dawa hizo, hazikuzingatiwa kutokana na ushawishi wa mabwanyenye waliohujumu sheria za nchi kwa manufaa yao binafsi. 

22) Kupitia kwa Mashauri pia, ufisadi unaendelezwa pale anaposhirikiana na Sagilu kufisidi vipusa na meno ya ndovu (uk. 127). 

23) Ufisadi unayawezesha mashtaka yaliyofikishwa kortini kuzimwa hata kabla ya kesi kuanza. 

24) Mtemi na Sagilu wanatumia vishawishi vya pesa kuwahonga vijana ili wazue vurugu na kuharibu kura za mpinzani wa Sagilu katika eneo la Matango (uk. 128). 

Utamaduni

Utamaduni ni ujumla wa maisha ya watu. Aina mbili za maudhui ya utamaduni zinajitokeza katika riwaya hii. 

Kuna utamaduni wa kiasili ambao unazingatia jadi na desturi za kiasili za jamii zinazozungumziwa, na ule unaokumbatia usasa. Huu ni ule utamaduni unaotokana na maisha ya kimji na athari zake ambazo zinachukua sehemu kubwa ya maudhuihaya. Kwa ujumla wake, jumuiya inayozungumziwa ni ile inayozingatia mfumo wa kuumeni. Huu ni mfumo  unaompa mwanamume nguvu na mamlaka zaidi ya mwanamke. Mfumo huu unajulikana pia kama mfumo wa ubabedume ambao humweka mwanamume katika nafasi ya juu kijamii akilinganishwa na mwanamke. Mfumo huu pia unagawanya majukumu tofauti baina ya mwanamume na mwanamke kulingana na jinsia yao. Hali kama hii tunaiona pale  Mangwasha anapotamani kuondoa uhasama wa Wakule na Waketwa lakini kwa vile yeye ni mwanamke, hangeweza kusikilizwa. Jamii yake pia haimtarajii yeye kuwa na ujasiri wa kwenda kuongea na wakuu wa nchi na Sio tu kwa sababu ya hali yake ya kijamii lakini pia kutokana na hali ya kuwa yeye ni mwanamke (uk. 8). 

Dhana ya kwamba mwanamke ni chombo tu cha kuchuuzwa na mwanamume inajitokeza katika uk.10 pale ambapo baadhi ya Waketwa waliochomewa nyumba zao wanatoa hoja kuwa kuna wale waliowauza wake zao kwa wakuu ili wapate ajira. 

Wanawake hawana sauti mbele ya wanaume kama anavyowaza Mangwasha kuwa "...walipaswa kusikiliza na kutenda bali si kusikilizwa na kutenda." (uk. 11). Maudhui haya yanaendelezwa pia na mhusika Mangwasha tunapojulishwa kuwa utamaduni uliomlea ulimfunza kutotumia sifa za kike kustarehesha wanaume ili kujinufaisha kimaisha. 

Utamaduni unamfunza mke kujitegemea katika maisha bali si kumtegemea mume kujikimu  katika maisha yake (uk. 12). Udanganyifu ili kufaidi kitu pia hauvumiliki kwa mwanamke na mila inayozingatiwa na jamii inabainishwa vyema na mhusika Mbungulu anaposema,  "Usimfuate mumeo kwenye makao ya starehe." (uk. 32). 

Maudhui ya imani asili ya jamii pia yanakaririwa na Mrima anayeamini kuwa mwanamke huwa na maneno mengi kama chiriku (uk. 40) na kwamba mke hapaswi kumuuliza mumewe kule aendako au atokako. Mrima anasema, "...wanawake wa kisasa wanavunja kila mwiko  uliowekwa na wazee." (uk. 40). Mifano anayotoa Mrima ya 'ngamia kumea pembe' au 'shingo 

kupita kichwa' ni ishara kamili ya jinsi utamaduni asilia unavyomfunza mwanamume kuhusu  mwanamke kumaanisha daima mwanamke hawezi kumpiku mwanamume. 

Kupitia kwa Mrima pia, maudhui ya jinsi utamaduni asilia unavyosawiriwa katika riwaya yanaonekana pale anaposema kuwa yeye ni mwanamume na mke hangemzuia kuoa; kwamba angeweza kuoa wakati wowote na idadi yoyote ya wanawake. Katika jamii nyingi hasa  barani Afrika, wanaume huweza kuoa zaidi ya mara moja na hii ni desturi kongwe miongoni mwa jamii nyingi. 

Utamaduni asilia pia unamtaka mume aweze kuitunza jamaa yake pamoja na kuisimamia. Hii ndiyo maana Mrima anasisitiza kuwa mila haimruhusu kutunzwa na mkewe. Anasema,  "Siwezi kuvunja mila kwenda kutunzwa kama mtoto." (uk. 101). Haya yanakaririwa na Sagilu anapomuuliza Mangwasha kwa nini hajamwambia ampe Mrima kazi. Hii inamaanisha si ada ya mume kutunzwa na mke. Dhana ya uovu wa mwanamke ni dhana inayoshikiliwa na jamii nyingi pia ulimwenguni. Dhana hii inaendelezwa kupitia kwa kisasili anachosimulia mhusika Sauni kinachobainisha uovu na kutoaminika kwa mwanamke (uk. 80-83). 

Utamaduni wa kisasa unajitokeza kwa sura mbalimbali. Desturi ya kuhodhi mali na kujilimbikizia pesa inatokana na ubinafsi unaofungamana na maisha ya kibepari. Mashindano  ya kujinufaisha kifedha na uchu wa kuwa na mali nyingi au vitu ndio unaowafanya watu  kutoweza kuwajali wengine hasa matajiri. Jamii inajigawa katika makundi mawili; walio  navyo na wasio navyo. 

Desturi ya mali kumilikiwa na wachache kama vile akina Sagilu, Mbwashu na jamaa ya Mtemi Lesulia inaendeleza ubeberu na unyanyasaji wa maadui wao. Usasa pia unabainika kutokana na wingi wa maisha ya raha na starehe. Jamii inazingatia maisha ya ufasiki, uzinzi na kutowajibika katika ndoa. Tunaambiwa Sagilu anabadilisha magari sawa na anavyobadilisha wanawake (uk. 18). Ngoswe pia anakumbatia maisha ya anasa na biashara haramu kama ile ya mihadarati (uk. 123). 

Wasichana wanatupilia mbali maadili na kukumbatia starehe na pesa kuliko utu kama vile Sihaba na Cheiya. Majukumu katika asasi ya ndoa yanabadilika. Pale ambapo mwanamume anahitaji kuwa kichwa kwa jamaa yake, tunamwona akihepa jukumu hili linalotwaliwa na mwanamke hasa katika ndoa za kisasa. Hivi ndivyo anavyofanya Mangwasha (uk. 29).  Wanaume nao wanakosa adabu wanapowanyemelea wake za watu. Tazama jinsi Sagilu  anavyomnyemelea Mangwasha au hata kuzaa na mke wa Mtemi Lesulia (uk. 161). 

Mangwasha anaonekana kukashifu mila zilizopitwa na wakati pale anapomwambia Mbungulu kwamba angeivunja mila ya kutomfuata mumewe katika starehe zake (uk. 32) na kudharau baadhi ya mila kama hizo. 

Maisha ya anasa, ulevi na matumizi ya dawa za kulevya

Ufasiki ni tabia ambayo hukiuka maadili ya kijamii. Tabia kama hii huhusishwa na uzinzi au uzinifu. Tunaonyeshwa jinsi Sagilu anavyoishi maisha ya anasa huku akifanya usuhuba na wanawake kama Sihaba nje ya ndoa. Anawanyang'anya wanaume wake zao hadi kuitwa mnyakuzi na dudumizi (uk. 18). Anamhangaisha Mangwasha kutaka kufanya usuhuba naye,  hata kutaka kumhonga kwa kutumia pesa ili akubali (uk. 30, 60). 

Ufuska wake unaonekana pia pale Mrima anaposema Sagilu alikuwa na masuria watoshao  kijiji kizima (uk. 18). Mrima anatumbukia katika anasa na kushiriki ulevi kupitia kwa Sagilu 

(uk. 30, 37, 39, 42). Anashindwa hata kuitunza jamaa yake. Barua aliyoandikiwa Mrima na mwanamke na 

ambayo inapatikana ndani ya mkoba wa Mangwasha pamoja na yaliyomo katika barua hiyo  ni ishara ya maisha ya uzinzi aliyoishi Mrima (uk. 77). 

Ulevi pia unamfanya Mrima kupotelea Majaani, pahali palipokuwa na walevi wa kila aina,  ilhali alikuwa na familia. 

Maisha ya anasa yanabainika kupitia kwa uhusiano wa Sagilu na Cheiya, uhusiano  uliojengwa juu ya ufasiki (uk. 119-123). Ngoswe pia anaendeleza maudhui ya anasa, ulevi na ufasiki pale tunapoambiwa anazifuja pesa kwa anasa mbalimbali. Vijana wengine wa kitajiri kama yeye pia wanajivinjari katika starehe kutokana na utajiri wa wazazi wao. 

Ngoswe ni kielelezo cha wale wanaofanya biashara ya dawa za kulevya (uk. 123) ambapo  mihadarati inaonekana kutumiwa kiholela nchini. 

Mandhari ya ulevi katika mtaa wa Ponda Mali yanaendeleza maudhui ya ulevi kwani pahali hapa palikuwa na walevi wa kila aina na unywaji pombe wa kupindukia (uk. 33). 

Unafiki 

Ni tabia ya mtu kujifanya rafiki au mwandani wa mtu ilhali sivyo. Tabia kama hii hudhihirisha uongo au udanganyifu. Sagilu anapomtuma Sihaba kuwapelekea Mrima na Mangwasha zawadi siku ya arusi yao ni dhihirisho ya unafiki. Hii ni kwa sababu Sagilu  alifahamu kilichokuwa katika kifurushi kilikuwa kilipuzi lakini akajifanya kuwakirimia zawadi ya arusi (uk. 25). 

Unafiki pia unaendelezwa na Sagilu pale ambapo anajifanya kumjali Mangwasha anapokumbwa na mateso huku akijua ndiye aliyekuwa akisababisha mateso hayo ya Mangwasha. Kwa mfano, Sagilu anamuuliza Mangwasha, "Mbona umekonda sana siku  hizi?" (uk. 60). Kwa upande wake, Mangwasha anamjua Sagilu kama mnafiki hasa pale anaposema kwamba Sagilu ni chua ndani ya mchele na kumwita lumbwi. Chua 

inapokuwa ndani ya mchele si rahisi kuitambua hadi pale unapoutafuna wali. Kadhalika,  lumbwi au kinyonga ana tabia ya kubadilisha rangi kiasi cha kumfanya mtu kutomtambua kwa urahisi ili kubaini rangi yake kamili. 

Maudhui ya unafiki yanajitokeza kupitia kwa Mtemi Lesulia ambaye alitaka kunyakua ardhi ya Matango kwa kisingizio kuwa serikali ilitaka kujenga soko (uk. 95). 

Chifu Mshabaha pia anaendeleza maudhui ya unafiki pale ambapo anawahujumu Waketwa na kupokea mlungula kinyume na sheria za nchi aliyoitumikia huku akishirikiana na mtemi kuwa serikali ilitaka kujenga soko. 

Nanzia na Mbwashu wanaendeleza unafiki pale wanapowatembelea watu waliochomewa nyumba zao pale kanisani ili kuwapa misaada ilhali wakijua lengo la kuwachomea watu hao  makazi yao. 

Tamaa na ubinafsi

Tamaa ni hali ya kutaka sana kitu, matamanio ya kitu au jambo. Tamaa kama hamu au utashi mkubwa wa kufaidi kitu huwa mbaya iwapo utafaidi mtu mmoja kutokana na ubinafsi wake 

au kundi la watu lenye maslahi yanayofanana. Ubinafsi hubainika pale mtu anapojipendelea yeye au kujifikiria yeye mwenyewe bila ya kuwajali wengine. Kuna wahusika kadha wanaoendeleza maudhui ya tamaa na ubinafsi hasa pale mwandishi anapotaja kuwa mtaa wa Majuu ulikuwa umeshiba ubinafsi na ubaguzi. 

Mtemi Lesulia anajawa na tamaa ya uongozi. Yuko tayari kuwadhulumu au hata kuwaua wapinzani wake kutokana na tamaa ya uongozi wa nchi. Anamteka nyara Lonare asiweze kuwa katika kinyang'anyiro cha uchaguzi mkuu anapohisi kwamba huenda akamshinda na kuwa mtemi (uk.10, 51, 164-172). 

Aidha, akiwa na wakwasi wenzake kama vile Sagilu na Mbwashu wanahujumu pato la nchi kutokana na tamaa ya kujilimbikizia mali. Ubinafsi wa Mtemi Lesulia unaonekana pale anapomiliki rasilimali za serikali hasa kupitia kwa unyakuzi unaoendelezwa na mkewe Nanzia. 

Mfano unaotolewa wa mchwa na kichuguu (uk. 93) unaonyesha pia ubinafsi wa mtemi kutokana na kufaidi jasho la wengine. Nanzia anaonyesha tamaa na ubinafsi pale anapojaribu  kubinafsisha jumba la Skyline Mall ambalo ni mali ya serikali (uk. 147) na ardhi ya Matango  kwa kushirikiana na mafisadi wenzake. 

Sagilu anaendeleza maudhui ya tamaa na ubinafsi pale utashi wake wa pesa unampofanya kuhodhi bidhaa kama vile ngano ili kuiuza kwa bei yajuu (uk. 17). Tamaa hiyo inamfanya hata kuhatarisha maisha ya watoto nchini Matuo anapoagiza maziwa yenye sumu kutoka ughaibuni (uk. 17). Ubinafsi wake unamfanya kuwazuia wengine wasimpiku kibiashara. 

Tunaambiwa, "Kwa wale waliomshinda kwq werevu, aliwafanyia hila, mizungu na visanga hata kuwafilisi kabisa kibiashara." (uk. 16). Tamaa ya uongozi na mali inamwingiza katika urafiki na mtemi ili kutosheleza maslahi ya kibinafsi. Ubinafsi pia unamfanya Sagilu  kumtumia Mrima ili kujinufaisha kisiasa kutokana na tamaa ya uongozi. Sagilu aliandamwa pia na tamaa za kimwili. Anawabadilisha wanawake hadi kuitwa dudumizi kutokana na kuvizia na kuwachukua wake wa wengine (uk. 18). 

Kupitia kwa Sagilu pia, tunamwona akiendeleza ubinafsi kwa jinsi anavyomtumia Sihaba Sio  tu kama kimada wake bali pia kutosheleza utashi wake wa kumiliki mali na biashara. 

Anaendeleza maudhui ya tamaa anapomnyemelea Mangwasha tangu pale alipokuwa msichana hadi baada ya kuolewa na Mrima ili kutosheleza uchu wake. Tamaa ya Sagilu  inamfanya hata kuzaa na mke wa Mtemi Lesulia kutokana na udhaifu uliodhihiri katika ndoa yake. Anatumiwa pia na mtemi kama kikaragosi ili kuwanyanyasa watu wa Matango huku  akitumaini kufaidika kibinafsi. 

Mrima anaendeleza maudhui ya tamaa na ubinafsi pale ambapo tamaa ya pesa inamtosa katika tabia potovu. Anadanganywa na Sagilu huku akipewa pesa hadi kuitelekeza jamaa yake. Ubinafsi wa kuyajali maslahi yake pekee unamfanya kukaidi masharti ya ndoa na uwajibikaji. 

Ubinafsi wa Mafamba unamfanya kuhujumu sheria za nchi kwa kuutetea ufisadi serikalini.  Ubinafsi pia unamfanya kudanganya kuwa vyeti vya kumiliki ardhi vya wenyeji wa Matango  vilikuwa ghushi (uk. 94), na kwamba serikali ilitaka kujenga soko katika mtaa wa Matango. 

Tamaa ya pesa inamfanya Sihaba kujiingiza katika biashara ya ulanguzi wa watoto wa kike (uk. 141-144). Usuhuba wake na Sagilu pia unajengwa juu ya misingi ya tamaa ya pesa na ubinafsi. Anatumiwa na Sagilu kuhujumu haki za Waketwa mbali na kutumiwa na Sagilu  kuwaangamiza maadui zake kibiashara (uk. 16). Hakujali maslahi ya wengine ila yake binafsi. 

Udanganyifu

Udanganyifu ni vitendo vya kughilibu watu au kufanya jambo ambalo mtu anajua ni uongo. 

Maudhui ya udanganyifu yanajitokeza katika serikali ya Mtemi Lesulia hasa kupitia kwa mwanasheria Mafamba anayedanganya mahakama kuhusu ujenzi wa soko katika ardhi ya Matango (uk. 94). Maudhui ya udanganyifu yanabainika kupitia kwa Sagilu anayeshirikiana na Sihaba kujaribu kuwaangamiza Mrima na Mangwasha siku ya arusi yao. Zawadi aliyobeba Sihaba haikuwa halisi bali kilipuzi cha kuwaangamiza maarusi hao. 

Ukatili

Hii ni tabia inayodhihirisha ukosefu wa huruma. Ukatili unatokana na moyo mgumu kiasi cha kuweza kutekeleza mauaji au kuleta hasara na mateso kwa wengine. 

Maudhui ya ukatili yanaendelezwa kupitia kwa Sagilu ambaye aliweza hata kuwaua washindani wake katika biashara (uk. 16). Ukatili wake unabainika pia pale anapoagiza maziwa ya watoto yenye sumu bila kujali maisha Yao. 

Sagilu anapovunja ndoa za Wengine anaendeleza ukatili. Anaendeleza maudhui ya ukatili pale anapomtesa Mangwasha kimawazo huku akihatarisha ndoa yake kwa kutumia pesa kumlewesha Mrima hadi akawa mlevi na mwishowe kuachishwa kazi. 

Sagilu anaendeleza maudhui ya ukatili anapompokonya mwanawe mpenzi wake na hivyo  kuuvunja uchumba wao. Kushiriki kwake katika kupanga njama ya kuwachomea Waketwa makazi yao ili yeye na jamaa ya mtemi wafaidi kisiasa ni mwendelezo pia wa maudhui ya ukatili. 

Ukatili unaendelezwa na Mtemi Lesulia pale anapowadhulumu raia wake kupitia kwa  vitendo vya kikatili ili kujinufaisha kisiasa. Anampangia Lonare mauti kwa sababu za kisiasa.  Ukatili wa serikali yake unabainika pale yeye na wenzake waliposhindwa kesi ya ardhi ya Matango. Tunaona hakimu akinyang'anywa leseni ya uanasheria hata kushushwa madaraka bila kuzingatia haki na ushahidi uliowasilishwa mahakamani. Kauli ya mtemi kwamba,  "Wale panya wamesharudi katika makao Yao..." (uk. 78) inaonyesha ukatili wake kwa wenyeji wa Matango. 

Mwanasheria Mafamba anatumiwa kuendeleza ukatili wa Mtemi Lesulia pale anapotimuliwa kutoka katika afisi za serikali bila kujali kazi aliyoifanyia serikali hiyo dhalimu. Maudhui ya ukatili yanaonekana wakati wa uchaguzi wa mchujo tunapomwona mtemi akiwapa vijana  pesa na kuwaamuru waharibu zoezi hilo ili mwishowe yeye na Sagilu wapate kuwashinda wapinzani wao. Hakujali iwapo vijana hao wangeuliwa na askari walinda usalama wala kujali rai za mwanawe Ngoswe (uk. 129- 130). 

Mtemi Lesulia anaendeleza maudhui ya ukatili pale anapohusika katika kutoweka kwa  Lonare siku chache kabla ya uchaguzi mkuu. Anafanya hivyo ili yeye abahatike kushinda kiti cha mtemi wa Matuo. 

Maudhui ya ukatili yanaonekana kupitia kwa Sihaba pale anaposhirikiana na Sagilu  kuwachomea Waketwa nyumba zao. Pia anakubali kusimamia ujenzi wa ua katika makazi ya Waketwa ilhali anajua kwamba kitendo kile ni cha kikatili. 

Maudhui ya ukatili yanaendelezwa na Sihaba pia pale anapowapelekea Mrima na  Mangwasha zawadi ya arusi akiwa na lengo la kuwaangamiza. Anapoanzisha makao ya Red  Beads Lodgings ili kuwachuuza vigoli kwa wanaume ni mwendelezo wa maudhui ya ukatili.  Kujinufaisha kwake kutokana na biashara hiyo haramu ni ukatili anaowatendea watoto kwani hakujali maisha yao ya baadaye (uk. 140-143). 

Mapenzi na asasi ya ndoa

Mapenzi ni hali ya mvuto na upendo alio nao mtu kwa mtu mwingine; hisia ya upendo aliyo  nayo mtu moyoni mwake kuhusu mtu mwingine. 

Ndoa ni maafikiano rasmi ya baina ya mwanamume na mwanamke ili waweze kuishi pamoja kama mke na mume. 

Maudhui ya mapenzi na asasi ya ndoa yanaelezwa kupitia kwa wahusika mbalimbali. Asasi ya ndoa inakumbwa na matatizo kadha yakichangiwa na tamaa za kimwili na pesa. Hata hivyo, hakuna ndoa inayovunjika hata kama misukosuko inakuwepo. 

Ndoa ya Mtemi Lesulia na mkewe Nanzia awali ilikumbwa na tatizo la ukosefu wa watoto  hadi kufikia kiwango cha mtemi kutaka kumtaliki mkewe. Tatizo hili linatoweka pale mtoto  anapozaliwa, hata ingawa baadaye tunafahamishwa kuwa mzazi wake si mtemi. Ingawa mtemi hafahamu hili, Ngoswe anaachwa na mshtuko mkubwa mama yake anapomweleza kuwa mzazi wake ni Sagilu. 

Ndoa ya Sagilu na mkewe pia inayumba pale Sagilu anapopatwa na kichaa. Mkewe anamtoroka hadi afueni inapomrejea mumewe, na ndoa hiyo kuimarika tena. 

Ndoa kati ya Mrima na mkewe Mangwasha pia ina misukosuko; tokea ulevi wa Mrima na kutowajibikia ndoa yake hadi vishawishi vya pesa za Sagilu vinavyomfanya kuachishwa kazi. Uvumilivu wa Mangwasha mwishowe unafaulu kuokoa ndoa yake. 

Mapenzi ni sehemu ya maudhui yanayojitokeza pia. Kuna mapenzi baina ya wanandoa na mapenzi baina ya vijana. Mapenzi baina yavijana hayaonekani kudumu. Mifano ni kama vile usuhuba wa Mashauri na Cheiya ambao unaonekana kuegemea upande mmoja. Cheiya anaonekana kumpenda Mashauri lakini mapenzi yake siyo ya dhati ila anavutiwa na maisha  ya anasa na pesa. Hali hii inaonekana pale anapofanya urafiki na mzazi wa Mashauri ili afaidi pesa zake. Sihaba naye anajifanya kumpenda Sagilu lakini mapenzi yake siyo ya dhati.  Anamfuata Sagilu ili kumtimizia mahitaji yake ya maisha. 'Pesa kwake zilikuwa kigezo cha penzi' (uk.16). Ngoswe haonekani kuwa na mpenzi mmoja bali anawabadilisha wanawake kutokana na uwezo wa kifedha alio nao. Hathamini mapenzi kati ya wapendanao kama anavyoeleza 

Ukiukaji wa haki za watoto

Haki ni utendaji, ufuataji na utumiaji wa sheria na kanuni katika kutimiza jambo. Maudhui ya ukiukaji wa haki za watoto yanabainika tunapomwona 

Mangwasha pale mwanzoni akihangaika na wanawe peke yake bila baba yao. Mrima anashiriki ulevi na maisha ya anasa hadi kuachishwa kazi. 

Hajishughulishi na malezi ya wanawe kama vile kuwalisha, kuwavisha, kuwasomesha na kuwapa malezi mema kama mzazi. Anakosa uwajibikaji hadi pale anaposhurutishwa kuishi na jamaa yake na kuwajibika (uk. 1, 29, 31, 101, 115). 

Maudhui ya ukiukaji wa haki za watoto yanaonekana pale wasichana wadogo  wanapozalishwa wakiwa bado hawajatimiza umri wa kujitwika majukumu kama hayo (uk.  137-138). Maudhui haya yanaendelezwa kupitia kwa taswira anayochora mwandishi kuhusu  watoto wenye umri mdogo. Hawa wanaishi katika barabara na vichochoro vya mji huku 

wakinusa gundi na magunia ya taka yakiwa migongoni. Huu ni ukosefu wa malezi mema unaotokana aghalabu na umaskini wa wazazi wao (uk. 138). Kwa ujumla maudhui haya yanaendelezwa katika nchi ya Matuo ambayo inahiari kukinyanyasa kizazi hiki kichanga bila kuwa na mpango mzuri wa maisha yao. 

Maudhui ya ukiukaji wa haki za watoto pia tunayaona kupitia kwa vitendo vya Sihaba. Huyu  anapowahusisha wasichana wadogo katika biashara ya ukahaba ili ajinufaishe kifedha huwa pia anakiuka haki za watoto (uk. 141-143). 

Nafasi ya mwanamke katika jamii

Maudhui ya nafasi ya mwanamke yanaendelezwa kupitia kwa taswira mbalimbali za mwanamke. 

Mangwasha ni mwanamke aliyejikomboa kimawazo. Anakaidi mila na desturi potovu za jamii zilizopitwa na wakati pamoja na zile zinazomdhalilisha mwanamke. Tunamwona akikataa ushauri wa Chifu Mshabaha aliyetaka kumchagulia mchumba. 

Anakataa ushauri wa Mbungulu pia pale anapomwambia mila hairuhusu mke kumfuata mumewe akiwa katika starehe zake (uk. 32). 

Maudhui ya nafasi ya mwanamke yanajitokeza kupitia kwa Mangwasha anayejitambulisha kama mtetezi na mpiganiaji wa haki za watoto, vijana na wanaodhulumiwa katika jamii. 

Mwanamke huyu akishirikiana na wengine kama Mbungulu anafaulu kuwanasua watoto wa kike waliokuwa wamenaswa katika mtego wa Sihaba aliyetaka kujitajirisha kupitia kwao. 

Tunamwona pia akiwashirikisha vijana na kuwapa usaidizi wa kujiendeleza katika maisha yao. Tunaarifiwa, "Mangwasha alifungua (uk. 154) afisi mjini ili kushughulikia vijana na watoto wa mitaani..." na kwamba alipata ufadhili kutoka katika mashirika mbalimbali ya kuwasaidia watoto. 

Maudhui ya nafasi ya mwanamke pia yanaendelezwa kupitia kwa Mbungulu anayejitokeza kama mhafidhina wa utamaduni wa jamii yake na majukumu ya mwanamke katika utamaduni huu. Anaendeleza uhifadhi wa mila zilizowekwa na jamii yake hasa pale anapomshauri Mangwasha kuhusu mafunzo aliyofunzwa na jamii yake (uk. 32). 

Maudhui haya pia yanajitokeza kupitia kwa Mrima anayezingatia masharti ya jamii yake iliyosheheni ubabedume unaomdhalilisha mwanamke kiasi cha kutomsikiliza mkewe.  Mangwasha anasimama kidete na kutimiza wajibu wake katika ndoa licha ya kwamba mumewe anamtupa. Tunamwona jinsi anavyojizatiti kuwatunza wanawe pale mumewe alipomtoroka kutokana na anasa za ulevi. 

Aidha, dhuluma dhidi ya mwanamke inajitokeza kupitia kwa kauli za Mrima hasa pale anapomtoroka mkewe na wanawe ili kufaidi starehe kupitia pesa alizokuwa akipewa na Sagilu (uk. 40-41). Maudhui haya pia yanaonyesha kwamba mwanamke hathaminiwi kama kiumbe sawa na mwanamume chini ya mfumo huu wa ubabedume hasa pale Mrima anaposema, "Tangu lini mke amuulize mumewe kule aendako au atokako?...Ama kweli,  wanawake wa kisasa wanavunja kila mwiko uliowekwa na wazee." (uk. 40). 

Maudhui ya nafasi ya mwanamke kama asiyeheshimiwa yanajitokeza kupitia kwa Sagilu  ambaye anamchukua mwanamke kama pambo tu na anayeweza kushawishiwa kwa urahisi kwa kutumia pesa. Hali hii inaonekana pale anapotaka kumpa Mangwasha pesa ili akubali kuwa mpenzi wake (uk. 60). 

Kwa upande mwingine, maudhui haya yanabainisha nafasi ya mwanamke kama katili, mzinzi na mwenye ubinafsi. Kupitia kwa Sihaba, mwanamke anajitokeza kama kielelezo kibaya kwa jamii hasa anapofananishwa na mabaya yote yanayokumba ulimwengu (taz. kisasili kinachosimuliwa na Sauni (uk. 81-83). 

Taswira mbaya ya mwanamke inaonekana pia kupitia kwa wahusika wa kike kama vile Mbwashu, Nanzia na Cheiya ambao wanajitokeza kama vitegemezi vya wanaume. Mbwashu anashirikiana na wanaume kama Mtemi Lesulia kujinufaisha kiuchumi ilhali Nanzia anaishi chini ya mbawa za mumewe ili kujiimarisha kiuchumi na kimaisha. Cheiya anaendeleza maudhui hayo ya utegemezi kwani tunaona akiwategemea Mashauri na Sagilu ili kujinufaisha. 

Umaskini

Umaskini ni hali ya kutokuwa na mali; ukata, uchochole. 

Maudhui ya umaskini yanaendelezwa kupitia kwa sera mbovu za uongozi katika serikali ya Mtemi Lesulia. Uongozi unatawaliwa na ubaguzi unaotokana na jamii mbili hasimu; Wakule wanaofaidi pato la nchi zaidi kutokana na utawala wa Mtemi Lesulia ambaye ni Mkule, na Waketwa wanaofukarishwa na ubaguzi huo. Utabaka na ufisadi pia unachangia kuleta umaskini. 

Kuna matajiri wenye vyeo na mali kwa upande mmoja na maskini wanaozumbua riziki kutokana na ajira za mapato ya chini. Maudhui haya pia yanaendelezwa kupitia kwa sera za nchi ambazo ziliwafaidi wachache (uk. 51). Umaskini unasababisha vijana kutumiwa na matajiri kutekeleza uovu. Katika (uk. 66), tunaona vijana wakitumiwa na matajiri kuteketeza makazi ya Waketwa. Umaskini unachangiwa na ukosefu wa ajira hasa kwa vijana  waliohitimu shuleni au vyuoni. Umaskini unawafanya hata wazazi kuwachuuza mabinti zao  wachanga ili wapate pesa (uk. 143). Maudhui ya umaskini yanabainishwa kupitia kwa sera za uchumi zisizozingatia maslahi ya wanyonge. Viongozi wa nchi wanatajirika ilhali wananchi walio wengi wanafukarishwa zaidi, lengo likiwa kuwafukarisha ili iwe rahisi kwao kuendelea kuwatawala. 

Ukosefu wa matumaini

Matumaini ni hali ya matarajio ya kupata kitu; matarajio, matamanio. 

Ukosefu wa matumaini ni hali ya kukataa tamaa; kukosa matarajio, kukosa matamanio,  Maudhui ya ukosefu wa matumaini yanabainika pale idadikubwa ya vijana inaonekana kuzurura mjini na kupoteza muda wao katika viambaza vya maduka kwa kukosa matumaini.  Mwandishi anaeleza kuwa "Ukosefu wa matumaini ya kuishi ulianza kuhasiri mifumo ya kijamii." (uk. 47). Ukosefu huu wa matumaini unasababisha maafa katika jamii pia (uk. 44-  47). Vijana waliomaliza masomo hawana pa kwenda. Ukosefu wa ajira kwa vijana hao  unawafanya kukosa matumaini. Umaskini wa wazazi wao pia unachangia katika ukosefu wa matumaini. Vibaka wa mji wanakosa matumaini na wanasalia kusubiri ghasia zizuke mjini ili waweze kuwapora watu mali zao. 

Uvumilivu

Uvumilivu ni hali ya kuvumilia mambo magumu; ustahimilivu. Maudhui ya uvumilivu  yanajitokeza kupitia kwa wahusika Mangwasha na Lonare. 

Mangwasha anavumilia vitisho na dharau za Chifu Mshabaha ilimradi aweze kuitunza jamaa yake. Anavumilia kazi nyingi afisini mwa chifu huyo ili aweze kuwakimu wanawe pale mumewe anapomtoroka. Anavumilia vitimbi vya chifu ilimradi apate mawili matatu kuhusu  njama za serikali na yale wanayopangiwa Waketwa. Anavumilia kauli za chifu za kumvunja moyo ili aweze kulinda ajira yake. Mangwasha anaendeleza maudhui ya uvumilivu pia pale anapovumilia lugha ya dharau na ushawishi wa pesa kutoka kwa Sagilu ili asitiri ndoa yake na Mrima. Aidha, anavumilia dharau, matusi na ulevi wa mumewe ili kusitiri ndoa yake.  Kwa upande wake, 

Lonare anaendeleza maudhui haya kupitia uvumilivu dhidi ya vitisho vya uongozi wa Mtemi Lesulia kutaka kumwangamiza au hata kuangamiza biashara yake (uk. 50). Maudhui ya uvumilivu pia yanaendelezwa na 

Lonare kutokana na jinsi anavyoteswa, kutekwa nyara hadi kuhatarisha maisha yake ili asaidie kuikomboa nchi yake kutokana na uongozi mbaya wa Mtemi Lesulia. 

Usaliti

Usaliti ni hali ya kwenda kinyume na matarajio ya mtu au nchi. Pia ni ile hali ya kuwafanya watu wakosane kwa kuwachonganisha kupitia matumizi ya uongo. 

Maudhui ya usaliti yanajitokeza kupitia kwa Chifu Mshabaha, Mrima, Sagilu, Mtemi Lesulia,  Nanzia, Mbwashu na Cheiya. 

chifu Mshabaha anaisaliti jamii ya Waketwa kwa kushiriki katika njama ya kuwaondoa kutoka katika makao yao (uk. 55). Chifu anamsaliti 

Mangwasha anapompa Mrima bahasha ya pesa kama hongo ya kuendesha kampeni za Mtemi Lesulia (uk. 110), kinyume na matakwa ya jamii yake. Aidha, usaliti unaendelezwa na chifu  pale anapomsaliti Mangwasha kwa kumleta msichana mwingine kazini kwake ili kumfuta yeye kazi (uk. 135). 

Maudhui ya usaliti yanajitokeza kupitia kwa Mtemi Lesulia pale anapousaliti uaminifu wa Ngoswe kwa kuwaambia waende kuvuruga amani wakati wa uteuzi wa viongozi ili kuhakikisha ushindi unamwendea Sagilu bila kujali iwapo wangeuliwa na askari (uk. 129). 

Mtemi anaisaliti nchi pamoja na wananchi wa Matuo kwa kuzorotesha uchumi kupitia kwa sera mbovu za uongozi na ufisadi uliokithiri. Isitoshe, anaisaliti jamii ya Waketwa kwa kuibagua katika ajira, biashara, hata katika makazi yao. 

Maudhui ya usaliti yanajitokeza kupitia kwa Mtemi Lesulia pia kwani licha ya mwanasheria Mafamba kuifanyia serikali yake kazi na kumfichia uovu wake katika kesi za ufisadi,  anamnyang'anya cheti cha uanasheria na kumtowesha kutoka mjini Taria. Pia anamnyang'anya hakimu cheti chake cha uanasheria na kumfuta kazi licha ya kwamba alikuwa akitekeleza majukumu yake kulingana na sheria. 

Maudhui ya usaliti yanaendelezwa na Sagilu anapoisaliti jamii ya Waketwa walioishi Matango kwa kushiriki katika kuchoma makazi yao licha ya kwamba yeye mwenyewe  alitaka achaguliwe kuwa mbunge wao. Anamsaliti Mrima kwa kumhonga pesa ashiriki katika anasa huku akijua alimtaka mkewe kimapenzi. 

Tunamwona akimsaliti Mangwasha kwa kumtembelea na kujifanya anayajali maslahi yake ilhali ndiye anayemfadhili Mrima kushiriki ulevi na anasa hadi kufutwa kazi. 

Sagilu anamsaliti mwanawe Mashauri kwa kumnyang'anya mchumba wake Cheiya bila kujali heshima yake. 

Pia anamsaliti Mtemi Lesulia kwa kumhakikishia kuwa kila kitu kiko shwari wakati wa uchaguzi mkuu huku akijua kwamba katu Lesulia hangeshinda katika uchaguzi huo (uk.  174). 

Kupitia kwa Mrima, maudhui ya usaliti yanabainika anapoisaliti jamaa Yake kwa kushirikiana na Sagilu huku mkewe na wanawe wakiteseka. 

Mrima pia anamsaliti mkewe kwa kufanya usuhuba na wanawake nje ya ndoa hasa kupitia kwa barua anayoipata Mangwasha (uk. 77), huku mkewe akijitahidi kuitunza familia bila usaidizi kutoka kwake. 

Usaliti pia unajitokeza pale Mrima anapoisaliti jamii yake hasa Lonare na wengine waliomwokoa kutoka katika maisha ya ulevi, pale anapochukua hongo ili amfanyie mtemi kampeni ilhali akijua huyu alikuwa adui wa Waketwa. 

Maudhui haya pia yanaendelezwa na Cheiya anayemsaliti Mashauri anapokubali kufanya usuhuba na Sagilu bila kujali kuwa huyu alikuwa mzazi wa Mashauri. Nanzia anamsaliti mumewe Mtemi Lesulia pale anapofanya usuhuba na Mhindi pamoja na Sagilu na kuzaa watoto nje ya ndoa. 

Usaliti wa Mbwashu unatokea pale anapotorokea Ulaya baada ya Mtemi Lesulia kushindwa katika uchaguzi mkuu. Anamtoroka baada ya kutajirika kutokana na utawala wake huku  akimwacha na fedheha ambayo hakutaka kushiriki wala kujihusisha na uovu waliofanya pamoja wakati wa utawala wake. 

Ulipizaji kisasi

Kisasi ni tendo la kulipiza ubaya aliofanyiwa mtu. 

Kulipa kisasi ni kulipiza maovu aliyotendewa mtu. 

Maudhui ya kulipiza kisasi tunayaona kupitia kwa Sagilu ambaye analipiza kisasi tangu pale penzi lake lilipokataliwa na Mangwasha. Anamtumia Mrima kulipiza kisasi pale anapofaulu  kumteka akili, kumpumbaza kwa pesa na anasa za ulevi ilimradi Mangwasha 

ateseke katika ndoa yake. Sagilu anahiari hata kujaribu kutoa uhai wa Mangwasha na mumewe siku ya arusi yao kwa kumtumia Sihaba ili awaangamize kwa kilipuzi. 

Ukombozi

Ukombozi ni hali ya kumwokoa mtu au watu kutoka katika hali mbaya kama vile udhalimu  au maonevu ya aina yoyote. 

Maudhui ya ukombozi yanajitokeza kupitia kwa michakato ya ukombozi wa nchi ya Matuo  dhidi ya uongozi mbaya wa Mtemi Lesulia na ukombozi wa Waketwa wanaodhulumiwa katika ardhi yao. Maudhui ya ukombozi yanajitokeza kupitia kwa Mangwasha anayefanya kila juhudi ya kutaka kuwakomboa Waketwa kutokana na dhuluma za utawala wa mtemi,  hata kama alikuwa mwanamke asiye na cheo wala fulusi' (uk. 8). 

Ijapokuwa Mangwasha hana mamlaka serikalini, anatumia nafasi yake kama mwajiriwa wa serikali katika afisi ya Chifu Mshabaha kuwaibia siri Waketwa wenzake dhidi ya njama wanazopangiwa na utawala dhalimu wa mtemi. Kupitia kwa Mangwasha pia, tunamwona akihitaji usaidizi wa Lonare na wengine ili kumkomboa mumewe kutoka katika maisha ya anasa na ulevi (uk. 97-100). 

Lonare anaendeleza maudhui ya ukombozi pale anapoingia katika kinyang'anyiro cha uchaguzi mkuu ili aweze kuchaguliwa na kuikomboa nchi ya Matuo kutoka katika utawala dhalimu. Tunamwona akishirikiana na wengine kama vile Mangwasha, Sagura na Mashauri kuikomboa nchi. 

Mwendelezo wa maudhui haya pia unajitokeza pale ambapo Mangwasha, Mbungulu na wengine wanafaulu kuvunja biashara haramu ya Sihaba na kuwakomboa watoto wa kike waliokuwa wakidhulumiwa kimapenzi. 

Kielelezo cha ukombozi pia tunakipata kupitia kwa mwanasheria Mwamba ambaye anatumia ujuzi wake wa kisheria na kushinda kesi ya ardhi ya Matango, na hivyo kuwakomboa Waketwa waliokuwa wamepokonywa ardhi yao. Kupitia kwa ushauri wa Lonare, Ngoswe anakombolewa kutoka katika maisha ya ufasiki na biashara haramu ya dawa za kulevya (Uk.  172-173). 

Ujasiri

Ujasiri ni utendaji wa jambo bila ya kuogopa; ushujaa. 

Maudhui ya ujasiri yanajitokeza kupitia kwa Mangwasha na Lonare. Mangwasha anaendeleza ujasiri pale anapofanya kila awezalo ili kuiokoa ndoa yake iliyokuwa ikihatarishwa na vitendo vya Sagilu. Anaendeleza maudhui ya ujasiri pale anapomsaka mumewe katika mabanda ya walevi na pale anapoandamana na wenzake kumwokoa Mrima kutoka Majaani ambapo palikuwa makao ya walevi na wahuni (uk. 99-102). 

Ujasiri pia unajitokeza kupitia kwa Mangwasha pale anapochomoka mbio kutoka afisini mwake akienda kurudufu stakabadhi alizochukua kutoka katika faragha ya afisi 

ya chifu. Hizi zilikuwa ushahidi kamili wa kuweza kurudishiwa ardhi yao (uk. 86-89). 

Maudhui haya pia yanabainika Mangwasha anaposimama mbele ya hadhara na kuwahamasisha Waketwq warydi katika ardhi yao (uk.74). 

Ujasiri kama maudhui unajitokeza pale Mangwasha anaposhirikiana na wanaume kama vile Lonare, Sagura na Sauni ili kuikomboa jamii yake na nchi kwa ujumla bila kujali ubabedume uliosheheni katika jamii. Mwanamke hakuthaminiwa wala kupewa nafasi kubwa serikalini au hata katika siasa. Maudhui haya pia yanajitokeza pale Mangwasha anapomkabili Chifu  Mshabaha baada ya kupigwa kalamu au pale anapomkabili Sagilu baada ya kugundua  alikuwa akiiharibu ndoa yake. 

Maudhui ya ujasiri kupitia kwa Lonare ni pale anapojasiri kuwania kiti cha mtemi wa Matuo  ilhali akijua hatari iliyomkabili. Anahatarisha maisha yake pale anapotekwa nyara na kuteswa lakini ujasiri huo unamwezesha kuchukua kiti cha mtemi wa Matuo. Ujasiri pia unabainika kupitia kwa meneja wa kampuni ya mabasi ya Lonare ambaye hata baada ya kutishwa na mahasimu wa Lonare, hakuacha kumfanyia Lonare kazi licha ya kwamba alikuwa Mkule. 

Uzalendo

Uzalendo ni hali ya mtu kuipenda nchi yake kwa dhati. 

Maudhui ya uzalendo yanabainika kupitia kwa Mangwasha hasa pale inapodhihirika kuwa,  "Alitamani sana kuzungumza na baadhi ya viongozi ili amani idumu nchini Matuo..." (uk. 7). 

Pale anapowaibia Waketwa siri kutoka katika afisi ya Chifu Mshabaha ili kuuondoa utawala dhalimu wa mtemi ni ishara ya mwendelezo wa maudhui ya uzalendo. Mangwasha anapomkabili chifu na kumwambia kwamba serikali ni ya kila mtu bali si ya watu binafsi (uk. 136) pia ni mwendelezo wa maudhui ya uzalendo. 

Maudhui ya uzalendo yanasawiriwa kupitia kwa Lonare anayeepuka vifo anavyopangiwa na maadui zake ili aokoe nchi yake kutoka katika mikono ya wadhalimu. Tunaambiwa kuwa,  "Alikuwa na ruwaza njema ya kusaidia wenyeji wote wa nchi ya Matuo bila ubaguzi." (uk.  10). 

Uzalendo wake unabainika pale anapowasaidia hata kuwaajiri watu wasiotoka katika jamii yake kwani aliwachukulia wote kuwa wananchi wa Matuo. Hotuba ya Lonare inashirikisha maudhui ya uzalendo (uk. 178-182). Baada ya kuchaguliwa kuwa mtemi wa Matuo,  anawataja wananchi wa Matuo kama ndugu zake bila kujali jamii wanazotoka. 

Umoja

Umoja ni hali ya kuwa na muungano; ushikamano, ushirikiano. 

Maudhui ya umoja yanaonekana kupitia kwa jamii ya Waketwa. Makazi yao yalipochomwa,  waliungana kama kitu kimoja kudai haki yao. 

Umoja wao uliwapa hamasa ya kukita mahema kwenye ardhi yao bila kuogopa vitisho vya utawala wa mtemi. Maudhui haya yanaonekana pale Waketwa waliposhirikiana kudai haki 

yao kisheria bila kujali dhuluma walizopitia hadi wakashinda kesi na kurejeshewa ardhi yao  (uk. 95). 

Maudhui ya umoja pia yanaendelezwa kupitia kwa mtaa wa Majengo ulioishi kila aina ya watu ambao walitangamana vizuri na kuishi kama ndugu (uk. 75). 

Maudhui ya umoja yanajengeka pia kupitia kwa vijana wa kizazi kipya. Mashauri anashirikiana kwa karibu na akina Lombo na Ngoswe licha ya uhasama uliokithiri miongoni mwa wazazi wao. Umoja na ushirikiano mzuri kati ya Mangwasha, Mbungulu, Lonare,  Mashauri, polisi na wengineo unawawezesha kuwakomboa watoto wa kike kutokana na ulafi wa Sihaba (uk. 143). 

Nafasi ya mwanamume katika jamii

Katika riwaya hii, nafasi ya mwanamume imebainishwa na wahusika wa kiume ambao  wamegawika kuwili. Wapo wale wanaotambua wajibu wao kama wazazi na walezi wa jamii kama vile Lonare na Sagura ambao kupitia kwa ushauri wao tunaona jinsi wanavyojaribu  kuielekeza jamii. 

Lonare anawalea wanawe kwa njia bora mbali na kuwasomesha kikamilifu (uk. 50). Sagura anawapa vijana kama vile Sauni ushauri inapohitajika, kuonyesha kwamba alijua namna ya kutangamana na watu vyema. 

Hata hivyo, kuna wanaume waliojaa kiburi kingi na mashauo kama vile Mtemi Lesulia,  Chifu Mshabaha, Mrima na Sagilu. Hawa wameshiba taasubi ya kiume inayoongozwa na mfumo wa ubabedume. 

Isitoshe, hatuoni wakiwapa watoto wao malezi bora. Kwa mfano, tunamwona Ngoswe,  mwanawe Mtemi Lesulia, akikosa malezi bora pale anapokuwa mlevi na kujishughulisha na biashara za dawa za kulevya. 

Aidha, Ngoswe hakufunzwa adabu na wazazi wake kwani tunamwona akimkemea Sagilu  katika hoteli ya Saturn na kumwita mwewe (uk. 133). Aidha, tunamwona Mrima pale mwanzo akishindwa kutekeleza majukumu yake ya ndoa kutokana na ulevi mwingi, na kumwachia Mangwasha jukumu la kuwalea watoto wao. Hii inamaanisha kwamba hata yeye huenda hakupata uongozi bora kutoka kwa wazazi wake. 

Kutokana na uongozi mbaya wa serikali pamoja na sera mbaya za ajira, ubinafsi na ukabila,  haya yanachangia kumlemaza mtoto wa kiume. 

Tunaonyeshwa wavulana na vijana wengi wa kiume wakirandaranda mitaani kutokana na ukosefu wa malezi bora, umaskini wa wazazi wao na ukosefu wa karo. Hakuna wazazi wa kiume wa kuwaongoza na kuwashika mkono ili wawe wanaume wa kutegemewa. Uchochole na harakati za kuyasaka maisha kumewafanya wazazi wengi kutowajibikia watoto wao. 

Kauli ya mhusika Mangwasha inapiga mwangwi hali halisi ya mtoto wa kiume pale anaposema, "Ole wako ewe mwanamume uishiye leo...Yu wapi baba aliyekutelekeza?" (uk.  138). 

Kutokana na athari za ukabila, hata wale vijana waliosoma hadi vyuo vikuu hawana ajira kwani ajira zinagawanywa kibubusa. Wengi waliotaalamika hawaajiriwi. Wanaoajiriwa ni wale wanaojulikana kwa misingi ya ukabila ambao unawanyima vijana wengi wa kiume 

mustakabali mzuri wa maisha. Idadi kubwa ya wanaume pia inaishia ulevini kutokana na ukosefu wa matumaini, kumaanisha kwamba umma wa kiume katika nchi hii umo hatarini na kizazi cha kiume cha kesho hakina matumaini. 

Elimu na ajira

Elimu ni mafunzo yanayotolewa na jamii kwa watu wake, darasani au pasipokuwa darasani.  Kwa upande mwingine, ajira ni kazi ya kulipwa mshahara. 

Katika jumuiya inayozungumziwa, elimu inaonekana kukosa thamani kwa sababu hata baada ya vijana wengi kupata elimu, kazi zinagawanywa kwa kujuana. Isitoshe, kazi zinatolewa bila utaalamu wowote. 

Mwandishi anasema, "Vijana wengi Waketwa waliohitimu shahada za vyuo vikuu  walihangaika mijini kutafuta kazi bila mafanikio." (uk. 44). Elimu basi, inawafaidi watoto wa matajiri Wakule ambao ndio wanaofikiriwa. Hata wale wasio na ujuzi wanaajiriwa kwa misingi iyo hiyo, ndiposa maendeleo nchini yanakwama na maafa mengi kutokea. 

Nafasi ya sheria

sheria ni kanuni zinazotungwa na bunge, halmashauri ya mji, manispaa, jiji au jamii fulani ili kuratibu shughuli za jumuiya pamoja na namna ya kuzisimamia ikiwa ni pamoja na adhabu  pindi kanuni hizo zikikiukwa. 

Nchi ya Matuo ina sheria lakini hizi aghalabu hazifuatwi hasa na wale walio na ushawishi mkubwa serikalini. Tazama jinsi wafuasi wa Mtemi Lesulia wanavyochoma makazi ya watu  Matango bila kuzingatia sheria. 

Tazama jinsi Mtemi Lesulia mwenyewe anavyoamrisha jalada la ardhi ya Matango lifichwe ili wenyeji wa ardhi hiyo wafukuzwe kwa manufaa yake na ya wandani wake. Tazama jinsi kiongozi huyo anavyopanga na wandani wake kuharibu zoezi Zima la uchaguzi ilimradi matakwa ya wandani wake yatimizwe. Anayedaiwa kuwa mwanasheria shupavu wa serikali na anayepaswa kutetea sheria, anazivunja kupitia ushawishi wa serikali dhalimu (uk. 93-95).  Kutokana na ufisadi uliokithiri nchini Matuo, sheria hazifuatwi na wale walio mamlakani ambao wanatumia hongo ili kufisha mfumo wa sheria za nchi. 

Afya ya kiakili

Afya ya kiakili inahusu ustawi wa mtu kisaikolojia na kijamii. Afya ya kiakili inatuathiri jinsi tunavyofikiria, kuhisi na kutenda. Inasaidia pia kuamua jinsi tunavyoshughulikia mafadhaiko,  kuhusiana na wengine na kufanya maamuzi. Afya ya kiakili ni muhimu katika kila hatua ya maisha, kutoka utoto na ujana hadi utu uzima. 

Katika riwaya hii, hatuwaoni wananchi wa kawaida wakikumbwa na msongo wa mawazo  hadi kuwa wagonjwa licha ya kwamba wanapitia madhila mengi. Tunaona hali hii ikiwakumba matajiri kutokana na uroho wao wa kuhodhi mali na ubinafsi. Tunamwona Nanzia akipatwa na msongo wa mawazo, akiweweseka ovyo (uk. 157) na kupatwa na mshtuko wa moyo pale alipoona ngawira alizoiba kwa njia ya udanganyifu 

Zikimponyoka taratibu hasa lile jengo la Skyline Mall (uk. 158). Hivyo, kifo chake kinachangiwa na hali hizo za kiakili kutokana na mali zake kuchukuliwa na serikali. Sagilu  pia anapitia masaibu kama ya Nanzia. 

Mali yake inatwaliwa na kumilikiwa na serikali na hali hii inamsababishia kichaa kama anavyosema Mashauri (uk. 154). Isitoshe, maisha ya ufuska aliyokuwa nayo hadi kumla mwanawe kivuli yanamsababishia kichaa, ikiwemo aibu pamoja na kukataliwa na Mashauri mwanawe. 

Ukahaba

Ukahaba ni tabia ya mwanamke au hata mwanamume kujiingiza katika biashara ya umalaya,  uasherati au ngono. Tunaweza kuiita pia biashara ya 'nipe nikupe' lakini bidhaa inayotumiwa hapa ni ya kimwili. 

Tunamwona Sihaba akifanya usuhuba na Sagilu ilimradi afaidi pesa zake. Pia tunamwona Cheiya akifanya usuhuba na Sagilu ilimradi afaidi pesa na zawadi alizokuwa akipewa kwa kutumia mwili wake (uk.121). 

Ukahaba pia unaendelezwa na Sihaba anayewachukua wasichana wadogo na kuwapeleka kwenye danguro lake liitwalo Red Beads Lodgings ili kufanya ukahaba (uk.140-142).  Tunaonyeshwa pia wazee na vijana wa kiume wanaoendesha magari ya kifahari wakiingia na kutoka kwenye makao hayo ya ufuska. 

Dini

Dini ni imani inayohusiana na kuwapo kwa Mungu au miungu. Wenyeji wa Matango  wanapochomewa nyumba zao na kukimbilia kanisani ili kujisitiri, kunaonyesha kwamba jumuiya inayozungumziwa ina washiriki wa dini ya Kikristo kutokana na kuwepo kwa maabadi hayo. Baadhi ya wahusika pia kama vile Mangwasha ni watu wanaomwamini Mungu kutokana na maombi wanayotoa na kutaja jina la Mungu wanapokuwa kwenye shida.  Aidha, licha ya kwamba mhusika Sauni anadhihirisha hamaki za haraka, anamwamini  Mungu hasa anapomwambia mkuu wa kitengo cha jinai kwamba wao watalindwa na Mungu  (uk.76). 

MANDHARI

Mandhari ni mazingira ya kazi ya kifasihi. Aidha, ni mahali maalumu kama vile mastakimu  au makazi mahususi ambapo mtunzi hujenga matukio fulani ili yaweze kutendeka katika kazi yake. 

Mandhari huweza kuwa mazingira maalumu ambamo wahusika huingiliana na kuendeleza shughuli au matukio fulani ya kazi ya kifasihi. 

Mandhari pia huweza kuhusisha mahali wahusika wahapokaa na kuingiliana ili kujenga maudhui ya kazi hiyo. Mahali hapa huweza kuhusisha, kwa mfano, mazingira ya kiuchumi,  kijamii, kisiasa au kitamaduni hivi kwamba mwingiliano huo wa wahusika ukatuwezesha kufahamu tabia au hulka na matendo yao. 

Katika riwaya ya Nguu za Jadi, mwandishi amejenga mandhari mbalimbali katika kutoa ujumbe wake. Kuna mandhari ya nchi ya Matuo ambapo tunajengewa picha za wananchi wake kama vile viongozi, wafanyabiashara na wananchi wa kawaida wakiwa katika harakati zao mbalimbali. Ndani ya nchi hii, tunachorewa picha za kimaumbile kama vile ardhi, ukataji wa miti, umegaji wa vilima na usombaji wa mchanga, vitu ambavyo vinatokana na ulafi wa viongozi. Haya yote tunaona yakiharibu mazingira na maliasili. Taswira ya mandhari haya ni 

nchi iliyokuwa na utajiri mwingi wa maliasili lakini sera potovu za uongozi zinadumaza maendeleo ya nchi. 

Umuhimu wa mwandishi kutuchorea picha hii ni kuonyesha jinsi uongozi mbaya unavyoweza kuleta hasara kwa nchi. 

Pia kuna mandhari ya mji wa Taria kunakoendelezwa shughuli na kadhia mbalimbali kupitia kwa mwingiliano wa wahusika mbalimbali. Taria ndio mji mkuu wa nchi ya Taria na kitovu  cha serikali. Tunaonyeshwa majengo makubwa ya kibiashara, afisi za serikali, korti, jela,  magari ainati na biashara mbalimbali zinazoendelezwa na wahusika, nyingi zikiwa haramu.  Mji wa Taria unatumiwa na mwandishi kuendeleza sera za uongozi mbaya na jinsi ufisadi unavyochangia kuzorotesha uchumi wa nchi. 

Pia kuna mandhari ya mitaa kama vile Majuu kunakoishi wakwasi na matajiri wa nchi ya Matuo na starehe zinazoendelea katika mtaa huu. Tunaonyeshwa watu wa tabaka la juu  wanaohusisha lile tabaka tawala na jinsi linavyomiliki utajiri wa nchi pamoja na kadhia za ufisadi zinazoendelezwa na wakwasi hawa. 

Mwandishi ametuonyesha pia mandhari ya mtaa wa Matango mnamoishi jamii ya Waketwa na harakati mbalimbali zinazoendelea katika mtaa huu zikiwemo zile za kisiasa.Tunaonyeshwa maonevu wanayofanyiwa wenyeji wa Matango wanaotoka katika matabaka ya chini kijamii na kiuchumi, na mtagusano wa wenyeji hao na vigogo wa kisiasa unaosababisha uadui baina ya Waketwa na Wakule. Umuhimu wa mandhari ya mitaa hii ni kuonyesha tofauti za kitabaka baina ya wananchi pamoja na migogoro inayotokana na tofauti hizi. Yapo pia mandhari ya kortini ambapo kesi ya ardhi ya Matango inafanywa.  Tunaonyeshwa jinsi wanasheria Mafamba na Mwamba wanavyoonyesha ubabe wa malumbano ya kisheria na hatima ya kesi hiyo. Umuhimu wa kesi hii ni kuonyesha jinsi ufisadi ulivyojipenyeza serikalini, mbali na kusawiri ubahili wa viongozi walio mamlakani.  Mandhari ya jela yanasawiriwa ili kuonyesha jinsi taasisi za serikali zinavyofisha haki na kuhujumu sheria.Tunaonyeshwa kuwa wanaoshtakiwa kwa makosa ya jinai wanaachiliwa bila kusomewa mashtaka kutokana na uozo ulioko katika taasisi za umma. 

Mandhari ya afisi ya Chifu Mshabaha yanasawiriwa na mwandishi ili kuonyesha jinsi maafisa serikalini wanavyotumiwa kuhujumu haki za raia na kuendeleza ubinafsi na ufisadi wa viongozi. Afisi hii pia inatumiwa ili kuonyesha juhudi za mhusika Mangwasha za kutokomeza uovu unaoendelezwa na serikali dhalimu. Afisi hii pia inatumiwa na mwandishi kumkuza Mangwasha kama mhusika mkuu katika riwaya hii. 

Mandhari ya mtaa wa Majengo yameonyeshwa na jinsi shughuli za wenyeji wa mtaa huu  zinavyochangia katika kufisha ukiritimba wa kisiasa na kiuchumi miongoni mwa matajiri wa nchi. 

Mwandishi anatupa taswira ya mtaa wa Majengo kama kielelezo cha jinsi jamii mbalimbali zinavyoweza kuishi kwa amani kupitia kwa umoja na ushirikiano wa wenyeji wake.  Mwandishi ametuonyesha pia mandhari ya kiwakati na kutupa taswira za nyakati mbalimbali pamoja na matukio mbalimbali yanayojitokeza. Tunaonyeshwa mandhari ya wakati wa uongozi wa Mtemi Lesulia ambapo nchi iliyokuwa na utajiri wa maliasili inabadilika na kuchukua sura ya kusikitisha. Maliasili inafisidiwa na mafisadi, uchumi unasambaratika,  ukosefu wa ajira kwa vijana unakuwa jambo la kawaida na vitendo viovu vinavyozorotesha 

maadili ya nchi vinashuhudiwa kama vile wizi wa mali ya umma, ukahaba na ulanguzi wa dawa za kulevya. 

Tunaonyeshwa pia kipindi cha harakati za kisiasa baina ya wale wanaotaka kusalia mamlakani na wale wanaopigana kwa jino na ukucha ili kuikomboa nchi ya Matuo na kuirudishia thamani yake. 

Mwisho, kuna kipindi cha ukombozi pale ambapo uchaguzi unafanywa na mabadiliko  yanatokea Lonare anaposhinda na kuwa mtemi wa nchi na ahadi anazotoa za kubadilisha nchi na kuleta maendeleo. 

Wahusika na Uhusika

Wahusika ni muhimu sana katika kukuza dhamira, kujenga na kuendeleza maudhui. 

Kila mwandishi ana mtindo wake wa kuwakuza wahusika wake — tofauti na mwandishi mwingine. Anaweza kuwakuza kutokana na matendo Yao, maelezo ya mwandishi mwenyewe kuwahusu, kuwalinganisha na kuwalinganua na wahusika wengine, uzungumzi wao wenyewe kwa wenyewe, kutokana na majina yao, jinsi wanahusiana na wenzao na kadhalika. 

Pana haja kubwa kuwagawa wahusika wa fasihi katika makundi mbalimbali. Baadhi ya makundi haya tunaweza kuyafafanua ifuatavyo: 

Wahusika wakuu

Hawa ni wahusika ambao hujitokeza mahali kwingi katika fasihi kiasi cha kwamba wanajitokeza kuanzia mwanzo wa kazi ya fasihi hadi mwisho. Kwa kawaida wahusika hawa hubeba maudhui makuu ya fasihi.  

Wahusika wadogo

Hujitokeza kwa uchache sana katika kazi ya fasihi. Hujitokeza katika sehemu fulani fulani japo hawaisawiri kazi nzima ya fasihi husika. Mara nyingi mwandishi huwatumia tu wahusika wadogo kutimiza lengo fulani mahususi. 

Wahusika bapa

Ni wahusika ambao hawabadiliki kwa kigezo cha tabia kutoka mwanzo wa hadithi hadi mwisho. Iwapo ni wabaya, mwandishi huwasawiri kuwa wabaya bila chembe ya wema wowote hadi mwisho na kama ni wema, wema wao hudumishwa hadi mwisho. 

Wahusika nguli

Ni wahusika ambao hutetea matakwa ya watu au wahusika wengine katika jamii. Mwandishi huwatumia kuwa watetezi wa haki za wale wanaodhulumiwa, kuteswa au kunyanyaswa. 

Wahusika mviringo au mduara

Ni wahusika ambao tabia zao hubadilikabadilika. Wanaweza kuanza hadithi wakiwa wabaya lakini mwishowe wakageuka kuwa wazuri, au waanze wakiwa wema halafu mwishowe wageuke kuwa waovu. 

Wahusika wajenzi

Ni wahusika ambao mwandishi huwatumia kuwajenga wahusika wengine. Wanaweza kuwa wahusika wadogo, bapa au mduara, lakini malengo yao huwa kuwaendeleza wenzao katika maudhui na tabia. Hawa husaidia kuelewa sifa na tabia za wahusika wengine. 

Wahusika mkengeuko

Ni wahusika wanaokwenda kinyume na matakwa ya wanajamii. Wanaweza kuwa katili,  wauaji, wanyanyasaji, wanafiki, fisadi na kadhalika. 

1. Mangwasha

Huyu ndiye mhusika mkuu katika riwaya. Ni mkewe Mrima na mhazili wa Chifu Mshabaha.  Sifa za Mangwasha 

Mvumilivu

Mangwasha anavumilia matatizo mengi ndani ya ndoa yake yanayotokana na ulevi wa mumewe. Hata baada ya kukimbiwa na Mrima, anavumilia mateso mengi ya ukosefu wa pesa za kuwatunza wanawe, kukiwemo pia kejeli za Sagilu. Anavumilia vishawishivya Sagilu anayemwonyesha pesa nyingi ili akubali kuwa mpenzi wake. Anavumilia dharau na matusi ya Chifu Mshabaha anapokuwa kazini: Anavumilia kazi nyingi anazompa ili aweze kuwatunza wanawe. 

Mzalendo

Mangwasha anaonyesha uzalendo pale anapotamani kukutana na viongozi wa Matuo ili amani iweze kudumishwa nchini. Anajali sana mustakabali wa nchi ya Matuo hasa pale anapowaona watoto na vijana wakiteseka bila matunzo mema ya wazazi wao au hata ajira.  Uzalendo wake unaonekana pale anapoungana na wanawake wengine kufanya kampeni ili Lonare achukue hatamu za uongozi na kubadilisha hali ya uchumi wa nchi. Kushirikiana na Lonare katika juhudi zake za kutaka kuwa mtemi wa nchi ni ishara ya uzalendo kwani alitaka maendeleo katika nchi yake iliyokuwa ikididimizwa na viongozi mafisadi. Mangwasha anapomkabili Chifu Mshabaha na kumwambia kuwa serikali ni ya kila mtu bali si ya mtu binafsi, anadhihirisha uzalendo wake (uk.136). 

Mwenye matumaini

Haonekani kufa moyo bali anaonyesha matumaini pale Chifu Mshabaha anapomdharau na kumdhalilisha akiwa kazini. Anaonyesha matumaini pale anapohangaika kutunza wanawe dhidi ya mateso aliyokuwa akipitia alipokimbiwa na Mrima. Anapochomewa nyumba yake pamoja na wenyeji wa Matango havunjiki moyo bali anakuwa na tumaini. 

Jasiri

Mangwasha anaonyesha ujasiri pale anapojitahidi kwa jino na ukucha kuiokoa ndoa yake kutoka kwa Sagilu aliyekuwa akiisambaratisha. 

Kule kumsaka mumewe kwenye mabanda ya uuzaji wa pombe mbali na kukabiliana na walevi ni ishara ya ujasiri (uk. 34-36). 

Ujasiri wa kuiokoa ndoa yake unaonekana pia pale anapoandamana na Lonare, Sauni na wengine kumsaka mumewe Majaani, pahali palipojulikana kuwa hatari kwa sababu paliishi watu waliotindikiwa kimaadili. 

Mangwasha anaonyesha ujasiri pale anapochukua barua ya Chifu Mshabaha na kwenda kuirudufu kinyume na idhini yake ilimradi apate ushahidi wa kuweza kushinda kesi yao ya ardhi. 

Tofauti na waajiriwa wengine wanapofutwa kazi, Mangwasha anamkabili Chifu Mshabaha kwa ujasiri na kumwita mkabila mkubwa (uk. 136). 

Ujasiri wa Mangwasha pia unaonekana aliposimama mbele ya kaumu na kuwahamasisha Waketwa wenzake kurudi katika ardhi yao ya Matango. Hakujali mila wala vitisho vya waliowapokonya ardhi yao bali aliwahamasisha warudi katika ardhi yao ambayo ilikuwa haki yao. 

Lonare anapopatikana nje ya nyumba yao baada ya kutekwa nyara, tunamwona Mangwasha akimkimbilia licha ya kwamba kulikuwa na umati mkubwa na hakuna aliyejaribu  kumsogelea kutokana na hofu iliyowapata (uk. 170). Anaungana na wanaume kama Lonare,  Sagura na Sauni ili kuikomboa nchi yao kutoka kwa utawala dhalimu, bila kujali mikatale ya utamaduni wake. 

Aliyejikomboa kimawazo

Mangwasha amejikomboa kimawazo dhidi ya utamaduni unaomdunisha na kumdhalilisha mwanamke. Anapinga kauli za Mbungulu kwamba azingatie yale aliyofunzwa na kungwi na kwamba asithubutu kumfuata mumewe katika starehe zake. Anaona hizi ni mila zilizopitwa na wakati. Mangwasha anasaili kauli ya mumewe kwamba Shingo haipiti kichwa pale anapomwambia pia kwamba hata hicho kichwa kisipotulia huchosha Shingo (uk. 40). 

Mchapa kazi

Mangwasha ni mchapa kazi kutokana na bidii yake kazini. Alifanya kazi zote alizopewa na chifu bila manung'uniko na kufanya hata zile zilizopaswa kufanywa na topasi. Tunaambiwa alikuwa wa kwanza kufika kazini lakini wa mwisho kuondoka (uk. 14). 

Mtiifu

Ni mtiifu kazini na anawatumikia watu wote kwa moyo mkunjufu hadi sifa zake zinavuma kote mjini Taria. Utiifu na umahiri wake vinamfanya kupandishwa cheo hadi kufikia gredi ya juu kabisa katika taaluma ya uhazili (uk. 14). Anafanya kazi zake kwa moyo wa kujituma  (uk. 47) na hakuna mtu anayenung'unika kuhusu kazi yake. 

Mtetezi wa haki

Anatetea haki za Waketwa kutokana na kuchomewa nyumba zao na kunyang'anywa ardhi yao. Anatetea haki za watoto pale anaposhirikiana na Mbungulu, Mashauri na wengine kuwaokoa watoto wa kike waliokuwa wakichuuzwa na Sihaba ili kujinufaisha. Alianzisha shirika la kutetea haki za vijana hasa kwa wale wasiokuwa na ajira. 

Mwenye upendo

Anampenda mumewe licha ya kwamba awali huyu alimtupa na watoto. Anaipenda jamaa na jamii yake kutokana na juhudi zake katika kuitunza jamaa yake na kushughulikia maslahi ya Waketwa wenzake. Anaonyesha upendo kwa watoto na vijana wa mitaani pale anapozungumza nao na kuwapa ushauri. 

Umuhimu wa Mangwasha

a) Ni kielelezo cha upiganiaji wa haki kwa wanaoteswa na mifumo dhalimu ya kiutawala.  b) Ni kielelezo cha utokomezaji wa ukabila katika jamii. 

c) Ametumiwa kuonyesha kwamba desturi na mila potovu katika jamii hazina nafasi katika jamii ya leo na kwamba zinapaswa kutokomezwa. 

d) Ametumiwa kupiga vita ufisadi na maovu mengine yanayofanywa na viongozi.  e) Ametumiwa kuonyesha kwamba mwanamke anahitaji kushirikishwa katika sekta zote za umma licha ya kwamba ni mwanamke, na anahitaji kuheshimiwa. 

f) Ametumiwa kutoa tahadhari kwa jamii kumjali mtoto wa kiume kwani hashughulikiwi ipasavyo. 

Lonare

Lonare ni kiongozi wa jamii ya Waketwa na mpinzani wa Mtemi Lesulia.  Sifa za Lonare

Mtetezi wa haki kwa wote

Lonare anapigania haki za wananchi wote wa Matuo. Habagui watu kwa misingi ya ukabila au jinsia yao bali anasimamia haki na usawa wa wananchi wote. Anamhamasisha Mangwasha kupigania haki za vijana bila ubaguzi na anasomesha watoto wake wote bila ubaguzi wa kijinsia. Anapigania haki kwa Waketwa wanaochomewa makazi yao na kufurushwa kutoka Matango hasa pale anapoungana na Mangwasha kupeleka kesi mahakamani. Anaukemea ukabila kwa sababu anaamini kwamba watu wote wanahitaji kutendewa haki bila kuzingatia misingi ya kikabila. 

Mvumilivu

Lonare anavumilia vitisho juu ya maisha yake vinavyoendelezwa na Mtemi Lesulia ikibainika kwamba anatishiwa uhai wake zaidi ya mara moja. Anavumilia biashara yake ya usafiri wa magari ya umma inapoathiriwa na vitendo dhalimu vya wafuasi wa mtemi hasa pale magari yake yanapokamatwa kwa makosa madogomadogo na madereva wake kupigwa faini (uk. 50). Anavumilia shutuma kutoka kwa wafuasi wake hasa pale anapotoweka ghafla bila kujua yaliyomfika, ilimradi afikie lengo lake la kuwakomboa wananchi wa Matuo. 

Mkombozi/mwanamapinduzi

Anaingia katika kampeni za kisiasa bila kujali vitisho vya mtemi ili kuikomboa nchi yake,  azma anayotimiza na kuwa mtemi wa Matuo. 

Akishirikiana na Mangwasha na wengine, anamkomboa Mrima kutoka katika maisha ya anasa na ulevi na kurudia familia yake. 

Aidha, anashirikiana na Sauni, Mangwasha na wengine kutibua njama za Sagilu kutaka kumhonga Mrima ili ampigie debe Mtemi Lesulia katika uchaguzi mkuu. Anakuwa 

mkombozi pale anapomtumia mwanasheria Mwamba, akashirikiana na Waketwa wenzake kuikomboa ardhi ya Matango na wenyeji wakarudishiwa makazi yao (uk. 94-96). Kupitia kwa ushauri wake, anamkomboa Ngoswe aliyekuwa amebobea katika maisha ya ulevi na dawa za kulevya. 

Jasiri

Kuwania kiti cha mtemi wa Matuo .licha ya vitisho na masumbufu aliyopitia, ni ishara ya ujasiri. Kupitia kwa ujasiri wake, anahiari kupitia mateso ya kutekwa nyara na kuumizwa lakini hakuvunjika moyo hadi anaposhinda uchaguzi na kuwa mtemi wa Matuo. Magari yake ya usafiri yanapokamatwa kwa visingizio visivyokuwa na maana hadi madereva wake kutozwa faini zisizoeleweka, hakuvunjika moyo bali aliendelea na biashara hiyo. 

Mzalendo

Lonare anaipenda nchi yake kiasi cha kuhatarisha maisha yake ili aikomboe kutoka katika utawala dhalimu wa Mtemi Lesulia. Anawathamini raia Wote wa Matuo bila ubaguzi wa kikabila kwani tunaambiwa aliweza hata kuajiri watu kutoka katika jamii ya Wakule. Hotuba anayotoa baada ya ushindi wake ni kielelezo cha uzalendo; anawataja raia wote wa Matuo  kuwa ndugu zake na kuwahimiza kuungana 'ili kujenga nchi yao. Kauli Zinazoashiria uzalendo wake ni kama pale anaposema kwamba ukabila ni sumu ya nyoka na kwamba huweza kuangamiza maendeleo ya nchi 

Mshauri

Ushauri wa Lonare unaonekana pale anapomshauri Mangwasha awe na subira katika kutatua matatizo yaliyowakabili. Tunamwona pia akimshauri Mrima kwa kutumia mafumbo ili aweze kubaini maana ya ndani. Kwa mfano, anamwambia kwamba ajifunze kutokana na makosa yake mwenyewe (uk. 101), na kwamba kamwe hawezi kusalimiana na mtu aliyekunja ngumi (uk. 114). Pia anamshauri Ngoswe kuacha kufanya biashara haramu na kufunga majumba ya ufasiki anayomiliki kama anaipenda nchi yake (uk. 171). 

Mwenye msimamo thabiti

Lonare anaonyesha msimamo thabiti pale anapokamia kupigania kiti cha mtemi wa Matuo,  liwe liwalo. Hata baada ya kupitia mateso na mitego mingi, habadilishi msimamo wake.  Isitoshe, habadilishi biashara ya usafiri wa magari licha ya masumbufu anayopitia. 

Umuhimu wa Lonare

1. Anawakilisha viongozi wanaozingatia demokrasia na haki za wananchi.  2. Kupitia kwake, wananchi wanakuwa na imani ya uongozi mzuri na matumaini katika maisha yao. 

3. Ni kielelezo cha watu wasiokata tamaa maishani. 

4. Ametumiwa kuonyesha jinsi ushirikiano miongoni mwa wananchi unavyoweza kubatilisha uongozi dhalimu. 

5. Ametumiwa kama chombo cha kuleta mabadiliko katika utawala usioridhisha.  Mtemi Lesulia

Huyu ni kiongozi wa nchi ya Matuo na mumewe Nanzia. Anajitokeza pia kama rafiki shadidi wa Sagilu. 

Sifa za Mtemi Lesulia 

Mwenye tamaa na ubinafsi

Tamaa yake inagawika kuwili; tamaa ya uongozi na tamaa ya mali na utajiri. 

Ni kielelezo cha uongozi mbaya kutokana na jinsi anavyojilimbikizia mali bila kujali raia wake. Ana tamaa ya kusalia mamlakani; tunamwona anafanya juhudi zote hata kujaribu kuua mpinzani wake ili asalie mamlakani. Tamaa yake inafanya uchumi wa nchi kuzorota  kutokana na sera mbaya za uongozi; akiwa na wenzake, anahujumu pato la nchi kutokana na ubinafsi wake. Tamaa ya mali inamfanya kujaribu kuwapoka wenyeji wa Matango ardhi yao. 

Fisadi

Ufisadi unamfanya Mtemi Lesulia kuajiri watu wasiokuwa na ujuzi au utaalamu katika sekta za umma huku akiacha wale wenye ujuzi (uk. 44). serikali yake inaajiri watu kwa kujuana huku ajira zikitolewa kibubusa. 

Akishirikiana na wenziwe, anazorotesha uchumi wa nchi kutokana na kutolipa ushuru au kuingiza bidhaa nchini kimagendo. 

Ufisadi katika serikali yake unafanya mashirika na taasisi za serikali kumilikiwa na mitandao  ya wezi huku akisaidia katika kuipoka nchi hadhi yake. Katika serikali yake "Ufisadi ulikithiri na maadili yakawapa mkono wa buriani" (uk. 45). Ufisadi wake pia unajitokeza  pale anapowahonga vijana kwenda kumuua Lonare lakini njama hiyo inatibuka. 

Anatumia ufisadi kuwahonga watu ili kuwachomea wenyeji wa Matango makao yao kwa lengo la kuwafanya wasimpigie mshindani wake kura wakati wa uchaguzi. 

Anatumia njia za kifisadi kuhakikisha kwamba jalada la ardhi ya Matango limefichwa ili kuficha umiliki wa sehemu hiyo. Pia anawahonga vijana wavuruge amani ili kuharibu kura za mpinzani wa Sagilu wakati wa uchaguzi wa mchujo (uk. 129). 

Mdanganyifu

Kupitia kwa uongozi wake, tunaona akidanganya kuwa ardhi ya Matango ingetumiwa kujenga soko ili awafaidi mke wake pamoja na Mbwashu. Baada ya kushindwa katika uchaguzi mkuu, Lesulia anawadanganya watu Waliomtembelea kuwa alikuwa amechoka kuwa mtemi. Anaposema pia kwamba hakutaka kushinda na kwamba• alichoka kuwatumikia anasema uongo (uk. 177). 

Katili

Mtemi Lesulia anadhihirisha ukatili pale ambapo anaungana na wengine kumpangia Lonare njama ya kuharibu biashara yake. Anapompangia njama ya kumuua au hata kufanya atekwe nyara wakati uchaguzi mkuu unapokaribia ni ishara ya ukatili wake, Hakujali pale watoto na

vijana nchini mwake walivyokuwa wakiteseka kutokana na mifumo mibaya ya uongozi wake. Anahiari wenyeji wa Matango wachomewe nyumba na kuteseka pamoja na jamaa zao  ilimradi atimize azma yake ya kunyakua ardhi yao. Anahiari kujaribu kumfukuza mkewe Nanzia kwa sababu hakuweza kuzaa alipomwoa. Baada ya kushindwa kesi ya ardhi ya Matango, anamnyang'anya hakimu aliyekata kesi cheti chake cha kazi na kumsimamisha 

kazi. Aidha, anamnyang'anya mwanasheria Mafamba cheti cha uanasheria na kumtokomeza kutoka Taria asijulikane aliko. 

Anawafukuza marafiki wanaofika nyumbani kwake kumpa pole baada ya kushindwa uchaguzi (uk. 177). 

Mnafiki

Kupitia kwa hila zake, anajaribu kuchukua ardhi ya Matango kuwafaidi mkewe Nanzia pamoja na Mbwashu huku akisema serikali ilitaka kujenga soko. Anajifanya kutojua yaliyomfika Lonare kabla ya uchaguzi mkuu ilhali njama za utekaji nyara wake zilitokana na maelekezo yake. 

Mwenye dharau

Anawaita wenyeji wa Matango panya baada ya kuchomewa nyumba zao na kurejea tena katika makao yao (uk.78). Anaonyesha dharau kwa mwanawe mbele ya rafiki zake anaposema, "Toto hili! Hata sijui lilitoka wapi." (uk.129). 

Mwenye ukabila

Utawala wake unatawaliwa na ukabila mwingi. Anawanyanyasa Waketwa na kuwathamini Wakule ambao ni jamii yake. Hili linabainika anapokosa kuwaajiri vijana Waketwa waliohitimu. Hawa wanaajiriwa kufanya kazi za kijungujiko kama vile wafanyakazi katika mashamba ya matajiri. 

Anamchukia Lonare kwa sababu huyu alikuwa Mketwa na akafanya kila juhudi ili kumzuia asiweze kuwa mtemi wa Matuo. Ukabila unamfanya kuhujumu biashara yake hata kumpangia mauti. Serikali yake inawaajiri watu kulingana na majina yao; aliye na jina la Kiketwa hakuweza kuajiriwa. Matajiri na wale walio katika ngazi za juu serikalini wanatoka katika jamii ya Wakule pekee na ndio walioweza kuishi katika mtaa wa kifahari kama vile Majuu. 

Msaliti

Anaisaliti nchi na watu wake kutokana na uongozi mbaya usiojali maslahi ya wanyonge.  Anaisaliti jamii ya Waketwa kwa kuwatenga katika ajira licha ya kwamba wao pia wanastahili kuwajibikiwa kama Wakule. Anamsaliti mwanasheria Mafamba aliyefanya kila juhudi za kumfichia maovu ya serikali yake kwa kumnyang'anya cheti cha uanasheria na kumtimua kutoka katika mji wa Taria. Kitendo cha kumnyang'anya hakimu cheti chake cha uanasheria na kumfuta kazi ni usaliti kwani hakimu alikuwa akitekeleza majukumu ya utetezi wa haki nchini mwake. 

Anausaliti uaminifu wa mwanawe Ngoswe kwa kuwataka vijana wenzake kufanya fujo  wakati wa uteuzi wa wagombea viti, bila kujali usalama wao. Anaisaliti imani ya marafiki zake kwa kuwafukuza walipofika kwake kumpa pole baada ya kushindwa katika uchaguzi mkuu. 

Umuhimu wa Mtemi Lesulia

1) Ametumiwa kama kielelezo cha utawala dhalimu usiojali maslahi ya wanyonge na wanaodhulumiwa. 

2) Ametumiwa kuonyesha jinsi ukabila unavyoweza kutinga maendeleo ya nchi.  3) Ametumiwa kuonyesha jinsi viongozi wenye ubinafsi wanavyoweza kuharibu uchumi wa nchi kupitia kwa sera na mienendo potovu. 

4) Ametumiwa kuonyesha jinsi kiburi na dharau hufanya mtu kujuta mwishowe.  Sagilu

Sagilu ni rafiki mkubwa wa Mtemi Lesulia na mzazi wa Mashauri. 

Sifa za Sagilu 

Mwenye ukabila

Anaonyesha ukabila pale ambapo anahiari kushirikiana na wengine kuwachomea wenyeji wa Matango nyumba zao akijua kwamba jamii ya Waketwa iliyokuwa na idadi kubwa iliishi humo. 

Ukabila unamfanya kushirikiana na Mtemi Lesulia ili Lonare ambaye ni Mketwa asichukue kiti cha mtemi wa Matuo. Kauli za Sagilu pia zinaonyesha ana ukabila hasa anaposema,  "Ndege mliolelewa kizimbani nyie hamwezi kuruka" akimaanisha Waketwa (uk. 176). 

Fisadi

Sagilu anajiingiza katika vitendo vya ufisadi hasa kutokana na urafiki wake wa karibu na Mtemi Lesulia. Tunamwona akishirikiana na mwanawe Mashauri kufisidi nchi kwa kuuza vipusa na meno ya ndovu (uk. 127). Anatowesha bidhaa na kuziuza kwa faida.' "...alizuia

meli nzima baharini isitie nanga bandarini na kupakua ngano hadi alipofaulu kuuza kwa bei ya juu ngano yote nchini." (uk. 17). Anaagiza ngano hiyo kimagendo pamoja na bidhaa nyingi ambazo hakulipia ushuru. Malori yake yanaposhikwa na polisi yakisafirisha bidhaa ghushi, anatoa mlungula. Malori yanaachiliwa kusambaza bidhaa zinazohatarisha maisha ya watu. Pia anaagiza maziwa ya watoto yenye sumu na kuhatarisha maisha ya watoto nchini kote (uk. 17). Anaimarisha mtandao wa mafisadi ambao hata polisi hawakuweza kuuangamiza. Wale wanaothubutu kufanya hivyo, wanatishwa kufutwa kazi. 

Kitendo cha kumhonga Mangwasha pesa ili afaidi penzi lake pia kinaashiria ufisadi wake.  Anajihusisha na ufisadi anapoungana na Mtemi Lesulia, Nanzia na Mbwashu  kuwanyang'anya wenyeji wa Matango ardhi yao. Anamtumia Sihaba kusambaza vijikaratasi kuwataka wenyeji wa Matango wahame kutoka katika ardhi yao hata kufanya mpango wa kuwachomea nyumba ili Lonare asipate kura mahali hapo. 

Anaposhirikiana na mtemi kuwahonga rafiki za Ngoswe ili kwenda kuzua fujo na kuharibu  zoezi la upigaji kura ni ufisadi (uk. 128). Anashiriki ufisadi pale anapokubali kuhakikisha kuwa jalada la ardhi ya Matango halipatikani kupitia ushauri wa mtemi (uk. 78).  Anashirikiana na mtemi kuhakikisha kwamba cheti cha ardhi ya Matango kimetolewa kabla ya uchaguzi huku yeye pamoja na Sihaba wakipokea mlungula kwa shughuli hiyo (uk. 91).  Sagilu anamhonga Mrima pesa ili amfanyie kampeni Mtemi Lesulia kinyume na matakwa ya Waketwa wenzake. Lonare anamwambia, "Chukua mzigo wako huu wa dhambi..." baada ya kumkabili Sagilu (uk. 116). Kule kumhonga Mrima pia aiharibu ndoa yake ni kitendo cha ufisadi. 

Mwenye tamaa na ubinafsi

Sagilu anabainisha tamaa ya pesa na mali. Anahodhi bidhaa kama vile ngano na kuiuza kwa bei ya juu ili apate faida zaidi. Tamaa ya pesa inamfanya kuhatarisha maisha ya watoto  nchini kwa kuagiza maziwa yenye sumu. Tamaa ya pesa inamfanya kupokea hongo kutoka kwa Mtemi Lesulia ili huyu awawezeshe Nanzia na Mbwashu kumiliki ardhi ya Matango.  Tamaa ya pesa na mali inamfanya kuingiza bidhaa nchini bila kulipia ushuru hata kufisidi maliasili za nchi kama vile vipusa na meno ya ndovu. Tamaa ya mali na utajiri inamfanya kuwatowesha wale anaoshindana nao kibiashara hata kutumia ujanja na hila kuwapiku  kibiashara. 

Tamaa ya uongozi inamfanya kumshawishi Mrima kwa kutumia pesa ili aweze kumpigia debe Mtemi Lesulia huku akijua kwamba huyu akishinda, naye pia atafaidika. Tamaa ya uongozi pia inamfanya kumsaidia Mtemi Lesulia na wengine kuwachomea wenyeji wa Matango makao yao ili wahame naye afaidi kisiasa. Tamaa hii inamwingiza katika urafiki wa karibu na mtemi ili aweze kufaidika kisiasa na kiuchumi. Kutokana na tamaa na ubinafsi,  anahiari kuwa kikaragosi cha mtemi kwa maslahi yake. 

Sagilu pia ni mwingi wa tamaa za kimwili. Aliweka 'masuria Watoshao kijiji kizima' (uk.  18). Tunaambiwa, 'Alibadilisha magari sawa na alivyobadilisha wanawake' (uk. 18).  Tunamwona akimtumia kimada wake Sihaba kutosheleza tamaa za kimwili mbali na za kibiashara. Anafanya hivyo kwa kumpa pesa kwani 'pesa kwake zilikuwa kigezo cha penzi'  (uk. 16). 

Tamaa inamsukuma kumtaka Mangwasha tangu akiwa msichana hata baada ya kuolewa,  Aliamua kumtumia Mrima kwa kumhonga pesa, kumwingiza katika anasa za ulevi au hata kumpa uhamisho kikazi kwa kutumia mamlaka yake ili apate nafasi ya kumpata Mangwasha.  Kutokana na tamaa yake, anawanyang'anya wanaume wengine wake zao hadi kuitwa mnyakuzi au dudumizi. Tamaa ya kimwili inamfanya kumtongoza mchumba wa mwanawe Mashauri na kuuvunja uchumba wao. Tamaa hii pia inamfanya kumwendea kinyume Mtemi Lesulia kwa kuzaa na mkewe Nanzia. 

Katili

Ukatili wa Sagilu unamfanya kudhulumu na hata kuua washindani wake kibiashara.  Tunamwona akimtumia Sihaba kuwatowesha mahasimu wake kibiashara (uk. 16). Bila kujali maisha ya watoto wa Matuo, anaagiza maziwa ya sumu na kuwafanya wengi kuwa wagonjwa. Akishirikiana na mtemi, anampangia Lonare njama ili kuharibu biashara yake na kumfanya awe muflisi. Anapovunja ndoa za wengine kwa kuwachukua wake zao ni ukatili wa kijamii. Ukatili wake pia unaonekana pale anapomtesa Mangwasha baada ya kumkataa.  Anamtesa kwa kumteka Mrima akili na kusababisha mateso kwake na kwa wanawe.  Anapomwingiza Mrima katika anasa na ulevi pia anamtesa Mangwasha kimwili na kiakili kutokana na madhila anayopitia. Akiwa na wengine, anapanga njama za kuwachomea wenyeji wa Matuo nyumba zao na kuwasababishia mateso. 

Mwenye ukabila

Akiwa na Mtemi Lesulia, walimiliki viwanda kadha ambapo waliwaajiri Wakule pekee (uk.  17). Anafanya kila njia Lonare na Mwamba wasiweze kushinda katika uchaguzi wa kisiasa kutokana na hisia za kikabila. Hii ni kwa sababu wao si Wakule kama yeye. Anamdhihaki Mangwasha kwa kumwambia, "Nyie Waketwa ni watu wa ajabu sana. Mwanzo Mwamba ni nani kwangu? Yule ni sawa na kidagaa tu." (uk. 103). Tunaona akionyesha hisia za kikabila 

baada ya wao kushindwa katika uchaguzi mkuu pale anapowaza juu ya Mangwasha na kusema, "Ndege mliolelewa kizimbani nyie hamwezi kuruka. Mtawezaje kuruka ilhali mnaishi mkifikiria kwamba kuruka ni ugonjwa?" (uk. 176). Waketwa hapa wanalinganishwa na ndege walio kizimbani kwani wakati wa Mtemi Lesulia, hawakuwa na madaraka yoyote kwa hivyo wakasalia kuwa kama wafungwa tus 

Mwenye wivu

Sagilu hataki wengine wampiku katika biashara kwani anataka kila biashara anayofanya pasiwe na wa kushindana naye. Wale wanaomshinda, anatumia hila na werevu hadi kuwashinda kibiashara (uk. 16). Wivu unamfanya kumkabili Mrima alipokuwa akimposa Mangwasha kwani hata yeye alimtaka. Anapomwambia, "Kijana, fahamu kwamba nahodha haogopi mawimbi." (uk. 19) ni ishara ya husuda aliyo nayo, Anamkabili Mangwasha huku  akimtazama kwa jicho la husuda pale anapofahamikiwa kwamba huenda akashindwa na Mwamba katika uchaguzi (uk. 103). 

Mwenye dharau

Anamdharau Mrima kutokana na hali yake ya kijamii na kujifananisha na papa asiyeweza kushindana naye. Anamdharau Mangwasha kutokana na hali yake ya uchochole baada ya kuachwa na mumewe (uk. 60). 

Anamdharau mpinzani wake Mwamba huku akimfananisha na kidagaa (uk. 103).  Anawafananisha Waketwa na ndege walio kizimbani wasioweza kuruka (uk. 176). 

Mnafiki

Anamtumia Sihaba kwenda kuwapa zawadi Mrima na Mangwasha siku ya arusi yao huku  akijua kwamba ile ilikuwa silaha ya kuwaangamiza. Anamwendea kinyume Mtemi Lesulia na kuzaa na mkewe huku akijifanya ni mwandani wake. Anajifanya kumjali Mangwasha anapopata shida baada ya Mrima kutorokea ulevini ilhali akijua kwamba yeye ndiye chanzo  cha matatizo yake. Anajaribu kumwonyesha Mashauri kuwa hakuna kitu kilichokuwa kikiendelea baina yake na Cheiya ilhali alikuwa akifanya usuhuba na mchumba wake.  Anamwambia Mtemi Lesulia atulie kwani kila kitu kiko shwari huku akijua kwamba kupatikana kwa Lonare kungemhakikishia ushindi dhidi yake (uk. 174). 

Msaliti

Anawasaliti wenyeji wa Matango kwa kushiriki katika kuwachomea makazi yao huku akijua kwamba alitaka kuwa mgombea kiti wa eneo hili kupitia kwa chama cha mtemi. Anamsaliti Mrima huku akijifanya ni rafiki yake pale anapompa pesa za kumlewesha na kujitenga na familia yake. 

Anamsaliti Mangwasha kwa kujionyesha kuwa anamjali huku akimwingiza Mrima katika maisha ya anasa ili aivunje familia yake. 

Anamsaliti Mashauri kwa kumchukua mchumba wake bila kujali kuwa yeye ni mzazi wake.  Anamsaliti Mtemi Lesulia kwa kuzaa na mkewe Nanzia huku akijifanya kuwa rafiki yake wa dhati. 

Anaisaliti jamii nzima ya Matuo kwa kuwauzia maziwa ya watoto yenye sumu bila kujali ingewadhuru watoto hao, mbali na kuwauzia bidhaa ghushi bila kujali afya yao. 

Mpenda anasa

Anajivinjari na wanawake kama vile Sihaba bila kujali kuwa ana mke. 

Anawabadilisha jinsi anavyobadilisha magari yake. Anastarehe na wake za watu bila kujali waume zao. Anamchukua msichana Cheiya ambaye si kufu yake na kwenda kustarehe naye bila kujali kuwa alikuwa mchumba wa mwanawe. 

Kigeugeu

Ana tabia ya kubadilikabadilika kama kinyonga. Hawezi kuaminika kwani tunaambiwa wakati mmoja alionyesha mwingi wa furaha, na wakati mwingine akajawa na kiburi na dharau (uk. 16). Anapomkabili Mangwasha, anaonekana mwenye furaha lakini furaha hiyo  inatoweka ghafla anapomwambia ukweli wa mambo kumhusu mumewe. 

Umuhimu wa Sagilu

1) Ametumiwa kama kielelezo cha uozo uiiosakini katika jamii. 

2) Ametumiwa kuonyesha jinsi ukabila unavyodumaza maendeleo. 

3) Kupitia kwake, tunafahamishwa jinsi ufisadi unavyoendelezwa na wale walio karibu  na serikali au hata ndani ya serikali. 

4) Ametumiwa kuonyesha jinsi utajiri na mali vinavyoweza kuumbua binadamu.  5) Ametumiwa kuonyesha namna ambavyo ubabedume unatumiwa kuwadhalilisha na kuwadunisha wanawake. 

Chifu Mshabaha

Chifu Mshabaha ni mwajiriwa katika serikali ya Mtemi Lesulia. 

Sifa za Chifu Mshabaha 

Mwenye ukabila

Madhila anayopitia Mangwasha kazini chini ya uongozi wake yanatokana na ukabila. Chifu  anatoka katika jamii ya Wakule ilhali Mangwasha ni Mketwa. Chifu anamwambia Mangwasha kuwa, "Waketwa ni watu wasio na akili hata ya kuchagua wachumba...mnabaki nyuma kama makoti." (uk. 20) kuonyesha chuki yake kwa jamii ya Waketwa. Afisi yake inakuwa pahali pa kupanga njama za kuwachomea wenyeji wa Matango nyumba zao pamoja na kuwahonga watu kama Mrima waweze kumfanyia Mtemi Lesulia kampeni. Anapomfuta Mangwasha kazi anaonyesha ukabila kwa sababu msichana anayeajiriwa na Chifu Mshabaha ni Mkule kama yeye (uk. 136). Katika afisi yake, ameajiri wafanyakazi wengi kutoka katika jamii yake. 

Fisadi

Anapokea hongo baada ya kujishughulisha katika harakati za kuwapokonya wenyeji wa Matango ardhi yao ili wakabidhiwe Nanzia na Mbwashu. Anamkabidhi Mrima pesa alizopokea kutoka kwa Sagilu kama hongo ili kumshawishi amfanyie mtemi kampeni ilhali akijua yeye alikuwa mfuasi wa Lonare (uk. 105). Anapomchukua msichana kutoka katika jamii yake ili kufanya kazi katika afisi yake badala ya Mangwasha ni kielelezo cha ufisadi.  Hakukuwa na makosa yoyote ya kumfuta Mangwasha kazi ila alitaka kumwondoa pale ili asiweze kubaini maovu aliyokuwa akifanya kwa niaba ya serikali ya Mtemi Lesulia. 

Katili

Ukatili wake unaonekana pale anaposhirikiana na Sagilu, Sihaba na wengineo kuwapoka watu wa Matango ardhi yao. Anamtendea Mangwasha uovu pale anapomfukuza kazi na kumleta msichana kumfanyia kazi badala yake. Anamfedhehesha Mangwasha na kumwonyesha dharau licha ya kwamba huyu anamfanyia kazi kwa utiifu na heshima. 

Msaliti

Anaisaliti jamii ya Waketwa na wote waishio Matango kwa kushiriki katika njama ya kuwaondoa kutoka katika makao yao; tunaona mipango ya kuwaondoa ikitekelezwa ndani ya afisi yake. Anamsaliti Mangwasha kwa vile alipokea bahasha ya pesa kutoka kwa Sagilu na kumpelekea 

Mrima kama hongo ili amfanyie Mtemi Lesulia kampeni kinyume na matakwa ya Waketwa wenzake. Pia kule kumleta msichana mwingine kinyemela ili amfanyie kazi badala ya Mangwasha ni ishara ya kumsaliti Mangwasha aliyekuwa mhazili wake wa muda mrefu. 

Mwenye dharau

Anamwonyesha Mangwasha dharau akiwa kazini kwa kutumia lugha isiyo na heshima. Kwa mfano, anamwambia Mangwasha Waketwa hawana akili hata ya kuchagua wachumba (uk.  20). Anaonyesha dharau pia pale anapomwambia Mangwasha hawana pesa hata za kuwapeleka katika fungate yao baada ya arusi, au kumdhihaki kwa kusema, "Hata kama hamtaenda kokote, mtakaa nyumbani mkipanga kuwa na jeshi la watoto..." (uk. 23). Baada ya kuwatembelea watu waliochomewa nyumba zao pale kanisani walipojisitiri, alitamka maneno ya dharau yaliyowasha moto wa ghadhabu (uk. 70). 

Umuhimu wa Chifu Mshabaha

1) Ametumiwa na serikali ya Mtemi Lesulia kama chombo cha kufaulisha njama zake dhalimu. 

2) Ametumiwa kama kiungo cha kuendeleza ufisadi katika serikali. 

3) Ametumiwa kuonyesha jinsi ukabila unavyoendelezwa serikalini. 

Mrima

Mrima ni mfanyakazi wa serikali, mfanyabiashara na mumewe Mangwasha.  Sifa za Mrima

Mwenye tamaa na ubinafsi

Ana tamaa ya pesa hasa pale anapokubali kuitelekeza jamaa yake kwa kufuata pesa za Sagilu  ili kujistarehesha. Anathibitisha hili kwa kusema, "Mhn, ati familia? Kwani mimi mjinga niache mapesa haya yote yanipite bila kuyafaidi." (uk. 37). Tamaa ya pesa na ubinafsi vinamfanya kukaidi masharti ya ndoa na kutomjali mkewe na watoto. Anasema, "Siku hizi kila mtu anazisaka chapaa, haijalishi ni kwa njia gani..." (uk. 107). 

Anaenda kinyume na jamii yake na kuchukua hongo kutoka kwa Sagilu ili kumfanyia kampeni Mtemi Lesulia. Tamaa na ubinafsi vinamfanya hata kufutwa kazi baada ya kuhamia Chakani kutokana na starehe nyingi. Tamaa ya pombe inamfanya kupotelea Majaani anakookolewa na jamii yake. 

Mpenda anasa na ulevi

Anapotelea Ponda Mali na Majaani, mahali palipokuwa na walevi wa kila aina ili kujihusisha na ulevi. Anakuwa mlevi kupindukia kiasi cha kutoweza kuitunza familia yake. Anafanya usuhuba na wanawake nje ya ndoa kutokana na barua ya mahaba anayoipata Mangwasha (uk.  77) na ambayo iliandikwa na mwanamke. Anakiri kwamba pombe ya bwerere haiachi na anahitaji kuvunja mifupa akiwa bado ana meno (uk. 37). Hata baada ya uhamisho kwenda Chakani, anaendelea na anasa za ulevi hadi anapigwa kalamu, Ulevi unamfanya kuokotwa Majaani na wenziwe akiwa katika hali mbaya na kupelekwa hospitalini. 

Mhafidhina

Anatoa kauli zinazoonyesha kwamba ingawa ni kijana wa kisasa, bado ameshikilia mawazo  na itikadi za utamaduni wake. Kwa mfano, anasema, "Tangu lini mke amuulize mumewe kule aendako au atokako?" (uk. 40). Baada ya kutibiwa katika hospitali kutokana na uraibu  wa pornbe, anakataa kwenda kwake. Tunaona akiuliza swali, "Hamwoni kwamba mila hairuhusu mie nikatunzwe na mke kama mgonjwa?" (uk. 100). 

Msaliti

Anaisaliti jamaa yake anaposhirikiana na Sagilu aliyekuwa adui wake wa muda, huku  akiwatesa Mangwasha na watoto wao. Kule kushirikiana na Sagilu pia ni kuisaliti jamii yake ya Waketwa ambao wanamwona Sagilu kama adui wao kisiasa na kijamii. Anamsaliti  mkewe kwa kuwa na mpenzi nje ya ndoa anayethubutu hata kumwandikia barua ya mapenzi. 

Mwepesi wa kushawishiwa

Anashawishiwa na Sagilu na kuingia mtegoni kwa haraka pale anapopewa mlungula ili kumfanyia mtemi kampeni. Sagilu anamshawishi kwa urahisi pale anapompa pesa kwa wingi ili atorokee ulevini huku akiacha familia yake bila kujali (uk. 36). 

Umuhimu wa Mrima

1) Ametumiwa kuonyesha kuwepo kwa utamaduni wa ubabedume miongoni mwa vijana katika jamii ya leo. 

2) Ametumiwa kuonyesha madhara ya ulevi na anasa katika asasg• ya ndoa.  3) Ametumiwa kuonyesha jinsi vijana wa kizazi cha sasa wanavyoweza kushawishiwa na pesa kwa urahisi na haijalishi njia wanazotumia kuzipata. 

4) Ametumiwa kuonyesha jinsi pesa zinavyoweza kubadilisha mtu kitabia.  Sihaba

Sihaba ni rafiki ya Sagilu anayemiliki makao ya Red Beads Lodgings. 

Sifa za Sihaba 

Fisadi

Anatumiwa na Sagilu kuendeleza vitendo vya ufisadi. Anatumiwa kuangamiza washindani wa Sagilu kibiashara. Anatumiwa katika uchomaji wa nyumba za wenyeji wa Matango kwa kusambaza vijikaratasi kuwaambia wahame. Anapokamatwa na kutupwa korokoroni kutokana na kusambaza vijikaratasi au kuwatumia watoto katika biashara ya ukahaba, 

tunaambiwa hakukaa humo bali anatumia njia za kifisadi na kutoka bila kufunguliwa mashtaka. 

Katili

Anashirikiana na Sagilu kuwachomea wenyeji wa Matango nyumba. Ukatili wake unaonekana pale anapojifanya kuwapelekea Mrima na Mangwasha zawadi ya arusi ilhali kilikuwa kifurushi cha kilipuzi. Kule kuwachukua wasichana wadogo na kuwaingiza katika biashara ya ukahaba bila kujali maisha yao ya baadaye ni ishara ya ukatili. 

Mnafiki

Anakwenda kuwapa zawadi Mrima na Mangwasha siku ya arusi yao lakini haikuwa zawadi bali kilipuzi cha kuwaangamiza. Anajifanya kuwa na urafiki na wakuu wa serikali huku  akijipendekeza kwao ilhali lengo lake ni kujinufaisha kiuchumi na kuishi maisha ya anasa. 

Mnyanyasaji wa haki za watoto

Anawachukua wasichana wadogo kwenda kuwachuuza kwa wanaume ili kujinufaisha bila kujali haki zao. Anashiriki katika uchomaji wa nyumba za wenyeji wa Matango bila kujali kuwa watoto katika makazi hayo wangeteseka. 

Umuhimu wa Sihaba

1. Ametumiwa kuonyesha jinsi wanawake wanavyoweza kutumiwa na wanaume kama vyombo vya kuendeleza maovu katika jamii. 

2. Ametumiwa kuendeleza madhara ya ukabila katika jamii. 

3. Ni kielelezo cha wale wanaovurujua haki za watoto kwa manufaa yao binafsi.  Mashauri

Mashauri ni mwanawe Sagilu na rafiki ya Lombo na Ngoswe. 

Sifa za Mashauri

Fisadi

Tunaona Mashauri akiajiriwa na Mtemi Lesulia kama mtaalamu mkuu wa usanifu majengo  mjini Taria. Pale mwanzo Mashauri anaonekana akishirikiana na baba yake kufisidi vipusa  na meno ya ndovu. Anauza maliasili za nchi ng'ambo hadi anaathiri utalii nchini, huku  akitumia cheo chake kuzima mashtaka yaliyofikishwa kortini (uk. 127). Kutokana na cheo  chake kama msimamizi wa ujenzi wa majengo, ana uwezo pia wa kuamuru kubomolewa kwa majengo yasiyojengwa kihalali au yasiyokuwa salama (uk. 117). Nafasi hii inamfanya kuchukiwa na watu kutokana na ubomoaji wa majengo Taria. 

Katili

Ukatili wake unabainika pale alipoamuru majengo ya watu kubomolewa kiholela kwa mpigo  wa kalamu yake (uk. 127). Anashirikiana na babake kufuja rasilimali za nchi na kusafirisha ng'ambo bila kujali hatima ya uchumi wa nchi yake au hata wananchi waliotegemea rasilimali hizo. Anadidimiza utalii nchini bila kujali matokeo kwa nchi yake.

Mwenye busara

Anaamua kumuunga mkono Lonare na kumfanyia kampeni kutokana na uhasidi aliotendewa na Sagilu na maovu yaliyokuwa yakiendelezwa na serikali ya Mtemi Lesulia. Anaamua kujiunga na vijana wenzake waliosoma kama yeye na ambao wana maono kama yake ili kuchagua viongozi wanaostahili kuongoza nchi. 

Msamehevu

Licha ya kwamba Sagilu anamtendea maovu kumwendea kinyume, anamsamehe na hata kumtafutia matibabu ya akili. 

Mvumilivu

Anamvumilia Sagilu hata baada ya kumkosea, akamchukua kutoka barabarani na kumpeleka kupata matibabu ili kuficha aibu. Anavumilia kauli za kuvunja moyo kutoka kwa Sauni na wengine wasiomwamini, akajiunga na Chama cha Ushirika cha Lonare ili kumfanyia kampeni. 

Umuhimu wa Mashauri

1. Ametumiwa kama kiungo cha kufanikisha ushindi wa Lonare. 

2. Kupitia kwake, tunaona uovu zaidi wa Sagilu. 

3. Ametumiwa kuonyesha jinsi vijana wanavyoweza kuwa na ushirikiano bila kujali mitazamo ya wazazi wao. 

4. Ametumiwa kuonyesha mui huweza kubadilika na kuwa mwema.  Ngoswe

Ngoswe ni mwanawe Mtemi Lesulia na rafikiye Lombo na Mashauri.  Sifa za Ngoswe

Mpenda anasa na ufasiki

Tunaambiwa anaishi maisha ya raha mustarehe katika kasri kubwa mtaani Majuu (uk.122).  Mbali na kwamba ni mraibu wa pombe, tunaona akifuja pesa kwa raha mbalimbali kutokana na ukusanyaji wa kodi za majumba na ushuru wa mashamba ya mtemi. Anastarehe na marafiki wa kitajiri na anafanya biashara haramu ya dawa za kulevya. Ndiye farisi katika biashara hii, huku dawa hizi zikisambazwa mitaani, magerezani, shuleni na vyuoni. Tunamwona akiwekeza kwenye majumba ya starehe na anasa na anawabadilisha wanawake wa mji kila uchao. Tunaambiwa katika vilabu vyake, vigoli wanamezwa usiku na kutapikwa asubuhi kuonyesha maisha ya ufuska yaliyokuwa yakiendelea (uk. 123). Tunaambiwa pia anawabadilisha warembo wa mji kila uchao kumaanisha alikuwa akiishi maisha ya ufuska.  Anakiri kwamba, "Mahusiano ya kimapenzi hayana maana tena." (uk. 125). 

Fisadi

Anajiingiza katika biashara haramu ya mihadarati na anatumia mitandao ya wahuni kufanya biashara hiyo ambayo ni kinyume na sheria za nchi. Pia anafisidi mali ya babake kutokana na usimamizi wa mashamba na majumba yake. Pesa alizofuja pia anawekeza katika majumba ya starehe (uk. 123). 

Mlevi

Anaonekana kuwa mlevi hasa pale katika hoteli ya Saturn tunapoambiwa kwamba U...alikuwa amepiga maji kupindukia" alipomkabili Sagilu na kumwaibisha mbele ya watu  (uk. 134). 

Mwenye msimamo thabiti

Mtemi Lesulia anapowashawishi rafiki zake waende kufanya fujo wakati wa uchaguzi,  Ngoswe anakataa katakata ushauri wa mzazi wake na kujiondoa kutoka katika mazungumzo  hayo (uk. 129). Anaamua kumwambia Mashauri kuhusu uhusiano wa Cheiya na babake, liwe liwalo. Hakujali kuvunja uhusiano wa Mashauri na babake bali alitaka ukweli ujulikane (uk.  120-125). 

Umuhimu wa Ngoswe

1. Ametumiwa kuonyesha jinsi dawa za kulevya zinavyotumiwa kuathiri vijana nchini.  2. Ametumiwa kuonyesha jinsi maisha ya ufasiki na anasa yanavyoharibU watoto  nchini. 

3. Ametumiwa kufichua uozo uliosakini katika jamii kama vile wazee kuwanyemelea wasichana wadogo bila kuzingatia mipaka ya umri. 

Sauni

Sauni anatoka katika jamii ya Waketwa na mfuasi halisi wa Lonare, 

Sifa za Sauni

Mtetezi wa haki za jamii

Anawatetea Waketwa wenzake pale kanisani waliochomewa nyumba zao hasa pale anapouliza watapiga kura wapi iwapo hawana makao (uk. 70). Anawahamasisha wenzake kung'oa mahema na kwenda kuyasimika Matango. Anamwambia mkuu wa polisi kwamba hawana haja ya ulinzi wake baada ya wao kurudi makwao kwani mlinzi wao ni Mungu (uk.  76). 

Mwenye hasira

Anaonyesha hasira pale anapomfokea Mrima baada ya huyu kukataa kwenda nyumbani kwake alipotolewa hospitalini. Anamkemea mkuu wa polisi baada ya kurejea Matango na wenzake anapomwambia atokomee (uk. 76). Tunaona akimkemea Mrima kwa kupokea hongo kutoka kwa Sagilu licha ya kwamba huyu alikuwa adui yao kijamii na kisiasa (uk.  114). Anamwambia, "Shetani wa mtu ni mtu. Shetani ni wewe mwenyewe." (uk. 115).  Anaonyesha hamaki pale anapotaka kumtimua Mashauri baada ya kuwaeleza yaliyomfika huku akimwita jasusi na kibaraka aliyetumwa kumharibia Lonare kura (uk. 126). 

Mwenye matumaini

Anaonekana kuwapa wafuasi wa Lonare matumaini hata ingawa Lonare hajulikani aliko na siku ya uchaguzi imefika (uk. 167). 

Umuhimu wa Sauni

1. Ametumiwa kama kipaza sauti cha Waketwa kuhusu taabu zinazowapata chini ya utawala wa Mtemi Lesulia. 

2. Ametumiwa kukemea maovu katika jamii. 

3. Ametumiwa kama mtetezi wa haki za jamii inayodhulumiwa. 

Sagura

Sagura ni rafiki wa karibu wa Lonare katika jamii ya Waketwa. 

Sifa za Sagura 

Mwaminifu

Anaonyesha uaminifu wake kwa Lonare pale anapoandamana naye katika kampeni za kisiasa na pale Lonare anapopata shida, tunamwona akiwa tayari kumsaidia. Anakuwa mwaminifu  kwa Waketwa wenzake na yuko tayari kutetea maslahi yao bila kwenda kinyume. 

Mtulivu

Tunaona mkuu wa kitengo cha jinai anapowasili Matango ili kulinda usalama, watu wanazua fujo lakini Sagura anamzungumzia kwa utulivu kumtaka aondoke (uk. 75). 

Mtetezi wa haki

Anatetea haki za Waketwa baada ya wao kugundua kwamba mtemi alitaka kunyakua ardhi yao. Anasema watapigania haki yao kwa jino na ukucha (uk. 92). 

Mpenda amani

Anaonekana kutopendelea ugomvi na badala yake anataka mambo yasuluhishwe kwa amani.  Sauni anapotamka maneno kwa hasira, Sagilu anamwambia, ('Heri ya mrama kuliko ya kuzama" (uk. 76) hasa pale Lonare anapomsihi Sauni asitamke maneno bila kuwa na hadhari. 

Mwenye hekima

Anasema kwamba kura watampigia Lonare hata kama haonekani (uk.165) na hili linazaa matunda baadaye kwani licha ya Lonare kupatikana, wafuasi wake tayari wameshahamasishwa kumpigia kura. 

Mwenye matumaini

Anawapa wafuasi wa Lonare matumaini na kuwahimiza kwenda kupiga kura licha ya kwamba Lonare hapatikani. 

Umuhimu wa Sagura

1. Ametumiwa kuendeleza mapambano dhidi ya uovu katika jamii. 

2. Ametumiwa kukuza sifa za wengine kama vile Mangwasha na Lonare.  3. Ametumiwa kuonyesha jinsi uaminifu unavyoweza kuzaa matunda katika jamii.  Mbungulu

Mbungulu ni rafiki shadidi wa Mangwasha, Mketwa na mfuasi wa Lonare.  Sifa za Mbungulu 

Mwaminifu

Anakuwa karibu na Mangwasha hasa wakati huyu anapopitia misukosuko ya ndoa pamoja na kazini mwake. Kwa mfano, anamhakikishia Mangwasha kuwa ataujua ukweli wote kuhusu  tabia ya Mrima kutokana na utafiti atakaoufanya (uk. 29). Uaminifu wake pia unajitokeza  pale anapomwambia Mangwasha kuwa alimwona Mrima akikokotwa kwa mkokoteni kuelekea Majaani palipoishi wachochole wa mji (uk. 97). Anashirikiana na Waketwa  wengine kumfanyia Lonare kampeni. Anakuwa mwaminifu kwa jamii pale anapoandamana na Mangwasha kufichua biashara haramu ya Sihaba ya kuwachuuza watoto wa kike (uk. 140-  143). 

Mhafidhina

Anamwambia Mangwasha mila hairuhusu mke kumfuata mumewe akiwa katika starehe zake (uk. 32) na kule kumshauri Mangwasha amsubiri mumewe hadi afike nyumbani kisha amuulize kilichokuwa kikimsumbua. Anamkumbusha Mangwasha yale aliyofunzwa na kungwi. 

Mshauri mwema

Anamshauri Mangwasha asimfuate mumewe ulevini kwani alijua pale si pahali pazuri pa  mke kwenda. Anamshauri Mangwasha amsubiri mumewe hadi afike nyumbani ili ajue kinachomsumbua (uk. 32). Anamshauri Mangwasha kukaa mbali na Sagilu kwani huenda akamtendea mabaya, na kumshauri aache wazee kushughulikia tatizo lao la ardhi ya Matango  (uk. 79). Mangwasha anapomwambia aandamane naye hadi Majaani kumsaka Mrima,  Mbungulu anamshauri kuwa pale hapakuwa pahali pa kwenda wanawake kama wao (uk.98).  Anamwambia, "Tutafute wanaume twandamane nao", kutokana na hatari ambayo  ingewakabili. 

Mtambuzi

Anatambua kuwa huenda wanyakuzi wa ardhi ya Matango wanatumia jina la serikali kuendeleza jinai (uk. 80), na hivi ndivyo ilivyokuwa baada ya Mangwasha kupata ithibati kamili kuhusu ardhi hiyo. 

Mwenye huruma

Anawaonea huruma watoto wa kike waliokuwa wakiteswa na Sihaba anapowaingiza katika ukahaba (uk. 140-143). Anamwonea huruma Sagilu anaporukwa na akili. Anasema,  "Amekuwa majununi. Maskini mzee wa watu." (uk. 146). Anamwonea Mangwasha huruma baada ya mumewe kupotelea ulevini na kutokana na huruma hiyo, anajaribu kila njia kumsaidia hata kuandamana naye Majaani kumsaka Mrima. 

Umuhimu wa Mbungulu

1. Ametumiwa kumkuza mhusika Mangwasha. 

2. Ametumiwa kufichua uozo unaoendelea katika jamii hasa biashara ya ukahaba wa watoto wa kike mjini. 

3. Ni kielelezo cha uhafidhina wa jamii inayozingatia ubabedume. 

Nanzia

Nanzia ni mkewe Mtemi Lesulia na mama yake Ngoswe. Ni mfanyabiashara mjini Taria.

Sifa za Nanzia 

Fisadi

Anashirikiana na mumewe pamoja na Mbwashu kuwanyang'anya Waketwa ardhi ya Matango  kupitia kwa njia za ufisadi kama vile kubadilisha cheti cha ardhi hiyo. Anawatumia Sihaba na Sagilu kutekeleza kitendo cha ufisadi cha kuchukua ardhi ya Matango kwa njia isiyo halali. 

Anashirikiana na mumewe kutoa hongo kwa Chifu Mshabaha, Sagilu na Sihaba kuhusu  umiliki wa ardhi ya Matango. Anahodhi mali nyingi za umma kinyume na sheria hata kumiliki jengo la Skyline Mall kupitia kwa njia za ufisadi. 

Mnafiki

Anashirikiana na mumewe kuwaambia watu kuwa serikali ilitaka kujenga soko kwenye ardhi ya Matango ilhali ardhi hiyo ilikuwa imilikiwe naye pamoja na Mbwashu. Anafanya urafiki wa kando na Sagilu na kumzaa Ngoswe huku akijifanya mtoto huyo ni wa mumewe.  Anajifanya kuwaonea huruma wenyeji wa Matango kwa kuwaletea vyakula kanisani walikojihifadhi, huku akijua kwamba yale yote yalitokana na unyakuzi walioufanya. 

Mwenye tamaa na ubinafsi

Anabinafsisha mali ya umma pamoja na jengo la Skyline Mall kutokana na tamaa ya mali.  Anashiriki katika unyakuzi wa ardhi ya Matango kutokana na ubinafsi na tamaa ya mali.  Tamaa yake ya kupata mtoto inamsukuma kuzaa na wanaume nje ya ndoa. 

Mdanganyifu

Anaficha siri yake ya kuzaa mtoto na Sagilu kutokana na kukosa uaminifu ndani ya ndoa.  Anashirikiana na wengine kudanganya kuwa serikali ilitaka kujenga soko katika ardhi ya Matango ilhali alitaka kumiliki ardhi hiyo na Mbwashu. Anahusika katika kuwachomea wenyeji wa Matango nyumba zao ilimradi apate kumiliki ardhi hiyo. Anawatesa wenyeji wa Matango na watoto wao ambao wanakosa makao na kuteseka pale kanisani. 

Msaliti

Anamsaliti mumewe pale anapofanya usuhuba na kuzaa na Mhindi pamoja na Sagilu.  Anaisaliti jamii nzima ya Matuo kwa kuhodhi mali ya umma kwa manufaa yake binafsi.  Anawasaliti wenyeji wa Matango kwa kushiriki katika kuchoma makazi yao ili afaidi na wengine. 

Msiri

Anamficha Ngoswe kuhusu baba mzazi hadi wakati anapofariki ndipo anapomwambia yeye ni mtoto wa Sagilu. Anamficha mumewe kUhUSU urafiki wake na Sagilu na kuzaliwa kwa Ngoswe hadi kuipeleka siri hiyo kaburini. 

Umuhimu wa Nanzia

1. Ametumiwa kama kielelezo cha ufisadi katika jamii. 

2. Ametumiwa kuonyesha kuzorota kwa maadili ndani ya ndoa. 

3. Kupitia kwake pia tunapata kujua jinsi walio na mamlaka wanavyoshirikiana na jamaa zao kufisidi na kuharibu uchumi wa nchi. 

Cheiya

Cheiya ni mpenzi wa Mashauri na mfanyakazi hospitalini. 

Sifa za Cheiya 

Mpenda anasa

Anafanya usuhuba na Mashauri kwa ajili ya kutimiza mahitaji yake bali si kutokana na penzi.  Tunamwona akimfuata Sagilu kutokana na utashi wake wa maisha ya anasa. Tunaambiwa aliishi maisha yasiyolingana na kipato chake (uk. 118), na alipenda pesa na maisha ya hali ya juu. 

Mwenye tamaa na ubinafsi

Anaonyesha utashi mkubwa wa pesa kwani urafiki wake na Mashauri pamoja na Sagilu  unajengwa juu ya tamaa ya pesa na ubinafsi. 

Msalitj

Anafumaniwa na Mashauri akitoka hotelini akiwa ameandamana na Sagilu, mzazi wa Mashauri (uk. 121). Hakujali kumkosea mpenzi wake bali anatoroka baada ya kufumaniwa. 

Katili

Anatumiwa na Mtemi Lesulia kumwekea Lonare sumu katika kinywaji chake ili kumuua (uk.  156) na kutokana na ukatili huu anakamatwa na kutupwa korokoroni. 

Mdanganyifu

Anamdanganya Mashauri kuwa alikuwa kazini ilhali alikuwa akistarehe katika hoteli ya Saturn na Sagilu. 

Umuhimu wa Cheiya

1. Ametumiwa kama kielelezo cha udanganyifu katika mahusiano ya vijana wa kisasa.  2. Ametumiwa kama kishawishi cha kumfanya Mashauri apiganie haki ili kuleta mabadiliko nchini kupitia kwa ushirikiano wake na Lonare. 

3. Ametumiwa kuonyesha jinsi uovu na upotovu wa maadili unavyotekelezwa na walio  na mamlaka serikalini. 

Mafamba

Mafamba ni mwanasheria anayewakilisha serikali katika kesi zake. 

Sifa za Mafamba 

Fisadi

Anajulikana kama fisadi mkubwa ndani na nje ya nchi ya Matuo. Ndiye anayetumiwa kufunika maovu yote yanayofanywa na viongozi wa nchi (uk. 93). Anatowesha majalada na nyaraka muhimu zinazohusu kesi za ufisadi, 

Mwenye kuogopewa

Anaogopewa Sio tu kutokana na uhodari aliodhaniwa kuwa nao katika kesi, bali kutokana na kesi za serikali alizokuwa akishughulikia. Anaogopewa na wale ambao hata hakuwahi kukumbana nao mahakamani. Anaogopewa hata na walinda usalama kutokana na ukuruba wake na serikali ya Mtemi Lesulia. 

Mchache wa utu/mdanganyifu

Anahiari kuwa mwongo na kutoa habari za uongo kwa niaba ya wale anaowakilisha.  Anadanganya kuwa wenyeji wa Matango walipata vyeti ghushi vya kumiliki ardhi.  Anadanganya kwa niaba ya serikali kuwa ilitaka kujenga soko kubwa pahali pale ili kuwaondoa wachuuzi kutoka barabarani. Anawasilisha stakabadhi ghushi katika kesi mbali na kuwasilisha ushahidi wa uongo (uk. 95). 

Mwenye maringo na kiburi

Anatembea kwa maringo huku kichwa amekiinamisha upande mmoja. Haikuwa rahisi kumwona akicheka sembuse kuyaona meno yake hadi pale alipozungumza. 

Msaliti

Anaisaliti jamii ya Matuo na nchi nzima kutokana na kuwakilisha viongozi wafisadi na waliodhamiria kupora mali ya umma. Mwenye ubinafsi 

Anapotetea ufisadi na kuhujumu sheria za nchi Sio tu kwa manufaa ya wale anaowawakilisha bali pia kwa manufaa yake binafsi. 

Umuhimu wa Mafamba

1. Ametumiwa kama kielelezo cha wanasheria ambao hutumia taaluma  1. zao kunyanyasa umma na kujinufaisha kupitia njia za ufisadi. 

2. Kupitia kwake, tunaonyeshwa jinsi serikali dhalimu inavyotumia 

3. wanasheria ili kuhalalisha maovu. 

Mwamba

Mwamba ni mwanasheria ambaye anawawakilisha wenyeji wa Matango katika kesi.  Sifa za Mwamba 

Mkweli

Anatoa ushahidi wa kweli katika kesi pamoja na kutoa kauli za kweli zenye ithibati.  Anazingatia ukweli hasa pale anapomwambia Mrima aseme ukweli hata kama ni mchungu ili aondoe chuki (uk. 113). 

Mwaminifu

Anakuwa mwaminifu kwa wenyeji wa Matango hata kuwapigania na kushinda kesi iliyowakabili. Anaonyesha uaminifu pale wenyeji wa Matango wanapomsihi apiganie kiti cha ubunge cha Matango, naye anakubali ombi lao. 

Mwenye subira

Anawaambia wafuasi wa Lonare wawe na subira na kwamba wampigie Lonare kura kwani walikuwa hawajaambiwa na yeyote kuwa Lonare hatarejea. 

Umuhimu wa Mwamba

1. Ametumiwa kama kielelezo cha matumizi ya haki katika jamii. 

2. Kupitia kwake, tunaona uongo ukishindwa na haki kusimama. 

Mbaji

Mbaji ni meneja wa kampuni ya mabasi ya Lonare na anatoka katika jamii ya Wakule.  Sifa za Mbaji

Mwaminifu

Ni mshirika wa karibu wa Lonare anayeaminika katika kazi yake (uk. 98). Anashawishiwa na Sagilu na Sihaba kuhujumu biashara ya Lonare lakini anaghairi. Anamjulisha Lonare  mipango yote dhalimu ya akina sagilu hata kumwonyesha barua ya jinsi njama ya hujuma ingetekelezwa na mahasidi wake. Kutokana na uaminifu wake, Lonare anamchukua kama nduguye. 

Mwenye kuwajibika

Anawajibikia kazi yake vyema licha ya vishawishi vya maadui wa tajiri wake. Lonare na wenzake wanapotaka kuondoka na kwenda katika hoteli ya Saturn ili kumkabili Sagilu,  Mbaji analiendea gari la mwajiri wake na kumkabidhi (uk.115). 

Mwenye heshima

Anakataa kuingia katika mitego ya adui wa Lonare kutokana na heshima aliyokuwa nayo  kwa mwajiri wake. Anamsaidia mwajiri wake kumletea gari lake pale alipoliegesha na kumkabidhi. 

Umuhimu wa Mbaji

1. Ametumiwa kufichua baadhi ya njama alizopangiwa Lonare na maadui zake.  2. Ni kielelezo cha wanajamii wanaozingatia haki na uwajibikaji katika utendakazi wao.  Mbwashu

Mbwashu ni mfanyabiashara maarufu na tajiri mkubwa mjini Taria anayemiliki msururu wa maduka na majumba ya ghorofa. Ni kikaragosi na mshirika mkubwa wa Mtemi Lesulia. 

Sifa za Mbwashu 

Fisadi

Akiwa na matajiri wengine, wanafisidi pato la nchi na kusababisha mfumko wa bei kila mara.  Anachangia katika kudidimiza uchumi wa nchi kupitia kwa magendo katika biashara.  Anaagiza bidhaa kutoka nje ya nchi na kukataa kulipa ushuru. Anawatumia maafisa wa ngazi za juu serikalini kuagiza bidhaa ghushi ambazo halipii ushuru. Bidhaa zake zinaposhikwa na maafisa wa forodha, anatoa mlungula na bidhaa hizo kupitishwa. Akisaidiwa na Mtemi Lesulia, yeye na Nanzia wanajaribu kuwapokonya wenyeji wa Matango kipande chao cha ardhi kwa kutumia njia za kimagendo kama vile kubadilisha cheti cha ardhi hiyo. Akiwa pamoja na Mtemi Lesulia na wengine, wanajaribu kuwahonga vijana kwa kutumia pesa ili 

waende kuvuruga zoezi la upigaji kura mbali na kuwahonga Watu kinyemela, Lengo hapa ni kuharibu upigaji kura ili wapinzani wa Mtemi Lesulia na Sagilu wasishinde katika uchaguzi (uk. 

Mwenye tamaa na ubinafsi

Anahonga maafisa wa serikali ili biashara yake inawiri bila kujali kwamba anahujumu  uchumi wa nchi. Anashiriki katika njama ya kuwahonga vijana kwenda kuvuruga uchaguzi ilimradi rafiki zake wapate uongozi naye azidi kujiendeleza kibinafsi. 

Mnafiki

Anawatembelea wenyeji wa Matango pale kanisani walipochomewa makao yao ilhali yeye ni mmoja wa wahusika wakuu katika njama ya kuwafurusha kutoka makwao (uk. 68). 

Katili

Anashiriki katika biashara zisizo halali na kuharibu uchumi wa nchi bila kumjali mwananchi wa kawaida. Mtemi Lesulia anaposhindwa katika uchaguzi mkuu, tunamwona akimwambaa.  Anaabiri ndege na kuelekea Ulaya bila kujali yale ambayo yangewafika mafisadi wenziwe (uk. 177). 

Msaliti

Anapoona mambo yamemharibikia Mtemi Lesulia, anamsaliti kwa kumtoroka na kumwacha pamoja na wale walioshiriki naye katika kulangua pato la nchi. 

Mdanganyifu

Anashiriki katika udanganyifu pale anapojaribu na Nanzia kumiliki ardhi ya Matango kwa kusingizia kuwa serikali ilitaka kujenga soko pahali hapo. 

Umuhimu wa Mbwashu

1. Ametumiwa kuyakuza na kuyaendeleza maudhui ya ufisadi. 

2. Kupitia kwake tunaona jinsi ubinafsi na usaliti unavyojitokeza katika tabaka la kitajiri.  3. Anawakilisha wanawake wanaowatumia wanaume kujikuza kiuchumi.  Lombo

Lombo ni mwanawe Lonare na daktari mjini Taria. 

Sifa za Lombo 

Mcheshi

Anaonekana mwingi wa bashasha na aghalabu anapozungumza na wenziwe kama Mashauri,  kauli zake huandamana na vicheko. Kwa mfano katika kurasa za 148 na 149, tunamwona akiandamwa na kicheko kila anapokuwa na wenzake kutokana na mizaha yake. 

Mwenye hekima

Tunamwona akihama kutoka Ujerumani alikokuwa akifanya kazi ya udaktari na kuamua kurudi nyumbani ili kumsaidia babake katika kampeni za uchaguzi na kumpa moyo. 

Mwenye upendo

Anamsaidia Sagilu kwa kumtibu anapokuwa mgonjwa ilhali akijua kwamba alikuwa hasimu  wa babake (uk. 151). 

Mshauri mwema

Anamshauri Mashauri kumsaidia babake hata kama alimkosea. Anasema, "Nenda ukamsaidie upate baraka" (uk. 150) kuonyesha kwamba ingekuwa aibu kama angemwacha mzazi wake kutembea uchi kutokana na ugonjwa wa akili aliokuwa nao. Aidha, anakuwa mmoja wa wale wanaomshauri Ngoswe kuacha biashara ya dawa za kulevya (uk. 173). 

Umuhimu wa Lombo

1. Ametumiwa kama kiungo cha kuleta mahusiano mema baina ya vijana na wazazi,  2. Kupitia kwake, tunaona ushirikiano na mahusiano mema baina ya vijana.  MBINU ZA UANDISHI

Mbinu za uandishi ni sehemu muhimu katika kazi ya sanaa kwa sababu ndizo humwezesha mwandishi kuwasilisha maudhui yake. Humsaidia mwandishi kufikisha ujumbe wake kwa wasomaji wake. Mbinu hizi zimegawika katika sehemu mbili: 

a) Mbinu za sanaa/Mtindo wa mwandishi

Mbinu za sanaa au mtindo wa mwandishi ni mbinu anazotumia mwandishi kuelezea ujumbe wake sawa na kuendeleza ploti ya kazi yake. Mbinu za sanaa hujumuisha mbinu za kimuundo, kama vile taharuki, mbinu rejeshi, kiangazambele, hadithi ndani ya hadithi na kadhalika, na mbinu za kimtindo, kama vile matumizi ya barua, ndoto, kinaya, majazi na kadhalika. 

b) Mbinu za lugha/TamathaIi za usemi/lugha

Mbinu za lugha au tamathali za lugha huhusu matumizi ya lugha kiufundi ili kuwasilisha ujumbe na pia kuipamba kazi ya kifasihi. Tamathali za lugha ni kama vile methali, misemo  na nahau, chuku, dhihaka, tashbihi, tanakali za sauti, takriri, tabaini na kadhalika. 

Mbinu za Sanaa/Mtindo wa Mwandishi

Baadhi ya mbinu za sanaa zilizotumika katika riwaya ya Nguu zaJadi ni:  Taharuki

Taharuki ni mbinu ya kisanaa ambayo humpa msomaji mshawasha wa kutaka kujua zaidi jambo lililotea baada ya tukio fulani. Humwacha msomaji akijiuliza maswaji ili kutaka kujua zaidi yaliyotokea baada ya kisa fulani, 

Hadithi inapoanza, Mangwasha na wanawe wako kanisani. Kuna jambo ambalo limekumba eneo Zima la Matango ambalo wasomaji hawana habari ni jambo gani. Wanawe Mangwashwa hawana taarifa kuhusu aliko baba yao, na wasornaji hawajui ni kitu gani kimetokea, hata mumewe Mangwasha kumwachia wanawe na umaskini (uk. 1). Wasomaji wanalazimika kuendelea kusoma ili kupata majibu ya maswali haya. 

• Barua anayopata Mangwasha wakati anachakura vitu vyake kuona kama vyeti vyake vipo  inamwacha msomaji katika taharuki. Hajui barua hiyo imeandikwa na nani na ujumbe wake ni upi. Hivyo, analazimika kuendelea kusoma ili kukata kiu yake kuhusu barua hiyo (uk. 3). 

• Taharuki inajitokeza wakati Sihaba anamtembelea Chifu Mshabaha na wanapotoka nje ya ofisi ya chifu, Sihaba anamkabidhi chifu bahasha. Msomaji anashangaa bahasha hiyo ina nini (uk. 85). Hata Mangwasha anapokimbia kwenda kurudufisha nyaraka zilizokuwa ndani ya bahasha hiyo, haijulikani mara moja nyaraka hizo zina taarifa gani hadi pale anapokutana na Lonare. 

Kisa cha kupotea kwa Lonare kabla ya uchaguzi mkuu kinajenga taharuki pia. Hata anapopatikana mapema siku ya uchaguzi, msomaji hapati taarifa zaidi kuhusu kilichokuwa kimejiri, anaachiwa kukisia kwamba pengine alitekwa nyara kwa amri ya mpinzani wake mkuu, Mtemi Lesulia. 

Hadithi ndani ya hadithi

Hadithi ndani ya hadithi ni hadithi au kisa ambacho husimuliwa ndani ya kisa au hadithi kuu.  Mara nyingi, hadithi ndani ya hadithi hutumiwa kuelezea jambo fulani ambalo kwa namna fulani linahusiana na kisa kikuu kinachosimuliwa. 

• Sauni anawasimulia marafiki zake, wakiwa nyumbani kwa Lonare, kisa cha mwanamke fulani ambaye alidhani alishabihiana sana na Sihaba (uk. 81). Mwanamke huyo aliitwa Lilith. Kisa cha Lilith kinatumiwa kuonyesha kwamba Sihaba si mwanamke mzuri. Sihaba anatumiwa kuvuruga harusi ya Mangwasha na Mrima, na anahusika katika njama ya kuwafurusha Waketwa kutoka katika eneo la Matango. Vilevile, anaendesha biashara haramu ya ukahaba ambako anawashirikisha wasichana wachanga wenye umri wa kwenda shuleni.  Kwa kiwango kikubwa, mhusika huyu anachangia pakubwa katika kuifisidi nchi kwa kuwaharibia vijana 

• Lombo na Mashauri wanapokutana wanakumbuka maisha yao wakiwa katika Shule ya upili (uk. 131). Katika kumbukumbu hiyo, tunasimuliwa kisa cha kijana mmoja ambaye aliugua ugonjwa wa pediculosis corporis ambao ulimfanya ajikune kila wakati. Visa vya jadi yao  shuleni vinaelezea uhusiano wao wa sasa kwani walikuwa marafiki wa karibu, na ndio maana pana msisimko mkubwa wanapopatana baadaye wakiwa wameshahitimu masomo na kila mmoja ana maisha mazuri. 

• Baada ya Nanzia kuugua kutokana na hofu ya kupoteza mali aliyomiliki kinyume cha  sheria, Mashauri anamsimulia Lombo kisa cha mfalme aliyeishi zamani huko Ufaransa (uk.  148). Mfalme huyo alichezea kamari pato la nchi hata wananchi wakamchukia kwani umaskini uliwafanya kula matunda ya mwituni. Wananchi hao, baada ya kufika mwisho wa madhila, waliwakamata mfalme, mkewe na mafasiki wengine wa utawala wake na kuwaangamiza (uk. 149). Mashauri ana uchungu wa kuendewa kinyume na babaye, na katika ari yake ya kimapinduzi, anaona kwamba viongozi wanaoiongoza Matuo, akiwemo babake kwa sababu 

Sagilu ni rafikiye Mtemi Lesulia, hawafai, kama huyo mfalme wa zamani aliyesimulia katika kisa chake. Kisa hicho kinaweza kuchukuliwa kama kiangazambele cha mabadiliko  yanayofanyika baadaye kwani Lonare, ambaye ni kiongozi mzalendo na mwenye kuzingatia 

maslahi ya watu, anachaguliwa kuwa mtemi, ishara kwamba sasa Matuo iko mikononi salama. 

Mbinu rejeshi/kisengerenyuma

Mbinu rejeshi au kisengerenyuma ni mbinu ya kisanaa ambapo mwandishi huyarejelea matendo yaliyotendeka awali kwa nia ya kufanikisha masimulizi. Mbinu hii imetumiwa ifuatavyo: 

• Hadithi ya kijana aliyeugua ugonjwa wa chawa, Pediculosis corporis, inasimuliwa katika mbinu rejeshi (uk. 131). Hii ni kwa sababu Mashauri na Lombo wanakumbuka matukio ya zamani walipokuwa wanasoma katika Shule ya upili. Umuhimu wa kisengerenyuma hiki ni kuweka msingi, kwa faida ya msomaji, kuhusu uhusiano wa Lombo na Mashauri. 

• Kisa cha jinsi Ngoswe ni mwanawe Sagilu na wala si Mtemi Lesulia kinasimuliwa katika mbinu rejeshi. Sagilu ndiye anayemfafanulia Ngoswe ilivyokuwa (uk. 160). Kutokana na kisa hiki, tunajua kwamba Nanzia ni mwongo. Yeye humwambia Ngoswe kwamba kakake,  Mdando, anasoma ilhali yuko na Mhindi ambaye ni babake, na ambaye alishurutishwa kuondoka naye akaenda uhamishoni Ulaya (uk. 161). 

• Riwaya inapoanza, tunaelezwa kuhusu Mangwasha, wanawe na watu wengine ambao  wamefurushwa kutoka Matango na sasa wamepata hifadhi katika kanisa fulani. Baadaye (uk.  14), tunaelezwa maisha ya Mangwasha akiwa msichana na kuhusu kuchumbiwa kwake na Mrima. Mbinu rejeshi hii inaweka wazi mambo kadhaa. Kwanza, Mangwasha ni msichana mwadilifu. Licha ya vishawishi vya Sagilu na Chifu Mshabaha, anaendelea kumpenda Mrima bila kumwendea kinyume (uk. 21). Pili, Chifu Mshabaha na Sagilu ni watu wenye dharau  (uk. 20). Wanamdharau Mrima kwa sababu hana utajiri na kumdharau Mangwasha kwa kumpenda mtu ambaye ni maskini. Tunafahamu pia kwamba Sagilu ni mkware/mzinifu  kwani licha ya kuwahi kuwa na wake watatu, Mrima anasema kwamba ana masuria/vimada watoshao kijiji kizima (uk. 18). 

Sadfa

Sadfa ni mbinu ya vitu viwili kutokea kwa wakati mmoja bila kutarajiwa. Vitu hivyo  vinapotukia pamoja huwa na umuhimu fulani katika muktadha husika. Ifuatayo ni mifano ya sadfa zinazotokea katika riwaya ya Nguu za Jadi. 

• Ni sadfa kwamba Ngoswe yuko karibu Sagilu anapotokea akiwa na Cheiya na kuingia kwenye hoteli. Ngoswe anaamua kumwambia Mashauri kwamba babake anamwendea kinyume, jambo ambalo linamfanya Mashauri kuamua kuachana na mchumba wake huyo,  ambaye ni wazi hampendi kwa dhoti kwani anaongozwa na tamaa ya pesa. 

• Ni sadfa kwamba Ngoswe anakosana na babake, Mtemi Lesulia wakati Mashauri, rafikiye,  anakosana na babake, Sagilu. Kutokana na sadfa hii, wawili hawa wanaamua kujiunga na kombi ya Lonare na kumsaidia kuwa kiongozi na kuleta mabadiliko ambayo yanahitajika katika nchi ya Matuo. 

• Ni sadfa kwamba Lombo, mwanawe Lonare, ni rafikiye Mashauri, mwanawe Sagilu  ambaye ni mpinzani wake wa kisiasa. Mambo yanapomharibikia Sagilu na Lonare anashinda uchaguzi, inakuwa rahisi kwa Lonare kumshawishi Ngoswe kuacha mienendo miovu kwani Ngoswe ni rafiki mkubwa wa Mashauri. Urafiki huu pia unamsaidia Lonare kuchaguliwa 

kwani sasa anaungwa mkono hata na baadhi ya watu ambao wangekuwa wakimshabikia Mtemi Lesulia. 

Ndoto

Ndoto ni maono yanayotokea usingizini. Pia huitwa njozi au ruya. Mbinu hii hutumiwa ili kuwasilisha ujumbe fulani kwa msomaji. Ndoto imejitokeza ifuatavyo: 

• Baada ya kuwa na makabiliano na Sagilu (uk. 60-61), Mangwasha anaota ndoto ya kutisha.  Anaota anafukuzwa na jinyama lenye sura ya kutisha. Pia, anakabiliwa na moto mkubwa mbele yake. 

Ndoto hii ni jazanda kwa kuwa:

i) jinyama linalomkimbiza linamwakilisha Sagilu ambaye ni mzee katili anayemhangaisha Mangwasha kwa kumtaka kimapenzi huku akimsababishia matatizo ya kifamilia kwa kumtokomeza Mrima, mumewe, kupitia kwa ushawishi wa pesa. 

ii) moto unaomkabili ni kiangazambele cha moto unaoteketeza makao ya Waketwa katika eneo la Matango. 

Matumizi ya Barua

Barua ni njia ya kuwasiliana kati ya watu wawili au zaidi kwa njia ya maandishi. Pia,  tunaweza kusema kuwa barua ni ujumbe wa maandishi unaotumwa kwa mtu kwa njia ya mkono au posta. Barua pia huitwa waraka. Barua imetumiwa ifuatavyo: 

Wakati Mangwasha anapekuapekua kwenye vitu alivyoweza kuokoa visichomeke makao yao  kule Matango yanapoteketezwa, anakumbana na barua ambayo baadaye (uk. 77) anagundua kwamba Mrima aliandikiwa na mwanamke fulani. Mangwasha anamhurumia mumewe ambaye haelekei kuelewa hatari inayomkabili kwa kujihusisha na wanawake ambao nia yao  hasa ni kumfilisi. Anajua tu kwamba Mrima amezuzuliwa na pesa. 

Taswira

Taswira ni picha ambazo hujengeka akilini mwa msomaji wa kazi za kifasihi. Taswira anazopata msomaji wa Nguu za Jadi ni nyingi, miongoni mwake: 

• Kuna taswira ya Mangwasha akivikagua vifurushi vya nguo na vitu vingine vichache alivyoweza kuokoa visichomeke (uk. 2). Taswira hii inakuza maudhui ya umaskini na hali ya uhitaji. 

• Kuna taswira ya Mrima akiwa na wasiwasi baada ya kumwona Sihaba amejiunga na watu  wengine kwenye foleni ili atoe zawadi (uk. 24). Mrima anashuku kwamba mwanamke huyu  hana nia nzuri. 

• Kuna taswira inayojengeka katika ndoto ya Mangwasha (uk. 61). Ni taswira yake akiwa anakimbia huku nyuma akifuatwa na jinyama la kutisha na mbele anakoelekea akikabiliwa na moto unaotishia kumteketeza. Jinyama hilo linamwakilisha Sagilu ambaye ni mzee anayemhangaisha Mangwasha kwa kumtaka kimapenzi. Moto nao ni kiangazambele cha  tukio ambapo makao ya Waketwa yanateketezwa kwa moto huko Matango. 

• Kuna taswira ya Mkurugenzi wa Ardhi ambaye anawahutubia watu wakiwa kanisani. Watu  hawa wamekasirika na hawataki kumsikiliza kwa kuwa anayowaambia ni uongo (uk. 69).  Taswira hii inaashiria namna Waketwa wanapopokwa haki yao kwa njama za watu wachache wenye ushawishi mkubwa serikalini. 

• Kuna taswira ya Mangwasha akiwa na wasiwasi sana anapokuta bahasha yenye pesa juu ya kabati, kisha anaamua kuificha baada ya kuona marundo ya pesa (uk. 105). Taswira hii inaeleza wasiwasi wake Mangwasha kuhusu mumewe, ambaye anapotoshwa na Sagilu kwa kumshawishi kwa helm 

• Kuna taswira ya makabiliano kati ya Sagilu na mwanawe, Mashauri, baada ya Mashauri kumfumania babake na mchumba wake, Cheiya (uk. 121). Hii ni taswira inayokuza maudhui ya ukengeushi kwani Sagilu anatenda mambo kinyume na maadili ya kijamii. Cheiya pia amekengeuka. Anamwandama Sagilu kwa sababu ya pesa, licha ya kwamba amesoma na anaweza kufanya kazi na kujitegemea. 

• Kuna taswira ya polisi wakiwatoa kwa nguvu wasichana kutoka katika vyumba vya ukahaba vya Sihaba (uk. 142). Taswira hii ni ya upotovu wa kimaadili unaoendelezwa na Sihaba huku akiwaharibia wasichana wadogo maisha yao pasi kujali lolote. 

• Kuna taswira ya watu wakiwa nyumbani kwa Lonare wakiomboleza na kuangua vilio (uk.  164). Taswira hii inatoa picha ya matumaini yaliyodidimia kwani wafuasi wa Lonare wanaamini ndiye kiongozi anayeweza kutegemewa. 

Jazanda

Jazanda ni mbinu ya kisanaa ambapo jambo hulinganishwa na jingine kwa kutumia lugha fiche. Katika jazanda, mambo huelezwa kwa kutumia lugha fiche au lugha ya kimafumbo. 

• Anwani ya riwaya hii ni ya kijazanda. Nguu ni kilele au upeo wa mlima. Kitamathali, nguu  ni vikwazo au matatizo ya ainati yanayokwamiza maendeleo ya kijamii, kama vile ukabila,  unyanyasaji wa wanawake, ubabedume, uongozi mbaya, umaskini, ukosefu wa ajira, ufisadi,  na kadhalika. 

Mtemi Lesulia analinganishwa na mjusikafiri. Kitendo cha mjusikafiri kuingia kwenye shimo  huku akiotea chakula cha mchwa, sawa na mchwa wenyewe, ni jazanda ya uongozi mbaya.  Mchwa ni wananchi wa kawaida, nao viongozi, kama vile Mtemi Lesulia, ni mjusikafiri ambao wanafakamia kila kitu, kiasi kwamba wananchi wa kawaida wanabaki katika dhiki kubwa (uk. 93). 

• Sihaba anatumia gari jekundu katika shughuli zake. Rangi nyekundu ni jazanda ya hatari.  Mwanamke huyu amejaribu kuwadhuru Mangwasha na mumewe wakati wa harusi yao. Yeye pia anamiliki jengo ambako anaendesha biashara ya ukahaba akiwatumia wasichana wachanga wanaostahili kuwa shuleni. 

• Ndoto anayoota Mangwasha ni jazanda, Anaota akikabiliwa na moto mkubwa huku  akikimbizwa na jinyama la kutisha. Moto huo ni kiangazambele cha moto unaoteketeza makao ya Waketwa kule Matango. Jinyama la kutisha ni Sagilu anayemhangaisha Mangwasha (uk. 61). 

• Sagilu anashindwa kuamini kwamba Lonare ameshinda kura ya utemi (uk. 176) kwani anajua Mtemi Lesulia ni "...sindano yenye uzi ambayo haiwezi kukosa kushona...". Hii ni jazanda inayoashiria kwamba Mtemi Lesulia anadhibiti vyombo vya dola, kwa hiyo ana uwezo wa kubatilisha matokeo ya kura hata akishindwa. 

• Siku ya uchaguzi mkuu, "...miale ya jua ilianza kuremba mbingu kwa rangi nzuri za kuvutia...". Hii ni jazanda ya matumaini kwa nchi ya Matuo kwani kiongozi mwenye maono,  Lonare anachaguliwa kuwa mtemi mpya (uk. 168). 

• Kuna jazanda ya siafu wengi wanaofanya msafara (uk. 161). Siafu hao wanafanya kazi kipunda lakini wanaokula ni wengine. Siafu hawa ni wananchi wafanyao kazi kwa bidii lakini wanaofaidika ni watu wachache, hasa wenye ushawishi mkubwa nchini. 

• Kuungana kwa Ngoswe (mwanawe Mtemi Lesulia) na Mashauri (mwanawe Sagilu) ni jazanda ya vijana kuungana katika kuleta mabadiliko chanya katika jamii. Hapo mbeleni,  walishirikiana na wazazi wao katika kuifilisisha nchi. 

• Mwandishi anasema kwamba Sagilu "Alipanda upepo sasa alikuwa akivuna tufani." (uk.  135). Hii ina maana kuwa maovu aliyofanya Sagilu sasa yalikuwa yanamsababishia matatizo  katika maisha kwani hata mwanawe, Mashauri, alishaungana na mpinzani wake wa kisiasa,  Lonare. 

• Sauni anamuuliza Mrima kama anaweza kumsalimia mtu aliyekunja ngumi (uk. 114). Mtu  anayerejelewa hapa ni Sagilu, ambaye hana nia nzuri na Mrima. Mrima alikuwa hatambui hili. Kifo cha Nanzia, mkewe Mtemi Lesulia kinaweza kuchukuliwa kama jazanda ya mwisho wa ufisadi. Mwanamke huyu anamiliki mali ambayo ameipata kwa ushawishi wa mumewe. Vivyo hivyo, matatizo ya kiakili yanayomvamia Sagilu ni ishara kuwa uovu  unashindwa na maadili kuchukua nafasi yake. 

• Lonare kuamua kumpinga Mtemi Lesulia kisiasa kunalinganishwa na kutia kichwa chake kinywani mwa simba (uk. 51), kumaanisha kwamba hatua hiyo ilikuwa ya hatari, kwani alikuwa anahatarisha maisha yake. Baadaye, anaonekana akitekwa nyara kabla ya uchaguzi mkuu na hatimaye kupatikana akiwa amejeruhiwa vibaya. 

Kinaya

Kinaya ni mbinu ya kisanaa ya kutoa maelezo kuhusu kitu au jambo fulani kwa kinyume.  Kinaya na kejeli huwa na uhusiano wa karibu sana. 

Ni kinaya kwamba watu wasiokuwa na elimu ya kutosha ndio wanaopata kazi katika nchi ya Matuo huku watu wengi waliohitimu vizuri, hasa wa kabila la Waketwa, wakiwa hawana kazi (uk. 44). 

Ni kinaya kwamba Mtemi Lesulia hataki kuachilia kiti cha utemi ilhali ni wazi kwamba uongozi wake umeiingiza nchi katika hali ya uhitaji, umaskini uliokithiri na hali ya maadili kuzorota. 

Ni kinaya kwamba Mzee Sagilu anamwona Mrima kama maskini wa mali huku yeye mwenyewe akiwa ni mkosa maadili. Anamtaka Mangwasha kimapenzi na baadaye,  inafahamika kwamba anatembea na mchumba wa mwanawe, ambaye ni msichana mdogo. 

• Ni kinaya kuwa Mbungulu haoni haja ya Mangwasha kuharakisha kumwokoa mumewe kutokana na sherehe zisizokuwa na maslahi. Hii ni kutokana na hali kwamba ametawaliwa na mila zinazowazuia wanawake kudai haki zao katika ndoa (uk. 32). 

• Ni kinaya kwamba Mrima anaitelekeza familia yake kwa kuandama pesa. Anasema kwamba Mangwasha na wanawe watajipanga (uk. 37). Hii inaashiria hali ya ukengeushi baada ya Mrima kushawishiwa na Sagilu kwa kutumia pesa ili anapoiacha familia yake,  Sagilu apate nafasi ya kumhangaisha Mangwasha. 

• Ni kinaya kwamba Chifu Mshabaha, ambaye ni mtumishi wa urnma, yumo kwenye njama ya kuifurusha jamii ya Waketwa kutoka kwenye makao yao. Yeye, kama mtumishi wa umma hatarajiwi kujihusisha na mambo ya siasa, ambayo ndiyo yanayowafanya Waketwa kufurushwa kutoka kwenye makao yao. 

• Ni kinaya kwamba serikali ambayo inafaa kuwa inapinga ufisadi inashiriki ufisadi.  Mbwashu anashirikiana na maafisa wa ngazi za juu serikalini kukwepa kulipa ushuru kwa bidhaa wanazoingiza nchini. Pia, wanaingiza nchini bidhaa ghushi (uk. 68). 

• Ni kinaya kwamba Mkurugenzi wa Ardhi mjini Taria anawaahidi Waketwa waliofurushwa kutoka makwao mablanketi, vyakula vya msaada, maji na mahema badala ya kuahidi suluhu  ya kudumu kwa tatizo lao la makao (uk. 70). Hii ina maana kwamba yeye pia yuko kwenye kundi linalowasababishia kero inayowakumba. 

Majazi

Majazi ni mbinu ya kisanaa ya kuipa sehemu au mhusika katika kazi ya fasihi jina kutokana na sifa, maumbile, tabia au mienendo yake. Baadhi ya wahusika na sehemu mbalimbali zimepewa majina ya kimajazi. Ifuatayo ni mifano ya matumizi ya majazi katika riwaya ya Nguu za Jadi. 

• Matuo: hili ni jina la nchi. Linatokana na kitendo cha kutua, au kutuama, kwa maana ya kutosonga mbele. Nchi hii haisongi mbele kwani inakumbwa na changamoto mbalimbali,  kama vile umaskini uliokithiri, hali ya vijana wengi kukosa ajira, mfumo wa ubabedume unaotatiza maendeleo ya wanawake, visasi vya kisiasa, utabaka na ukabila. 

• Waketwa: jina hili linatokana na kitenzi 'keta', kumaanisha hali ya kumpiga mtu na kumwangusha. Waketwa ni watu wanaodharauliwa na wamenyimwa nafasi ya kujiendeleza ingawa tunaambiwa kwamba wana bidii katika masomo na kazi. Hivyo, wameketwa na utawala dhalimu katika nchi yao. Wachache wao wanashikilia nafasi za uongozi huku  viongozi wengi wakitoka katika jamii ya Wakule, licha ya kwamba wengi wa hawa hawajahitimu vizuri kimasomo. 

• Wakule: hawa Wako mbali sana kimaendeleo. Wao wanahodhi nafasi za uongozi nchini Matuo. Pia, kwa kuwa wengi wao wako serikalini, wanaifisidi nchi kwa kujifaidisha wenyewe na nafasi zao. Kwa ufupi, wako mbele katika kujinufaisha kama jamii mahususi. 

• Chifu Mshabaha: shabaha ni lengo, kusudi au nia. Huyu chifu ana nia ya kuisambaratisha ndoa ya Mangwasha akishirikiana na Sagilu. Pia, anatekeleza nia ya kumfuta kazi Mangwasha. Aidha, ana nia pia ya kuwahujumu Waketwa wanaoishi Matango kwani yeye ni mkabila na anashirikiana na uongozi wa Mtemi Lesulia ambao hauwavumilii Waketwa. 

• Mpenda Bure: huu ni mkahawa unaomilikiwa na Sagilu. Hapa, ndipo wanapokutana Mangwasha na Mrima, ambao wanapendana kwa dhati, japo Mrima ni maskini. Sagilu  anamtamani Mangwasha licha ya kwamba anajua yeye ni mchumba, na baadaye mke wa mtu. 

• Ponda Mali: hii ni sehemu ambako kunauzwa pombe haramu. Humu ndimo watu kama vile Mrima wanakuja kuharibia pesa zao kwenye vileo hivyo. Wanapondea mali zao humo. 

• Sihaba: mhusika Sihaba ni mwanamke mwenye mambo si haba (si machache). Yeye ndiye anayetumwa na Sagilu kuja kuvuruga harusi ya Mangwasha na Mrima. Pia, yumo kwenye njama ya kuwafurusha Waketwa kutoka kwenye eneo la Matango. Yeye ndiye anayesafirisha vijana wanaokwenda kuteketeza eneo hilo 

kwa moto. Baadaye, inafahamika pia kwamba anaendesha biashara ya ukahaba ambapo  anawashirikisha vijana wa kike wanaostahili kuwa shule. 

• Bwana Mafamba: huyu ni mwanasheria. Maana ya mafamba ni uongo. Mwanasheria huyu  ni fisadi na mwongo (uk. 95). Jina hili pia lina maana ya mambo yaliyofanywa vibaya.  Bwana huyu anatumiwa na upande wa watetezi katika kesi kuhusu ardhi ya Matango. Hata hivyo, hafui dafu na anashindwa na mwanasheria mwenzake, Mwamba, ambaye ana ushahidi wa kuaminika kuhusu kesi hiyo. 

• Mwamba: huyu ni mwanashefia mahiri sana. Hata Mangwasha anamlinganisha na mlima uliojengwa kwa mwamba. Kutokana na umahiri wake katika sheria, anashinda kesi ya ardhi ya Matango. 

• Majaani: jaa ni mahali panapotupwa takataka. Majaani ni sehemu chafu ambako Mrima anapatikana baada ya kusukumwa kwenye pombe na Sagilu kwa hadaa za pesa. Hii ndiyo  sehemu ambayo takataka zote za mji hutupwa (uk. 98). 

• Mashauri: hili ni jina la kimajazi. Lombo anamwambia Mashauri, "l say, Mashauri.  Ninaona leo una mashauri ya kufanya na mzee wako..." (uk. 134). 

Dayalojia

Dayalojia ni mazungumzo baina ya wahusika wawili, au hata zaidi. Dayalojia huwa na dhima anuwai katika kazi za fasihi. Kwa mfano, dayalojia hutumika kupunguza uchovu unaotokana na kusoma maandishi mengi bila mapumziko. Pili, kupitia dayalojia, msomaji anaweza kujua

hisia za wahusika na hata sifa zao, kando na kwamba dayalojia hudhihirisha baadhi ya maudhui na mbinu za kimtindo zinazotumiwa katika kazi za fasihi. Katika riwaya hii,  dayalojia imejitokeza sana. Katika sehemu hii, yapo maelezo ya kifupi kuhusu baadhi ya dayalojia hizo, na umuhimu wake pale inapostahili. 

• Kuna dayalojia kati ya Mangwasha, mhusika mkuu, na mumewe, Mrima. Kupitia dayalojia hizi, tunamwelewa Mangwasha kama mke mwenye mapenzi ya dhati na anayejali maslahi ya familia yake. 

Kuna dayalojia pia kati ya Mangwasha na rafiki yake, Mbungulu. Kupitia kwa dayalojia hizo, tunamwelewa Mbungulu kama mhusika ambaye ni rafiki wa dhati aliye tayari kumsaidia Mangwasha kwa hali na mali. Pia, Mbungulu anajitokeza kama mwanamke ambaye bado hajajikomboa kimawazo. Anamwonya Mangwasha dhidi ya kumfuata Mrima 

huko ulevini alikoenda, na badala yake amsubiri mpaka aje nyumbani. Yeye ni mtamaduni ambaye anaona kwamba Mangwasha anafaa kumkabili Mrima kwa hadhari kwani yeye ni mwanamke (uk. 32). 

• Kuna mazungumzo kati ya Mangwasha, Sagilu na Chifu Mshabaha. Kupitia dayalojia hizi,  tunaelewa kwamba Chifu Mshabaha ni mpyaro na mwenye taasubi ya kiume. Sagilu naye ni mwenye kiburi. Anamdharau Mrima kwa sababu si tajiri, na anaona kwamba Mangwasha anapaswa kumkubali yeye kwa sababu yeye ni tajiri. 

• Kuna dayalojia zinazomhusisha Lonare na ambazo zinamsawiri kama kiongozi jasiri na mwenye maono ya kuiinua Matuo na kuiweka kwenye ramani ya maendeleo. Zipo dayalojia zinazomhusisha Mtemi Lesulia, (uk. 78), ambazo zinamwashiria kama mhusika katili,  mpyaro na mwenye kiburi. Yeye anashirikiana na Sihaba na Sagilu katika njama ya kuwafurusha Waketwa kutoka katika ardhi yao huko Matango. 

• Kuna dayalojia kati ya Mashauri na Ngoswe, baada ya Ngoswe kuwafumania Cheiya na Sagilu. Dayalojia hii inafichua mengi, kwanza suala la utabaka kwani hawa wanatoka katika familia tajiri na kwamba Sagilu amepujuka kimaadili (uk. 123). 

• Kuna mazungumzo kati ya Mtemi Lesulia na mwanawe, Ngoswe (uk. 129). Mazungumzo  hayo yanamdhihirisha Lesulia kama kiongozi katili ambaye yuko tayari kuua ili atwae uongozi. Kwa upande wake, Ngoswe anajitokeza kama mwanamapinduzi kwani haafiki mpango wa babake, na kwa sababu hii, anaamua kujiunga na mrengo unaomshabikia Lonare,  mpinzani mkubwa wa kisiasa wa Mtemi Lesulia. 

• Kuna dayalojia katiya Lombo na Mashauri. Kutokana na dayalojia hii, tunapata kujua kwamba hawa ni vijana waliojikomboa kimawazo, na wako tayari kuondoa utawala mbaya pamoja na vikaragosi vya watawala sampuli ya Mtemi Lesulia. 

Uzungumzinafsia

Uzungumzinafsia ni mazungumzo anayokuwa nayo mhusika fulani akiwa peke yake. Mara nyingi, mbinu hii hutumiwa kuonyesha mawazo waliyo nayo wahusika na migogoro katika nafsi zao. Ifuatayo ni mifano ya matumizi ya mbinu hii katika riwaya. 

• Mangwasha anajizungumzia baada ya kusoma barua anayoandikiwa Mrima na mwanamke ambaye biia shaka ni kimada wake (uk. 4). Anashangaa kwamba muda wote Mrima alikuwa na siri hii ambayo yeye hakuijua. 

• Mangwasha anajizungumzia anapopanga viti ndani ya chumba pale kanisani ambamo  amejificha (uk. 5). Uzungumzinafsia huo unaashiria hali yake ya kutokuwa na usalama  mahali hapo ambapo alihisi wangeingia watu wabaya na kumvamia yeye na watoto wake.  Mangwasha anajisemea, "Laiti wangalivuta fikira zaidi, wangalijua chanzo cha mateso  Yao..." (uk. 9). Mangwasha anajua kwamba taarifa walizonazo watu kuhusu chanzo cha moto  uliochoma nyumba zao huko Matango si sahihi. Yeye anajua kwamba hata Chifu Mshabaha anahusika. Mangwasha anawaza, "Je, akipuuza nitakalomwambia, hataniona mie ni mwongo  tu?" (uk. 11). Hapa, Mangwasha hana hakika kama Lonare atamsikiliza kwani utamaduni unawafanya wanawake kutokuwa na sauti mbele ya wanaume. 

Mangwasha anajizungumzia baada ya Sagilu kumuuliza kama anajua aliko Mrima na anakotoa pesa zake (uk. 31). Hapa ndipo Mangwasha anaanza kugundua kwamba Sagilu  ndiye anayehusika katika kumtokomeza mumewe. 

Mangwasha anapotafuta pesa kwenye nguo zake (uk. 58), anajiambia, "Pesa zimeamua kuniambaa kama muuaji..." kumaanisha kwamba hana pesa hata kidogo. 

Mashauri anajizungumzia akiwa katika hoteli ya Saturn, anaposubiri kumwona babake akiwa na Cheiya. Anashangaa, "Babangu mzazi anaweza kuwa na makuruhu kiasi hiki..." (uk. 120). 

Kuchanganya ndimi

Kuchanganya ndimi ni mbinu ya kutumia zaidi ya lugha moja katika uandishi. Kuna mifano  kadhaa ya matumizi ya mbinu hii. Ni muhimu kuelewa mbinu hii hutumiwa kwa nini. 

• Mbinu hii wakati mwingine huashiria uwezo wa mhusika katika kutumia zaidi ya lugha moja. Pia, ni njia moja ya kuashiria hadhi ya mtu. Kwa mfano, katika mazungumzo kati ya Mrima na Mangwasha (uk. 21), wanaitana darling, honey na guardian angel kwa kuwa wao  ni wapenzi. 

• Kwa upande mwingine, mazungumzo kati ya Ngoswe na Mashauri, (uk. 123-125) na kati ya Mashauri na Lombo (uk. 132-133) yanaashiria hadhi ya kielimu, na kwa namna fulani,  kuibua maudhui ya utabaka, kwani wote wamesoma sana na wanatoka katika familia tajiri. 

• Baadhi ya wahusika wanaweza kutumia maneno au msamiati fulani kutoka lugha nyingine kwa sababu ni msamiati wa kitaaluma. Kwa mfano, katika riwaya hii, tuna msamiati kama vile Panic Disorder (uk. 157), Schizophrenia (uk. 147), Pediculosis corporis (uk. 131), ambao  ni msamiati wa kimatibabu. 

Usimulizi

Usimulizi wa kazi yoyote ya kifasihi hufanywa kwa kutumia moja kati ya nafsi tatu za usimulizi. Nafsi hizo ni: 

Nafsi ya Kwanza

Katika nafsi ya kwanza, msimulizi anahusika katika usimulizi wenyewe na anashiriki pia kwenye matendo yanayozungumziwa katika kazi husika. 

Kiwakilishi cha nafsi hii kwenye vitenzi huwa ni 'ni' katika umoja na 'tu' katika wingi.  Tazama mfano ufuatao: 

Nilikuwa sijaonana na Timo kwa muda mrefu. Tangu apate nafasi ya kwenda Marekani kwa masomo ya Chuo kikuu, tuliwasiliana tu kwa njia yajumbe za Facebook na WhatsApp. Sasa alikuwa anarejea nchini na hamu yangu ya kuonana naye ilipanda vidato kila siku  iliyokucha... 

Nafsi ya Pili

Nafsi hii huwakilishwa na kiambishi 'u' katika umoja na 'm' katika wingi. Zipo kazi chache sana zilizosimuliwa kwa kutumia nafsi hii. Hata hivyo, mfano ufuatao unatoa picha ya jinsi nafsi hii inaweza utumiwa kusimulia kazi ya kifasihi. IJmeketi kwenye matatu, unaelekea mjini. Matatu imejaa abiria, kilo mtu ametulia kitini mwake. Mara dereva anaisimamisha gari 

kando ya barabara, mahali ambapo hapana stendi. Mnashangaa ana nia gani. Taratibu,  anachukua simu yake na kumpigia jamaa fulani msiyemjua. Mnapandwa na mori kwa kuhisi kwamba dereva huyu anawapotezea muda. Anamaliza kuongea na kuwaambia, "Samahani sana. Nimetanabahi bosi wangu ametuma ujumbe kutaka kujua nilipo. 

Singeweza kuijibu arafa yake wala kumpigia simu huku ninaendesha gari, kwa sababu  kufanya hivyo ni kuhatarisha maisha yenu, wateja wangu, barabarani..." Unajiambia kimoyomoyo, "Huyu ni mzalendo halisi." 

Nafsi ya Tatu

Nafsi hii huwa haishiriki katika matendo yanayosimuliwa katika kazi husika. Msimulizi husimulia yale anayoona, kushuhudia au kuambiwa. 

Nafsi hii huaminiwa sana kwani msimulizi hana haja ya kuficha au kubana maelezo fulani,  kama inavyoweza kufanyika katika usimulizi wa nafsi ya kwanza. Kazi nyingi za kifasihi zimesimuliwa kwa kutumia nafsi hii. Riwaya ya Nguu za Jadi imesimuliwa kwa kutumia nafsi hii. 

Tazama mfano ufuatao: 

Mangwasha hakuwa na hamu ya kuzikimbilia zile noti wala kuchota zile sarafu.  Alipozitazama, zilimtafishi na kumtia kichefuchefu. Hapo alipata nafasi ya kulikimbia na kujisalimisha. Jinamizi hilo lilimshtua sana hadi akaamka. Mwili wote uliloajasho. Alijaribu  kulala tena lakini akashindwa kabisa. Hapo ndipo aliposikia mayowe huko nje. Wanaume kwa wanawake, wote walipiga mayowe mfulu/izo. Kuna nini? Alifungua dirisha la chumba choke akatazama nje. Mama yangu! Mtaa mzima wa Matango ulikuwa unateketea. Moto  ulikuwa ukisambaa kila mahali kwa haraka sana. Kelele za watu zilizidi kuhanikiza. Ndipo  alipowaamsha wanawe waondoke upesi. Alijua hakuna usalama pale. Maneno ya Chifu  Mshabaha yalipiga mwangwi akilini mwake. (uk. 62) 

Mbinu za Lugha/TamathaIi za Usemi/Lugha 

Sitiari

Sitiari pia huitwa istiara. Hii ni mbinu ya kufananisha kitu kimoja na kingine moja kwa moja bila kutumia vilinganishi kama ilivyo katika tashbihi. 

Kuna sitiari nyingi sana zinazojitokeza katika riwaya ya Nguu za Jadi. Baadhi ya sitiari hizi ni: 

Mbungulu anamwambia Mangwasha kwamba amwepuke Sagilu sana kwani yeye ni 'moto wa kuotea mbali' (uk. 79). Hii ina maana kwamba Sagilu ni mtu hatari sana au mwovu. 

• Mangwasha anamwambia Mbungulu kwamba "...Sagilu ni chua ndani ya mchele lakini wakati mwingine hufanana na huo huo mchele..." (uk. 80), kumaanisha kuwa Sagilu ni kigeugeu, ni mtu hatari huku wakati mwingine akijifanya mtu mzuri. 

• "Sasa punje za mkufu wa uhalifu zimeanza kupangika vizuri sana... (uk. 91). Mkufu  unaorejelewa ni watu wanaohusika katika njama ya kuwapunja Waketwa ardhi yao kinyume na sheria. ...Mchwa kwake ni akina nani? Ni watu wanaodharauliwa tu. Si lolote si chochote..." (uk. 93). Hapa, Mtemi Lesulia anawalinganisha wananchi wa kawaida na mchwa 

ambao hawana hadhi yoyote kwake. ...Mwamba alikuwa mwamba ambao Mafamba hangeweza kuupasua hata kwa baruti za maneno..." (uk. 95). Mwamba alikuwa mwanasheria mzuri kiasi kwamba Mafamba hangeweza kumshinda katika kesi ya ardhi ambako alikuwa akiwawakilisha Waketwa. "Mhn, tangu lini mlima wa changarawe ukashindana na mlima wa mwamba?" (uk. 103). Hapa Mangwasha anamlinganisha Sagilu na mlima wa changarawe na kumlinganisha Mwamba na mlima wa mwamba. Sagilu hangeweza kumshinda Mwamba katika uchaguzi waliotarajia kwani mwamba alikuwa na umaarufu kuliko Sagilu. 

• Mtemi Lesulia anamrejelea Ngoswe kama lumbwi (uk. 129), kumaanisha kwamba Ngoswe ni kigeugeu, haaminiki. Hii ni baada ya Ngoswe kuamua kujiunga na wafuasi wa Lonare,  mpinzani wa kisiasa wa babake. 

Vijana wa mitaani, wengine wao wamehitimu masomo vizuri lakini hawana ajira, huku wale wa kike wakizalishwa mapema, wanaitwa majeruhi wa jamii (uk. 138). Hapa, vijana hao  wanateseka kutokana na hali mbaya ya mambo katika jamii, ndio maana wanaitwa majeruhi.  Wameathiriwa vibaya na jamii na hawana msaada. 

"...Kwa miaka mingi, Mshabaha alikuwa akikusanya mzigo wa miba..." (uk. 155). Mzigo wa miba unarejelea mabaya ambayo 

Chifu Mshabaha alijizolea katika maisha yake ambayo sasa matokeo yake yanaanza kumwathiri. ...Kumbe alikuwa akimposa nyoka. Mungu alimnusuru alipoachana naye..." (uk.  156). Hapa, nyoka ni Cheiya. Mashauri anajutia kuwahi kuwa katika uhusiano na Cheiya,  ambaye sasa inagunduliwa alikuwa mtu mwovu, hata aliwahi kutaka kumwangamiza Mashauri kwa kutaka kuchumbiana na mzazi wake. Pia, alikuwa ametumwa na Mtemi Lesulia kumtilia Lonare sumu katika chakula (uk. 155). ...Ndege mliolelewa kizimbani nyie hamwezi kuruka..." (uk. 176). 

Hapa, Sagilu anawalinganisha Mangwasha na Lonare na ndege wasioweza kuruka,  kumaanisha kwamba hawana uwezo wa kubadilisha maisha yao kwa mafanikio.  "...Tunafahamu kwamba, masukuzi ya leo ndio msitu wa kesho..." (uk. 180). Vijana kama masukuzi au miche michanga ya miti, wakipewa nafasi huweza kuwa watu wa kutegemewa na wenye kuimarisha jamii. 

Mangwasha anawaza kwamba Lonare ataweza kuwatoa wananchi wa Matuo kutoka katika mchanga wa moto unaowaunguza. Mchanga unaowaunguza wananchi wa Matuo ni matatizo  chungu nzima yanayowakumba wananchi hao (uk. 182). 

Tashbihi

Tashbihi pia huitwa tashbiha au mshabaha. Katika mbinu hii, mwandishi hufananisha kitu  kimoja na kingine. Baadhi ya maneno yanayotumiwa kufananisha huwa kama, mfano wa,  sawa na, na mithili ya. Zifuatazo ni baadhi tu ya tashbihi zilizotumiwa katika riwaya ya Nguu  za Jadi, kwani ni nyingi sana kitabuni. 

"...Amsahau kama vile mtoto anavyolisahau titi la mamaye..." (uk. 

1): Mangwasha anawazia kumsahau mumewe kabisa. "Huku macho yakiangaza kama anayesaka hirizi iliyopotea..." (uk 3) kama mtu anayetafuta kitu muhimu sana. 

• "...Mtu anapomtazama, kitu cha kwanza kuona ni sharafa la ndevu, nyeupe pepepe mithili ya theluji... (uk. 16) kumaanisha sharafa nyeupe sana. 

• "Mangwasha alisema huku akipumua kama mtu aliyetua mzigo... (uk. 38) kumaanisha Mangwasha alizungumza akipumua kama mtu aliyekuwa amechoka sana. 

• "Pesa zimeamua kuniambaa kama muuaji... (uk. 58) kumaanisha Mangwasha ameishiwa kabisa na pesa. 

• "Mangwasha alikimbia kama mwehu, pumzi zikimtoka kama anayekimbizwa..." (uk. 87)  kumaanisha Mangwasha alikimbia kwa kasi sana. 

• "Alikuwa mrefu kama komanzi, mwenye masharubu yaliyofunika mdomo wote wa juu."  (uk. 93-94) kumaanisha kwamba Mafamba alikuwa mrefu sana. 

• "Alikuwa na uhakika kama mchana kwamba angemkuta mumewe mahali hapo..." (uk. 99)  kumaanisha Mangwasha alikuwa na imani 

kabisa kwamba angempata mumewe pahali pale. 

"...alitupatupa vitu ovyo kama mwehu..." (uk. 106) kumaanisha Mangwasha alitupatupa vitu  bila mpangilio au utaratibu wowote. 

• "Mwishowe, (Mrima) alisalia kimya mithili ya kondoo aliyekuwa akipelekwa machinjioni..." (uk. 115) kumaanisha Mrima alitulia kabisa. 

• "Mashauri alisema kisha akachomoka kutoka pale mithili ya mshale..." (uk. 144)  kumaanisha Mashauri alitoka pale mbio. 

• "Maisha ni kama kidau kinachoelea baharini..." (uk. 158) kumaanisha hakuna mtu aliye na hakika juu ya maisha, chochote kinaweza kutokea wakati wowote. 

• "Wengine waliomboleza na wengine wakiangua vilio utadhani kifo kimezuru makazi Yao..." (uk. 164) kumaanisha watu waliokuwa wakiomboleza kupotea kwa Lonare walikuwa na huzuni sana. 

• "Mrima aliuliza akirudi kinyumenyume kama aliyeona kizuu..." (uk. 170) kumaanisha Mrima alihofu sana. 

Tashihisi/uhaishaji

Tashihisi pia huitwa uhaishaji au uhuishi. Hii ni mbinu ambapo kitu kisicho na uhai hupewa sifa za binadamu. 

• "Kauli hii ilimzoa Ngoswe na kumtosa ndani ya kilindi cha wahaka,.." (uk. 171) (kauli imepewa uwezo wa kumzoa Ngoswe) kumaanisha kwamba ushauri wa Lonare ulimgusa sana. 

• "(Mangwasha) hajatembelewa na usingizi kwa sababu ya wingi wa mawazo..." (uk. 169)  (usingizi umepewa uwezo wa kutembea) kumaanisha kwamba Mangwasha hajaweza kulala kutokana na kuwaza sana. 

• "Wengine wakiomboleza na wengine wakiangua vilio utadhani kifo kimezuru makazi hayo..." (uk. 164) (kifo kimepewa uwezo wa kuzuru) kumaanisha waliomboleza kana kwamba walikuwa wamefiwa. 

• "Akrabu za saa iliyotundikwa ukutani zilitangaza saa kumijioni..." (uk. 121) (akraba za saa zimepewa uwezo wa kutangaza) kumaanisha kwamba saa ilionyesha ilikuwa imetimu saa kumi jioni. "Upendo ukatoroka kupitia dirishani, uhitaji ulipobisha mlango..." (uk. 47)  (upendo umepewa uwezo wa kutoroka nao uhitaji umepewa uwezo wa kubisha mlango)  kumaanisha umaskini ulipoingia, upendo ulikosekana katika familia. 

"Chuki iliwavaa Wakule, ikawavisha mashauo na wingi wa tadi..." (uk. 6) (chuki imepewa uwezo wa kuvaa) kumaanisha Wakule waliingiwa na chuki ambayo iliwafanya kuwa na kiburi na ujeuri. 

Methali

Methali ni usemi mfupi, wenye maana pana, busara au hekima ulio na mizizi katika jamii fulani na unaelimisha, kuasa au kukejeli watu au vitendo fulani katika jamii lakini kwa njia iliyofumbwa na kuwekewa tasfida. Hivyo basi, jamii tofauti zina methali tofauti kuambatana na tamaduni na mila zilizomo. Zifuatazo ni baadhi ya methali zilizotumiwa riwayani na maana zake kimuktadha, 

"...chakani mwa simba halali nguruwe..." (uk. 6) hii inarejelea uhusiano wa chuki kati ya Wakule na Waketwa. 

• "...Heri nusu ya shari kuliko shari kamili..." (uk. 13) methali hii inarejelea hali ya Mangwasha kuona ugumu kumweleza Lonare matatizo yake, hasa ikizingatiwa kwamba yeye ni mwanamke. 

• Sagilu anamwambia Mrima, "...nahodha kamwe haogopi mawimbi..." (uk. 19) kama njia ya kumtisha kuhusu uhusiano wake na Mangwasha kwani Sagilu anamtaka Mangwasha kimapenzi. Kauli "...nahodha kamwe haogopi mawimbi... " inatokana na methali "Nahodha hodari hachelei dhoruba". 

• Mrima anamwambia Sagilu, "...kaa ukijua kwamba ghadhabu ya bahari ni furaha ya papa..."  (uk. 19) kumaanisha kwamba yeye haogopi vitisho vya Sagilu. 

• "...Ama kweli, kabla hujafa hujaumbwa..." (uk. 29) Mbungulu anatumia methali hii kumaanisha kwamba unapokuwa hai, lazima yatakufika mambo mengi ambayo utajifunza kutoka kwayo. "...afungaye kibwebwe si bure ana kazi..." (uk. 75) kumaanisha afanyaye kitu  fulani si bure pana sababu ya kutosha. "Hakuna marefu yasiyokuwa na ncha..." (uk. 80)  Mangwasha anatumia methali hii kumaanisha karibuni watajua ukweli kuhusu njama ya kuwafurusha Waketwa kutoka katika ardhi yao kule Matango. ...usilolijua ni usiku wa giza..."  (uk. 85). Mangwasha anashindwa kuelewa ni kitu gani kilitokea hata Sihaba akaachiliwa  huru wakati yeye akidhani yuko jela. "...subira ni ufunguo wa heri..." (uk. 89) kumaanisha kwamba Mangwasha ametulia, hana haraka ya kuwajuvya marafiki zake kuhusu karatasi alizopata kutoka ofisini mwa Chifu Mangwasha ambazo zilikuwa na siri kubwa kuwahusu  Waketwa na njama ya kuwafurusha kutoka katika ardhi yao. ...mzoea tamu huhalalisha haramu..." (uk. 110) kumaanisha kuwa Mrima alitegwa kwenye mitego ya Sagilu hata akasahau maslahi ya familia yake. 

• "Shetani wa mtu ni mtu..." (uk. 115). Sauni anawaza hivi baada ya kutambua jinsi Mrima alivyokubali kubadilishwa na Sagilu, akakosa mwelekeo katika maisha yake. 

• "Aliye juu, msubiri chini..." (uk. 136). Mangwasha anamwambia Sagilu methali hii kwani ana matumaini mambo yatabadilika na kumharibikia Sagilu serikali mpya ikiingia madarakani. 

• "Msiba wa kujitakia huu. Hauna kilio..." (uk. 146). Mangwasha anatumia methali hii kumrejelea Sagilu ambaye amerukwa na akili kutokana na maovu aliyowafanyia  watu. ...palipo na wazee hapaharibiki neno..." (uk. 180). Haya ni maneno ya Lonare  akiwaeleza wananchi kwamba serikali yake itawahusisha wazee wa nchi ili kuhakikisha uthabiti wa nchi. 

Maswali ya balagha

Maswali ya balagha ni mbinu ambapo mwandishi hutumia maswali yasiyohitaji majibu.  Lengo la maswali haya ni kumfanya aliyeulizwa ajisake na ajikosoe au ajifikirishe. Wakati mwingine, maswali ya balagha huwa yanakusudiwa kukejeli. 

Yafuatayo ni baadhi ya maswali ya balagha yaliyotumiwa riwayani na maelezo kuyahusu. 

Starehe ya usingizi itoke wapi ikiwa vurumai na mahangaiko yale yalimwacha fukara? (uk.  1) kumaanisha kwamba hali ya zogo na mahangaiko ilimkosesha usingizi. 

• Lakini...lakini hata akikitegua, salama itoke wapi? (uk. 1) kumaanisha kwamba hata kama angejua alikokuwa mumewe, haingesaidia chochote kwani mumewe alikuwa tayari keshamwachia madhila mengi. 

• Barua ile ina maana gani kwake sasa hata akiisoma? (uk. 3). Mangwasha anashangaa barua anayopata itasaidia nini kwani mumewe hayupo karibu kumsaidia katika hali yake. 

• Kuna mtu akaiba mali yake mwenyewe ya kumhifadhi baadaye? (uk. 47). Mangashwa anaajabia hali ya nchi ya Matuo kuwa na watu ambao wako mbioni kuifilisi nchi bila kuwazia kesho yao. 

• Sare zipi ila magwanda yale? Nguo za 'kauka n'kuvae'? (uk. 63). Maana hapa ni kwamba sare za wanawe Mangwasha zilikuwa mbovu na hawakuwa na nyingine; walilazimika wakati mwingine kuzingoja zikauke ili wazivae tena. Hii inaashiria hali ya umaskini. 

• Kwa nini aletwe hapa kwa gari aina hii? (uk. 68). Mangwasha anashangaa inakuwaje Mbwashu analetwa na gari la serikali anapokuja kuwatembelea Waketwa waliofurushwa kutoka Matango, kwani Mbwashu hakuwa mwakilishi wa kundi lolote hapo Matango.  Mangwasha anashuku ujio wa mwanamke yule mahali hapo. 

• Leo hii amejiwa na malaika gani? (uk. 72). Mangwasha anashangaa kumwona Nanzia,  mkewe Mtemi Lesulia, ambaye hakuwa na mazoea ya kuwatembelea watu walio na shida,  anakuja pale na gari lililojaa vyakula, hasa vya watoto. 

Hajui Chui si rafiki wa kukumbatiwa? (uk. 77). Mangwasha anamwonea huruma mumewe ambaye ana uhusiano na mwanamke ambaye bila shaka hana nia nzuri naye. 

Ardhi hiyo ilimhusu vipi? (uk. 80). Sauni na Sagura wanashangaa namna Sihaba anavyohusika na ardhi ya Matango anapoonekana hapo wakati wa mzozo kuhusu ardhi hiyo. 

Sihaba alitolewa kule lini? Au alifunguliwa mashtaka kisha kuachiliwa kwa dhamana? (uk.  85). Mangwasha anashangaa kumwona Sihaba ambaye alikuwa ametiwa mbaroni, kwani hakutarajia kumwona mahali hapo. 

Misemo na nahau

Misemo ni kauli zenye maana isiyo ya moja kwa moja, na aghalabu huanza kwa nomino.  Nahau ni semi ambazo kwa kawaida huanza kwa kitenzi na kama ilivyo katika misemo,  maana ya nahau haitokani na maana ya jumla ya maneno yaliyotumiwa. Misemo na nahau  mara nyingi hutumiwa ili kuleta uhai na ladha ya mawasiliano. Ifuatazo ni baadhi tu ya misemo na nahau nyingi zilizotumiwa katika riwaya ya Nguu za Jadi. 

• Hakupata hata lepe la usingizi (uk. 1), kumaanisha Mangwasha hakuweza kulala hata kidogo. Mrima wake keshaonjeshwa asali, sasa yu radhi kuchonga mzinga (uk. 37),  kumaanisha kwamba Mrima ameshashawishiwa kabisa kwa pesa, na sasa hata familia haijali tena. 

Mabepari wachache wakaanza kuhodhi vyakula na kuviuza kwa bei ya dhahabu (uk. 45),  kumaanishaa wakaanza kuviuza kwa bei ya juu sana. 

Mwamba alitia masikio pamba, akaendelea na kampeni zake (uk. 53), kumaanisha Mwamba alipuuza masuto ya Sagilu. 

Bila shaka tutajua mbivu na mbichi kuhusu mkasa ute (uk. 73), kumaanisha tutajua ukweli wote kuhusu mkasa huo. 

Alijua akishikwa pale, kitumbua chake kitakuwa kimeingia mchanga (uk. 86), kumaanisha kwamba mambo yake yatakuwa yameharibika. 

Tunahitaji kumzuia kwa jino na ukucha (uk. 92), yaani tunahitaji kumzuia kwa vyovyote vile au tunahitaji kumzuia kwa kila njia. Au hujatosheka kulisha na kuvisha mtu asiye na be wala te (uk. 102), kumaanisha hajatosheka kumlisha na kumvisha mtu asiyekuwa na chochote,  maskini. 

• Mrima pia alikuwa hoi bin taabani (uk. 109), kumaanisha Mrima pia alikuwa katika hali ya kuhangaika. 

Alipobahatika kujenga usuhuba na Mashauri, alijua angeupiga teke uhitaji (uk. 118),  kumaanisha Cheiya alijua angeyaacha maisha ya umaskini. 

Haya yote Mashauri aliyafumbia macho, akatia komango masikioni (uk. 128), kumaanisha Mashauri alipuuza kila kitu babake alitaka kufanya. 

• Mambo yalianza kumwendea mvange (uk. 134), kumaanisha kwamba mambo yalianza kumharibikia Sagilu. 

"Huyo kicheche wako anayeitwa Sihaba asipokoma kuharibu watoto wa nchi hii,  yatamtumbukia nyongo..." (uk. 144), kumaanisha mambo yatamharibikia. 

Hakuamini hasidi yule angemwendea na kofia mkononi kutaka usaidizi wake (uk. 155),  kumaanisha kwamba Mangwasha hakuwahi kutarajia Chifu Mshabaha angekuja kwake kwa heshima kutaka msaada wake. 

Waketwa wakayapungia mkono matumaini ya kumpata Lonare (uk. 167), kumaanisha walikosa matumaini ya kumpata Lonare. Wengi wamedumazwa na mihadarati na wengi tayari wamesharudisha namba (uk. 173), kumaanisha wengi wao wameshaaga dunia kutokana na matumizi ya mihadarati. 

• Wezi na walaghai wamekuwa wakichukua kibubusa rasilimali za nchi kujinufaisha (uk.  178), kumaanisha wamekuwa wakichukua rasilimali za nchi kisiri. 

Chuku

Chuku ni mbinu ambayo huhusisha kutilia kauli au habari chumvi ili kuleta msisitizo. Mbinu  hii imetumiwa ifuatavyo: 

• Baada ya Lonare kushinda uchaguzi, tunaambiwa kwamba watu wanasakata densi na kuvimba miguu kama walioshikwa na ugonjwa wa matende (uk. 177), kumaanisha kwamba walisherehekea kwa msisimko mkubwa. 

Mbungulu anamwambia Mangwasha kwamba Mrima amekonda kiasi kwamba akipuliziwa pumzi ataanguka (uk. 97), kumaanisha kwamba Mrima amekonda sana. 

• Mwandishi anasema kwamba eneo la Matango lilikuwa kichaka kikavu kilichohamwa hata na panya (uk. 65), kumaanisha eneo hilo lilionekana kama ambalo halikuwa na faida. 

• Mrima anasema kwamba Sagilu aliwahi kuwa na masuria (vimada) watoshao kijiji kizima (uk. 18), kumaanisha kwamba Sagilu alikuwa na vimada wengi sana. 

Dhihaka/kejeli

Kejeli ni mbinu ya kisanaa inayotumiwa kumdhihaki au kumkebehi mtu kutokana na vitendo  au hali fulani. Mbinu hii mara nyingi hutambuliwa kwa namna mtu anavyosema kuhusu  jambo. Kejeli imetumiwa katika riwaya ya Nguu za Jadi ifuatavyo: 

• Chifu Mshabaha anamdhihaki Mangwasha anapomwambia, "Toka mbele yangu. Kwenda!  Waketwa ni watu wasio na akili hata ya kuchagua wachumba..." (uk. 20). Chifu huyu  anaudhika kwa sababu 

Mangwasha amemkataa Sagilu na anaelekea kuolewa na Mrima, ambaye hana mali. 

• Sagilu anamdhihaki Mangwasha anapomuuliza kama hajachoka kulisha na kuvisha mtu  asiye na be wala te (uk. 102) kisha anamuuliza kwa nini hataki kujibu swali muhimu kama lile. Bila shaka, Sagilu anajua kwamba anamuudhi Mangwasha.  

• Dhihaka inajitokeza pale tunapoambiwa, "...Ngoswe alikenua meno akatoa kicheko ghafla.  Papachi kinywani zikicheka pamoja naye..." (uk. 133) kumaanisha kwamba Ngoswe hakupendeza kutokana na papachi kinywani mwake. 

• Sagilu anapoambiwa kwamba Mwamba ameshinda uteuzi, anauliza, "...Waliozoea tumbaku, tambuu wataiweza vipi..." (uk. 145) ambayo inaashiria kwamba anamdharau  Mwamba. 

• Sagilu anamdhihaki Mangwasha anapomwambia, "...Kwenda huko! Ndege mliolelewa kizimbani nyie hamwezi kuruka..." (uk 176). Sagilu anamaanisha kwamba hata kama Lonare ameshinda uchaguzi, hana uwezo wa kuongoza. 

Tabaini

Tabaini ni mbinu ya kutoa msisitizo wa jambo fulani kupitia ukanushaji. Kitenzi kishirikishi kikanushi 'si' hutumiwa kuashiria msisitizo huo. 

• Alikuwa akijikuna kila wakati. Si nywele si mabega si...si... (uk. 131), kumaanisha kwamba kijana huyo alikuwa akijikuna kila mahali. 

• Mahakama ilisaki watu. Si matajiri si maskini (uk. 93), kumaanisha watu kutoka katika matabaka yote walihudhuria mahakama. 

• Ni mtaa ulioishi kila aina ya watu. Si matajiri si maskini (uk. 75), kumaanisha watu wa matabaka yote waliishi katika mtaa huo. 

• Si majumba ya aushi si ghorofa na wingi wa maduka (uk. 65), kumaanisha kulikuwa na maendeleo makubwa. 

Tanakali za sauti

Tanakali za sauti ni kauli ambazo huiga sauti za vitendo au kuelezea hali fulani. Mbinu hii hutoa msisitizo wa vitendo au hali zinazorejelewa. 

Tazama mifano ifuatayo. 

• Bure bilashi (uk. 36) inamaanisha bure kabisa. ...Lonare alikuwa amenyamaza jii... (uk. 76),  kumaanisha Lonare alikuwa amenyamaza kimya bila kutamka neno. 

• Punde si punde, duka likawa linafurika wateja furi furi (uk. 102), kumaanisha duka lilijaa watu. 

• Sasa Mrima anaiona natija hiyo ikimponyoka na kupeperuka peperu (uk. 108), kumaanisha natija hiyo inampotea kabisa. 

• Mwamba aliwaeleza wafuasi wa Lonare waliojaa sisisi nje ya mahakama... (uk. 167),  kumaanisha watu walikuwa wengi nje ya mahakama. 

• Ndoto ya kumwona kiongozi wao ilikuwa imedidimia di di di (uk. 169), kumaanisha matumaini ya kumwona Lonare yalikuwa yamefifia kabisa. 

• Wakademka dem dem kwa kila aina ya ngoma (uk. 177), kumaanisha walicheza kwa kusisimka. 

• Lazima myakatae katakata (uk. 181), kumaanisha lazima wayakatae kabisa.  Ucheshi

Ucheshi ni mbinu ya kutumia lugha kwa namna ya kuchekesha. Mara nyingi, mbinu hii hutumiwa kwa ajili ya kuburudisha. 

• Kuna ucheshi pale ambapo Mashauri anamkumbusha Lombo jinsi alivyoogopa kumshika nzige. Naye Lombo anamkumbusha Mashauri kwamba alikuwa mwoga sana, hata aliwahi kutoroka Shule kwa siku mbili baada ya kuombwa na mwalimu wake kumsaidia kumshika nyoka wakiwa katika Shule ya upili (uk. 131). 

Mangwasha anaonyesha ucheshi anapouliza ni kwa nini mtu aamue kuanguka kingalingali kama mende (uk. 158), naye Sauni anamjibu kwamba ukianguka ukiangalia juu unaweza kuinuka na kuendelea na safari. 

Takriri

Takriri ni mbinu ya kurudiarudia neno, kifungu cha maneno au sentensi ili kusisitiza jambo  au kauli fulani. Mbinu hii imetumiwa ifuatavyo: 

• "...Aidha (Mtemi Lesulia) hakubainikiwa kwamba uongozi hauna misingi yake katika utawala pekee. Haikumbainikia kwamba uongozi ni uhamasishaji wa umma..." (uk. 78).  Takriri hii imetumiwa kusisitiza kwamba Mtemi Lesulia hakujua maana ya uongozi. 

...Alimlaumu kwenye majumba ya starehe. Akamlaumu katika mihadhara ya kisiasa.  Alimlaumu katika afisi za umma. Akamlaumu popote pale ambapo watu walimpa sikio..."  (uk. 128), kumaanisha kwamba Sagilu alimlaumu mwanawe, Mashauri, kila mahali. 

"...Aah, ameshashinda tayari mume wangu hata kabla ya vita. Ushindi wa mteremko tu.  Ushindi wa bwerere. Ushindi asioutaiia wala kuuamkia..." (uk. 167), kumaanisha Mangwasha anaona kwamba Mtemi Lesulia atashinda uchaguzi bila kupingwa, kwa sababu mpinzani wake, Lonare, ameshatekwa nyara na hakuna aliye na habari kuhusu kule aliko. 

Tasfida

Hii ni mbinu ya kutumia lugha ambayo inapunguza ukali wa maneno kwa kuzingatia adabu  njema. Ifuatayo ni mifano ya matumizi ya tasfida katika riwaya ya Nguu za Jadi. 

• Sauni anasema, "...Tamaa ya kinywaji cha Firauni bado inamghilibu...- (uk. 101). Kinywaji cha Firauni ni tasfida ya 'pombe' au 'ulevi'. 

• Sagilu anamwambia Mangwasha, "...Mtabakia kushika tama (Uk. 103). sagilu na kuramba vidonda. Msalie kukalia vigoda..." anamaanisha kwamba Mangwasha na wafuasi wengine wa Lonare watabakia maskini. 

• Mashauri anamuuliza babake, Sagilu, "...Jinsi nilivyokuheshimu baba leo wanila kivuli..."  (uk. 121). Kumla mtu kivuli ni kumwendea 

kinyume.

• Mwandishi anasema, "...Ngoswe alijua sasa mzee huyo zake zinaanza kwenda likizoni tena..." (uk. 161), kumaanisha kwamba Sagilu alikuwa ameanza kuharibikiwa na akili. 

• Mwandishi anamrejelea Mangwasha kwa kusema, "...Aidha, alifunzwa kujihadhari na vitu  vya kupewa. Wazazi watiasa, 'Nguo ya kuazima haisitiri makalio'..." (uk. 12). Neno 'makalio'  limetumjwa badala ya neno 'matako' ambalo lina aibu au linaweza kuonekana kuwa kali. 

 

 

 

Share On:

Support Our Website

Ads help us keep our content on kenyalivetv.co.ke free for you. Please consider supporting us by disabling your ad blocker or whitelisting our site in your ad blocker settings.

You are currently offline.
You are back online.